Tovuti Hii Imefungwa. Tumehamia Kwenye Parstoday Kiswahili
Jumatatu, 29 Februari 2016 12:19

Usekulari Katika Mizani ya Uislamu (11)

Usekulari Katika Mizani ya Uislamu (11)

Ni matumaini yangu kuwa hamjambo wapenzi wasikilizaji popote pale mlipo. Karibuni kusikiliza kipindi hiki, ambacho lengo lake ni kuuchambua Usekulari kwa kutumia mizani ya mafundisho ya Uislamu ili kuweza kuelewa kasoro, dosari na udhaifu wa fikra na nadharia hiyo ambayo chimbuko lake ni Ulimwengu wa Magharibi. Ni mategemeo yangu kuwa mtanufaika na kuelimika na yale mtakayoyasikia katika kipindi hiki. Endeleeni kuwa pamoja nami basi kuitegea sikio sehemu hii ya 11 ya mfululizo huu.

Kwa wale mnaofatilia kwa karibu kipindi hiki bila ya shaka mnakumbuka kuwa katika kipindi kilichopita tulianza kuzungumzia misingi ya kifikra ya Usekulari, na tukauataja Umwanadamu, kwa kimombo Humanism kuwa ni moja ya misingi ya mfumo huo. Tukaelezea chimbuko la fikra hiyo, mitazamo yake, na hatimaye tofauti zilizopo baina ya Umwanadamu wa Magharibi na fikra za Kiislamu juu ya mwanadamu.

Tukiendelea na maudhui ya kuchambua na kuhakiki misingi ya kifikra ya Usekulari, leo tutatupia jicho msingi wa Usayansi, kwa kimombo Scientism. Madhumuni ya Usayansi hapa ni elimu ya jarabati ambayo ina mafungamano kamili na milango mitano ya hisi za mwanadamu. Wanausayansi wanaitakidi kuwa njia ya ujarabati, yaani ya ufanyaji majaribio na ushuhudiaji wa kihisi, ndio njia pekee ya kuufahamu ulimwengu; na kitu chochote kile kisichoweza kuthibitishwa kupitia njia ya jarabati na majaribio si cha kisayansi, hakina maana na ni cha kutupiliwa mbali. Kwa maana hiyo, masuala kama vile Mungu, roho na ufufuo, kwa kuwa hayawezi kuchunguzwa na kuthibitishwa kwa njia ya hisi na majaribio, si ya kisayansi na hayawezi kukubalika; hayo yanachukuliwa kuwa ni mambo ya khurafa na udhanifu tu.

Wanausayansi aidha wanaitakidi kuwa umaanawi pamoja na masuala ya akhlaqi yanapasa yawe na hali na sura ya kimaada na kijarabati ili yaweze kukubalika. Kwa mintaarafu ya hayo, hata thamani za kimaisha, nazo pia zinapasa zipatikane kwa njia ya jarabati na ushuhudiaji. Akhlaqi zinazokubalika ni zile zinazothibitishwa na elimu ya jarabati, kwa kimombo, empirical knowledge. Akhlaqi za aina hiyo zinapaswa zidhamini manufaa ya kimaada ya mwanadamu na kuwa na tija na faida kwake. Ndiyo kusema kuwa wanafikra wa Usayansi hawakuwa wakiamini kuwepo kwa misingi thabiti ya akhlaqi, bali walilichukulia hilo kuwa ni suala la ukadirifu, yaani relatively.

Elimu ya jarabati ilipiga hatua kwa kasi kubwa katika nyuga za utabibu, usafirishaji, sayansi za anga za mbali na nyanja nyenginezo za mahitaji ya mwanadamu; na sambamba na maendeleo hayo, jamii ya mwanadamu ikaingiwa na hisia ya "ghururi ya kielimu" ambayo ilifikia kileleni katika karne ya 19. Maendeleo hayo yalikuwa ndio kitu kilichokuwa kwenye uwezo wa elimu ya jarabati; lakini kosa kubwa kabisa lililofanywa na wana nadharia wa Usayansi ni kutozingatia mpaka na uwezo wa elimu za jarabati; na kutaka njia ya uthibitishaji mambo kwa majaribio itumike katika nyuga zote za kifikra za mwanadamu. Watetezi wa Usayansi sio tu hawakuyajali wala kuyapa thamani maarifa na utambuzi wa kidini wa mwanadamu bali waliichukua akili ya mwanadamu na mafanikio yake yote yaliyotokana na akili na mantiki na kuyatupa kwenye debe la mambo ya khurafa. Ni kwa sababu hiyo, ndiyo maana watetezi wa Usayansi waliandamwa na radiamali ya haraka ya upinzani na ukosoaji wa wanafikra mbalimbali. Kama tutaukubali Usayansi, hata Hisabati na Mantiki navyo pia vitatolewa nje ya mduara wa wazo na fikra ya kielimu.

Wakosoaji wa Usayansi walikuwa wakiamini kuwa elimu ya jarabati imevuka mpaka kwa kutia mguu wake kwenye uga ulio nje ya uwezo wake, ambao ni wa masuala ya ulimwengu wa nje ya maumbile, dunia ya masuala ya akili na mantiki, uga wa falsafa, akhlaqi, elimu ya kumtambua mwanadamu, elimu ya utambuzi wa asili, elimu ya utambuzi wa ufufuo na mtazamo wa kiujumla juu ya ulimwengu wa maumbile. Miongoni mwa wapinzani wa Usayansi, ambao ni Walahidi, yaani wasioamini Mungu walikuwa wakiyachukulia mambo hayo kuwa ni sehemu ya uga wa masuala ya akili na dini. Alla kulli hal si yeyote kati ya walahidi au watu wa dini, waliokubaliana na dhana hiyo ya Usayansi, kwamba kubainisha lengo la maisha, elimu ya kuutambua ulimwengu, elimu ya kumtambua mwanadamu na ulimwengu wa masuala ya akili na mantiki ni mambo ya khurafa kwa sababu tu hayawezi kuthibitika kwa jarabati na njia za majaribio. Bali waliyaelezea yote hayo kuwa ni mambo yaliyo katika upeo wa juu zaidi na wa kina zaidi ya fikra ya mwanadamu ambao elimu za jarabati haziwezi kuufikia.

Katika zama za kutamba na kutokuwa na mpinzani elimu za jarabati, namna ambavyo Kanisa liliamiliana na maendeleo ya kisayansi ilikuwa moja ya sababu muhimu iliyoifanya dini ijondoe kwenye uwanja wa maisha ya mwanadamu. Muamala wa Kanisa kuhusiana na elimu za jarabati ulikuwa ni wa kufurutu na kupindukia mpaka; iwe ni katika kipindi cha kufifia kwa sayansi cha zama za Enzi za Kati (Middle Ages) au cha wakati wa kukua na kustawi kwake katika zama za

 Mvuvumko mkubwa wa Sanaa na Maarifa, kwa kimombo Renaissance. Katika zama za Enzi za Kati, Kanisa lilikuwa likitoa tafsiri potofu na isiyo ya kielimu kuhusu vitu vya ulimwengu wa maumbile na halikuwa likimruhusu mtu yeyote afanye utafiti au kupingana na tafsiri hiyo. Kanisa liliifanya baadhi ya misingi na kanuni za kimaumbile na kielimu kuwa ni vitu vitakatifu na vya kidini na kuvitafsiri kuwa ni sehemu ya mambo ya kidini yasiyo na shaka yoyote. Lakini maendeleo ya kielimu yakaonyesha waziwazi kuwa tafsiri na mitazamo hiyo ilikuwa batili. Mfano wa wazi kabisa ulikuwa ni wa imani ya jua kuizunguka sayari ya dunia, ambao ulikuwa ni mtazamo wa kidini wa Kanisa, lakini Galileo Galilei akathibitisha kuwa ukweli ni kinyume na imani hiyo. Radiamali na jibu la Kanisa kwa ugunduzi na ubunifu wa wanasayansi na wataalamu wa jarabati lilikuwa ni hasi na kanushi; kiasi kwamba sayansi na elimu hizo mpya zilitangazwa na Kanisa kuwa ni kitu kisicho na utakatifu; na wanasayansi na wataalamu wa elimu hizi wakakufurishwa na hatimaye kupandishwa kizimbani kwenye mahakama za udadisi wa itikadi na kuhukumiwa kwa kupewa adhabu mbalimbali.

Kanisa lilikuwa haliukubali mfumo wa kuwepo sababu katika vitu vya kimaada vya ulimwengu huu, bali lilikuwa likiyahusisha na kuyanasibisha moja kwa moja mambo yote na Mwenyezi Mungu. Lakini mbali na vitu vya kimaumbile kama mvua na tufani, mambo kama vile muujiza, irada ya Mungu na kutawakali kwa Mwenyezi Mungu, nayo pia lilikuwa likiyabainisha kwa msingi na sura hiyo hiyo, yaani kuingilia moja kwa moja Mwenyezi Mungu katika mambo bila ya kuwepo pia na sababu. Baada ya kugunduliwa na kutambuliwa na elimu ya sayansi mahusiano yaliyopo baina ya vitu vilivyoko katika ulimwengu wa maumbile, mitazamo ya kikristo na ya kidini ikaanza kutiliwa shaka. Elimu ya jarabati na majaribio ilikuwa ikikitolea kila kitu cha kimaada sababu yake ya kimaada. Mwenendo huo ulianza kuyashusha hadhi mafundisho ya Kanisa hatua kwa hatua. Katika hali hiyo, Kanisa halikuwa na chaguo wala njia nyengine isipokuwa kukubali kwamba uwanja wa elimu ya sayansi ni tofauti na wa dini; na dini haina budi kujificha ndani ya kuta za Kanisa. Msimamo huo wa kusalimu amri Kanisa uliibua hisia na tafsiri kwa wanasayansi na watu wa kawaida kwamba dini na elimu ya sayansi hazitangamani; na kama mtu anaitaka sayansi hana budi kuachana na dini.

Wapenzi wasikilizaji, muda uliotengwa kwa ajili ya kipindi hiki umefikia tamati. Hivyo sina budi kuishia hapa kwa leo nikiwa na matumaini kuwa mumenufaika na yale mliyoyasikia katika sehemu hii ya 11 ya kipindi cha Usekulari Katika Mizani ya Uislamu. Basi hadi tutakapokutana tena wiki ijayo kwa majaaliwa ya Mola katika sehemu ya 12 ya kipindi hiki nakuageni huku nikikutakieni kila la kheri maishani…/

 

Andika maoni


Msimbo salama (Security code)
Upyesha (Refresh)

Hadithi ya Uongofu (39)

Ni matarajio yangu kuwa, hamjambo wapenzi wasikilizaji na tunakutana tena katika sehemu nyingine ya kipindi hiki cha Hadithi ya Uongofu. …

Ufeministi, Itikadi na Misingi yake (26)

Assalaamu Alaykum wafuatiliaji wa kipindi hiki na karibuni kuwa nasi katika sehemu nyingine ya kipindi hiki kinachokosoa itikadi ya ufeministi …

Ulaji wa Lishe Bora katika Kipindi Chote cha Maisha

Wataalamu wa Afya wanasema kuwa, awamu mbalimbali za maisha zinahitajia ulaji wa chakula wa aina tofauti. Iwapo wewe ni mtoto, …

Maua mawili ya Mtume wa Allah (31) Sauti

Bismillahir Rahmanir Rahim. Assalaamu Alaykum Warahmatullahi Wabarakaatuh Karibuni wapenzi wasikilizaji wa Idhaa ya Kiswahili Radio Tehran na wasomaji wa mtandao …