Tovuti Hii Imefungwa. Tumehamia Kwenye Parstoday Kiswahili
Alkhamisi, 17 Machi 2016 10:50

Uhusiano wa Iran na Afrika mwaka moja uliopita

Uhusiano wa Iran na Afrika mwaka moja uliopita
Hamjambo wapenzi wasikilizaji na karibuni kujiunga nasi katika kipindi hiki maalumu ambacho kitaangazia kwa kifupi baadhi ya nukta kuhusu uhusiano wa Iran na nchi za Afrika katika kipindi cha mwaka moja uliopita.

Katika kipindi cha mwaka mmoja uliopita, tumeshuhudia kustawi uhusiano wa Iran na nchi za Afrika katika nyanja mbali mbali za kisiasa, kiuchumi, kiutamaduni na kimichezo. Safari ya wakuu wa nchi za Afrika nchini Iran kama vile Rais wa Ghana, kuzinduliwa mradi wa maji safi uliofadhiliwa na Iran nchini Kenya,kuundwa Baraza la Kibiashara la Wairani Afrika Mashariki na safari za waziri wa mambo ya nje wa Iran katika baadhi ya nchi za Kiafrika zimefayika kwa lengo la kuimarisha uhusiano wa pande mbili.

Bara la Afrika ni bara la pili kwa ukubwa duniani na lina idadi ya watu bilioni moja na nchi 54. Bara la Afrika lina nafasi muhimu na ya kipekee katika sera za kigeni za Jamhuri ya Kiislamu ya Iran.

Hivi sasa pia, Jamhuri ya Kiislamu ya Iran ina uhusiano wa kidiplomasia na nchi nyingi za Afrika na ina ushirikiano mzuri na nchi hizo katika nyanya mbali mbali.

Naibu Waziri wa Mambo ya Nje wa Iran anayeshughulikia masuala ya Afrika hivi karibuni alisema: "Kuimarisha kiwango cha uhusiano na nchi za Afrika ni kati ya vipaumbele muhimu vya sera za kigeni za Jamhuri ya Kiislamu ya Iran.

Ni kwa msingi huo ndio mwezi Februari Rais John Dramani Mahama wa Ghana aliitembelea Iran ambapo katika safari hiyo Iran na Ghana zilitiliana saini mapatano kadhaa ya uhusiano.

Katika safari hiyo Rais wa Ghana alikutana na kufanya mazungumzo na Rais Hassan Rouhani wa Iran ambaye alisema Iran iliwaunga mkono watu waliodhulumiwa Afrika wakati wa mapambano dhidi ya mfumo wa ubaguzi wa rangi. Katika kikao hicho, rais wa Iran alisema kuna nyanja nyingi za kuimarisha uhusiano wa pande mbili. Pande hizo zilizungumza kuhusu masuala ya kiuchumi, kiutamaduni, kielimu na huduma za kijamii.

Aidha zilijadili kuhusu masuala ya kieneo na kimataifa na mapambano dhidi ya misimamo mikali barani Afrika.

Kabla ya safari ya Rais wa Ghana nchini Iran, Makamu wa Kwanza wa Rais wa Afrika Kusini Cyril Ramaphosa akiwa na ujumbe wa watu 160 wakiwemo wafanya biashara, wenye viwanda na wawekezaji alifika Tehran kwa lengo la kutathmini uimarishwaji uhusiano wa nchi hizi mbili.

Hivi sasa Afrika Kusini inatathmini ujenzi wa kituo cha kusafisha mafuta ambacho kitakuwa maalumu kwa ajili ya kusafisha mafuta ghafu ya petroli kutoka Iran.

Katika mkutano wake na Ramaphosa, Rais Hassan Rouhani wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran alisema kustawisha uhusiano na nchi za Afrika ni katika msingi wa sera za kigeni za Jamhuri ya Kiislamu ya Iran. Rais Rouhani aliashiria uwezekano uliopo wa kustawishwa uhusiano wa Iran na Afrika Kusini na kusema kuna udharura wa kutumia uwezo uliopo katika mkondo wa kuboresha ushirikiano wa pande zote baina ya nchi mbili. Rais wa Iran pia alisisitiza udharura wa ushirikiano wa Tehran na Pretoria katika nyanja za kupambana na ugaidi ambao ni tatizo sugu duniani na kuongeza kuwa, Jamhuri ya Kiislamu ya Iran inafuatilia kwa uzito suala la kupambana na ugaidi na misimamo mikali duniani na inaamini kuwa wote wanapaswa kushirikiana katika suala hili.

Kwa upande wake, Makamu wa Rais wa Afrika Kusini aliishukuru Iran kwa kuunga mkono mapambano ya Waafrika Kusini dhidi ya utawala wa ubaguzi wa rangi. Alisema watu wa Afrika Kusini kamwe hawatasahau msaada na uungaji mkono wa Iran katika zama za kupambana na ubaguzi wa rangi nchini humo.

Mwaka uliopita wa Kiirani Waziri wa Mambo ya Nje wa Iran alitembelea eneo la Afrika Kaskazini. Zarif alitembelea Tunisia na Algeria kwa lengo la kuimarisha uhusiano wa kisiasa na kiuchumi na nchi hizo.

Katika safari hiyo nchini Tunisia, Zarif alikutana na Waziri Mkuu wa nchi hiyo Habib Essid. Katika kikao hicho, Zarif alisema, kwa kuzingatia kuongezeka ugaidi ambao ni tishio kwa nchi zote za eneo, Tehran na Tunis zinaweza kuimarisha uhusiano wao katika vita dhidi ya ugaidi. Baada ya safari ya Tunisia Zarif alielekea Algeria na kukutuana na wakuu wa nchi hiyo akiwemo Rais Abdulazizi Buteflika na Waziri wa Mambo ya Nje Ramadan Lamamra.

Mwaka uliopita wa Kiirani maafisa wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran walishiriki katika kikao cha viongozi wa nchi za Umoja wa Afrika AU. Kikao cha 26 cha Viongozi wa AU kilifanyika katika makao makuu ya umoja huo huko Addis Ababa mji Mkuu wa Ethiopia. Jamhuri ya Kiislamu ya Iran hushiriki katika vikao vya Umoja wa Afrika kama mwangalizi.

Mwaka uliopita kulifanyika mazungumzo ya kuimarisha uhusiano wa kibiashara na uwekezaji baina ya Iran na nchi za Afrika kama vile Kenya, Uganda, Niger, Zimbabwe n.k. Kwa mujibu wa Shirika la Ustawi wa Uuzaji Biashara Nje, Iran iko tayari kuwekeza dola bilioni tano barani Afrika.

Kati ya nukta zinazofuatiliwa katika kuimarisha uhusiano wa kibiashara baina ya Iran na Afrika ni kuwepo safari za moja kwa moja za ndege na meli, mikopo kwa wafanyabiashara n.k

Mwaka uliopita wa Kiirani Makamu wa Kwanza wa Rais wa Iran Ishaq Jahangiri alitembelea Algeria na kufanya mazungumzo na wakuu wa nchi hiyo sambamba na kufanyika kikao cha pili cha Tume ya Pamoja ya Ushirikiano wa Kiuchumi baina ya Iran na Algeria. Akiwa huko alifanya mazungumzo na Rais Abdulaziz Bouteflika na maafisa wengine wa ngazi za juu nchini humo. Bouteflika alisisitiza kuhusu kuimarishwa uhusiano wa Iran na Algeria na pia ulazima wa kushirikiana nchi mbili kuhusu bei ya mafuta duniani.

Aidha alisisitiza kuhusu umuhimu wa kuwepo jitihada za kuimarisha umoja wa Waislamu na kukabiliana na njama za maadui.

Mwaka uliopita wa Kiirani Waziri wa Mambo ya Nje wa Nigeria Geoffrey Onyeama aliitembelea Iran kwa lengo la kufanya mazungumzo kuhusu kuimarishwa uhusiano wa Tehran na Abuja. Katika mazungumzo hayo na mwenzake wa Nigeria, Waziri wa Mambo ya Nje wa Iran Mohammad Javad Zarif alisema nchi mbili zinaweza kushirikiana katika nyanja za kiuchumi, kisayansi na kiteknolojia. Waziri wa Mambo ya Nje wa Algeria naye aliitaja Jamhuri ya Kiislamu ya Iran kuwa nchi yenye uwezo mkubwa na hivyo akataka kuimarishwa uhusiano wa pande mbili.

Mwaka uliopita i pia Rais Muhammadu Buhari wa Nigeria aliitembelea Iran kushiriki katika Mkutano wa Tatu wa Nchi Zinazouza Kwa Wingi Gesi Duniani. Katika safari hiyo, Buhari alikutana na kufanya mazungumzo na Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu. Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu Ayatullah Khamenei alisema kuna udharura wa kuimarishwa ushirikiano wa nchi za Kiislamu katika kulinda utamblisho wa Kiislamu na Waislamu. Ayatullah Khamenei alisema ni makosa kuwa na matarajio ya ushirikiano na msaada wa Marekani na Magharibi katika kupambana na mirengo ya kigaidi kama Daesh na Boko Haram. Aliongeza kuwa, ripoti za kuaminika zinaonesha kwamba, Wamarekani na baadhi ya nchi zilizobakia nyuma za eneo hili wanalisaidia moja kwa moja kundi la Daesh nchini Iraq na kushiriki katika uharibifu.

Alisema kuwa kuzidishwa ushirikiano wa nchi za Kiislamu hakuna maana ya kufunga na kukata uhusiano na nchi nyingine na kuongeza kuwa, Jamhuri ya Kiislamu ya Iran ina uhusiano mpana na nchi zote isipokuwa Marekani na utawala wa Kizayuni wa Israel lakini inaamini kuwa, nchi za Kiislamu zinapaswa kukaribiana zaidi.

Mwezi Machi 2016 Balozi wa Iran nchini Tanzania allisema maafisa wa kijeshi wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran na wa Jamhuri ya Muungano ya Tanzania wamekubaliana kuendelea kufanywa kwa utaratibu maalumu safari za manowari za operesheni na za utoaji mafunzo za Iran huko nchini Tanzania.

Mehdi Agha Jaafari aliyasema hayo hivi karibuni katika bandari ya Dar es Salaam, kwenye hafla ya kuuaga msafara wa manowari ndogo 39 za jeshi la wanamaji la Jamhuri ya Kiislamu ya Iran na kueleza kuwa safari ya manowari hizo imewapa izza na heshima Wairani wanaoishi nchini Tanzania na wapenzi wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran.

Admeri Mkuu wa Pili Babak Abdollahi, kamanda wa msafara wa 39 wa manowari za Jeshi la Wanamaji la Iran amesema safari hiyo ya ukusanyaji taarifa, operesheni na utoaji mafunzo nchini Tanzania ilikuwa ya mafanikio na kuongeza kwamba kushiriki kikamilifu vikosi vya wanamaji vya jeshi la Iran katika operesheni za kuhakikisha amani na uthabiti unapatikana duniani ni ishara ya kuzidi kuongezeka nguvu na uwezo wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran.

Baada ya kutia nanga na kubaki kwa muda wa siku nne katika bandari ya Dar es Salaam, manowari ndogo 39 za jeshi la wanamaji la Iran ziliondoka nchini humo baada ya kufanyika hafla ya kuziaga iliyohudhuriwa na maafisa wa ubalozi wa Iran na wa jeshi la Tanzania.

Mwaka uliopita wa Kiirani Rais Uhuru Kenyatta wa Kenya alizindua mradi wa maji safi uliofadhiliwa na Iran katika eneo la Faza Kaunti ya Lamu.

Mradi huo ujulikanao kama Faza-Vumbe utawasaidia wakaazi wa eneo hilo ambao hawakuwa na maji safi na ni kati ya miradi kadhaa ya Iran ya kusaidia wananchi mashinani Barani Afrika.

Kwa ujumla ni kuwa uhusiano wa Iran na Afrika katika kipindi cha mwaka mmoja uliopita umekuwa mzuri na wenye kustawi kwa kasi.

Inaelekea kuwa katika kipindi hiki cha baada ya kuondolewa Iran vikwazo, fursa nyingi zimejitokeza za kuimarisha uhusiano wa kibiashara wa Iran na Afrika. Aidha Iran ina uwezo wa kushiriki katika miradi ya misaada na ujenzi wa miundo mbinu barani Afrika. Kuimarika uhusiano wa Iran na Afrika katika nyanja mbali mbali za kisiasa, kiuchumi na kiutamaduni kuna maslahi kwa pande zote.

Andika maoni


Msimbo salama (Security code)
Upyesha (Refresh)

Hadithi ya Uongofu (39)

Ni matarajio yangu kuwa, hamjambo wapenzi wasikilizaji na tunakutana tena katika sehemu nyingine ya kipindi hiki cha Hadithi ya Uongofu. …

Ufeministi, Itikadi na Misingi yake (26)

Assalaamu Alaykum wafuatiliaji wa kipindi hiki na karibuni kuwa nasi katika sehemu nyingine ya kipindi hiki kinachokosoa itikadi ya ufeministi …

Ulaji wa Lishe Bora katika Kipindi Chote cha Maisha

Wataalamu wa Afya wanasema kuwa, awamu mbalimbali za maisha zinahitajia ulaji wa chakula wa aina tofauti. Iwapo wewe ni mtoto, …

Maua mawili ya Mtume wa Allah (31) Sauti

Bismillahir Rahmanir Rahim. Assalaamu Alaykum Warahmatullahi Wabarakaatuh Karibuni wapenzi wasikilizaji wa Idhaa ya Kiswahili Radio Tehran na wasomaji wa mtandao …