Tovuti Hii Imefungwa. Tumehamia Kwenye Parstoday Kiswahili
Jumatatu, 06 Mei 2013 14:00

Matatizo ya Familia katika Nchi za Magharibi (20) + Sauti

Matatizo ya Familia katika Nchi za Magharibi (20) + Sauti

Assalamu Alaykum wasikilizaji wapenzi wa Idhaa ya Kiswahili Sauti ya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran. Ni wakati mwingine umewadia wa kuwa nanyi katika mfululizo huu wa vipindi vinavyojadili kwa kina matatizo ya familia katika nchi za Magharibi.

Fikra na mitazamo ya kila mtu ndio roho ya maisha ya mtu huyo. Tangu huko nyuma hadi sasa mfumo wa ubepari katika familia ya Kimagharibi umekuwa ukiwasilisha vigezo na mitindo mbalimbali kama wanamitindo na wasanii na hata vifaa vya kuchezea watoto na kubadilisha silika na fikra za watu katika familia za Magharibi kupitia njia hiyo. Katika kipindi hiki cha 20 cha Matatizo ya Familia katika Nchi za Magharibi tunaanza kuchunguza taathira mbaya za baadhi ya vifaa hivyo vya kuchezea watoto na mfumo wa elimu katika kudhoofisha thamani na maadili katika familia ya Kimagharibi. Tafadhalini kuweni name hadi mwisho wa kipindi.

XXXX

Ni wazi kuwa vifaa vya kuchezea watoto hususan mwanasesere vina nafasi muhimu katika malezi na ukuaji wa shakhsia ya watoto wa kike. Watoto wa kike ni wanawake wa baadaye wa kila taifa na kupotoka kila taifa kunafungamana na watoto wa kike na wanawake wa taifa hilo. Mwanasesere aliyepewa jina la Barbie hivi sasa amekuwa moja ya vigezo mashuhuri na vyenye taathira katika ulimwengu wa Kimagharibi. Mwanasesere huyo amapeta umashuhuri duniani kote na hakuna mtu asiyejua jina lake. Mwanasesere huyo alitengenezwa mwaka 1959 yaani karibu miaka 50 iliyopita na kampuni ya Mattel. Utengenezaji wa  mwanasesere huyo ulifanyika kwa kuiga sura ya mwanamke mmoja kahaba raia wa Kijerumani. Miaka miwili baada ya kutengenezwa mwanasesere Barbie, rafiki yake wa kiume kwa jina la Ken naye pia aliingia sokoni ili kuwafunza watoto wa kike tabia ya kuwa na marafiki wa jinsia tofauti yaani wanaume na uhusiano usiojali maadili. Mwanasesere Barbie unawafunza mabinti wa Kimagharibi kuwa kila mmoja wao anahitaji kuwa na rafiki wa kiume na kuwafunza namna gani wanapasa kuamiliana na marafiki zao wa kiume wakati wa mapumziko, wakiwa kazini, shuleni, na wakati wa faragha.

Kwa sasa kila mwaka hufanyika maonyesho mawili ya mitindo na mavazi  kwa ajili ya misimu ya joto na baridi kali kwa jina la Barbie na Ken  ambapo nguo hizo huuzwa kwa familia za Kimagharibi kwa bei ya juu. Wanaserere hao wamekuwa kigezo na mizani ya kupimia uzuri na urembo wa watu katika familia na jamii za Magharibi. Kwa mujibu wa vigezo vilivyowekwa na wabunifu wa mwanasesere Barbie inaelezwa kuwa, kujikondesha kumetambuliwa kuwa ni sawa na kuwa na mwili maridadi, na unene unatajwa kuwa ni sawa na kuwa mwili usiofaa; kwa msingi huo wasichana na wanawake wa nchi za Magharibi hujitia katika mashaka makubwa kupita kiasi ya kujikondosha kwa kutumia njia mbalimbali na kufuata vigezo vya mwanasesere Barbie wakishindana na wanawake wenzao kwa shabaha ya kuwashawishi wanaume au kuwavutia waume zao. Kampeni na propaganda kubwa zinazofanywa katika uwanja huo zimewaelekeza wanawake wengi wa Kimagharibi na maeneo mengine ya dunia katika programu ngumu kupita kiasi za kujikondesha kwa kufuata utaratibu maalumu wa chakula kwa ajili ya kupunguza uzito (diet) na kutumia gharama kubwa ya fedha na pengine upasuaji wa miili yao. Wakati mwingine wanaume huwataka wake zao kuwa na miili kama ule wa mwanasesere Barbie la sivyo suala hilo huzusha matatizo ndani ya familia na hata kusababisha talaka.

Zaidi ya hayo ni kuwa kwa miaka kadhaa sasa kizazi kipya cha mwanasesere Barbie kimeingia katika dunia ya watoto. Wanasesere hao walitengenezwa mwaka 2001 na kuingizwa sokoni wakiwa katika maumbo mbalimbali na sura zenye vipodozi chungu nzima. Tofauti ya wanasesere hawa na wale wa kizazi kilichotangulia ni kuwa, mbali na kuwa na maungo yanayoshawishi na kuchochea zaidi hisi za ngono huwa na mavazi yasiyochunga heshima na maadili yakilinganishwa na mavazi ya wanasesere wa zamani. Wanasesere hao huvaa sketi fupi, soksi ndefu za nyavunyavu huku nyuso zao zikiwa zimepakwa vipodozi kupitia kiasi.

Kwa utaratibu huo japokuwa Barbie ni mwanaserere tu lakini kifaa hicho cha kuchezea kimebadili vigezo na mwenendo wa mwanadamu wa Kimagharibi na mwanasesere huyo ameweza kuwa na ushawishi na taathira kubwa katika   harakati, mienendo na fikra za familia katika ulimwengu wa Kimagharibi na katika pembe nyingine za dunia.

Wanasesere wengine kama Spider Man, Batman, Shrek na kadhalika pia wanawaingiza watoto katika dunia ya ndoto, ukatili na utumiaji mabavu. Vifaa hivyo vya kuchezea watoto si tu kuwa huwafanya watoto wa kiume kupenda kutumia mabavu na ukatili, bali humfunza mtoto vitendo visivyokubalika katika jamii kama kuuwa, kutekanyara, wizi na jinai na hivyo kuacha taathira kubwa katika mahusiano yake ya kijamii. Kwa msingi huo shakhsiya ya baadaye ya watoto na vijana hujengwa kwa mujibu wa vifaa na suhula zao za kuchezea.

XXXX

Michezo huunda sehemu nzuri zaidi ya maisha ya watoto; kwa msingi huo kuna udharura wa kuwa makini katika kuchagua vifaa bora na vinavyofaa kwa ajili ya michezo ya watoto. Chunguzi mbalimbali zinaonyesha kuwa, shakhsia ya mwanadamu hujengwa kwa vifaa vya kuchezea watoto na michezo mingine ya ya kipindi cha utotoni. Suhula za michezo ya watoto zinapasa kuwa zenye kuinua uwezo wao wa kiakili na mbali na kumfurahisha na kumpa burudani, vifaa hivyo vinapasa kumhimiza mtoto kufanya mambo mazuri na kulea vipawa na uelewa wake.  Wataalamu wa malezi wanaamini kuwa, vifaa vya kuchezea watoto vinapasa kuwa sababu ya kumkurubisha mtoto kwenye uhakika wa mambo na utamaduni wa jamii na si kumfanya aishi kwenye. Ni wazi kuwa mtoto mwenye umri wa chini ya miaka minne hana haki ya kuchagua peke yake na hununua vifaa vya michezo kwa mujibu wa uamuzi wa wazazi. Ni vifaa hivi vya michezo anavyonunuliwa na wazazi ndivyo hutayarisha uwanja mzuri wa mtoto kuchagua vifaa kama hivyo baada ya kuwa na umri wa juu ya miaka mine na kutumia vifaa kama hivyo anapoingia katika umri wa barobaro. Hata hivyo utumiaji wa vifa vya michezo kama mwanasesere Barbie sit u kwamba kunaharibu malezi ya mtoto ndani ya nyumba bali pia humpa kigezo kisichofaa na malezi yasiyochunga stara na heshima.

Mfumo wa utoaji elimu usiofaa ni moja ya masuala yanayotishia kusambaratisha misingi ya familia katika jamii ya Kimagharibi. Weledi wengi wa masuala ya Magharibi wana wasiwasi kutokana na kukosekana mfumo sahihi wa kielimu. Mfumo wa kielimu wa Magharibi uliojengeka juu ya fikra za kiliberali na kibepari unawafanya watoto wadogo wakabiliane uso kwa uso na wazazi wao katika masuala mengi. Vilevile katika baadhi ya shule za nchi za Kimagharibi na zile zinazoiga kibubusa sera zao, mafunzo ya ngono na uhusiano wa mke na mume yamekuwa yakitolewa katika shule za watoto wadogo tena kwa njia ya wazi na kwa kutumia maneno yasiyoendana na umri wao. Suala hilo linafanyika ili kuwaondolea vijana haya ya kujiingiza au kuzungumzia masuala ya ngono na kujamiiana bila ya kizuizi chochote.

Ala kulli hal, inatupasa kutambua kwamba elimu na malezi ya watoto ndio msingi wa maisha yao ya baadaye. Watoto hupitia awamu mbalimbali za mabadiliko ya kimwili na kifikra na mabadiliko kama hayo yumkini yakawa sababu ya kuchanua vipawa vyao na kujenga shakhsia sahihi na salama au kuwatumbukiza watoto hao katika dimbwi la otovu wa maadili na maangamizi kama inavyoshuhudiwa sasa katika baadhi ya nchi za Magharibi na nchi nyingine zinazoiga na kufuata sera zao za kimaisha na kimalezi. 

XXX

Wapenzi wasikiliza muda wa kipindi chetu cha leo umefikia ukingoni. Tukutane tena wiki ijayo katika kipindi kingine kwa majaaliwa ya Mola. kwaherini

Sauti na Video

Andika maoni


Msimbo salama (Security code)
Upyesha (Refresh)