Tovuti Hii Imefungwa. Tumehamia Kwenye Parstoday Kiswahili
Jumanne, 21 Mei 2013 15:53

Matatizo ya Familia katika Nchi za Magharibi (22)

Matatizo ya Familia katika Nchi za Magharibi (22)

Wasikilizaji wapenzi ni wasaa na wakati mwingine umewadia wa kujiunga nanyi tena katika mfululizo huu wa vipindi vinavyochunguza matatizo ya familia katika nchi za Magharibi, hiki kikiwa ni kipindi cha 22. Kama mnakumbuka, katika vipindi vilivyopita tuliashiria sababu na mambo mbalimbali yanayosababisha kusambaratika familia katika ulimwengu wa Kimagharibi. Tulisema kuwa baadhi ya mambo hayo yalipata nguvu kutokana na misingi ya kifikra na aidiolojia za humanism, saikulalism, modernisim na feminism. Misingi hiyo ya kifikra iliathiri pakubwa nyanja mbalimbali za jamii ya Kimagharibi baada ya zama wa Rainassance na mapinduzi ya viwanda. Fikra hizo za kimaada zilipenya pia katika uhusiano na kanuni za taasisi ya familia na kudhoofisha taasisi hiyo. Baadhi ya mambo mengine yaliyochangia mgogoro wa familia katika ulimwengu wa Kimagharibi ni uundaji wa vyombo vya mawasiliano vyenye kupotosha jamii kama intaneti, filamu chafu, michezo ya intaneti na kadhalika, masuala ambayo yanazidisha ufisadi na maafa ya kifamilia na kijamii katika jamiii. Katika kipindi chetu hiki tunaanza kutupia jicho matokeo ya maafa hayo ya kijamii na kuenea ufisadi katika jamii ya Kimagharibi jambo lililopelekea kusambaratika familia katika jamii hiyo. XXXX

Sambamba na  kuenea mirengo iliyo dhidi ya familia na mtazamo hasi kwa taasisi hiyo katika ulimwengu wa Kimagharibi familia ya kawaida na yenye maadili bora imepoteza nafasi yake kwa uhusiano usio wa kawaida na wa kufurutu ada wa mwanamke na mwanaume ambao unakinzana na maumbile asilia ya mwanadamu. Ukweli ni kuwa tangu nusu ya pili ya karne ya 20 zinaa na mahusiano haramu ya kujamiiana yamekuwa yakiongezeka sana sambamba na kupungua ndoa na kuongezeka talaka kwa kasi.

Maingiliano haramu ya ngono yamewafanya mwanamke na mwanaume katika ulimwengu wa Kimagharibi kuonekana kama bidhaa inayowekwa mnadani. Kwa mfano duka moja kubwa limefunguliwa huko Paris , Ufaransa ambalo ni mahsusi kwa wanawake wasio na waume. Wanawake wasio na waume wa Ufaransa sasa hawana tena haja ya kuwa na urafiki na wanaume mitaani au kwenye maeneo mengine baada ya kufunguliwa duka hilo, kwani wanaume hupatikana dukani humo na wanaweza kupendwa na kununuliwa na wanawake hao. Wanaume wanaotaka kuuzwa ni lazima waandikishe majina yao katika tovuti ya duka hilo. Picha, maelezo ya mtu na bei ya maelfu ya wanachama wa duka hilo hukabidhiwa kwa wasichana ambao hawajaolewa.

Kwa msingi huo moja ya maafa yanayosababishwa na mgogoro wa familia katika nchi za Magharibi ni kuongezeka ufisadi na mporomoko wa maadili. Kwa bahati mbaya mporomoko huo wa maadili kama maingiliano ya watu wenye jinsia moja na ndoa za watu wa aina hiyo, uhusiano wa mke na mme nje ya muundo wa familia, maisha ya pamoja na mwanamke na mwanaume bila ya kufunga ndoa na kupuuza maadili, kumeyumbisha misingi ya familia.   Kukanyagwa misingi ya maadili katika jamii ya Kimagharibi kunapata sura mapya kila siku katika jamii hiyo. Inaonekana kuwa sasa kuna mashindano ya nani anatumbukia zaidi katika ufuska na zinaa ambayo yanazidi kupiga mishale yake kwa taasisi ya familia na maadili bora katika nchi za Magharibi.

Gazeti la Lastampa la nchini Italia hivi karibuni lilifichua katika ripoti yake kuhusu kupungua sana thamani za kimaadili nchini humo. Ripoti hiyo ilihusu matukio ya wanaume kubadilishana wake kwa ajili ya burudani na kujifurahisha zaidi katika mialiko, suala ambalo imelitambua kuwa ni moja ya njia mpya zinazomtumia mwanamke kama wenzo na mwanasesere wa kuchezewa na wanaume na kielelezo cha kuporomoka thamani za kimaadili kama ghera, staha na uungwana. Jambo hilo chafu ni pigo kubwa kwa uhusiano wa kudumu wa mke na mme katika familia. Gazeti la Lastampa limeandika kuhusiana na jambo hilo kuwa: "Katika kitendo kisicho cha kibinadamu na cha kushangaza, Waitalia hubadilishana na kuazimana wake zao kwa ajili ya kustarehe." Limeandika kuwa wanawake wengi na wanaume wa Kiitalia ambao hupewa barua za mialiko kwa ajili ya kwenda mapumziko ya wakati wa likizo za msimu wa joto katika eneo la kuvutia la Tuskana lililoko katikati ya Rome mji mkuu wa Italia, wanapaswa kwanza kufikiri vizuri kabla ya kukubali mwaliko huo. Hii ni kwa sababu wanawake hao na waume zao huenda wakalazimika kubadilisha wake na wanaume zao mkabala wa kukubali mwaliko huo."

Kitendo cha kubadilishana mke katika jamii za Kimagharibi mbali na kuwa kimezidisha ufisadi na ufuska, kimeshadidisha pia vitendo vya utumiaji mabavu na jinai. Kwa mfano jarida moja mashuhuri la Australia liliandika kuwa: "Nyie mnaotaka kubadilishana wake zenu na wake wa marafiki zenu mnaweza mara moja kwenda katika mahakama ya mji wa Melbourne na kushuhudia kwa karibu kwa macho yenu mafaili ya kesi mbalimbali za uhalifu na jinai zilizosababishwa na kubadilishana wake."

Mafaili mengi ya mauaji yaliyopo katika mahakama ya Melbourne, Australia yanahusiana na kesi za mauaji yaliyotokana na vitendo visivyo vya kibinadamu vya kubadishana wake au kufanyiana hiana na usaliti katika ndoa. Mfano wa kesi hizo ni ya kutoweka kabisa mwanaume aliyekuwa na umri wa miaka 51. Mwanaume huyo miezi kadhaa kabla ya kutoweka alibadilishana mke wake na mmoja wa wafanyakazi wenzake kwa siku kadhaa. Ilipangwa kuwa siku kadhaa baadaye mwanaume huyo angebadilishana mke wake huyo na mke wa rafiki yake mwingine ambaye alikuwa miongoni wa jamaa wa karibu na Waziri Mkuu wa New Zealand. Jaji wa kesi hiyo alisema kuwa moja ya sababu za kutoweka mwanaume huyo ilikuwa ni kuazimana na kubadilishana wanawake na marafiki zake.

Miongoni mwa vielelezo vya mporomoko wa maadili na misingi ya taasisi ya familia ni ndoa za watu wenye jinsia moja. Kwa sasa watu katika nchi za Magharibi na zile zinazoiga kibubusa utamaduni wao wanapuuza thamani za kibinadamu, sheria za Mwenyezi Mungu na hata maumbile ya kimwili ya mwanaume na mwanamke na kukubali kuoa au kuolewa na mtu mwenye jinsia sawa na zao kwa ajili ya kushibisha kiu zao za matamanio ya kihayawani. La kusikitisha zaidi ni kuwa, badala ya kukabiliana na mambo kama hayo, serikali za nchi za Magharibi zimehalalisha vitendo hivyo vichafu na hata baadhi ya serikali hizo zimeruhusu kufungwa ndoa na kuanzishwa familia baina ya watu wenye jinsia moja kwa maana ya ndoa au familia ya mwanamke na mwanamke mwenzake na mwanaume na mwanaume mwenzake. Kwa mfano tu bunge la Uingereza limepasisha sheria inayowapa haki za familia ya kawaida watu wawili wenye jinsia moja wanaokhitari kuoana na kujamiiana. Inasikitisha kuwa waungaji mkono wa ndoa kama hizi za wanaume kwa wanaume na wanawake kwa wanawake wanaongezeka siku baada ya siku na kupanua shughuli na harakati zao katika nchi mbalimbali duniani. Hii ni pamoja na kuwa maumbile na muundo wa mwili wa mwanadamu umetayarishwa kwa ajili ya mahusiano baina ya mwanamke na mwanaume na si mwanaume na mwanaume mwenzake au mwanamke na mwanamke mwenzake.

Ukweli ni kwamba ndoa kama hizo za watu wenye jinsia moja zinapingana na maumbile halisi ya mwanadamu na haziwezi kujenga uhusiano salama wa kimwili na kiroho baina ya watu hao. Hii ni pamoja na kuwa moja kati ya malengo ya ndoa baina ya mke na mume ni kujenga hali ya upendo na rehma baina yao na wanachama wote wa familia kama inavyoashiria aya ya 21 ya Suratur Rum. Katika upande mwingine ndoa kama hizo zinazofanyika baina ya wanaume na wanaume wenzao au kati ya wanawake na wanawake wenzao haziwezi kuwa na matunda ya watoto wanaoleta furaha na vuguvugu la aina yake katika maisha ya kifamilia. Vilevile tunapaswa kukubali kuwa maingiliano baina ya watu wenye jinsia moja ni aina fulani ya kudhalilisha maumbile safi na asili ya mwanadamu.

Uislamu umempa mwanadamu thamani kubwa na hauruhusu hata kidogo kudhalilishwa na kushushwa hadhi ya kiumbe huyo. Kwa muhtasari ni kuwa vitendo vya kuingiliana watu wenye jinsia moja au ndoa baina ya watu wa aina hiyo ni vitendo viovu, vichafu, visivyokuwa vya kibinadamu, vinavyopingana na sheria za Mwenyezi Mungu na maumbule ya asili ya mwanadamu.    XXXXXX

Wapenzi wasikilizaji muda uliotengwa kwa ajili ya kipindi hiki unaelekea ukingoni. Tutakutana wiki ijayo katika kipindi kingine panapo majaaliwa ya Mwenyezi Mungu. Kwaherini.

Andika maoni


Msimbo salama (Security code)
Upyesha (Refresh)