Tovuti Hii Imefungwa. Tumehamia Kwenye Parstoday Kiswahili
Jumamosi, 09 Aprili 2016 16:54

Usekulari Katika Mizani ya Uislamu (14)

Usekulari Katika Mizani ya Uislamu (14)

Ni matumaini yangu kuwa hamjambo wapenzi wasikilizaji popote pale mlipo. Karibuni kusikiliza kipindi hiki, ambacho lengo lake ni kuuchambua Usekulari kwa kutumia mizani ya mafundisho ya Uislamu ili kuweza kuelewa kasoro, dosari na udhaifu wa fikra na nadharia hiyo ambayo chimbuko lake ni Ulimwengu wa Magharibi. Ni mategemeo yangu kuwa mtanufaika na kuelimika na yale mtakayoyasikia katika kipindi hiki. Endeleeni kuwa pamoja nami basi kuitegea sikio sehemu hii ya 14 ya mfululizo huu.

Katika kipindi kilichopita, tuliendelea kuelezea ukosoaji wa Uislamu kwa nadharia ya Urazini (Rationalism), baada ya kusisitiza kwamba kimsingi Uislamu, sio tu hauipingi akili na utumiaji akili, bali huwa mara kadha wa kadha unamtaka mwanadamu kutumia akili, kwa kuitaja akili kuwa ni “mjumbe wa batini” wa kiumbe huyo. Hata hivyo uwezo wa akili una mipaka yake. Kwa mujibu wa mafundisho ya Uislamu akili haiwezi kuwa chanzo pekee cha utambuzi wa mambo kwa mwanadamu; na haitoshi peke yake kumdhaminia kiumbe huyo saada ya duniani na akhera.  Mwanafikra mkubwa wa Kiislamu wa Kiirani, shahidi Ayatullah Murtadha Mutahari, anasema, kulingana na mafundisho ya Uislamu, akili ya mwanadamu, sio tu inahitajia mwongozo wa wahyi ili kuwa na utambuzi sahihi wa kumjua Mwenyezi Mungu na ulimwengu wa akhera, lakini pia, akili peke yake haijitoshelezi kwa ajili ya maisha ya kijamii na ya binafsi ya mtu katika ulimwengu huu. Maisha ya mwanadamu ni maisha ya kijamii; lakini kinyume na wanyama ambao nao pia wana maisha ya kijamii, maisha ya kijamii ya wanadamu si ya kighariza. Kinyume na wanyama, mwanadamu amejaaliwa kuwa na hiyari. Shahidi Mutahari anaizungumzia nukta hiyo kwa kusema:”Kutokana na kuwa mwanadamu ameumbwa akiwa huru na mwenye hiyari ya kuchagua, wakati wote huwa na uwezekano wa kuhalifu kutekeleza wajibu wake; na kwa sababu ya kuwa na ghariza za maisha, na kwa kuwa anataka kuishi, ameumbwa na hali ya kupigania manufaa yake na kupata yale yenye manufaa na yeye; na ni kwa sababu hiyo, ndiyo maana kile ambacho kila mtu huwa anafikiria kwanza katika jamii ni kufikia malengo yake binafsi, si kufanikisha malengo ya jamii”. Lakini Mitume walionesha kuwa kuna manufaa na maslahi ya juu zaidi ya mtu binafsi na ya kimaada na kuiongoza akili ya kimatendo ya mwanadamu kuelekea kwenye saada na uokovu.”

Kwa mtazamo wa Uislamu, akili, jarabati, ushuhudiaji mambo kwa moyo na tab’an pamoja na wahyi ndivyo vyanzo vya utambuzi wa mambo vya mwanadamu. Bila ya shaka akili inayokusudiwa na Uislamu ina maana pana mno. Lakini kwa vyovyote vile, akili ina nafasi ya msingi katika utambuzi wa masuala katika msingi wake na kuelewa kiujumla ukweli wa msingi juu ya ulimwengu. Uislamu umeiweka akili katika nafasi yenye hadhi tukufu na ya juu. Lakini pamoja na yote hayo haujaghafilika na ukweli kuhusu mpaka wa uwezo wa akili na uwezekano wake wa kuteleza na kukosea. Kwa mtazamo wa Uislamu, wahyi na akili ni mabawa mawili, ambayo endapo mwanadamu atalikosa lolote kati ya mawili hayo hatoweza kuruka na kupaa kwenye anga ya utambuzi wa haki na hakika ya mambo.

Baada ya kuzungumzia misingi mitatu ya kifikra ya Usekulari, yaani Umwanadamu (Humanism), Usayansi (Scientism) na Urazini (Rationalism) na kubainisha mitazamo ya Uislamu kuhusiana na kila moja kati ya misingi hiyo tunaendelea na kipindi chetu kwa kutupia jicho msingi wa nne wa kifikra wa Usekulari ambao ni Uliberali au Uhuria, kwa kimombo Liberalism. Kilugha, Uliberali maana yake ni kupigania kuwa huru au kuwa asili kwa uhuru. Uhuru uliokusudiwa na Uliberali una sifa zake maalumu ikiwemo ya nadharia hiyo kujikita kupindukia kwenye nafasi ya mtu binafsi. Kwa hakika Uliberali unataka kuwepo uhuru wa kujivua na udhibiti au mwongozo wa serikali au wa chombo kingine chochote kile kitakachotaka kuuwekea mipaka uhuru wa mtu binafsi.

Uliberali una matawi kadhaa yakiwemo ya Uliberali wa kisiasa, wa kiuchumi na wa kiakhlaqi. Lakini nukta ya pamoja ya aina zote hizo ni kutetea uhuru wa mtu binafsi kwa namna ya kufurutu mpaka, kueneza mazoea ya kuchukulia mambo kiwepesi na kuvumiliana kwa sura ya kutobali, kutojali na kutoshughulishwa na chochote, kutokubaliana na “umutlaki wa jambo” na vilevile kukataa majukumu. Kwa hakika Ubinafsi, kwa maana ya Individualism ndiyo kiini hasa cha Uliberali. John Locke na Thomas Hobbes, wanafalsafa wa Uingereza wa karne ya 17, ambao wanajulikana kama viranja wa nadharia hii wanampa mtu binafsi umuhimu wa kiwango cha juu mno. Hobbes anasema:”Sisi hatutaki kuwa na jamii kwa sababu ya jamii yenyewe. Hayo (matashi ya mtu binafsi) ndiyo matashi yetu tangulizi; na kuitaka jamii kunafuatia baada ya hayo”, mwisho wa kumnukuu Hobbes. Kutetea Ubinafsi, kwa hakika lilikuwa jibu na radiamali kwa Ujamii wa kufurutu mpaka ambao ulitawala katika zama za Enzi za Kati.

Uliberali unatilia mkazo juu ya uhuru na kujitawala mtu binafsi unaoambatana na tafsiri na maana maalumu ya uhuru huo. Uhuru huo ambao ni maarufu kama “uhuru hasi” au “kuwa huru kutokana na” maana yake ni kwamba mtu lazima awe huru na kila kizuizi katika kufikia matakwa yake na anayoona kuwa yana maslaha kwa yeye binafsi. Lazima mtu aweze kuamua na kuchagua bila ya kushinikizwa au kulazimishwa na nguvu ya nje. “Uhuru hasi” uko mkabala na “uhuru chanya” au “uhuru kwa ajili ya“ ambao unazingatia na kulipa umuhimu zaidi lengo la uhuru huo. Uhuru unaokusudiwa na Uliberali haukibani na kukiwekea mipaka kitu kingine ghairi ya uhuru wenyewe. Yaani mtu yuko huru katika kutekeleza matakwa yake na kukidhi matamanio yake ila pale tu atakapohatarisha uhuru wa mtu mwengine. Kwa hivyo kwa mtazamo wa Uliberali nafasi ya serikali inapasa kuwa ndogo mno na isiyo ya uingiliaji mambo, bali jukumu lake kuu ni kudumisha nidhamu na amani katika jamii. Katika mtazamo huu, serikali haitakiwi kuwa na utashi na muelekeo wowote wa kidini au wa kiidiolojia.

Moja ya sifa kuu na ya msingi iliyonayo fikra ya Uliberali ni kuufanya “uhuru” wa mtu binafsi kuwa ni tunu na thamani mutlaki na kuipa nafasi ya mbele zaidi ya thamani nyenginezo za kiutu kama usawa, uadilifu, imani na utukufu wa kiakhlaqi. Maana ya utangulizaji na utoaji kipaumbele huo ni kwamba haiwezekani kuubana uhuru binafsi wa watu kwa kisingizio cha kuilinda yoyote kati ya thamani hizo. Katika uhuru unaokusudiwa na Uliberali “haki” ya mtu inaitangulia “kheri” yake. Waliberali wanaitakidi kuwa utangulizi huo uko katika nyuga zote za kisiasa, kiuchumi na kijamii, bali hata katika nyanja zote za maisha ya mwanadamu. Kwa mtazamo wa Waliberali “uhuru na kujitawala mtu binafsi” kunapaswa kusiwekewe mpaka wala masharti yoyote; na kila mtu, kulingana na tafsiri yake mwenyewe inapasa achague na kujiamulia kile anachokihisi kuwa ni maisha mazuri na ya saada kwake. Serikali au chombo kingine chochote hakiwezi kuyawekea mpaka matakwa ya mtu. Hoja wanayojenga Waliberali ni kwamba machaguo na maamuzi ya watu tofauti yanakubalika kiakili kwa uzito ulio sawa; na kwa kuwa haliwezi chaguo na uamuzi wa mtu mmoja kufadhilishwa na kuwa bora kuliko wa mwengine, serikali haina haki ya kutumia kisingizio cha kuwa na hadhi ya juu zaidi baadhi ya tafsiri kuhusu kheri na saada na kuingilia mipaka ya mtu ya kujichagulia na kujiamulia.

Wapenzi wasikilizaji, kutokana na kumalizika muda uliotengwa kwa ajili ya kipindi hiki, sina budi kuishia hapa kwa leo nikitumai kuwa mtajiunga nami tena wiki ijayo inshallah katika siku na saa kama ya leo. Basi hadi wakati huo nakuageni huku nikikutakieni kheri na fanaka maishani…/

 

Andika maoni


Msimbo salama (Security code)
Upyesha (Refresh)

Hadithi ya Uongofu (39)

Ni matarajio yangu kuwa, hamjambo wapenzi wasikilizaji na tunakutana tena katika sehemu nyingine ya kipindi hiki cha Hadithi ya Uongofu. …

Ufeministi, Itikadi na Misingi yake (26)

Assalaamu Alaykum wafuatiliaji wa kipindi hiki na karibuni kuwa nasi katika sehemu nyingine ya kipindi hiki kinachokosoa itikadi ya ufeministi …

Ulaji wa Lishe Bora katika Kipindi Chote cha Maisha

Wataalamu wa Afya wanasema kuwa, awamu mbalimbali za maisha zinahitajia ulaji wa chakula wa aina tofauti. Iwapo wewe ni mtoto, …

Maua mawili ya Mtume wa Allah (31) Sauti

Bismillahir Rahmanir Rahim. Assalaamu Alaykum Warahmatullahi Wabarakaatuh Karibuni wapenzi wasikilizaji wa Idhaa ya Kiswahili Radio Tehran na wasomaji wa mtandao …