Tovuti Hii Imefungwa. Tumehamia Kwenye Parstoday Kiswahili
Jumapili, 23 Juni 2013 22:57

Mgogoro wa Familia katika nchi za Magharibi (26)

Mgogoro wa Familia katika nchi za Magharibi (26)

Assalam Alaykum wapenzi wasikilizaji na karibuni kuwa nami tena katika dakika chache za kipindi cheti cha leo katika mfululizo wa makala zinazozungumzia mgogoro wa familia katika nchi za Magharibi. Katika kipindi kilichopita ambacho kilikuwa cha 25 katika mfululizo huu tulizungumzia athari mbaya za dawa za kulevya na vileo kwa familia za Magharibi hususan tabaka la vijana. Kipindi chetu leo kitatupia jicho moja ya taathira mbaya za mgogoro wa familia katika nchi za Magharibi ambayo ni ukatili na utumiaji mabavu. Karibuni.   

XXXXX

Familia ndio sehemu ambako watoto hujifunza mazuri na mabaya kutokana na mwenendo wa wazazi wao. Wazazi, vyombo vya mawasiliano ya umma na jamii ndio wanaomfunza mtoto kuwa mtu katili na anayependa kutumia mabavu au mtu mwema na mpole. Inasikitisha kwamba hii leo kunashuhudiwa ongezeko na vitendo vya ukatili na utumiaji mabavu kati ya wanafamilia kwenye nchi za Magharibi. Vitendo hivyo vinasababisha matatizo mengi kati ya wanandoa wawili na baina ya wazazi na watoto wao. Kwa mfano tu nchi ya Marekani inasumbuliwa na matatizo mengi ya kijamii ikiwa ni pamoja na vitendo vya ukatili, uhalifu na jinai za aina mbalimbaali, ubakaji, utekaji nyara, ukosefu wa amani katika maeneo ya kazi, mashuleni na kwengineko. Uhalifu huo pia umepenya na kuingia katika familia na kuifanya taasisi hiyo muhimu iporomoke zaidi siku baada ya siku. Ripoti ya Wizara ya Sheria ya Marekani inasema kuwa uhalifu na jinai zinazotokana na ukatili na utumiaji mabavu uliongezeka kwa asilimia 18 nchini humo mwaka 2011.

Ukatili unadhihiri katika familia za Kimagharibi katika sura mbalimbali za maneno na vitendo. Ukatili mwingi unaofanyika katika nchi za Magharibi humlenga zaidi mwanamke kuliko mwanaume.

Uchunguzi wa maoni uliofanyika nchini Uingereza umeonesha kuwa mmoja kati ya kila wanawake watatu wanaopelekwa katika vitengo vya dharura vya hospitali mbalimbali nchini humo huwa ni mhanga wa ukatili na vitendo vya utumiaji mabavu ndani ya familia. Takwimu zilizotolewa na taasisi ya Refuge nchini Uingereza zinasema kuwa, mmoja kati ya kila wanawake wanne nchini humo aliwahi kupigwa nyumbani na ndani ya familia. Vilevile mwanamke mmoja kati ya kila kumi walioshiriki kwenye uchunguzi huo wa maoni ambao wamekiri kuwa wamepigwa na kunyanyaswa na waume zao, amesema kuwa anayaona maisha yake kuwa yamo hatarini. Taasisi hiyo imetangaza kuwa kila wiki wanawake wawili huuawa na waume zao wa sasa au wa zamani huko Uingereza na Wales. Vilevile polisi ya London inasema kuwa kila mwezi huripotiwa kesi nyingi za ukatili na unyanyasaji unaofanyika ndani ya familia dhidi ya wanawake  ambao hujumuisha matusi na kuvunjiwa heshima, mbinyo wa kunyimwa fedha na matumizi, kuzuiwa kukutana na ndugu, jamaa wa karibu na marafiki, ubakaji na kupigwa. Hali ya wanawake katika nchi nyingi za Magharibi inashabihiana au hata kuwa mbaya zaidi ya ile ya wanawake wa Uingereza. Wakati mwingine ukatili huo hufanywa na wanawake dhidi ya wanaume ndani ya familia.

Ukatili na unyanyasaji baina ya mke na mume huwa na athari mbaya sana ikiwa ni pamoja na kupooza uhusiano baina ya wawili hao, kutoroka mwanamke, talaka na mustakbali wenye giza wa watoto wa familia husika. Mazingira hayo ya ukatili na vitendo vya kutumia mabavu pia huwa na taathira mbaya sana za kiroho kwa watoto na kuwafanya wachukie kuwa nyumbani na kujiweka mbali na wazazi wao na hatimaye kuangukia mikononi mwa makundi na magenge ya wahalifu.

Hii leo jamii za nchi za Magharibi zimekumbwa na mabalaa ya ukatili, unyama na utumiaji mabavu wa kutisha. Mwenyekiti wa zamani wa Kamisheni ya Mahakama ya Baraza la Seneti la Marekani Joseph Biden anaamini kuwa ukatili unaofanyika ndani ya familia ndio tatizo kubwa zaidi nchini humo. Vyombo vya habari kila siku vimekuwa vikitangaza habari za kutisha na kusikitisha za ukatili na unyama unaofanyika ndani ya familia za nchi za Magharibi. Inasikitisha kuwa mbali na ukatili unaofanyika baina ya mke na mume, ukatili dhidi ya watoto pia unazidi kuongezeka. Miezi michache iliyopita dunia ilitikiswa na habari ya baba mmoja wa Marekani ambaye alihitimisha maisha ya watoto wake watatu waliokuwa na umri wa miaka 5, 8, na 11 kwa kuwadunga kisu shingoni. Mwanaume huyo wa jimbo la North Dakota aliwaua mabinti zake hao watatu alipokwenda kumtembelea mke wake wa zamani katika jimbo la Wisconsin. Watoto wa bwana huyo katili walikuwa kwa yaya wao. Baada ya kutekeleza mauaji hayo Mmarekani huyo aliwasiliana na mke wake wa zamani na kumwambia kwamba sasa unaweza kurudi nyumbani kwani tayari nimewaua watoto wote.    

XXXXX

Pamoja na hayo yote suala la kutisha zaidi ni ukatili wa akina mama dhidi ya watoto wao wenyewe na wakati mwingine kuwaua watoto hao. Ghariza na hisi ya kuwa mama ni tunu na neema kubwa ya Mwenyezi Mungu na sifa makhsusi ya mwanamke. Kwa sababu hiyo wakati mwanamke anapopoteza hisi hii hubadilika na kuwa kiumbe hatari sana na katili kupita kiasi. Uchunguzi uliofanyika katika nchi za Magharibi umebaini kuwa asilimia 61 ya ukatili unaofanywa dhidi ya watoto wadogo hutendwa na akina mama. Magazeti ya Uingereza yaliripoti kuwa mama mwenye umri wa miaka 23 alimnyonga mwanaye aliyekuwa na umri wa miaka 4 tu na kubakia na maiti yake nyumbani kwa kipindi cha siku mbili. Tukio hilo la kusikitisha limetokea katika mji wa Liverpool.

Swali linalojitokeza hapa ni kuwa inakuwa vipi mama ambaye anapaswa kuwa kielelezo na dhihirisho la upendo na huruma kwa watu wa familia hususan watoto wake anabadilika na kuwa katili mkubwa na kumuua mwanaye kipenzi tena kwa njia ya kushangaza?

Huko Ufaransa kumeripotiwa kuwa kijana mmoja mwenye umri wa miaka 16 amewaua watu wote wa familia yake ambao ni wazazi wawili na ndugu zake wawili kwa kuwafyatulia risasi usiku wakiwa wamelala. Kuongezeka kwa matukio kama haya ya kikatili kunafichua ongezeko kubwa la unyama na utumiaji mabavu ndani ya familia na jamii za Magharibi na kwamba wazazi hawakutekeleza vyema wajibu wao wa kimalezi. Ni wazi kuwa baba na mama si wahusika pekee wa vitendo kama hivyo vinavyofanywa na watoto wao bali jamii nzima ikiwa ni pamoja na vyombo vya mawasiliano ya umma, mazingira ya shule na jamii huwafunza mengi watoto wadogo na kuwa na taathira kubwa katika mienendo na tabia zao.

Kueneza silaha za aina mbalimbali baina ya watu wa familia pia kunazidisha mauaji na uhalifu katika nchi za Magharibi. Mtaalamu wa masuala ya usalama wa Marekani Charles Shoebridge anasema kuhusu suala la kukithiri ukatili na mauaji nchini Marekani kwamba, katika miaka ya hivi karibuni jinai za kutumia silaha zimeongezeka sana katika miji mbalimbali ya Marekani. Anasema miongoni mwa sababu za suala hilo ni utamaduni wa kumiliki silaha. Kesi za mauaji ya silaha nchini Marekani zimeongezeka kwa kiwango cha kutisha ikilinganishwa na nchi nyingine ambako watu hawaruhusiwi kumiliki silaha isipokuwa polisi na askari usalama.       XXXXX

Ukweli wa mambo ni kuwa ongezeko la talaka na kutengana wazazi wawili, ufuska na mmomonyoko wa maadili, kutoweka akhlaqi na tabia njema za kibinadamu, ukosefu wa masuala ya kiroho na dini, kupungua mapenzi na upendo baina ya watu wa familia na kadhalika vimezitumbukiza familia nyingi katika hali ya kutojali na kukosa hisia za kiutu na kibinadamu. Kwa mfano tu wataalamu wengi wa Kimagharibi wanasisitiza kuwa ongezeko la ukatili na roho mbaya ndani ya watu wa familia linatokana na kughafilika na masuala ya kidini na kiroho.

Mwandishi maaarufu wa Marekani Thomas Moore anatoa wasifu wa jamii ya nchi hiyo akisema: Sisi Wamarekani tumetupilia mbali dini kwa miaka mingi sasa. Maisha bila ya dini yamekuwa sawa na eneo la majitaka na machafu. Kwa sababu hiyo tumepotea njia. Moore anaendelea kusema: "Tumeondoka katika mikono ya Malaika na kujitumbukiza wenyewe katika moto wa Jahannam..."

Dini tukufu ya Uislamu inasisitiza mno juu ya mambo mawili ambayo ni rehma na mahaba baina ya mke na mume na kuvitaja kuwa ndio ufunguo wa kuondoa ukatili ndani ya taasisi ya familia na kuweka hali ya utulivu baina ya wanandoa na mazingira ya familia. Kwa msingi huo katika mtazamo wa Uislamu moja ya funguo za kuondoa hasira na kueneza utulivu na usalama ndani ya familia ni kusamehe, rehma na upendo na mahaba baina ya wanafamilia hususan mke na mume. Mbali na hayo wazazi wanapaswa kuwafunza watoto wao jinsi ya kusamehe wanapokuwa na hasira kwani hasira na matatizo mengi ya kinafsi yanaweza kutibiwa kwa kusamehe, upendo na mahaba, suala ambalo huwa na taathira kubwa katika uzima na usalama wa familia na jamii nzima.  

XXXXX

Wasikilizaji wapenzi muda uliotengwa kwa ajili ya kipindi hiki umefika ukingoni. Msikose kuwa nami juma lijalo katika sehemu nyingine ya kipindi hiki. Kwaherini.

Andika maoni


Msimbo salama (Security code)
Upyesha (Refresh)