Tovuti Hii Imefungwa. Tumehamia Kwenye Parstoday Kiswahili
Jumatatu, 13 Mei 2013 13:48

Matatizo ya Familia katika Nchi za Magharibi (21)

Matatizo ya Familia katika Nchi za Magharibi (21)

Karibuni wasikilizaji wapenzi katika mfululizo wa vipindi vya Matatizo ya Familia katika nchi za Magharibi hiki kikiwa kipindi cha 21. Katika kipindi hiki ninaanza kuchunguza mavazi yasiyo ya staha katika jamii za Magharibi, mtazamo unaowaona wanawake kama chombo tu cha kushibisha matakwa ya kingono ya wanaume, maingiliano ovyo baina ya wanawake na wanaume na taathira zake katika kudhoofisha misingi ya familia. Basi bila ya kupoteza muda karibuni muwe nami kutegea sikio haya machache lakini yenye manufaa niliyoweza kuwaandalia kwa leo. XXXX

Ni muda sasa ambapo matatizo ya kimadili na masuala ya kujamiana ovyo yameongezeka sana katika ulimwengu wa Magharibi. Kwa sasa uzururaji ovyo usiku, mawasiliano na maingiliano huru baina ya wanawake na wanaume kwenye baa na klabu za usiku pamoja na mavazi yasiyofaa ya wanawake vimedhoofisha zaidi thamani za kifamilia. Mwandishi George Ryley Scott wa Uingereza ameandika kuwa: Ufuska na vitendo vichafu, uzururaji ovyo nyakati za usiku na ukosefu wa staha na haya baina ya wanawake wa kisasa vimekuwa miongoni mwa mambo yanayoambatana na maisha ya anasa ya zama hizi. Utumiaji wa madawa ya kulevya, pombe kali, kupaka rangi nyekundu kwenye kucha na mdomo na kuzungumza mambo machafu na ya ufuska pia ni moja ya mambo yanayotambuliwa kuwa ya udharura kwa mwanamke wa kisasa katika jamii ya Kimagharibi."

Kwa upande wake mwandishi Wendy Shalit wa Marekani analinganisha vidaftari viwili vya kuandikia kumbukumbu vya wasichana wawili walioishi katika zama tofauti za miaka ya 1880 na 1980 na kufikia natija kuwa: "Kuishi vizuri na kuwahudumia wazazi yalikuwa matarajio makubwa ya msichana wa mwaka 1880 ilhali yule wa mwaka 1980 alikuwa na matarajio ya kuwa mwenye hadaa, kujipamba kwa mitindo ya kisasa, kubadili rangi ya macho na nywele na kadhalika."

Suala la kuwa mbali na maadili bora jamii ya Kimagharibi limezidisha kiwango cha vitendo vichafu na ukahaba katika jamii ya Kimagharibi katika kipindi cha sasa kuliko huko nyuma. Kanali ya televisheni ya Fox News imetangaza kuwa, ukahaba na zinaa limekuwa jambo linalokubalika katika jamii ya Marekani. Kanali hiyo imeeleza kuwa kwa sasa wanawake wa Kimarekani wananunua kitabu kinachokiuka maadili ambacho ndani yake kina mambo mabaya sana. Katika kitabu kicho kumechorwa picha zenye kuchochea hisia za kujamiana zile zinazohusiana na utumwa wa ngono. Ripoti ya televisheni hiyo imesema, nakala milioni ishirini za kitabu hicho zimeuzwa nchini Marekani pekee. Kuchapishwa na kusambazwa kwa wingi kitabu hicho kunaonyesha namna vitendo vya ukahaba na zinaa vilivyoenea sana miongoni mwa wanawake wa Kimarekani katika zama za sasa kuliko huko nyuma. Aidha kanali ya Fox News imeeleza kuwa: "Hata akina mama wa Kimarekani wanawahamasisha mabinti zao wajikwatue na kuwavutia wanaume katika masuala ya ngono na kuwatayarishia mavazi yanayowafanya kama chambo cha kuwavutia wanaume."

Dharau kubwa zaidi inayofanywa dhidi mwanamke ni kuwa, sasa mwanamke hatazamwi kama binadamu bali huangaliwa kama chombo cha kushibisha matakwa ya ngono ya mwanaume. Maafa hayo yanatokea sasa katika jamii ya Kimagharibi na katika nchi zinazofuata utamaduni na mwenendo wa kimaisha wa Wamagharibi, na mwanamke ambaye anaweza  kuwa msingi wa familia na mlezi wa vizazi vijavyo, sasa amegeuzwa na kufanywa bidhaa isiyo na thamani. Ni wazi kuwa katika jamii isiyokuwa na mavazi ya staha na ya heshima, usalama wa mtu binafsi na familia na baadaye usalama wa jamii hutumbukia hatarini. Moja ya taathira mbaya za  kuvaa mavazi yasiyo ya heshima na stara katika jamii za Kimagharibi ni kuyumbayumba kwa familia. Kwani pale ushawishi na mvuto wa kingono katika maeneo ya umma unapogeuzwa na kuwa sifa na thamani za kijamii, wanawake wanaoshindwa kushindana katika uwanja huo kutokana na sababu mbalimbali huonekana wenye thamani duni na wasiofaa. Katika upande wa familia pia wanawake walioolewa nao huhisi kushindwa na kuwa duni mbele ya wanawake vijana, warembo na wenye mvuto mkubwa zaidi.

Katika upande mwingine ni kuwa, nguo na mavazi yasiyokuwa ya staha ya wanawake kwa upande mmoja, na tabia ya wanaume wengi ya kutaka kuburudika bila ya mpaka wala kizuizi chochote katika nchi za Kimagharibi vimewaelekeza wanaume wengi katika upande wa kusaka wanawake vijana zaidi, warembo na wenye mvuto wa kingono hususan katika jamii kama hizo zinazoweka mbele na kuthamini zaidi mapambo ya kidhahiri ya mwanamke. Kwa hiyo uwezekano wa kushawishika kingono wanaume kwa wanawake wengine wasiokuwa wake zao unakuwa mkubwa zaidi hususan tunapozingatia ongezeko kubwa la uhusiano haramu na wa nje ya ndoa na familia. Kwa msingi huo inabainika kuwa kutoheshimiwa mavazi yenye staha na heshima ni moja ya sababu za kutoweka ladha ya maisha ya kifamilia, kuweko uhusiano baridi kati ya wanandoa na mwishowe kuongezeka kiwango cha talaka katika jamii za Kimagharibi. XXXX

Kwa sasa zinaa na kuwatumia wanawake kama wenzo katika nyanja mbalimbali hususan katika masuala ya kijamii na kiuchumi vimeongezeka pia katika nchi za Magharibi. Vilevile ripoti zinaonesha kuwa moja ya sababu za kuongezeka vitendo vya kubakwa wanawake ni mavazi yasiyo ya heshima na yasiyo ya staha ya wanawake. Habari kutoka katika jimbo la California zilieleza kuwa binti aliyekuwa na umri wa miaka 15 alivamiwa na wavulana saba wakati akirejea nyumbani baada ya kuhudhuria masomo yake ya muziki katika shule ya upili kutokana nguo aliyokuwa amevaa iliyokuwa ikichochea hisia za ngono.  Maombi ya binti huyo hayakusaidia kitu kwani wavulana hao saba walimnajisi kweupe tena mbele ya wanawake na wanaume 20 waliokuwa wakishuhudia. Polisi waliwasili na kumpeleka binti huyo hospitalini akiwa mahututi masaa mawili baada ya kutoweka wavulana hao. Baada ya kuwatia nguvuni vijana hao washari na kufanyika uchunguzi, polisi walifikia natija kwamba chanzo kikuu cha tukio hilo ni nguo isiyo ya staha na heshima ya msichana huyo. Vilevile baada ya kesi kadhaa za kunajisiwa wanawake katika mji wa New York, polisi ya mji huo ililazimika kuanzisha doria ili kuwakumbusha na kuwatahadharisha wanawake wanaovalia mavazi yasiyo ya heshima.

Gazeti la Wall Street Journal pia limeripoti kuwa, katika radiamali yake kwa mfululizo wa matukio ya kubakwa wanawake yaliyotokea katika bustani moja ya mji wa New York, polisi waliotumwa katika eneo hilo waliwasimamisha wanawake ambao walihisi kuwa mavazi yao hayafai na kuwataka wabadili mavazi yao. Aidha polisi ya New York ilidai kuwa, katika  kesi nyingi za ubakaji, watu waliofanya uhalifu huo waliwashambulia wanawake waliokuwa wamevalia sketi fupi na zisizofaa.

Katika hali ambayo mwanamke katika ulimwengu wa Magharibi anatazamwa kama bidhaa ya kupigia propaganda na wenzo wa kuchochea hisi za ngono, Uislamu unamtazama mwanamke kama binadamu na shakhsia yenye hadhi na heshima kubwa. Kwa sababu hiyo Uislamu umewataka wanawake wajistiri na kutoonyesha maungo ya miili yao katika jamii ili kulinda misingi ya familia kwa utulivu na amani. Dini Tukufu ya Kiislamu inatambua thamani ya kijamii ya mwanamke katika elimu, heshima, kujisitiri, kujitolea, uchamungu, na huruma ya mke na mama. Vazi la hijabu ndio njia ya ufumbuzi ya Kiislamu kwa ajili ya kuwakinga wanawake na macho ya matamanio na kishetani pamoja na kulinda nguzo ya familia. Uzoefu unaonyesha kuwa pale mwanamke anapokuwa na staha, mwenye mavazi ya heshima na msafi wa maadili hatolengwa wala kusumbuliwa na wahuni na huweza hujikinga na zinaa na maingiliano haramu. Katika uga huo Mwenyezi Mungu anasema katika aya ya 59 Suratul Ahzab kuwa: "Ewe Nabii, waambie wake zako, na mabinti zako na wake wa waumini: Wateremshe juu yao shungi zao. Hilo ni karibu zaidi kuweza kujulikana wasiudhiwe, na Mwenyezi Mungu ni Mwingi wa kusamehe, Mwenye kurehemu." Mbali na hilo, hijabu huimarisha misingi ya familia pia. Kwani pale wanaume katika jamii wanaporidhisha matamanio yao nje ya mipaka ya ndoa au kukutana na wanawake wasio na mavazi ya staha na heshima kila siku ambao yumkini wakapunguza mvuto na mapenzi yao kwa wake zao, suala hilo linaweza kupunguza pia uhusiano wa kiroho na kimapenzi kati ya mke na mume na mwishowe kusambaratisha kifamilia yao. Katika jamii ya aina hiyo hali ya kuaminiana hutoweka kabisa baina ya mke na mume  na kila mmoja kati yao hufikiria kuwa mwenzake huvutiwa na wanawake au wanaume wengine. Vilevile takwimu rasmi zinaonyesha kuwa moja ya sababu za kuongezeka kiwango cha talaka na zinaa ni mavazi yasiyo na staha ya wanawake.

Kwa msingi huo vazi lenye staha na heshima huboresha usalama wa kijamii wa mwanamke na kuimarisha misingi ya familia. Hivyo basi mafunzo ya Uislamu kuhusu vazi la staha la hijabu na mipaka iliyowekwa na dini hiyo katika mahusiano ya wanawake na wanaume kwenye jamii inapaswa kusisitizwa na kutekelezwa barabara ili dunia yetu ya leo iondokewe na maradhi na balaa linalotishia familia na jamii zetu.  XXXX

Wapenzi wasikilizaji muda wa kipindi chetu cha leo umemalizika. Tukutane tena wiki ijayo panapo majaaliwa yake Mola Muumba. Asanteni kwa kunitegea sikio na kwaherini.

Andika maoni


Msimbo salama (Security code)
Upyesha (Refresh)