Tovuti Hii Imefungwa. Tumehamia Kwenye Parstoday Kiswahili
Jumatatu, 10 Juni 2013 14:08

Mgogoro wa Familia katika Nchi za Magharibi (24) + Sauti

Mgogoro wa Familia katika Nchi za Magharibi (24) + Sauti

Hamjambo wasikilizaji wapenzi na karibuni kuwa nami tena katika sehemu nyingine ya kipindi chetu hiki kinachochunguza mgogoro wa familia katika nchi za Magharibi. Kama mnavyojua moja kati ya matokeo ya kudhoofika taasisi ya familia katika nchi za Magharibi ni kupungua uhusiano wa upendo ndani ya familia na kujielekeza vijana nje ya taasisi hiyo muhimu kwa ajili ya kufidia suala hilo. Matokeo ya uamuzi huo wa vijana na watoto ni kukithiri kwa ufuska na mmomonyoko wa maadili katika nchi za Magharibi.

Kipindi chetu hiki ambacho ni cha 24 cha mfululizo wa makala za Mgogoro wa Familia katika Nchi za Magharibi kitajadili ongezeko la ufuska na uchupaji mipaka kati ya tabaka la vijana na mabarobaro wa Kimagharibi na taathira zake za kutisha. Karibuni....

XXXXX

Kudhoofika kwa taasisi ya familia na uhuru usio na mipaka wala mantiki katika nchi za Magharibi kumekuwa na taathira kubwa na kusababisha matatizo mengi kwa watoto na vijana. Ripoti na takwimu mbalimbali zinaonesha kuwa, idadi ya wanaharamu na watoto wasio na wasimamizi wala walezi inaongezeka kwa kiwango cha kutisha katika jamii za Magharibi. Mfano wa suala hilo unaonekana waziwazi nchini Ujerumani. Ripoti ya hivi karibuni ya Idara ya Takwimu ya Ujerumani inasema kuwa mmoja kati ya kila watoto watatu wanaozaliwa nchini humo ni mwanaharamu, kwa maana kwamba amezaliwa kutokana na uhusiano haramu yaani zinaa na kwamba baba wa mtoto huyo hajulikani.

Gazeti la Die Welt la Ujerumani limeripoti kuwa hadi mwaka 2010 Ujerumani ilikuwa bado haijawahi kuwa ni kiwango kikubwa kama cha sasa cha wanaharamu na watoto waliozaliwa nje ya ndoa.

Ripoti ya Idara ya Takwimu ya Umoja wa Ulaya (Eurostat) inasema kuwa kiwango cha juu kabisa cha kuzaliwa wanaharamu katika nchi za Umoja wa Ulaya kinapatikana katika nchi ya Estonia ambayo ina asilimia 59 ya wanaharamu na cha chini zaidi kiko nchini Ugiriki kwa asilimia 7. Ripoti hiyo inasema: Kiwango cha kuzaliwa watoto haramu kutokana na wazazi ambao hawajafunga ndoa nchini Ufaransa ni cha asilimia 53, Uingereza ni asilimia 46, Austria asilimia 39 na Italia ni asilimia 24.

Baadhi ya wahakiki wanasema kuwa kuongezeka idadi ya familia za mzazi mmoja ni matokeo ya kuongezeka uhusiano haramu na zinaa katika nchi za Magharibi. Gazeti la Newsweek limeripoti kuwa, asilimia 57 ya wanaharamu wazungu nchini Marekani wanaishi na mama zao tu katika familia ya mzazi mmoja. Mbali na hayo, wasichana wengi wamekuwa wakibeba mimba kutokana na zinaa na uhusiano haramu na kujiunga na familia zenye mzazi mmoja au kukhitari kuziavya mimba hizo.

Mwandishi habari Joyce Bruce wa Marekani anasema kuhusu taathira za kupungua familia zenye wazazi wawili kwa maana ya baba na mama kwamba: Kupungua kwa familia zenye wazazi wawili kunaiweka jamii ya Marekani katika mkondo wa kuangamia.

Mahusiano haramu ya zinaa sasa yamezagaa na kuenea hata baina ya vijana na barobaro katika nchi nyingi za Magharibi na zile zinazofuata mitindo ya maisha ya Kimagharibi. Mara kwa mara vyombo vya habari vimekuwa vikipasha habari za kutia wasiwasi kuhusu wasichana wachanga wa shule za msingi wanaopachikwa mimba na kuzaa watoto wa haramu.

Wiki kadhaa zilizopita kuliripotiwa habari ya kutisha huko Marekani iliyokuwa na kicha cha habari: "Msichana mwenye umri wa miaka 14 ajifungua kwa siri bafuni." Msichana Cassidy Goodison aliyefanikiwa kuficha mimba na ujauzito wake kwa muda mrefu alijifungua bafuni nyumbani kwao na katika mazingira magumu. Habari hiyo ilizusha gumzo zaidi baada ya kueleweka kuwa, msichana huyo amekinyonga kichanga chake na kuficha maiti yake katika boksi la viatu. Kisa hicho cha kikatili cha msichana Goodison kimewastaajabisha watu wengi nchini Marekani na kuzusha maswali mengi. Watu wanajiuliza vipi msichana huyo mwenye umri mdogo ameweza kuficha ujauzito kwa kipindi cha miezi tisa? Siku tatu baadaye wakati mama wa msichana huyo alipokuwa akisafisha chumbani kwake aligundua kiboksi cha viatu na alipokifungua alikuta maiti ya kichanga na kupiga simu polisi. Mama wa Goodison anasema wakati mmoja alishakia hali ya kimwili ya binti yake lakini apomfanyia majaribio ya mimba matokeo hayakuonesha kuwa alikuwa mja mzito. Anasema anashangaa vipi mtoto wake ameweza kujifungua katika mazingira magumu akiwa peke yake. Takwimu zinaonesha kuwa zaidi ya thuluthi moja ya wasichana wa Marekani hujifungua kabla ya kukamilisha umri wa miaka 20.

Hii leo wasichana wengi wamekuwa wakipatwa na matatizo mengi kutokana na ukosefu wa usimamizi wa wazazi wao. Jarida la Reader's Digest limeandika katika moja ya matoleo yake, mahojiano ya daktari mmoja wa Marekani na msichana mmoja. Msichana huyo aliyeathirika na hali iliyomkuta anasema: Laiti zama na wakati ungekuwa ukirejea nyuma. Natamani kama ningekuwa naishi na wazazi wangu kama mwanachama katika familia. Nasikitika kwamba sikufikiria vyema kuhusu mustakbali wangu kabla ya kutumbukia kwenye zinaa na uhusiano haramu.....  Jarida hilo linamalizia kwa kuandika kuwa, ghamu na majuto, ukimbizi na kukosa makazi, jinai na uhalifu, kusambaratika familia na kushindwa kuona mbali na kukadiria mustakbali ni miongoni mwa matokeo ya uhusiano usio na mpaka katika jamii ya Marekani.

Miongoni mwa matatizo yanayoisumbua jamii ya sasa ya Magharibi ni kuongezeka baba na mama wenye umri ndogo. Nchi kama Uingereza inakabiliwa na tatizo kubwa na uhuru wa maingiliano haramu ya ngono na kubalehe mapema kwa watoto wadogo ambao kutokana na zinaa na kujifungua mapema, wanalazimika kuwa baba au mama katika umri mdogo. Wimbi la vijana wanaolazimika kubeba majukumu ya kulea mtoto wao wenyewe wakiwa watoto limekuwa tatizo kubwa sana katika nchi nyingi hususan huko Magharibi. Kwa mfano tu inaripotiwa kuwa, mvulana mwenye umri wa miaka 13 na msichana mwenye umri wa miaka 15 walipata mtoto hivi karibuni nchini Uingereza kutokana na zinaa na uhuru wa vitendo vya kujamiiana. Mvulana huyo ambaye hadi sasa anapewa fedha za mahitaji yake ya shuleni kutoka kwa baba yake na ambaye kwa mujibu wa kauli ya baba yake angali anacheza PlayStation, anataka kulea mtoto wake licha ya upinzani wa wazazi wake. Kuongezeka kwa tatizo hilo nchini Uingereza kumewafanya wataalamu wa mambo walipe jina la: Maafa ya Watoto Wenye Watoto.

Kwa sasa mporomoko wa maadili na zinaa, maingiliano haramu kati ya wanawake na wanaume hususan wanafunzi wa shule nchini Uingereza vinazitia wasiwasi mkubwa familia nyingi nchini humo. Septemba 26 mwaka 2011 gazeti la Daily Mail la Uingereza liliandika kuwa: Hali ya mambo imewafanya wazazi wengi wafadhilishe kuwapeleka watoto wao katika shule zisizo za mchanganyiko baina ya wavulana na wasichana. Wazazi wa Uingereza, linaendelea kuandika gazeti la Daily Mail, wanaamini kuwa katika shule mchanganyiko watoto wao huathiriwa na wanafunzi wenye jinsia tofauti na matokeo yake ni kutotilia maanani masomo wanapokuwa darasani."

Wataalamu wa elimu nafsi ya jamii na weledi wa masuala ya kijamii wanasema kuwa sababu kuu ya kuishi pamoja wanawake na wanaume bila ya kufunga ndoa kisheria ni uchupaji mipaka katika uhusiano wa mwanamke na mwanaume.

Ni kwa sababu hiyo ndio maana dini tukufu ya Uislamu imetambua kwamba kushibisha matakwa ya kimaumbile baina ya mwanamke na mwanaume kunapaswa kufanyika katika mazingira ya ndoa halali na kwamba jamii inapaswa kuwa uwanja wa kazi na harakati za kijamii.

XXXXXX

Wasikilizaji wapenzi kipindi chetu cha leo kinaishia hapa. Ni matarajio yangu kuwa mmefaidika na niliyokuandalieni na hadi tutakapokutana tena juma lijalo nakuageni nikikutakieni kila la kheri.

Sauti na Video

Andika maoni


Msimbo salama (Security code)
Upyesha (Refresh)