Tovuti Hii Imefungwa. Tumehamia Kwenye Parstoday Kiswahili
Jumatatu, 03 Juni 2013 15:15

Mgogoro wa Familia katika nchi za Magharibi (23)

Mgogoro wa Familia katika nchi za Magharibi (23)

Hamjambo wasikilizaji wapenzi na karibuni kuwa nami tena katika sehemu nyingine ya kipindi hiki kinachozungumzia mgogoro wa familia katika nchi za Magharibi. Nadhani bado mnakumbuka kuwa katika kipindi cha wiki iliyopita tulizungumzia baadhi ya matatizo ya kijamii na ya mtu binafsi na kuenea ufuska katika jamii za nchi za Magharibi kutokana na kusambaratika taasisi ya familia. Kipindi chetu cha leo kitaendelea kujadili suala hilo. Karibuni.

XXXX

Katika karne hii ya 21 mwandamu wa Magharibi ameendelea kujitenga zaidi na fitra na mauambile asili ya mwanadamu kadiri siku zinavyopita. Kwa sasa kunashuhudiwa mabadiliko yenye uharibifu mkubwa katika familia za nchi za Magharibi. Kwa kadiri kwamba wanyama kama mbwa wamechukua nafasi ya upendo na mahusiano ya kibinadamu baina ya watu wa familia moja. Kwa maneno mengine ni kuwa, watu wa familia moja ambao ilibidi wawe na uhusiano wa karibu unaotawaliwa na upendo wanajihisi kuwa na mapungufu katika masuala ya  kiroho yanayosababishwa na kuyumbayumba kwa taasisi ya familia ambao wanaamua kuziba na kufidia mapungufu hayo kwa kujielekeza kwenye wanyama kama mbwa. La kusikitisha zaidi ni kuwa uhusiano wa mwanadamu na wanyama unazidi kupanuka na kuwa mkubwa zaidi kwa kadiri kwamba sasa Wamagharibi wanaingiliana kingono na wanyama. Tumesikia mara nyingi habari za kufanyika ndoa baina ya mwanadamu na mnyama katika jamii zilizobakia nyuma kama baadhi ya makabila ya India lakini la ajabu zaidi ni kuona vitendo kama hivyo viovu vikienea katika jamii za Magharibi tena katika karne hii ya 21.  Mara kwa mara tumekuwa tukisikia majina ya watu wanaotaka kuoa wanyama na soko la uhusiano wa kingono baina ya wanadamu na wanyama limeshamiri na kunawiri sana katika nchi za Magharibi na wavuti mbalimbali za picha chafu za ngono zinatangaza kwa wingi vitendo kama hivyo vichafu. Vilevile idadi ya vituo cha kuzalisha wanyama wanaotajwa kuwa wanaofaa kwa ajili ya maingiliano ya kingono na wanadamu pia imeongezeka sana.

Kwa sasa katika jamii za Kimagharibi baadhi ya wanaume na wanawake wamekuwa wakioa au kuolewa na wanyama wa kufuga nyumbani mithili ya mbwa. Hususan baadhi ya wanawake wajane au wenye umri mkubwa wamekuwa wakielekea zaidi kwa mbwa kwa ajili ya kushibisha haja zao za kujamiiana. Kwa mfano tu miezi kadhaa iliyopita mashirika ya habari yaliripoti kuwa mwanamke mmoja wa Kimarekani ambaye ameachika mara nne kwa kile anachodai ni hiana na ukosefu wa uaminifu wa waume zake, alifanya sherehe rasmi ya kuolewa na mbwa kwa ajili eti ya kujikomboa na hiana na kutowaamini wanaume. Kuhusu sababu ya kuolewa na mbwa mwanamke huyo wa Marekani anasema: Mbwa wake ni mwaminifu zaidi kuliko waume zake wa zamani. La kustaajabisha ni kuwa katika siku ya harusi mwanamke huyo alivaa veli na mapambo kamili ya bibi harusi na mbwa alivishwa koti na suruali. Kwa hakika sherehe hiyo ya harusi ilishabihiana zaidi na komedi ya kusikitisha.

Ni wazi kuwa uhusiano wa kujamiiana nje ya ndoa na vitendo vya kutokuwa na uaminifu kwa mwanamke vimekuwa vikisambaratisha ndoa nyingi katika nchi za Magharibi na kwengineko. Hata hivyo la kusikitisha zaidi ni kuwa baada ya kufeli ndoa kama hizo upande mmoja wa ndoa husika unapotoka zaidi na kuamua kufunga ndoa na kujamiiana na mnyama kwa shabaha ya kufidia nakisi ya kukosa upendo na kushibisha matakwa yake ya kimwili.

XXXX

Japokuwa ndoa za watu kuoa wanyama bado hazijahalalishwa rasmi katika nchi za Magharibi na hakuna ndoa ya aina hiyo iliyosajiliwa rasmi lakini serikali za nchi hizo pia hazizuii ndoa kama hizo. Kwa sasa kuna wasiwasi kwamba katika siku za usoni ndoa za wanadamu na wanyama zitahalalishwa na kufanywa rasmi kama zilivyohalalishwa ndoa baina ya watu wenye jinsia moja kwa maana ya ndoa kati ya mwanaume na mwanaume mwenzake na kati ya mwanamke na mwanamke mwenzake. Suala hilo la kuruhusu vitendo vya liwati, na kujamiiana wanawake kwa wanawake linatajwa kuwa ni miongoni mwa vielelezo vya uhuru katika nchi za Magharibi!

Sasa viongozi wa ngazi za juu wa jeshi la Marekani wanataraji kuwa kuruhusiwa uhusiano wa ngono baina ya wanajeshi na wanyama kutapunguza takwimu za ubakaji na vitendo vya kunajisiwa wanawake na hata wanaume ndani ya jeshi hilo. Mwaka 2011 Baraza la Seneti la Marekani lilifuta sheria ya adhabu dhidi ya wanajeshi wanaolawitiana au kufanya ngono na wanyama. Sheria hiyo ilifutwa katika majimbo ya Marekani na kuondoa sheria ya jeshi iliyotambua uhusiano kama huo kuwa si wa kawaida, mbaya, na usio wa kisheria. Kwa maana kwamba tangu baada ya kupasishwa sheria hiyo mwanajeshi yoyote atakayekuwa na uhusiano kama huo wa watu wa jinsia moja au na mnyama atafikishwa katika mahakama ya kijeshi.

Ala kulli hal, mwanadamu wa Magharibi amefunzwa kwamba yuko huru hata kufunga ndoa na kujamiiana na mnyama kwa kutumia jina la uhuru japokuwa suala hilo linahatarisha maslahi na usalama wake. Katika mtazamo wa Uislamu mwanadamu anatambuliwa kuwa ndio kiumbe bora zaidi na mwenye hadhi na nafasi ya juu mbele ya Mwenyezi Mungu. Kwa msingi huo mbali na uhuru dini hiyo pia inatilia maanani maslahi ya kiumbe huyo. Kwa sasa kunajitokeza swali kwamba inakuwa vipi mwanadamu akaporomoka na kujiweka katika safu ya wanyama kama mbwa?

Ni wazi kuwa pale anaposhindwa kuelewa lengo la kuumbwa kwake hapa duniani anaweza kufanya kila kitu. Kwa utaratibu huo kuenea mahusiano ya ngono baina ya wanadamu na wanyama ni miongoni mwa taathira za kudhoofika na kuporomoka misingi ya familia katika nchi za magharibi. Inastaajabisha sana kuona katika zama hizi za karne ya 21 ambapo mwanadamu wa Magharibi anadai kwamba amepiga hatua kubwa za maendeleo katika taaluma za tiba, afya na katika ustaarabu lakini badala ya kuwa na uhusiano wa kimapenzi na mwanadamu mwenzake katika mipaka ya familia na ndoa halali anakhitari kufanya ngono na wanyama! Hii ni pamoja na kuwa madaktari wengi wanautambua uhusiano kama huo kuwa ni hatari sana kwa afya ya mwanadamu na unaweza kusababisha maradhi ya aina mbalimbali. Kwa mfano tu maradhi ya zoonotic(yaani maradhi au maambukizo yanayosababishwa na wanyama kwenda kwa binadamu au kinyume chake) ambayo ya chini kabisa miongoni mwayo ni yale ya kuambukiza ya mapafu, tishu za bongo, vimelea vya utumbo na matatizo ya kupumua na figo hususan kwa watoto wadogo na wanawake huambukizwa kupitia kwa wanyama.

Miongoni mwa sababu nyingine za kusambaratika misingi ya familia katika nchi za Magharibi ni kujamiiana kwa watu maharimu yaani mahusiano ya ngono ya mwanamke na ndugu zake wa damu. Inasikitisha kwamba mahusiano kama hayo yanashika kasi sana katika jamii za nchi za Magharibi.

Taasisi ya Ujerumani ya Max Planck mwaka 2007 ilitoa ripoti ikitangaza kuwa kufanya zinaa na maharimu katika nchi kama China, Ufaransa, Ivory Coast, Uholanzi, Russia, Uhispania na katika utawala haramu wa Israel huhalalishwa kisheria na wala hakupingwi iwapo pande mbili zitakubaliana kufanya tendo hilo.

Ni wazi kuwa tendo la ndoa kati ya watu maharimu linakirihisha na wala halikubaliwi na akili na maumbile safi ya mwanadamu. Uhusiano wa aina hii huwa na taathira mbaya sana kwa kizazi cha baadae na unatishia sana misingi ya familia. Hii ni pamoja na kuwa mke na mume huwatazama watoto wao au hata jamaa zao wa karibu kama tonge nono la kushibisha matakwa yao ya kingono. Kuenea kwa tabia hiyo chafu pia kunatokana na kudhoofika mahusiano sahihi na imani ya kidini katika familia. Kwani wakati jamii inapokuwa mbali na dini na masuala ya kiroho huwa rahisi kutumbukia katika ufuska, utovu wa maadili na kuchupa mipaka, suala ambalo hutoa mwanya wa kuenea uhusiano haramu na mchafu wa maingiliano kati ya maharimu.

Miongoni mwa matokeo mabaya ya kuyumba misingi ya familia katika nchi za Magharibi na zile zinazoiga sera na mienendo yao ya maisha ni watu wazima kuwaingilia kingono watoto wadogo. Ni vyema kukumbusha hapa kuwa kuenea utamaduni mbaya wa mavazi nusu uchi na yasiyo ya staha na uhuru wa maingiliano ya kujamiiana katika nchi mbalimbali duniani kunamuelekeza mwanadamu katika shimo kubwa la maangamizi na maradhi ya aina mbalimbali ya kimwili na kiroho. Habari za hivi karibuni zilisema kuwa polisi katika jimbo la Florida huko Marekani wamewatia nguvuni wanaume 23 ambao ni wanachama wa genge moja linalowanyanyasa watoto wadogo na kuwaingilia kimwili. Vilevile takwimu za kutisha zinasema kuwa kumekuwepo ongezeko la watu wazima kuwaingilia watoto wenye umri wa chini ya miaka 12.

XXXX

Muda hauturuhusu kusonga mbele na kipindi chetu wasikilizaji wapenzi, basi tukutane tena juma lijalo katika mfululizo wa vipindi hivi vya matatizo ya familia katika nchi za Magharibi. Dumuni katika kheri.

Andika maoni


Msimbo salama (Security code)
Upyesha (Refresh)