Tovuti Hii Imefungwa. Tumehamia Kwenye Parstoday Kiswahili
Jumapili, 15 Januari 2012 12:14

Ulevi, Madhara na Athari Zake (5)

Tulisema katika makala zetu zilizotangulia kwamba, utumiaji ulevi hupelekea kupatikana madhara mengi ya kimwili na kiroho kwa mtumiaji wa kinywaji hiki kilichoharamishwa. Kiungo kinachoathirika zaidi na ulevi ni ini. Athari ya pombe katika ini hupelekea kujitokeza maradhi ya ini kuvimba na mwishowe ni mhusika kupata maradhi ya saratani.
Wataalamu wa masuala ya tiba wanasema kuwa, kutumia ulevi kwa muda mrefu hupelekea kudhoofisha ukuaji wa seli za ubongo na mwishowe ni kutofanya kazi kabisa kwa seli hizo. Seli za ubongo ni miongoni mwa seli nyeti na muhimu mno na kuzihuisha kwake sio kazi nyepesi. Aidha utumiaji wa ulevi hupelekea kuathirika kwa ubongo na hivyo kumfanya mtumiaji wa pombe kuanza kukumbwa na maradhi ya kusahau. Baadhi ya watu wanajidanganya kwa kudai kwamba, kunywa pombe huwasaidia kuwaondolea msononeko na mazonge ya mawazo. Hii ni katika hali ambayo utafiti wa kitaalamu unaonyesha kuwa, moja ya sababu za msononeko, mazonge ya mawazo na kujiua ni kutumia pombe. Inasikitisha kuwa, licha ya madhara yote ya ulevi yanayoelezwa na wataalamu kwa mtu binafasi na jamii kwa ujumla, lakini kiwango cha utumiaji pombe kinazidi kuongezeka kwa kasi ulimwenguni na baadhi ya jamii hata zimefikia hatua ya kuifanya pombe kama ndio kinywaji bora cha kumkirimu mgeni. Mashirika yanayotengeneza pombe nayo yamepuuza madhara yote ya kinywaji hicho ambayo yameelezwa baada ya tafiti chungu nzima za kitaalamu na badala yake kila siku yamekuwa yakitoa matangazo mapya ya kutangaza pombe na hivyo kujiongezea kipato chao. Utafiti uliofanywa nchini Marekani unaonyesha kuwa, asilimia 90 ya watu waliobaleghe wanakunywa pombe, ingawa hakuna takwimu za kuaminika zaidi kabisa kuhusiana na watu wenye uraibu wa pombe nchini humo.
Maelfu ya watu nchini Marekani hupoteza maisha yao kila mwaka kutokana na ulevi na utumiaji pombe. Kiujumla pombe inahesabiwa nchini Marekani kuwa sababu ya tatu inayosababisha vifo vya watu katika nchi hiyo. Nchini Russia idadi ya watu wanaomili katika kutumia ulevi imeongeza mno. Takwimu zinaonyesha kuwa, nusu ya watu wanaofariki dunia kila mwaka nchini Russia ambao umri wao ni kati ya miaka 15 hadi 45, kifo chao kinatokana na kutumia pombe. Kituo cha Kitaifa cha Marekani cha Kupambana na Madawa ya Kulevya kimetangaza kuwa, vijana ambao wanakunywa pombe wana uwezekano wa asilimia 50 wa kutumia madawa ya kulevya ikilinganishwa na vijana wengine wasiokunywa pombe. Kiwango cha watu wanaopoteza maisha yao kutokana na kutumia pombe ni mara sita zaidi ya vifo vya watu wanaotumia madawa ya kulevya. Utafiti uliofanywa unaonyesha kuwa, zaidi ya asilimia 40 ya watu ambao walianza kutumia pombe kabla ya kufikisha umri wa miaka 15, walighiriki katika ulevi na kuwa waraibu wakubwa wa ulevi.
Nchini Uingereza takwimu zinaonyesha kuwa, vifo vilivyotokana na maradhi yanayosababishwa na utumiaji ulevi katika kipindi cha miaka 25 iliyopita viliongezeka mara tatu.
Kama tulivyotangulia kusema katika vipindi vyetu vilivyotangulia ni kuwa, Uislamu ukiwa dini iliyokamilika kabisa miongoni mwa dini za Mwenyezi Mungu, umeharamisha na kupiga marufuku utumiaji ulevi. Sababu ya kuharamishwa kwake ni madhara makubwa yanayotokana na kutumia pombe; madhara ya kimwili na kiakili ya mtu binafsi na jamii kwa ujumla. Mwenyezi Mungu anasema katika Surat al-Maida aya ya 90 na 91 kwamba:
"Enyi mlio amini! Bila ya shaka ulevi, na kamari, na kuabudu masanamu, na kupiga ramli, ni uchafu katika kazi ya Shet'ani. Basi jiepusheni navyo, ili mpate kufanikiwa. Hakika Shet'ani anataka kutia kati yenu uadui na chuki kwa ulevi na kamari, na akuzuieni kumkumbuka Mwenyezi Mungu na kusali."
Wataalamu wa masuala ya tiba wanaamini kwamba, miongoni mwa madhara mabaya yanayosababishwa na utumiaji pombe, ni athari mbaya kwa mama mja mzito ambapo matokeo yake ni kuzaliwa mtoto mwenye maradhi ya kurithi. Baadhi ya watoto wanaozaliwa na kuwa na matatizo au nakisi ya viungo, hayo hutokana na utumiaji wa pombe mama zao wakati walipokuwa waja wazito. Wataalamu wa masuala ya tiba wanaamini kuwa, pombe ni sumu ya viungo vinavyokuwa. Inaponywewa na mama mjamzito huingia katika mishipa ya damu ya mtoto kupitia konsdo la nyuma au "placenta" kwa kitaalamu. Pombe hudhuru viungo dhaifu vya mtoto vinavyokuwa.
Watoto wanaozaliwa na wanawake walevi huwa na tatizo la ukuaji dhaifu wa ubongo hivyo kuwafanya wasiwe na akili "nzuri". Uzito mdogo wakati wa kuzaliwa, matatizo ya moyo, figo na macho, matatizo ya mifupa pia huweza kuwapata watoto hawa. Wakati mwingine hatua ya mama mjazito ya kunywa pombe hupelekea kubadilisha umbo halisi la mtoto na hata kupelekea kuzaliwa mtoto mwenye nasiki katika viungo. Aidha wataalamu katika uga huo wanasema kuwa, hatua ya mama mjazito kunywa pombe husababisha madhara makubwa kwa mtoto ambapo pindi anapozaliwa huwa na matatizo ya mtindio wa ubongo.

Andika maoni


Msimbo salama (Security code)
Upyesha (Refresh)

Hadithi ya Uongofu (39)

Ni matarajio yangu kuwa, hamjambo wapenzi wasikilizaji na tunakutana tena katika sehemu nyingine ya kipindi hiki cha Hadithi ya Uongofu. …

Ufeministi, Itikadi na Misingi yake (26)

Assalaamu Alaykum wafuatiliaji wa kipindi hiki na karibuni kuwa nasi katika sehemu nyingine ya kipindi hiki kinachokosoa itikadi ya ufeministi …

Ulaji wa Lishe Bora katika Kipindi Chote cha Maisha

Wataalamu wa Afya wanasema kuwa, awamu mbalimbali za maisha zinahitajia ulaji wa chakula wa aina tofauti. Iwapo wewe ni mtoto, …

Maua mawili ya Mtume wa Allah (31) Sauti

Bismillahir Rahmanir Rahim. Assalaamu Alaykum Warahmatullahi Wabarakaatuh Karibuni wapenzi wasikilizaji wa Idhaa ya Kiswahili Radio Tehran na wasomaji wa mtandao …