Tovuti Hii Imefungwa. Tumehamia Kwenye Parstoday Kiswahili
Jumatano, 02 Disemba 2015 14:39

Usekulari Katika Mizani ya Uislamu (1)

Usekulari Katika Mizani ya Uislamu (1)

Ni matumaini yangu kuwa hamjambo wapenzi wasikilizaji popote pale mlipo. Karibuni kusikiliza kipindi hiki kipya, ambacho lengo lake ni kuuchambua Usekulari yaani kwa kimombo 'Secularism' kwa kutumia mizani ya mafundisho ya Uislamu ili kuweza kuelewa kasoro, dosari na udhaifu wa fikra na nadharia hiyo. Ni mategemeo yangu kuwa mtanufaika na kuelimika na yale mtakayoyasikia katika kipindi hiki. Endeleeni kuwa pamoja nami na kuitegea sikio sehemu hii ya kwanza ya kipindi hiki.

Dini, siku zote imekuwa moja ya taasisi kuu za kijamii za wanadamu. Katika zama zote za historia tunaweza kuona jinsi dini zenye chimbuko la Tauhidi zilivyokuwa na taathira kubwa katika maisha ya watu. Pamoja na hayo, nafasi ya dini katika uga wa kijamii na siasa, siku zote limekuwa moja ya masuala muhimu na tab'an lenye mjadala mkubwa. Katika aghalabu ya jamii za wanadamu zimekuwepo changamoto na misuguano baina ya thamani na mafundisho ya dini kwa upande mmoja mkabala na taaluma nyenginezo za maarifa na utambuzi wa mwanadamu kwa upande mwengine. Misuguano baina ya mawili hayo na changamoto zilizoibuka kutokana na misuguano hiyo ni muhimu na za msingi kwa kiasi ambacho zimekuwa na athari kwa ufahamu wa watu juu ya maana hasa ya dini. Leo hii inashuhudiwa mitazamo ya aina mbili iliyo tofauti kabisa waliyonayo wanafikra katika kuifahamu na kuitafsiri kwao dini. Mtazamo wa kwanza ni wa wale wanaotaka dini iwe na nafasi katika uga wa kijamii na kisiasa na katika masuala ya kidunia ya watu; na mtazamo wa pili ni wa wanafikra ambao, kwa kutilia maanani historia ya Magharibi katika kukabiliana na Ukristo, wanataka mduara wa dini utenganishwe na dunia ya leo na kuiwekea mipaka dini ndani ya kuta nne za masuala ya binafsi ya mtu. Mtazamo na ufahamu huu wa pili wa dini umekuwa maarufu kwa jina la 'Secularism' yaani Usekulari. Tunaweza kwa muhtasari kusema kwamba Usekulari, maana yake ni kuyoyoma, kufutika na kukengeushwa dini na kupunguza uwepo wake ndani ya jamii, ndani ya maisha halisi, utamaduni, sanaa, elimu, uchumi, siasa, utawala na uendeshaji. Tukiichunguza maana ya Usekulari na jinsi ulivyojitokeza tutabaini kuwa dhana ya Usekulari ina uhusiano mkubwa na misingi ya kifikra na kifalsafa ya Magharibi. Muelekeo huu wa kifikra una mfungamano na uhusiano na mitazamo ya Utu yaani Humanism, Usasa (Modernism), Uhuria au Uliberali (Liberalism), Usayansi (Scientism), Umantiki (Rationalism), Uwingi (Pluralism) na Uvitendo yaani Pragmatism. Kwa maneno mengine, mabadiliko ya kiutamaduni yaliyotokea kwenye jamii za Magharibi, uwezo na utoshelezi wa mafundisho ya dini ya Ukristo, matukio yaliyojiri katika historia pamoja na utendaji wa viongozi wa kidini na taasisi zenyewe za kidini katika jamii za Kikristo, ndizo sababu na mambo muhimu yaliyochangia kujitokeza kwa fikra ya Usekulari.
Lakini tukiuangalia Usekulari katika jamii za Kiislamu, ukweli ni kwamba hii ni dhana na fikra ngeni na ya kuingizwa, kwa sababu kiasili misingi ya Ukristo ndiyo iliyosababisha kujitokeza kwake katika Ulimwengu wa Magharibi. Kwa kuzingatia kwamba Uislamu ni dini ya kijamii na kisiasa, si mtazamo sahihi kuuhusisha Usekulari na Uislamu. Kwa kuzitupia jicho kwa muhtasari tu aya za Qur'ani tukufu na mafundisho ya dini ya Uislamu inatosha kubaini kwamba dini katika mtazamo wa Uislamu ni majimui na mkusanyiko wa itikadi, akhlaqi, sheria na taratibu zilizowekwa kwa ajili ya uendeshaji wa masuala ya binafsi na ya jamii ya watu na kwa madhumuni ya kuwadhaminia watu hao saada ya duniani na akhera. Kwa hivyo katika fikra za Kiislamu, kuishusha hadhi na nafasi ya dini hadi kwenye kiwango cha chini cha masuala ya utashi na matendo ya mtu binafsi tu kunatokana na ufahamu wenye kasoro wa maana ya dini na nafasi yake katika saada ya mwanadamu.
Kutokana na hali zake tata ulizonazo, Usekulari ni kitu ambacho mara nyingi hujikita katika fikra ya mtu bila ya yeye mwenyewe kujijua na bila ya kudhamiria, hali ambayo huipata jamii na hata dini yenyewe pia. Yamkini hatua na utendaji wa makundi tofauti ya watu, yenye nia na dhamira tofauti kabisa, ukaishia kwenye kitu kimoja ambacho ni Usekulari. Si ajabu walahidi wasioamini kuwepo kwa Mungu wakaamua kwa nia mbaya na kwa lengo la kuwatenganisha watu na dini kupanga na kueneza fikra za Usekulari; kama ambavyo wanaomuamini Mungu, kwa nia njema na kwa dhana na kusudio la kuiokoa dini, nao pia wakaishia kwenye tendo hilo hilo la Usekularishaji dini. Kwa sababu hiyo ni muhimu sana tuwe na uelewa kamili juu ya Usekulari, sababu za kujitokeza kwake na matokeo na athari za kuwa na fikra hii ili tuweze kuchukua hatua kwa uelewa katika kukabiliana na Usekulari ambao hivi sasa umepenya na kuwa na ushawishi katika jamii za Kiislamu kwa njia na sura tofauti. Ni kutokana na lengo na madhumuni hayo tumekuandalieni kipindi hiki cha "Usekulari Katika Mizani ya Uislamu" hii ikiwa ndiyo sehemu yake ya kwanza.

Katika kipindi hiki cha "Usekulari Katika Mizani ya Uislamu", kwanza tutatoa tafsiri ya dini na maana ya Usekulari. Kisha tutaeleza kwa muhstasari fikra za kisekulari, usuli na misingi ya Usekulari, sababu za kujitokeza kwake na tofauti zilizopo kati ya Uislamu na Ukristo kuhusiana na suala hilo. Lakini pia, tutauchanganua Usekulari katika nyanja tofauti za kijamii, kiutamaduni na kisiasa na kuchunguza ishara za kupenya kwa fikra hii katika mtindo wa maisha wa Kiislamu.
Tukianza na neno lenyewe, Usekulari asili yake ni neno la Kilatini la "Saeculorum" au "Seculum" yenye maana ya "karne". Istilahi ya "Usekulari" imetumiwa kufikisha maana ya "zama za sasa" na "dunia hii". Kwa mujibu wa wataalamu, matumizi ya kwanza ya neno Usekulari yanarejea mwishoni mwa karne ya tatu Miladia. Katika zama hizo neno hili lilikuwa likitumika kuelezea wale viongozi wa dini walioamua kuacha maisha ya kujtenga ya utawa na kuelekea kwenye maisha ya kidunia. Istilahi hii aidha ilitumika kwa lengo la kupambanua kati ya mahakama za umma na zile za Kanisa. Baada ya kipindi hicho, neno Usekulari likawa linatumika katika lugha mbalimbali za Ulaya ili kuelezea mali na milki ambazo hazimo tena kwenye umilikaji na uangalizi wa Kanisa na kuwa chini ya mamlaka ya watu wengine.
Kutokana na utata wa tafsiri na maana ya dini na kuishi kidini, pamoja na tofauti za kiutamaduni za jamii mbalimbali, zimetolewa tafsiri na maana chungu nzima za Usekulari, ambapo baadhi ya wakati, baadhi ya tafsiri hizo zinaonesha kuwa na mgongano baina yao. Lakini pia baadhi ya istilahi, zimetumika kwa maana ya Usekulari, ilhali kimsingi hasa hazifikishi maana ya Usekulari. Baadhi ya tafsiri hizo ni pamoja na Ufutaji dini, Ufanyaji usio wa dini, Ufanyaji kidunia, Kuwa kidunia, Ufanyaji kiada na Ufutaji utakatifu. Ufanyaji usio wa dini una maana ya mabadiliko katika mahusiano ya dini na taasisi nyenginezo. Ufutaji utakatifu ni istilahi iliyotumika kwa maana ya kutoweka muhtawa na hali ya utakatifu ya shakhsia, watu, mwahala na shughuli zifanywazo. Neno jengine lililotumiwa kutoa tafsiri na maana ya Usekulari ni "Ufutaji kasumba" kwa maana ya kufanya kimantiki na kuzikataa nguvu za kitafkira na zisizohisika. Vile vile kuna istilahi ya "Ukanaji irada" iliyotumika kukabiliana na " Muelekeo wa kimaajaliwa wa Ukristo" na pia kuna istilahi ya "Kuachana na Ukale" kwa maana ya kukatwa mahusiano ya dini na mambo ya kale; na zote hizo ni miongoni mwa tafsiri zilizotolewa kuuelezea Usekulari. Japokuwa istilahi hizi zote hazina muhtawa wa Usekulari, lakini kila moja imebeba ndani yake sifa mojawapo maalumu iliyonayo fikra na nadharia hiyo. Huenda haitokuwa makosa tukisema kwamba Usekulari unajumuisha maana zote hizo tulizotaja, lakini tafsiri na maana yake halisi si sawa na yoyote kati ya hizo tulizozieleza.
Wapenzi wasikilizaji, sehemu ya kwanza ya kipindi cha Usekulari Katika Mizani ya Uislamu imemalizika. Hivyo tusite hapa kwa leo hadi juma lijalo inshaallah tutakapoendelea na sehemu ya pili ya kipindi hiki. Nakushukuruni kwa kunisikiliza, na endeleeni kutegea sikio sehemu iliyosalia ya matangazo yetu

 

 

 

Andika maoni


Msimbo salama (Security code)
Upyesha (Refresh)

Hadithi ya Uongofu (39)

Ni matarajio yangu kuwa, hamjambo wapenzi wasikilizaji na tunakutana tena katika sehemu nyingine ya kipindi hiki cha Hadithi ya Uongofu. …

Ufeministi, Itikadi na Misingi yake (26)

Assalaamu Alaykum wafuatiliaji wa kipindi hiki na karibuni kuwa nasi katika sehemu nyingine ya kipindi hiki kinachokosoa itikadi ya ufeministi …

Ulaji wa Lishe Bora katika Kipindi Chote cha Maisha

Wataalamu wa Afya wanasema kuwa, awamu mbalimbali za maisha zinahitajia ulaji wa chakula wa aina tofauti. Iwapo wewe ni mtoto, …

Maua mawili ya Mtume wa Allah (31) Sauti

Bismillahir Rahmanir Rahim. Assalaamu Alaykum Warahmatullahi Wabarakaatuh Karibuni wapenzi wasikilizaji wa Idhaa ya Kiswahili Radio Tehran na wasomaji wa mtandao …