Tovuti Hii Imefungwa. Tumehamia Kwenye Parstoday Kiswahili
Jumatano, 26 Juni 2013 13:30

Mgogoro wa Familia katika Nchi za Magharibi (27)

Mgogoro wa Familia katika Nchi za Magharibi (27)

Hamjambo wapenzi wasikilizaji na karibuni kuwa nami tena katika kipindi hiki ambacho ni cha mwisho katika mfululizo wa makala za Mgogoro wa Familia katika Nchi za Magharibi. Katika vipindi vilivyopita tulizungumzia baadhi ya matokeo mabaya ya mgogoro wa familia katika nchi za Magharibi na kusema kuwa, taasisi muhimu ya familia imepoteza mwelekeo na kudhoofika sana huko Magharibi kutokana na kuathiriwa na mitazamo ya kisekulari, feminism, liberalism na humanism na vilevile athari mbaya za picha chafu, matangazo ya vyombo vyenye programu chafu vya mawasiliano ya umma, kuongezeka kwa tabia na mienendo ya kuchupa mipaka katika masuala ya ngono, ufuska na kadhalika. Kwa maneno mengine ni kuwa, athari mbaya za kupenda sana anasa za kupita za kidunia, kujali maslahi ya mtu binafsi, kujitenga na dini na masuala ya kiroho na maadili yote hayo yameiweka taasisi ya familia katika nchi za Magharibi kwenye njia ya mporomoko mkali wa kuelekea kwenye maangamizi.

Kipindi chetu cha leo kitatupia jicho umuhimu wa familia katika kuimarisha misingi ya nguzo za jamii. Karibuni.

XXXX

Familia yenye uzima na sahihi huwa na umuhimu mkubwa katika kubakisha kizazi cha mwanadamu, kulea itikadi na hisia safi za wanadamu, kudhibiti na kuongoza vyema hisia za kimaumbile za kujamiiana, kudhamini mahitaji ya kijamii na kiuchumi na kutoa malezi na mafunzo ya kidini na kadhalika. Hata hivyo hii leo familia nyingi katika nchi za Magharibi zimepoteza mwelekeo na haziwezi tena kudhamini mahitaji ya kimsingi na halisi ya taasisi ya familia. Kwa sababu hiyo wanafikra wengi wanaamini kuwa, taasisi ya familia ama imesahau majukumu yake mengi au majukumu hayo hutekelezwa na taasisi nyingine ghairi ya familia. Ongezeko kubwa la idadi ya familia zenye mzazi mmoja, idadi kubwa ya wasichana wanaojifungua wanaharamu, maisha ya mwanamke na mwanaume bila ya kufunga ndoa, ongezeko la maingiliano ya watu wenye jinsia moja baina ya vijana na kadhalika vimekuwa tatizo kubwa linalotishia taasisi ya familia na kuhatarisha kizazi cha mwanadamu. Inasikitisha kwamba watawala wa nchi za Magharibi badala ya kutilia maanani na kutafuta njia ya kutatua matatizo hayo kivitendo wamekuwa wakipiga vita mwenendo sahihi wa kuanzisha familia kwa kutambua rasmi ndoa baina ya watu wenye jinsia moja na mahusiano haramu baina ya mwanamke na mwanaume nje ya misingi ya familia.

Mhakiki James C. Dobson wa Marekani anasema: Wanaharakati wa mrengo unaotetea ndoa baina ya watu wenye jinsia moja wamelenga akili, fikra na nyoyo za watoto na vijana. Shule za serikali hususan katika majimbo ya California na Massachusetts zinawaelekeza wanafunzi upande huo na zinawafundisha waziwazi kwamba vitendo hivyo vichafu ni jambo la kawaida na linalokubalika na kwamba uhusiano wa kijadi na unaotilia maanani maadili kati ya mwanamke na mwanaume umejaa chuki na taasubi.

Miongoni mwa utendaji usio sahihi wa taasisi ya familia katika nchi za Magharibi ni kupuuza nafasi na mchango mkubwa wa mwanamke ndani ya familia na kufumbia macho mchango na nafasi yake kubwa katika kulea watoto na kuongoza familia. Ni vyema kukumbusha hapa kuwa kutokana na utawala wa fikra zinazotanguliza mbele matakwa ya mtu binafsi na itikadi za kimaada katika nchi za Magharibi, Wamagharibi wamepuuza kabisa roho nyepesi na hisia safi na za upendo za mwanamke. Kwa sababu hiyo mwanamke amepoteza nafasi yake muhimu kama mke na vilevile nafasi na mchango wake muhimu kama mama na mlezi wa watoto na kizazi cha baadaye. Badala yake mwanamke amepachikwa nafasi nyingine isiyooana na fitra ya maumbile yake. Kwa msingi huo moja kati ya sababu za mgogoro wa sasa wa familia katika nchi za Magharibi ni kupuuzwa nafasi hiyo muhimu ya mwanamke.

Ni vizuri pia kuashiria hapa kwamba, mtazamo unaotawala jamii za Magharibi haukusimama juu ya misingi ya kuitukuza familia; kwa sababu hiyo wanaume huuona mchango wa mwanamke katika jamii tu na si katika familia, ilhali mtazamo wa Uislamu umeweka mbele nafasi na mchango wa mwanamke katika familia na kusisitiza kwamba, wajibu na mchango mkubwa na asili wa mwanamke ni ule anaofanya ndani ya familia. Katika mtazamo wa Uislamu ni kuwa, wadhifa wa kwanza kabisa wa mwanamke ni kupata maarifa ya dharura ya kustawisha nafsi yake na familia yake. Mwanamke katika mtazamo huo wa Kiislamu ana wadhifa muhimu wa kutekeleza vyema nafasi yake kama mke na kushughulikia vyema malezi na tabia za watoto wake ambao ndio kizazi cha taifa la baadaye. Mwanamke ana kazi ya kuongoza vyema taasisi ya familia na kutayarisha mazingira bora ya ustawi wa kiroho, kifikra na kimwili wa wanachama wake.

Ni kwa msingi huo ndio maana Uislamu umekutambua kulinda taasisi ya familia na kuchungu vyema nyumba kuwa ni ibada ya jihadi kwa mwanamke na kumtambua mwanamke anayetekeleza vyema majumu yake hayo kuwa ni sawa na wapiganaji wa vita vya jihadi katika njia ya Mwenyezi Mungu. Hata hivyo tunapaswa kutambua kuwa kushughulikia masuala ya nyumba na familia hakuna maana ya kumzuia mwanamke kujishughulisha na kazi na harakati za kijamii, kisiasa na kiuchumi, bali anaweza kufanya shughuli hizo na kushirikiana na mwanaume katika kujenga jamii na taifa sambamba na kulinda shughuli na kazi yake ya msingi ya kuwa mama na mke ndani ya familia.

Katika mtazamo wa Uislamu pia mwanaume ana nafasi muhimu sana kama mume na baba katika kulinda na kuimarisha familia. Uislamu unasisitiza kuwa, mwanaume ana jukumu la kudhamini mahitaji ya kimaisha ya familia, kumsaidia na kumpenda mke na watoto wake na anawajibika pia kuamiliana nao kwa upole, upendo na maadili mema. Vilevile unawatambua mke na watoto kuwa ni amana ya Mwenyezi Mungu katika mikono ya mume na baba wa familia. Mtume Muhammad (saw) amemtaja mwanaume anayemsaidia mke wake kuwa ni sawa na watu wanaouawa shahidi katika vita vya jihadi au Swiddiqina wenye daraja za juu peponi, suala ambalo linaonesha umuhimu wa kuisaidia na kuipenda familia katika Uislamu.

XXXX

Katika mtazamo wa Magharibi kunasisitizwa zaidi haki za mtu binafsi ndani ya familia na ni mara chache sana kuashiriwa wajibu na majukumu ya wanachama wa familia ndani ya taasisi hiyo muhimu. Suala hili limemfanya kila mmoja kati ya mume, mke na watoto kuwa na matarajio makubwa bila ya kutilia maanani wajibu na majukumu yao mkabala wa wenzao. Wakati huo huo katika Uislamu haki ya kila mmoja kati ya wanafamilia inaambatana na majukumu na wajibu, na kila mwenye haki ndani ya familia huwa na majukumu na wajibu wa kufanya mkabala wa haki hiyo. Mtume wetu mtukufu Muhammad (saw) anasema: Kila mmoja wenu ana wajibu na majukumu mkabala wa mnaosimamia mambo yao. Naam, mwanaume ni mlinzi na ana majukumu na wajibu wa kufanya mkabala wa familia yake na mke ni mwangalizi na mlinzi wa familia, mume na watoto na ana majukumu na wajibu wa kufanya mkabala wa anaoshughulikia mambo yao.

Inasikitisha kuwa hii leo katika jamii za Magharibi kumepuuzwa kabisa mchango na nafasi ya wanafamilia hususan nafasi ya mwanamme kama mume na baba na nafasi ya mwanamke kama mke na mama. Huko Magharibi pia kunasisitizwa sana juu ya uhuru wa mtu binafsi bila ya msisitizo kama huo huo kuhusu wajibu na majukumu yake. Kwa maneno mengine ni kuwa, maslahi ya mtu binafsi yamewekwa mkabala na uso kwa uso na maslahi ya familia na jamii.

Kwa msingi huo ili kulinda na kukarabati familia katika nchi za Magharibi kuna ulazima wa kuimarishwa na kutiliwa maanani masuala ya familia na vielelezo vyake vikuu kama upendo, uaminifu, ushirikiano, maadili mema na na kadhalika. Kwani mambo na sifa hizo ndio nguzo zinazolinda na kuimarisha taasisi hiyo muhimu. Ni kwa msingi huo ndio maana wanafikra na wasomi wakubwa wa Marekani wakasisitiza juu ya umuhimu wa kuhuishwa nafasi ya familia katika nchi hiyo. Katika uwanja huo mwandishi William Raspberry wa Marekani anasema: "Lau kama ningeweza kuandika waraka wa dawa mujarabu ya kutibu matatizo ya Marekani basi ningeandika juu yake kwamba: "Rejesheni tena familia."   

XXXX

Wapenzi wasikilizaji muda uliotengwa kwa ajili ya kipindi chetu cha leo umefikia ukingoni. Ni matarajio yetu kwamba vipindi hivi vimeweza kuweka wazi picha jumla kuhusu mgogoro wa familia katika nchi za Magharibi. Basi tutakapokutana tena katika kipindi na makala nyingine nakutakieni maisha mema. Kwaherini.

Andika maoni


Msimbo salama (Security code)
Upyesha (Refresh)