Tovuti Hii Imefungwa. Tumehamia Kwenye Parstoday Kiswahili
Jumapili, 15 Januari 2012 12:11

Ulevi, Madhara na Athari Zake (1)

Ni matumaini yangu kuwa, hamjambo wapenzi wasomaji na karibuni katika makala hii itakayojadili na kuzungumzia ulevi, madhara na athari zake. Katika mfululizo huu tutatupia jicho sababu za kuelekea kwenye ulevi pamoja na taathira zake mbaya kwa familia na jamii kwa ujumla. Kwa kuzingatia kwamba, kwa mujibu wa mafundisho ya Kiislamu pombe au ulevi kwa ujumla umeharamishwa, makala hii itachambua na kuchunguzwa pia kuharamishwa kwa ulevi katika mafundisho ya Kiislamu na kubainisha mtazamo wa Uislamu kuhusiana na suala zima la ulevi, athari na madhara yake kwa mtu binafsi na jamii kwa ujumla. Bila shaka mtanufaika na mfululizo huu. Hii ni sehemu ya kwanza.
Hii leo mwanaadamu amepiga hatua kubwa katika uga wa kielimu na kiviwanda na ameweza kupiga hatua kubwa pia katika kudhamini mahitaji yake muhimu na ya lazima. Hata hivyo mwanaadamu huyu anaandamwa na kukabiliwa na vikwazo vingi katika njia yake ya kufikia maisha salama. Wataalamu wa masuala ya kisaikolojia wanasema kuwa, moja kati ya sifa muhimu ya ulimwengu wa leo ni watu kuwa mbali na masuala ya kimaanawi na vilevile kushtadi suala la mmomonyoko wa maadili. Katika jamii suala la mmomonyoko wa maadili limekuwa tishio kubwa mno katika nchi zilizoendelea kiasi cha kuwafanya baadhi ya watu kukata tamaa ya kuendelea kuishi. Hata hivyo suala la utovu wa maadili na mmomonyoko wa maadili haliishi tu katika jamii za ulimwengu wa Magharibi kwani jambo hili linaonekana kuvuka mipaka na kuingia katika nchi nyingine. Ustadh Mahmoud Hakimi mwandishi wa Kiirani ameandika katika kitabu chake cha " Magharibi Inayozongwa na Maradhi" kwamba: "Maendeleo ya kiteknolojia na kiviwanda bila ya kuzingatia pande za kimaanawi na utu wa kibinaadamu, zimeufanya ulimwengu wa Magharibi na Mashariki kukumbwa na misiba. Haya yote yanatokana na vitu vya mashine kuwa na satwa kwa roho za Wamagharibi na kufifia misingi ya Kiakhlaqi na kimaadili."
Moja ya mambo yanayochangia pakubwa kuporomoka misingi ya familia ni ulevi. Taasisi moja ya utafiti ya Kimarekani imeandika katika makala moja kwamba, utumiaji kileo, madhara na matokeo yake hupelekea kuongezeka kwa vitendo vya utumiaji mabavu, ubakaji na hata kukithiri ajali ambazo husababisha mauaji hususan baina ya vijana. Hii inatokana na kushuka kwa umri wa watumiaji ulevi.
Katika Ulimwengu wa Magharibi wazazi huwaruhusu watoto wao wadogo kutumia ulevi na hata baadhi yao huwafundisha watoto wao na kuwashajiisha kunywa pombe. Hii ni katika hali ambayo, madhara ya kutumia ulevi huwa na taathira hasi katika kipindi cha kukua watoto hao kimwili na kifikra na hivyo kukabiliwa na hatari kubwa.
Ulevi una athari na madhara mengi ambayo si rahisi kuyataja yote. Kumeandikwa vitabu vingi na kufanywa utafiti mwingi na wa kina kuhusiana na suala hilo. Yanayogunduliwa kila wakati yanaonesha wazi hatari ya jambo hili na athari zake mbaya. Kwa hakika mambo haya yanaonesha utukufu wa sheria ya Kiislamu pale ilipoliharamisha ovu hili. Athari ya kwanza na hatari zaidi kwa Muislamu ni athari katika imani. Maasi yanaathiri imani ya Muislamu na hivyo imani yake inapungua na moyo wake unakuwa na giza. Athari ya pili ya ulevi ni kwa mtumiaji mwenyewe. Pombe, kilevi au kileo kina madhara makubwa ya kimwili kwa kila sehemu ya mwili wa mnywaji na kina sumu inayoathiri moja kwa moja kwenye mfumo mzima wa mwili. Aidha, madhara ya ulevi yanafika kwenye chembe chembe za mfumo wa ngozi na kwenye viungo vinavyohusika na utengenezaji wa nishati; viungo ambavyo vinapoteza uwezo wake wa kufanya kazi ndani ya masaa ishirini na nne tangu kunywa funda la kwanza la pombe au tangu kutumia kwa mara ya kwanza ulevi. Ulevi unadhuru hususan moyo ambao baada ya muda unabadilika. Hali hii huishia kwenye kushuka kwa mapigo ya moyo na hatimaye kifo. Athari ya tatu ya ulevi ni kwa jamii. Hapa tutatosheka na kutaja takwimu za baadhi ya matukio yaliyo sababishwa na ulevi.
Mwaka 1968 theluthi moja (1/3) ya matukio ya kujinyonga au ya kutaka kujinyonga yaliyotokea ulimwenguni yalisababishwa na ulevi.
Kwa mujibu wa Shirifa la Afya Duniani (WHO), mwaka 1980 asilimia (86%) ya makosa ya jinai yakiwemo ya kuua, na asilimia hamsini (50%) ya matukio ya uporaji na kutumia nguvu yalisababishwa na ulevi.
Mwaka 1976 madhara ya ulevi yalisababisha ajali za barabarani kama ifuatavyo:
* Nchini Marekani asilimia sitini na saba 67% ya ajali za barabarani zilisababishwa na ulevi.
* Nchini Ufaransa asilimia 46% ya ajali za barabarani zilisababishwa na ulevi.
* Nchini Australia asilimia 50% ya ajali za barabarani zilisababishwa na ulevi.
Madhara mengine ya ulevi ni matatizo ya kifamilia na ya kikazi. Na vile vile hasara za kiuchumi kwa mtu binafsi na kwa jamii kwa ujumla. Tukutane katika sehemu ya pili.

Zaidi katika kategoria hii: « Ulevi, Madhara na Athari Zake (2)

Andika maoni


Msimbo salama (Security code)
Upyesha (Refresh)

Hadithi ya Uongofu (39)

Ni matarajio yangu kuwa, hamjambo wapenzi wasikilizaji na tunakutana tena katika sehemu nyingine ya kipindi hiki cha Hadithi ya Uongofu. …

Ufeministi, Itikadi na Misingi yake (26)

Assalaamu Alaykum wafuatiliaji wa kipindi hiki na karibuni kuwa nasi katika sehemu nyingine ya kipindi hiki kinachokosoa itikadi ya ufeministi …

Ulaji wa Lishe Bora katika Kipindi Chote cha Maisha

Wataalamu wa Afya wanasema kuwa, awamu mbalimbali za maisha zinahitajia ulaji wa chakula wa aina tofauti. Iwapo wewe ni mtoto, …

Maua mawili ya Mtume wa Allah (31) Sauti

Bismillahir Rahmanir Rahim. Assalaamu Alaykum Warahmatullahi Wabarakaatuh Karibuni wapenzi wasikilizaji wa Idhaa ya Kiswahili Radio Tehran na wasomaji wa mtandao …