Tovuti Hii Imefungwa. Tumehamia Kwenye Parstoday Kiswahili
Jumamosi, 12 Disemba 2015 19:10

Kwa Vijana Wote wa Magharibi (1) (Mapitio ya Muhtawa wa Barua ya Kiongozi Muadhamu)

Kwa Vijana Wote wa Magharibi (1) (Mapitio ya Muhtawa wa Barua ya Kiongozi Muadhamu)

Assalamu Alaykum wapenzi wasikilizaji. Karibuni kuwa nami katika kipindi kingine cha Makala ya Wiki, ambapo kwa wiki hii tutaanza kuchambua pande tofauti za barua ya pili ya Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu Ayatullah Sayyid Ali Khamenei kwa vijana wa Magharibi, tukianza kwa kutupia jicho muhtawa wa barua hiyo. Ni matumaini yangu kuwa mtaendelea kuwa nami hadi mwisho wa kipindi kusikiliza niliyokuandalieni katika makala hii.
MUZIKI
Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu ameamua kuzungumza tena kwa mara ya pili na vijana wa Magharibi kwa kuwaandikia barua ya upendo na ya kimwamko. Kabla ya hapo, takribani miezi kumi nyuma pia, baada ya kufikia kilele wimbi la uenezaji hofu na chuki dhidi ya Uislamu huko Magharibi, Ayatullah Khamenei alichukua hatua ambayo haijawahi kushuhudiwa kabla, ya kuwaandikia barua ndefu vijana wa Magharibi, akiwataka watafakari kwa uhuru kuhusu Uislamu na kutafuta ukweli kuhusu dini hiyo bila ya kupitia kiunganishi wala wasita wowote. Katika barua yake hiyo ya kihistoria, aliwataka vjana hao wafanye utafiti wao wenyewe kwa kuvisoma vyanzo vikuu vya Uislamu, yaani Qur'ani tukufu na mafundisho ya Mtume wa mwisho, badala ya kutosheka na yale yanayosemwa na vyombo vya habari kuhusu Uislamu na Waislamu. Hivi sasa baada ya matukio ya kigaidi yaliyojiri hivi karibuni nchini Ufaransa, kwa mara nyengine, Ayatullah Khamenei, akiwa mmoja wa viongozi wakubwa zaidi wa kidini duniani, amezungumza na vijana wa Magharibi, ili kuwafikishia ujumbe wa kutetea haki na fikra huru wa Uislamu katika anga safi isiyogubikwa na wingu la makelele na propaganda za vyombo vya habari duniani.
Katika barua yake ya karibuni, Ayatullah Khamenei ameashiria matukio ya kigaidi yaliyotokea mjini Paris, Ufaransa na katika pembe nyengine za dunia na kusema:"Kila mtu ambaye amenufaika na mahaba na ubinadamu ataathirika na kuumizwa kwa kuyashuhudia matukio haya popote yanapotokea, yawe yanatokea nchini Ufaransa, Palestina, Iraq, Lebanon au Syria. Hapana shaka kuwa Waislamu bilioni moja na nusu wana hisia hiihii na wanachukizwa na kukerwa na wafanyaji na wasababishaji wa maafa haya. Lakini suala muhimu hapa ni hili, kwamba ikiwa machungu ya leo hayatapelekea kujengwa kesho iliyo bora na iliyo na amani zaidi, yataishia kuwa kumbukumbu tu za matukio machungu na yasiyo na faida yoyote. Mimi ninaamini kuwa, ni nyinyi vijana tu ndio mnaoweza kujifunza kutokana na misukosuko ya leo ili kuweza kubuni njia za kujenga mustakbali na kuzuia upotovu ambao umeifikisha Magharibi ilipo hivi sasa."
Tarehe 13 Novemba 2015, mnamo saa 10 na dakika 21 kwa saa za Ulaya ya Kati ulijiri mlolongo wa mashambulio yaliyoratibiwa ya kigaidi katika mji wa Paris, yaliyosababisha kuuawa watu 130 na kujeruhiwa wengine 368 na kufuatiwa na kutangazwa hali ya hatari nchini Ufaransa. Mashambulio hayo ni tukio kubwa zaidi la maafa ya roho za watu kutokea nchini humo tangu wakati wa Vita Vikuu vya Pili vya Dunia. Baada ya mashambulio hayo, kundi la kigaidi na kitakfiri la Daesh (ISIS) lilitangaza kuwa ndilo lililohusika; nazo tarumbeta za propaganda za Magharibi, bila ya kuashiria chochote kuhusu utambulisho halisi wa kundi hilo la kigaidi zikaanza kwa mara nyengine tena kupuliza na kueneza sumu ya hisia za hofu na chuki dhidi ya Uislamu na kuelekeza moja kwa moja mashambulio yake kwa Waislamu; Waislamu ambao, kwa miaka na miaka, wamekuwa ndio waathirika wakuu wa ugaidi wa kitakfiri katika nchi zenyewe za Kiislamu, lakini kilio na mayowe yao dhidi ya dhulma hiyo kikapuuzwa katika dunia ya ulaghai, uzandiki na undumakuwili. Jamii ya Magharibi imekuwa katika maombolezo ya watu waliouliwa katika mashambulio ya Novemba 13 mjini Paris, katika hali ambayo vyombo vya habari vya Magharibi havijasikika kuripoti chochote kuhusu uungaji mkono wa Marekani na madola mengine ya Magharibi kwa kundi la Daesh.
MUZIKI
Ayatullah Khamenei ameashiria kwamba, leo ugaidi ni machungu ya pamoja baina ya Ulimwengu wa Magharibi na wa Mashariki, na akaandika kuwahutubu vijana wa Magharibi kwa kusema:" Lakini pamoja na hayo ghasia na wasiwasi ambao mmeupitia katika matukio ya hivi karibuni, una tofauti mbili muhimu na machungu ambayo watu wa Iraq, Yemen, Syria na Afghanistan wamekuwa wakiyapitia kwa miaka mingi. Tofauti ya kwanza ni kuwa, Ulimwengu wa Kiislamu umekuwa mhanga wa unyama, hofu na ghasia kubwa zaidi na kwa muda mrefu sana; na pili ni kwamba, kwa masikitiko makubwa, ghasia hizo zimekuwa zikichochewa na kuungwa mkono na madola makubwa na kwa njia tofauti na zenye taathira." Kisha baada ya kueleza hayo, Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu ameashiria jinsi Marekani ilivyohusika na kuchangia waziwazi katika kuundwa, kuyaimarisha au kuyazatiti kwa silaha makundi ya Taliban, Al-Qaeda na mengine maovu yaliyofuatia na akaukosoa muungano wa Magharibi na waungaji mkono wanaojulikana, wa ugaidi wa kitakfiri katika eneo hili la Mashariki ya Kati.
Ayatullah Khamenei alikemea pia muamala wa kindumakuwili wa Magharibi katika kukabiliana na vuguvugu la Mwamko wa Kiislamu na mgongano uliopo katika siasa za Wamagharibi na akalitaja suala la Palestina kuwa moja ya mifano ya migongano hiyo na akaandika:" Ikiwa watu wa Ulaya hivi sasa kwa siku kadhaa wamekuwa wakijificha kwenye nyumba zao na kujepusha kushiriki kwenye mikusanyiko na sehemu zenye umati mkubwa wa watu, ni kwa makumi ya miaka sasa familia za Kipalestina hazina usalama hata ndani ya nyumba zao kutokana na mashine ya mauaji na uharibifu ya utawala wa Kizayuni. Utawala huo kila siku hubomoa nyumba za Wapalestina na kutokomeza konde na mashamba yao bila hata kuwapa fursa ya kuhamisha vyombo vyao vya matumizi wala kukusanya mazao yao ya kilimo. Na mara nyingi yote hayo hufanyika mbele ya macho yanayobubujika machozi ya wanawake na watoto waliojawa na hofu kubwa ambao hushuhudia jamaa zao wakipigwa na kujeruhiwa na mara nyingine kupelekwa kwenye jela za kuogofya na za mateso (za Wazayuni)." Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu amekemea vikali kimya cha dhamiri za walimwengu kuhusiana na ushenzi na unyama huo.
Ayatullah Khamenei aliielezea hatua ya miaka ya karibuni ya Marekani na madola mengine ya Magharibi ya kutuma majeshi katika Ulimwengu wa Kiislamu na kusababisha kupotea mamia ya maelfu ya roho za watu wasio na hatia, kuteketezwa miundombinu ya kiuchumi na kiviwanda ya mataifa hayo kuwa ni mfano mwengine wa mantiki yenye mgongano ya Magharibi na akafafanua kwa kusema:"Je, ni vipi nchi ambazo zimeharibiwa kwa kiwango hiki na miji na vijiji vyao vimefanywa jivu zitaambiwa: Tafadhali msijichukulie kuwa ni watu mliodhulumiwa?! Badala ya kuwataka watu wajifanye kama hawafahamu au wayasahau maafa, si bora kuomba msamaha wa dhati? Machungu ambayo yameupata Ulimwengu wa Kiislamu katika miaka ya hivi karibuni kwa wahujumu walio na nyuso mbili na zilizorembwa si madogo kuliko hasara ya kimaada."
MUZIKI
Wapenzi wasikilizaji baada ya matukio yenye kutia shaka ya mashambulio ya Septemba 11, 2001, Marekani ilizivamia na kuzishambulia Afghanistan na Iraq kwa kisingizio cha kupambana na al-Qaeda, ambapo katika kipindi cha karibu miaka 14 tangu ulipofanyika uvamizi huo imeua zaidi ya raia milioni moja na nusu, mbali na kuangamiza na kuteketeza miundombinu ya nchi hizo. Lakini suali la kujiuliza hapa ni al-Qaeda ilitokea tokeaje? Aliyekuwa Waziri wa Mambo ya Nje wa Marekani Hillary Clinton aliungama haya yafuatayo mbele ya kikao cha Kongresi ya nchi hiyo aliposema:"Sisi tuna historia ya pamoja na mtandao wa al-Qaeda. Watu tunaopigana nao leo Afghanistan na Pakistan, tuliwaleta sisi wenyewe mnamo miaka 20 nyuma kwa sababu tuliwatumia wao katika vita dhidi ya Urusi".
Katika sehemu nyengine ya barua ya Ayatullah Khamenei, imesisitizwa kwamba madamu ugaidi unaendelea kugawanywa mbele ya macho ya waungaji mkono wenye nguvu, katika aina mbili za ugaidi mzuri na mbaya, na madamu maslahi ya madola yanaendelea kufadhilishwa mbele ya thamani za utu na maadili, lisitafutwe mahala pengine chimbuko la machafuko na vitendo vya ukatili.
Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu alikosoa hujuma laini na za kimyakimya za Magharibi kwa tamaduni nyenginezo na kuandika katika barua yake kwamba:" Mimi ninaamini kuwa, kuutwisha utamaduni wa Magharibi kwa mataifa mengine na kudunisha tamaduni huru ni utumiaji mabavu wa kimyakimya na wenye madhara makubwa sana. Kudhalilisha tamaduni tajiri na kuvunjia heshima matukufu makubwa zaidi ya tamaduni hizo kunafanyika katika hali ambayo, utamaduni mbadala hauna sifa na uwezo wa kuchukua nafasi ya tamaduni hizo."
Kwa ujumla ni kwamba barua ya karibuni ya Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu, kama ilivyokuwa barua yake iliyotangulia imeripotiwa sana na vyombo vya habari duniani. Japokuwa mtandao wa kijamii wa Twitter ulikurupuka na kuchukua hatua ya kuzifunga akaunti za watumiaji wa mtandao huo walioamua kuisoma na kuitolea maoni barua hiyo, lakini hakuna shaka kuwa hatua kama hizi zitazidi kuwafanya vijana wawe na hamu na shauku zaidi ya kutaka kujua muhtawa na yaliyomo ndani ya barua hiyo. Radiamali za vijana wa Magharibi kwa barua hiyo ni za kuvutia na zinaonyesha nguvu ya kuleta mwamko ya maneno yaliyomo ndani yake. Chris Eldrigde, msanii na mwanaharakati wa kisiasa wa Pennsylvania nchini Marekani amesema haya yafuatayo baada ya kuisoma barua hiyo:"Barua hii imeandikwa ikiwa na ujumbe mzito mno. Imelenga moja kwa moja na kwa ukamilifu kwenye maudhui iliyokusudiwa. Ina lugha tamu mno na tab'an nzito. Ndani yake haina maneno ya njozi na ya matamanio. Barua hii inalenga kujenga hoja mpya au iliyo tofauti kwa ajili ya kukomesha mauaji. Hiki ni kitu kinachopasa kuelezwa kila mahala; lakini inavyoonekana hakiwezi kueleweka na watu kirahisi. Inadhihirika wazi katika barua hii, kwamba amani na heshima kwa watu ni sehemu ya itikadi za kidini za Waislamu".
Wapenzi wasikilizaji sehemu hii ya kwanza ya Makala ya Wiki iliyotupia jicho muhtawa wa barua ya Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu kwa vijana wote wa Magharibi imefikia tamati. Msiache kuwa nasi tena wiki ijayo inshaallah katika sehemu nyengine ya mfululizo huu

Andika maoni


Msimbo salama (Security code)
Upyesha (Refresh)

Hadithi ya Uongofu (39)

Ni matarajio yangu kuwa, hamjambo wapenzi wasikilizaji na tunakutana tena katika sehemu nyingine ya kipindi hiki cha Hadithi ya Uongofu. …

Ufeministi, Itikadi na Misingi yake (26)

Assalaamu Alaykum wafuatiliaji wa kipindi hiki na karibuni kuwa nasi katika sehemu nyingine ya kipindi hiki kinachokosoa itikadi ya ufeministi …

Ulaji wa Lishe Bora katika Kipindi Chote cha Maisha

Wataalamu wa Afya wanasema kuwa, awamu mbalimbali za maisha zinahitajia ulaji wa chakula wa aina tofauti. Iwapo wewe ni mtoto, …

Maua mawili ya Mtume wa Allah (31) Sauti

Bismillahir Rahmanir Rahim. Assalaamu Alaykum Warahmatullahi Wabarakaatuh Karibuni wapenzi wasikilizaji wa Idhaa ya Kiswahili Radio Tehran na wasomaji wa mtandao …