Tovuti Hii Imefungwa. Tumehamia Kwenye Parstoday Kiswahili
Jumapili, 15 Januari 2012 12:14

Ulevi, Madhara na Athari Zake (4)

Makala yetu ya leo leo itaanza kwa kutupia jicho ripoti ya taasisi ya juu ya afya ya nchini Italia.
Hivi karibuni Taasisi ya Juu ya Afya nchini Italia ilitangaza kuwa, nchini Italia kila mwaka watu 25,000 huwa wahanga wa utumiaji ulevi. Watu elfu kumi na nane kati yao ni wanaume na idadi iliyobakia ni wanawake. Akthari ya wahanga hao hupoteza maisha yao kutokana na figo kutofanya kazi au ajali za barabarani ambazo chanzo chake ni kulewa. Takwimu hizo zinaonyesha kuwa, mabinti na vijana wadogo laki saba wa Kiitalia wanatumia ulevi; suala ambalo limepelekea taasisi mbalimbali za kijamii nchini humo kuonyesha wasi wasi wake juu ya mustakabali wa baadaye wa jamii, hasa kwa kuzingatia kuwa vijana ndio taifa la kesho. Barani Ulaya maelfu ya watu hususan vijana wadogo hupoteza maisha yao kutokana na matumizi ya ulevi. Shirika la Afya Duniani WHO linakisia kwamba, gharama za kimatibabu na kijamii zinazotokana na utumiaji ulevi huko barani Ulaya zinafikia Yuro bilioni 125 kwa mwaka. Matumizi ya ulevi huwa na taathira kwa mtu kama vile mto uliofurika kwani, utumiaji ulevi huondoa akili na busara. Pindi mtu anapolewa na akili kutofanya kazi yake kama kawaida na hivyo kutokuwa na udhibiti wa matendo na maneno yake, huwa mfano wa mto uliofurika ambao husomba kila kilichoko mbele yake. Dakta Parker wa nchini Marekani yeye anaamini kwamba, nusu ya matukio ya ukichaa na kuwehuka sambamba na yale matatizo ya kisaikolojia yanatokana na utumiaji ulevi na anasema kwamba, athari ya kwanza mbaya ya pombe ni kumuondolea akili na hekima mhusika.
Masuala mengi ambayo leo yamegunduliwa kielimu kwamba, yanatokana na athari mbaya za matumizi ya ulevi, ni uhakika ambao kwa karne kadhaa dini na mafundisho ya Mwenyezi Mungu hususan dini tukufu ya Kiislamu ziliubainisha. Mwenyezi Mungu Mtukufu, amemkataza kwa uwazi kabisa, mwanaadamu kutumia kinywaji chenye madhara cha ulevi na kukitaja kuwa, chimbuko la madhambi makubwa. Mwenyezi Mungu anasema katika Surat al-Maida aya ya 90 na 91 kwamba:
"Enyi mlio amini! Bila ya shaka ulevi, na kamari, na kuabudu masanamu, na kupiga ramli, ni uchafu katika kazi ya Shet'ani. Basi jiepusheni navyo, ili mpate kufanikiwa. Hakika Shet'ani anataka kutia kati yenu uadui na chuki kwa ulevi na kamari, na akuzuieni kumkumbuka Mwenyezi Mungu na kusali."
Aya hii inatuonyesha moja ya madhara makubwa kabisa ya pombe na ulevi ambayo ni kumzuia mja kumkumbuka Mwenyezi Mungu na kusali.
Moja ya sababu kubwa ya kuharamishwa kunywa pombe katika Uislamu ni madhara mabaya yanayotokana na kutumia kinywaji hiki ambapo kama tulivyosema huko nyuma, ni kumuondolea akili na busara mtumiaji wa kinywaji hiki. Uislamu ni dini ambayo imesimama juu ya hekima na utumiaji akili. Tofauti kubwa ya mwanaadamu na viumbe wengine kama wanyama ni akili. Mwenyezi Mungu amempa mwanaadamu akili na hivyo kumtofautisha na viumbe wengine wote. Ni kutokana na tunu na hadia ya akili ndio maana mwanaadamu anapiga hatua na kupata maendeleo makubwa na ya kustaajabisha. Ni kwa kutumia akili ambapo mwanaadamu huwa na mipango na tadbiri katika maisha. Ni kwa kutumia akili ambapo mwanaadamu huweza kuendesha maisha yake na kufanya vitendo vinavyoendana na ubinaadamu.
Thamani ya akili na umuhimu wa hekima na busara pamoja na kutafakari ni mambo ambayo yana umuhimu mkubwa kiasi kwamba, imekuja katika hadithi kwamba, kutafakari lisaa limoja kunahesabiwa kuwa ni bora kuliko ibada za muda wa miaka sabini.
Bwana mmoja siku moja alimuuliza Imam Sadiq AS, kwa nini Mwenyezi Mungu ameharamisha ulevi? Imam akamjibu kwa kumwambia, "kwa sababu, ulevi ni chimbuko la fitina, machafu na mabaya yote."
Kama tulivyoashiria katika vipindi vyote vilivyopita, ulevi humfanya mlevi kuondokewa na akili na hivyo humfanya afanye mambo ambayo ni kinyume na maadili mambo ambayo akiwa hajalewa hawezi kuyafanya. Imam Ali bin Mussa Ridha Imam wa Nane katika silsila ya Maimamu kumi na mbili wa Nyumba Tukufu ya Bwana Mtume SAW anasema:
"Kila aina ya kinywaji ambacho kinambadilisha mtu akili, kiwe kidogo au kingi ni haramu." Wataalamu wa masuala ya tiba wanaamini kwamba, kuna jumla ya magonjwa 60 yanayosababishwa na unywaji wa pombe. Wataalamu hao wa uga wa tiba wanayataja baadhi ya magonjwa hayo kuwa ni mfarakano katika familia, maambukizi ya ugonjwa wa ukimwi, unene kupita kiasi, utapiamlo hasi, mimba kuharibika, kisukari na kadhalika. Baadhi ya wataalamu wa masuala ya tiba wanasema kuwa, kuna madhara ya aina mbili yanayosababishwa na ulevi. Kwanza ni kuathirika kwa mishipa ya fahamu mwilini kote kwa kupunguzwa uwezo na pili ni kuungua baadhi ya ogani za mwili hasa tumbo pindi mtu anapotumia ulevi.

 

Andika maoni


Msimbo salama (Security code)
Upyesha (Refresh)

Hadithi ya Uongofu (39)

Ni matarajio yangu kuwa, hamjambo wapenzi wasikilizaji na tunakutana tena katika sehemu nyingine ya kipindi hiki cha Hadithi ya Uongofu. …

Ufeministi, Itikadi na Misingi yake (26)

Assalaamu Alaykum wafuatiliaji wa kipindi hiki na karibuni kuwa nasi katika sehemu nyingine ya kipindi hiki kinachokosoa itikadi ya ufeministi …

Ulaji wa Lishe Bora katika Kipindi Chote cha Maisha

Wataalamu wa Afya wanasema kuwa, awamu mbalimbali za maisha zinahitajia ulaji wa chakula wa aina tofauti. Iwapo wewe ni mtoto, …

Maua mawili ya Mtume wa Allah (31) Sauti

Bismillahir Rahmanir Rahim. Assalaamu Alaykum Warahmatullahi Wabarakaatuh Karibuni wapenzi wasikilizaji wa Idhaa ya Kiswahili Radio Tehran na wasomaji wa mtandao …