Tovuti Hii Imefungwa. Tumehamia Kwenye Parstoday Kiswahili
Jumanne, 18 Juni 2013 16:17

Mgogoro wa Familia katika nchi za Magharibi (25) + Sauti

Mgogoro wa Familia katika nchi za Magharibi (25) + Sauti

Hamjambo wasikilizaji wapenzi na karibuni kuwa nami tena katika sehemu nyingine ya makala ya Mgogoro wa Familia katika Nchi za Magharibi. Ikiwa bado mnakumbuka katika kipindi cha wiki iliyopita tulizungumzia baadhi ya athari mbaya na za kutisha za uchupaji mipaka na utovu wa maadili kati ya vijana na mabarobaro katika nchi za Magharibi. Tulisema kuwa miongoni mwa athari hizo mbaya za mgogoro wa familia ni kupungua ndoa, kuongezeka zinaa na mimba za haramu zinazotokana na mahusiano hayo machafu kati ya vijana na kadhalika. Katika sehemu ya leo ya kipindi chetu ambayo ni ya 25 tutaashiria athari nyingine mbaya za mgogoro wa familia katika nchi za Magharibi. Karibuni. 

XXXXX

Moja kati ya athari mbaya za ufuska na mmomonyoko wa maadili katika nchi za Magharibi hususan huko Marekani ni kutoroka vijana hususan wasichana na kuacha familia zao. Kutoroka familia kwa upande mmoja huwatumbukiza vijana na mabarobaro katika matatizo mengi ya kijamii na katika upande mwingine huitumbukiza familia nzima katika anuwai mbalimbali za mashaka na tabu. Takwimu za kuaminika zinasema kuwa, nchini Marekani kila mwaka vijana na barobaro zaidi ya milioni moja hutoroka familia zao na nusu yao ni wasichana ambao kutokana na kuwa na umri mdogo hawawezi kupata kazi; hivyo hulazimika kuiba, kutumbukia kwenye biashara ya mihadarati na dawa za kulevya na uasherati. Kasisi Bruce Ritter wa Marekani anasema: Wasichana wadogo laki tano wenye umri wa chini ya miaka 17 wanajishughulisha na ukahaba nchini Marekani.

Mbali na hayo wakati wa kutoroka familia zao wasichana hao wadogo hutumbukia katika mitego ya magenge ya magendo ya wanadamu ambayo huwachukua na kuwauza katika nchi nyingine. Mara nyingi wasichana hao hutumiwa kama watumwa wa ngono. Shirika la habari la Ujerumani limeripoti kuwa polisi ya nchi hiyo imetangaza kwamba imelitia nguvuni kundi moja linalofanya magendo ya binadamu nchini humo. Polisi ya Ujerumani imesema genge hilo limetorosha wasichana 50 kuelekea Ulaya magharibi. Viongozi wa Ujerumani wanasema kundi hilo limeuza wasichana hao waliotolewa jamhuri za Yugoslavia ya zamani katika nchi za Ujerumani, Ufaransa, Ubelgiji na nchi za Scandinavia. Kwa utaratibu huo wakati familia inapokosa mazingira mazuri ya kulea na kulinda watoto hukumbwa na matatizo mengi kama hayo na misiba chungu nzima. Matatizo na misiba hiyo ya familia hatimaye huikumba pia jamii nzima.

Miongoni mwa taathira mbaya za mgogoro wa familia katika nchi za Magharibi ni familia kushindwa kudhibiti watoto na ongezeko la matumizi ya dawa za kulevya hususan kati ya vijana. Vijana wengi katika nchi za Magharibi na zile zinazoiga mitindo yao ya maisha wamepatwa na janga la kutumia dawa za kulevya wakijaribu kukimbia uhusiano baridi unaotawala familia zao, au taathira mbaya za talaka baina ya wazazi wao. Mwandishi Hood Keynes Fan wa Marekani anaashiria athari mbaya za talaka na kutengana wazazi wawili kwa watoto wao na kusema, asilimia 63 ya vijana wanaoishi bila ya kuwa na baba zao hutoroka makwao na asilimia 37 miongoni mwao hutumia dawa za kulevya. Anasema vijana wengi wa aina hiyo pia hutumbukia zaidi katika ulevi wakilinganishwa na wale wanaoishi pamoja na wazazi wao wawili.

XXXXX

Kwa sasa matumizi ya dawa za kulevya kama bangi, hiroini, cocaine na dawa za kulevya zinazotengenezwa viwandani yameongezeka sana kati ya familia nyingi za nchi za Magharibi hususan baina ya vijana. Mwandishi Willian Gairdner wa Canada ameandika katika kitabu alichokipa jina la "Vita dhidi ya Familia" kwamba asilimia 50 ya wanafunzi wa kuanzia shule za sekondari nchini Marekani wametumia bangi na asilimia 15 miongoni mwao wamevuta cocaine.

Utafiti wa hivi karibuni umebaini kuwa ongezeko la asilimia 15 la matumizi ya dawa za kulevya na vileo kati ya vijana wa Marekani litakuwa na taathira nyingi mbaya kwa maisha ya vijana wa kizazi cha sasa.

Utumiaji wa dawa za kulevya si tu kwamba huwaathiri vijana pekee bali watu wote wa familia hususan akina mama waja wazito na vichanga wanavyobeba matumboni mwao. Siku chake zilizopita iliripotiwa kuwa, mama mmoja wa Marekani ametiwa nguvuni kwa sababu ya kumfanya mtoto wake mchanga kuwa mraibu wa dawa za kulevya. Mwanamke huyo wa Marekani alikuwa akitumia kupindukia dawa za kulevya kama cocaine na heroini wakati alipokuwa mja mzito suala ambalo limemwathiri pia mtoto wake baada ya kuzaliwa. Mtoto huyo alikuwa akisumbuliwa na maumivu makali baada ya kuzaliwa na madaktari walilazimika kumuweka chini ya uangalizi makhsusi. Naam, hivi ndivyo dawa za kulevya zinavyowaathiri vibaya watu wote wa familia bila ya kuvionea huruma hata vitoto vichanga.

Miongoni mwa matokeo ya kusikitisha ya migogoro ya familia katika nchi za Magharibi ni kuongezeka utumiaji wa pombe na vileo hususan baina ya vijana. Utumiaji wa pombe unasababisha matatizo mengi ya kijamii katika nchi hizo. Takwimu zinasema kuwa utumiaji wa pombe na vileo vya aina mbalimbali umeongezeka sana nchini Uingereza katika miaka ya hivi karibuni. Gazeti la Daily Mirror limeandika kuwa: Uchunguzi mpya umeonesha kuwa idadi ya watoto wanaotumia pombe nchini Uingereza imeongeza sana katika miaka ya hivi karibuni. Matokeo ya uchunguzi huo yamebaini kuwa, zaidi ya watoto elfu tatu wa Uingereza wenye umri wa chini ya miaka 12 mwaka jana walilazimika kuomba msaada kutokana na tatizo la kutumia pombe na vileo. Matokeo ya uchunguzi huo yamesisitiza kuwa, takwimu hizo zinaonesha kwamba matumizi ya pombe na vileo kati ya watoto wadogo yameongezeka kwa asilimia 12 katika kipindi cha miaka 8 iliyopita kwa kadiri kwamba kila siku watoto 6 huingizwa katika kitengo cha wagonjwa mahututi kutokana na kutumia pombe kupita kiasi. Vilevile ripoti zinasema kuwa wasichana wa Uingereza ndio wanaotumia pombe zaidi kuliko wenzao katika nchi za Magharibi kwa kadiri kwamba mmoja kati ya kila wasichana watatu ni mraibu wa pombe nchini humo.

Dini ya Uislamu kwa upande wake imetambua kila kitu chenye madhara kwa mwili na roho ya mwanadamu kuwa ni haramu. Hii ni pamoja na kuwa madaktari na wataalamu wa elimu nafsi wanasisitiza kuwa dawa za kulevya na pombe zina taathira hatari sana kwa mwili na roho ya mwanadamu. Uchunguzi wa wataalamu hao pia umethibitisha kuwa, dawa za kulevya na vileo kama pombe husababisha maradhi na matatizo mengi ya kinafsi kwa kadiri kwamba baadhi ya madaktari wa Kimagharibi wanasema kwamba pombe na vileo vina mfungamano mkubwa sana na uendawazimu na kichaa. Wanasisitiza kuwa idadi ya vichaa na wendawazimu inanasibiana na idadi ya mabaa na maeneo ya kunywea pole na vileo katika nchi kubwa za Magharibi.

Athari nyingine mbaya za matumizi ya pombe na vileo ni zile zinazoathiri kizazi cha mwanadamu kama kuzaliwa watoto vilema, kuzidisha shinikizo la damu na kusababisha jinai za mauaji na kadhalika.

Ni kwa sababu hiyo ndiyo maana Uislamu unapambana vikali na vileo na dawa za kulevya na umepiga marufuku na kuharamisha vitu hivyo kutokana na athari na madhara yake kwa mtu binafsi na jamii hususan familia.

XXXXX

Wasikilizaji wapenzi muda wa kipindi chetu cha leo umemalizika. Msikose kuwa nasi tena juma lijalo katika kipindi kingine kama hiki. Kwaherini.

Sauti na Video

Andika maoni


Msimbo salama (Security code)
Upyesha (Refresh)