Tovuti Hii Imefungwa. Tumehamia Kwenye Parstoday Kiswahili
Alkhamisi, 26 Novemba 2015 10:03

Jamhuri ya Kiislamu ya Iran; Mfumo wa Kiislamu na wa Wananchi (48)

Jamhuri ya Kiislamu ya Iran; Mfumo wa Kiislamu na wa Wananchi (48)

Assalamu Alaykum wasikilizaji wapenzi. Karibuni kuwa nami tena katika kipindi hiki kinachotoa mwanga wa kuuelewa Mfumo wa Jamhuri ya Kiislamu unaotawala hapa nchini Iran, ambao ni utawala wa kidini unaotokana na ridhaa ya wananchi. Ni matumaini yangu kuwa mtafaidika na yale mtakayoyasikia katika kipindi hiki. Karibuni basi kuitegea sikio sehemu hii ya 48 na ya mwisho ya mfululizo huu.

Katika mfululizo huu wa vipindi 47 tumejaribu kuzungumzia kwa muhtasari tofauti iliyopo kati ya demokrasia ya Magharibi na utawala wa kidini unaotokana na ridhaa ya wananchi na kuziarifisha taasisi za kidemokrasia zilizoko katika Jamhuri ya Kiislamu ya Iran pamoja na utenganishaji wa mihimili mitatu mikuu ya dola; na kuonyesha kwamba mfumo wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran ni miongoni mwa mifumo ya utawala wa wananchi duniani wenye ufanisi mkubwa zaidi. Madola ya Magharibi ambayo yanaitakidi kuwa Demokrasia ya Kiliberali ndio upeo wa mwisho wa mafanikio ya wanadamu katika uendeshaji utawala, na kuipima mifumo ya kisiasa duniani kuwa ni yenye kutokana na ridhaa ya wananchi kwa kutumia vigezo vya demokrasia ya Magharibi, yamekuwa yanautangaza mfumo unaotawala katika Jamhuri ya Kiislamu ya Iran kuwa  ni mfumo usio wa kidemokrasia. Licha ya mfumo unaotawala katika Jamhuri ya Kiislamu ya Iran kuwa na mambo kadhaa yanayofanana na muundo wa demokrasia ya Magharibi, lakini pia unatofautiana katika mambo kadhaa kwa upande wa muhtawa na dhati yake. Magharibi na mfumo wa ubeberu wa vyombo vya habari vilivyoko chini ya satua na udhibiti wao vinazitumia tofauti hizo hizo kuwa kisingizio cha kutaka kuonyesha kuwa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran ni utawala usio wa kidemokrasia. Lakini ukweli ni kwamba tofauti hizo ndizo nukta chanya zinazoonyesha ubora wa utawala wa kidini unaotokana na wananchi kulinganisha na demokrasia za Magharibi. Kwani kama ambavyo Mapinduzi ya Kiislamu ya Iran yana mambo kadhaa, kwa upande wa muundo na dhati yake yanayotafautiana na mapinduzi makubwa mengine yaliyotokea duniani, utawala ulioundwa kutokana na mapinduzi hayo nao pia una mambo kadhaa yanayotafautiana na mifumo mingine ya kisiasa iliyoko ulimwenguni. Mfumo ulioasisiwa baada ya ushindi wa Mapinduzi ya Kiislamu nchini Iran umetokana na kura za wananchi, na tofauti kubwa iliyopo baina yake na demokrasia ya kiliberali ni katika utambulisho wake wa kidini ambao madola ya Magharibi yamejiweka mbali nao.

Mhimili wa kidini katika utawala wa kidini unaotokana na ridhaa ya wananchi ni Utawala wa Faqihi. Imam Khomeini, Mwasisi wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran alikuwa akiitakidi kwamba dini haitenganiki na siasa na alikuwa akijenga hoja kwa kutumia aya za Qur’ani, hadithi na mantiki kuonyesha mfungamano uliopo kati ya dini na utawala. Kwa kuhuisha fikra ya utawala wa Kiislamu kulingana na nadharia ya Utawala wa Faqihi na kuasisi Jamhuri ya Kiislamu, Kiongozi Mkuu wa Mapinduzi ya Kiislamu ya Iran alionyesha kivitendo jinsi ulivyo uhusiano huo baina ya dini na siasa na kubatilisha dhana na fikra kwamba dini ni suala la mtu binafsi tu au kitu cha kuwashughulisha na kuwapumbaza watu. Akiwa ni faqihi mwenye utambuzi mpana na wa kina, alikuwa akiipa umuhimu maalumu nafasi ya wananchi katika uundaji wa utawala na uchaguzi wa kiongozi wa utawala huo. Ni kutokana na imani na itikadi hiyo aliyokuwa nayo kuhusu mchango na nafasi ya wananchi katika utawala, baada ya mwezi mmoja na nusu tu tangu kuangushwa utawala wa Muhammad Reza Pahlavi, Imam Khomeini (R.A) aliitisha kura ya maoni ya kuamua kuhusu aina ya mfumo wa kisiasa wa kutawala nchini, ambapo zaidi ya asilimia 98 ya wananchi wa Iran walipiga kura ya “ndiyo” kuunga mkono kuasisiwa Mfumo wa Jamhuri ya Kiislamu. Baada ya hapo pia wananchi walikuwa na nafasi ya moja kwa moja au isiyo ya moja kwa moja katika uundwaji wa Baraza la Wataalamu wa Kutunga Katiba, upitishaji wa Katiba ya kwanza na kuundwa kwa mihimili yote ya Mfumo wa Jamhuri ya Kiislamu, kufikia hadi kwamba katika mwaka wa kwanza pekee wa ushindi wa Mapinduzi ya Kiislamu, wananchi wa Iran walipiga kura mara tano kwa minasaba na sababu tofauti. Hali ya kuwa si katika mapinduzi yoyote yale ya umma duniani ambapo wananchi wamewahi kupewa nafasi ya kuchangia kwa kiwango hicho katika uundaji wa mfumo mpya baada ya kuanguka tawala za kiimla na kidikteta.

Katika nafasi ya juu kabisa ya tawala ambazo msingi wao ni demokrasia ya kiliberali huweko mtu aitwaye Rais au Waziri Mkuu ambaye kivitendo huwa ndiye mkuu wa nchi. Katika Jamhuri ya Kiislamu ya Iran pia, japokuwa Rais, anayechaguliwa moja kwa moja kwa kura za wananchi, ndiye mtu mwenye mamlaka ya juu kabisa ya utendaji nchini, lakini kiuongozi, katika nafasi ya juu kabisa ya mfumo wa utawala kuna Faqihi Mtawala, anayechaguliwa kwa kura zisizo za moja kwa moja za wananchi na ambaye ndiye anayesimamia mihimili yote mitatu mikuu ya dola. Katika utawala wa kidini unaotokana na ridhaa ya wananchi, Jamhuri ya Kiislamu ya Iran ikiwa ndio mfano na kielelezo cha mfumo na utawala huo, kwa kuzingatia kwamba kumchagua Faqihi Mtawala mwenye sifa na masharti yanayotakiwa ni kazi ya kitaalamu inayohitaji maoni na mawazo ya watu weledi na wataalamu, kiongozi huyo huchaguliwa na wananchi kwa njia isiyo ya moja kwa moja kupitia wawakilishi wao katika “Baraza la Wanazuoni Wataalamu.” Baraza la Wanazuoni Wataalamu wa kumchagua Kiongozi Mkuu ni chombo huru cha kitaalamu kinachochaguliwa kwa kura za wananchi.

Kama ilivyo katika mifumo ya tawala za kidemokrasia, kwa mujibu wa ibara ya 57 ya Katiba ya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran, mihimili mitatu ya dola, yaani Serikali, Bunge na Mahakama ndiyo inayotawala katika Jamhuri ya Kiislamu ya Iran ikiwa chini ya usimamizi wa Faqihi Mtawala na kila mmoja kufanya kazi kwa uhuru bila kuingiliwa na mhimili mwengine. Kwa upande wa Bunge, ambalo nchini Iran linajulikana kwa jina la Majlisi ya Ushauri ya Kiislamu, chombo hicho ndio nguzo muhimu zaidi ya upitishaji maamuzi katika Jamhuri ya Kiislamu ya Iran. Kwa sasa, Majlisi ya Ushauri ya Kiislamu ya Iran ina wabunge 290; na idadi yao huongezeka kulingana na ongezeko la idadi ya watu nchini. Majlisi ya Ushauri ya Kiislamu ndio nguzo kuu na muhimu zaidi ya utungaji sheria na usimamizi katika Mfumo wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran, ambapo wabunge wa bunge hilo huchaguliwa moja kwa moja kwa kura za wananchi. Kipindi kimoja cha ubunge katika Majlisi ya Ushauri ya Kiislamu ya Iran ni miaka minne. Na hakuna wakati ambapo Iran inabaki bila ya kuwepo na Bunge.

Baada ya Bunge mhimili wa pili wa dola katika Mfumo wa utawala wa kidini unaotokana na ridhaa ya wananchi ni Serikali inayoongozwa na Rais ambaye huchaguliwa moja kwa moja kwa kura za wananchi na kuongoza nchi kwa kipindi cha miaka minne akiwa na haki ya kuhudumu katika wadhifa huo kwa vipindi viwili mtawalia endapo ataamua kugombea tena. Rais akiwa mkuu wa mhimili huo na vilevile shakhsia nambari mbili nchini baada ya Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu, yaani Kiongozi Mkuu. Mhimili wa tatu wa dola hapa nchini ni Mahakama. Majukumu na maingiliano yaliyopo kati ya Rais na Mahakama ni madogo mno kulinganisha na Bunge; na hii inatokana na haja ya mhimili wa Mahakama kuwa na uhuru kamili na kuepusha ushawishi wa viongozi kwa kazi za mhimili huo.

Kama kufanyika uchaguzi ni moja ya vielelezo vya tawala za kidemokrasia, ni vyema tukaelewa kwamba katika kipindi cha miaka 36 ya umri wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran, kwa wastani, kila mwaka Iran imeshuhudia chaguzi ima za Urais, Bunge, Baraza la Wanazuoni Wataalamu wa Kumchagua Kiongozi Mkuu au Mabaraza ya Kiislamu ya Miji na Vijiji.

Tuhatimishe sehemu yetu hii ya mwisho ya kipindi hiki kwa kunukuu maneno ya Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu ya Iran Ayatullahil Udhma Sayyid Ali Khamenei katika kuuelezea Mfumo wa utawala wa kidini unaotokana na ridhaa ya wananchi unaotawala hapa nchini. Ayatullah Khamenei amesema:”Mfumo huu wa utawala wa wananchi (wa kidini) chimbuko lake halina uhusiano wowote na demokrasia ya Magharibi. Mfumo huu ni kitu kingine kabisa. Mfumo wa Utawala wa Kidini wa Wananchi hauwezi pia kuelezewa kwa hali mbili zifuatazo. Kwanza hatuwezi sisi kuichukua demokrasia ya Magharibi tukaibandika kwenye dini na kuweza kuwa na majimui ya kitu kilichokamilika; na pia hatuwezi kusema kuwa Mfumo wa Utawala wa wananchi unatokana na dini.” Wapenzi wasikilizaji kipndi chetu cha Jamhuri ya Kiislamu ya Iran; Mfumo wa Kiislamu na wa Wananchi kinaishia hapa. Ni matumaini yangu kuwa yale mliyoyasikia katika kipindi hiki yameweza kukupeni mwanga japo kwa muhtasari wa kuelewa ukweli halisi wa mfumo wa kisiasa unaotawala hapa nchini Iran. Basi hadi siku nyengine tutakapokutana tena inshallah katika kipindi kingine kipya, nakuageni huku nikikutakieni kheri na fanaka maishani…/

 

 

 

 

Andika maoni


Msimbo salama (Security code)
Upyesha (Refresh)

Hadithi ya Uongofu (39)

Ni matarajio yangu kuwa, hamjambo wapenzi wasikilizaji na tunakutana tena katika sehemu nyingine ya kipindi hiki cha Hadithi ya Uongofu. …

Ufeministi, Itikadi na Misingi yake (26)

Assalaamu Alaykum wafuatiliaji wa kipindi hiki na karibuni kuwa nasi katika sehemu nyingine ya kipindi hiki kinachokosoa itikadi ya ufeministi …

Ulaji wa Lishe Bora katika Kipindi Chote cha Maisha

Wataalamu wa Afya wanasema kuwa, awamu mbalimbali za maisha zinahitajia ulaji wa chakula wa aina tofauti. Iwapo wewe ni mtoto, …

Maua mawili ya Mtume wa Allah (31) Sauti

Bismillahir Rahmanir Rahim. Assalaamu Alaykum Warahmatullahi Wabarakaatuh Karibuni wapenzi wasikilizaji wa Idhaa ya Kiswahili Radio Tehran na wasomaji wa mtandao …