Tovuti Hii Imefungwa. Tumehamia Kwenye Parstoday Kiswahili
Jumanne, 22 Machi 2016 11:34

Usekulari Katika Mizani ya Uislamu (13)

Usekulari Katika Mizani ya Uislamu (13)

Ni matumaini yangu kuwa hamjambo wapenzi wasikilizaji popote pale mlipo. Karibuni kusikiliza kipindi hiki, ambacho lengo lake ni kuuchambua Usekulari kwa kutumia mizani ya mafundisho ya Uislamu ili kuweza kuelewa kasoro, dosari na udhaifu wa fikra na nadharia hiyo ambayo chimbuko lake ni Ulimwengu wa Magharibi. Ni mategemeo yangu kuwa mtanufaika na kuelimika na yale mtakayoyasikia katika kipindi hiki. Endeleeni kuwa pamoja nami basi kuitegea sikio sehemu hii ya 13 ya mfululizo huu.

Katika kipindi kilichopita tulizungumzia msingi mwengine wa Usekulari ambao ni Urazini kwa kimombo Rationalism kwa maana ya kutegemea misingi ya akili katika fikra, mwenendo na matendo. Tukasema kuwa waasisi wa fikra na nadharia hii iliyoibuka katika karne ya 17 walikuwa ni René Descartes, Baruch Spinoza na Gottfried Leibniz; na kwamba makusudio yao kuhusu Urazini yalikuwa ni kwamba akili ya mwanadamu ndio chanzo pekee cha kuaminika kwa ajili ya utambuzi wa mambo. Wanaurazini wengi kama Spinoza na Descartes walikuwa wakitumia hoja ya kiakili kuthibitisha kuwepo kwa Mungu na ulimwengu wa akhera; na katika hilo walikabiliana na wanafikra wenye mielekeo ya kijarabati, ambao walikuwa wakisema, kwa kuwa Mwenyezi Mungu hawezi kufahamika kwa njia ya hisi, kwa hivyo haiwezekani kumtambua.

Lakini Immanuel Kant, mwanafalsafa mkubwa wa karne ya 18, yeye alidai kwamba imani na kusadikisha kuwepo kwa Mungu ni katika mafundisho "yasiyoendana na akili" na kwamba msingi wa kumthibitisha Mungu unapasa utokane na dhamiri na akhlaqi tu. Kilichofuata baada ya hapo ilikuwa ni kwa Urazini wa kufurutu mpaka kuja na madai makubwa na mapana zaidi ya kudai kwamba akili inatosha kutumika katika nyuga tofauti za maisha ya mwanadamu ikiwemo za utawala, akhlaqi, siasa na uchumi na kupinga kuwepo haja ya dini katika nyanja zote za maisha ya mwanadamu.

Kutokana na Ukristo kuwa na mafundisho yasiyokubaliana na akili ulijikuta ukikabiliana na akili na watu waliokuwa wakitetea akili na nafasi ya urazini na utumiaji akili katika maarifa na utambuzi wa mambo.

Katika vipindi vilivyopita tulisema kuwa mafundisho ya “Utatu”, “Mungu katika umbo la mwanadamu”,”Dhambi ya asili”, “Suala la Mungu”, “Uuzaji wa Maghufira” na “Utakatifu na Umaasumu wa Kanisa na Papa” yalikuwa ni baadhi ya mafundisho ya Ukristo ambayo hayakuweza katu kujengewa hoja ya kukubalika kimantiki na kiakili. Lakini mbali na hayo kulikuwemo na migongano lukuki pia ndani ya Kitabu Kitakatifu. Kwa kutegemea kasoro hizo za mafundisho yasiyokubalika kiakili, Warazini wakadhoofisha na kuiondolea itibari hoja na ukweli wa dini. Ushindi wa akili dhidi ya baadhi ya usuli na misingi ya mafundisho ya Ukristo ulimtia ghururi mwanadamu wa zama za Fikra za Utaalamishaji kwa kimombo Enlightenment juu ya uwezo na kujitosheleza kwa akili.

Nadharia ya Urazini (Rationalism), kama zilivyo nadharia nyengine nayo pia ilifanyiwa ukosoaji na wapinzani wake. Miongoni mwa ukosoaji huo ni kwamba japokuwa Warazini wamekuwa kila mara wanasisitiza juu ya akili kuwa hoja na msingi wa yakini juu ya mambo lakini muda wote kumekuwepo na hitilafu na migongano baina yao katika kubainisha hakika ya ulimwengu. Takribani kila kile ambacho mwanafalsafa mmoja alidai kwa yakini na imani kamili kuwa ni hakika ya jambo, kwa kipimo cha yakini na imani hiyohiyo kilipingwa na kukataliwa na mwanafalsafa mwengine kwa kutoa rai na fikra inayogongana na ya mwanafalsafa huyo. Pamoja na hayo tuelewe kwamba kukosolewa kwa nadharia ya kutegemea akili tupu, yaani Urazini, hakumaanishi kuipinga na kuikataa nafasi na uwezo wa akili, bali ni kutaka kuonyesha kwamba akili ya mwanadamu haiwezi peke yake kufahamu na kujua kwa usahihi hakika ya mambo bila ya kutegemea vyanzo vingine vya utambuzi.

MUZIKI

Katika kipindi kilichopita tuligusia mtazamo wa Uislamu kuhusu elimu za jarabati na majaribio pamoja na mafanikio ya elimu hizo. Na katika vipindi vya kabla yake tuliwahi kuzungumzia mtazamo wa dini hiyo kuhusu akili na juu ya uhusiano baina ya imani na akili. Uislamu, sio tu hauipingi akili na utumiaji akili, bali huwa mara kadha wa kadha unamtaka mwanadamu kutumia akili, kwa kuitaja akili kuwa ni “mjumbe wa batini” wa kiumbe huyo. Kutotumia akili kumekemewa katika aya kadhaa za Qur’ani tukufu. Kwa hivyo kwa kutumia mafundisho ya Uislamu, tunachotaka kujua sasa ni je madai kwamba akili ndiyo chanzo pekee cha utambuzi wa mambo kwa mwanadamu ni sahihi au la?

Uislamu umetaja vyanzo vinne kwa ajili ya kufahamu sharia na hukumu za dini. Akili ni moja ya vyanzo hivyo vinavyojumuisha pia Qur’ani na Suna za Bwana Mtume SAW. Ayatullah Murtadha Mutahari, mwanafikra mkubwa wa Kiirani amelizungumzia suala hilo kwa kusema:”Uislamu umeegemea kwenye akili katika upangaji sharia. Yaani umeitambua rasmi akili kuwa ni msingi na kianzio cha kutungia sharia. Na hili linaweza kuonekana kuwa ni jambo la ajabu, kwamba katika dini fulani, akili imewekwa katika mizani moja na Kitabu cha mbinguni”, mwisho wa kumnukuu Ayatullah Mutahari. Hii inaonyesha kuwa katika Uislamu hakuna mgongano baina ya akili, Kitabu cha mbinguni na Sunna. Lakini kwa mujibu wa mafundisho ya Uislamu akili haiwezi kuwa chanzo pekee cha utambuzi wa mambo kwa mwanadamu; na haitoshi peke yake kumdhaminia kiumbe huyo saada ya duniani na akhera.

Kiujumla ni kwamba kwa kutumia hoja na burhani za kimantiki na kiakili, mwanadamu anaweza kuthibitisha kuwepo kwa Mungu mmoja tu na mwadilifu ambaye ndiye muumba wa ulimwengu. Vilevile kwa kuitumia kwa namna sahihi akili, inawezekana kuthibitisha kwamba mwanadamu ni kiumbe wa kuishi milele, kuthibitisha kuwepo ulimwengu baada ya kifo na pia juu ya udharura wa kuwepo Mitume wa Mwenyezi Mungu na viongozi wa dini kwa ajili ya kumwongoza mwanadamu kuufikia uongofu. Haya ni masuala ambayo kulingana na Uislamu, kila Muislamu anapaswa kuwa na yakini nayo kwa kutumia akili yake. Lakini pamoja na kwamba hakika hizo zinaweza kufahamika kijumla na akili ya mwanadamu, lakini utambuzi na ujuzi sahihi juu ya Mwenyezi Mungu pamoja na sifa zake ni suala ambalo akili peke yake haiwezi kulifikia; na katika suala hilo, mwanadamu anahitaji chanzo chenye upeo wa juu zaidi ya akili yake. Chanzo hicho si kingine ila ni wahyi wa Mwenyezi Mungu.

 Suala jengine muhimu ambalo akili ya mwanadamu inao uwezo wa kuwa na utambuzi wa kiujumla juu yake ni kuhusu kuwepo kwa ulimwengu wa akhera na maisha baada ya kifo. Lakini kufahamu undani wa ulimwengu wa akhera na jinsi maisha ya baada ya kifo yanavyokuwa na vilevile aina ya uhusiano uliopo baina ya dunia mbili hizi ni miongoni mwa masuala mengine muhimu ambayo bila ya mwongozo wa wahyi, akili peke yake haina uwezo wa kuyatambua. Shahidi Ayatullah Murtadha Mutahari anasema hivi kuhusiana na nukta hiyo:”Kama ni kulikubali tu suala la (kuwepo) akhera, bila ya shaka elimu na akili ya mwanadamu vinatosha; lakini kama ni kufanya uhakiki juu ya masuala ya akhera na kutambua ni kitu gani kina faida kwa ajili ya saada ya akhera na kitu gani kina madhara; akili ya mwanadamu pekee haitoshi”.

Wapenzi wasikilizaji, kutokana na kumalizika muda uliotengwa kwa ajili ya kipindi cha Usekulari katika mizani ya Uislamu, sina budi kuishia hapa kwa leo, nikiwa na matumaini kuwa mtajiunga nami tena wiki ijayo katika siku na saa kama ya leo katika sehemu nyengine ya kipindi hiki. Basi hadi wakati huo nakuageni huku nikikutakieni heri na fanaka maishani…/

Andika maoni


Msimbo salama (Security code)
Upyesha (Refresh)

Hadithi ya Uongofu (39)

Ni matarajio yangu kuwa, hamjambo wapenzi wasikilizaji na tunakutana tena katika sehemu nyingine ya kipindi hiki cha Hadithi ya Uongofu. …

Ufeministi, Itikadi na Misingi yake (26)

Assalaamu Alaykum wafuatiliaji wa kipindi hiki na karibuni kuwa nasi katika sehemu nyingine ya kipindi hiki kinachokosoa itikadi ya ufeministi …

Ulaji wa Lishe Bora katika Kipindi Chote cha Maisha

Wataalamu wa Afya wanasema kuwa, awamu mbalimbali za maisha zinahitajia ulaji wa chakula wa aina tofauti. Iwapo wewe ni mtoto, …

Maua mawili ya Mtume wa Allah (31) Sauti

Bismillahir Rahmanir Rahim. Assalaamu Alaykum Warahmatullahi Wabarakaatuh Karibuni wapenzi wasikilizaji wa Idhaa ya Kiswahili Radio Tehran na wasomaji wa mtandao …