Tovuti Hii Imefungwa. Tumehamia Kwenye Parstoday Kiswahili
Jumapili, 28 Aprili 2013 17:59

Matatizo ya Familia katika Nchi za Magharibi (19) + Sauti

Matatizo ya Familia katika Nchi za Magharibi (19) + Sauti

(Sikiliza)

Hamjambo wapenzi wasikilizaji na karibuni kuwa nami tena katika sehemu nyingine ya kipindi cha Mgogoro wa Familia katika nchi za Magharibi. Kama bado mnakumbuka katika kipindi cha wiki iliyopita tulizungumzia athari mbaya za filamu za katuni zinazotengenezwa katika nchi za Magharibi na matumizi mabaya na yasiyofaa ya simu za mkononi kwa taasisi ya familia. Kipindi chetu cha wiki hii kitaendelea kujadili athari mbaya za simu za mkononi katika kudhoofisha familia. Karibuni.

XXXX

Hii leo watu wengi katika jamii hawajui jinsi ya kutumia vyema na ipasavyo zana mbalimbali za elektroniki kama simu za mkononi, suala ambalo hutayarisha mazingira ya kutokea ufuska na ufisadi wa kimaadili. Miongoni mwa matumizi mabaya na yasiyofaa ya simu za mkononi ni kusumbua watu wenye simu kama hizo, kutuma ujumbe wenye vitisho au masuala yasiyokuwa ya kimaadili, kutazama au kutuma filamu za ngono na uchi, kuwapiga watu picha wakiwa katika hali zisizofaa na kuzisambaza kwa watu wengine na kadhalika. Tatizo hilo linakuwa kubwa zaidi kwa kuelewa kuwa, katika nchi nyingi zilizoendelea au zenye uchumi wa wastani mabarobaro wengi na hata watoto wadogo wanatumia simu za mkononi.

Moja ya maeneo yanayotumiwa vibaya na wenye simu za mkononi ni kusambaza taarifa za siri za watu, picha zao na hata vitisho kwa njia ya Bluetooth. Suala hilo huwa na taathira mbaya sana kwa mahusiano ya kifamilia. Kwa mfano usambazaji wa siri za wanandoa unaweza kusababisha hali ya kutoaminiana kati yao na kujenga uadui na hata kutengana.

Simu za mkononi pia zinatumiwa kwa wingi katika nchi mbalimbali hususan zile za Magharibi kwa ajili ya kusikilizia miziki isiyokuwa na stara, inayochochea hisia za matamanio ya ngono, ukatili na vitendo vya utumiaji mabavu. Wamagharibi wanadai kuwa kusikiliza miziki ya aina hii huwaondolea ghamu na msongo wa mawazo japokuwa ukweli wa mambo ni kinyume chake. Uhakika ni kuwa miziki kama hiyo si tu kwamba haipunguzi matatizo kama hayo bali huhatarisha usalama na uzima wa mwili na fikra na taratibu hudhoodhisha na hata kuteteresha misingi ya familia.

Wataalamu wa mambo wanasema kuwa muziki unaoambatana na midundo ya kuchochea hisia kama ile ya Rap, Metal na kadhalika huwa na taathira kubwa sana kwa wasikilizaji wake. Uraibu wa vijana kwa miziki ya aina hiyo huwasukuma katika matatizo mengi ya kijamii kama uraibu wa dawa za kulevya, msongo na msononeko, ufuska na pengine kujiua. Wakati huo mwili na fikra za vijana hukosa mlingano kutokana na kusikiliza miziki kama hiyo na kumuelekeza katika matatizo mengine mengi.

Baadhi ya miziki hiyo ya Kimagharibi husababisha msononeko na matatizo ya kiroho na kuzusha matatizo katika mfumo wa neva na fikra za mwanadamu. Suala hilo hupelekea kupungua umri wa msikilizaji wa miziki hiyo inayochochea hisi za matamanio na kusababisha mauti ya ghafla. Takwimu za kimataifa zinaonesha kuwa, kujiua katika nchi nyingi ndio sababu ya tatu ya vifo vya mabarobaro na vijana na sababu ya nane ya vifo kote duniani. Sehemu kubwa ya matatizo ya msononeko hususan kati ya vijana husabababishwa na miziki inayotoa nishati hasi na yenye muhtawa na mafundisho maovu, isiyokuwa na staha na inayozusha jazba na midadi kama miziki ya Metal, Rap Rock na miziki ya kuhuzunisha sana na kutia simanzi au kukatisha matumaini ambayo humuelekeza mwanadamu na msikiliaji wake katika kujiua. Watu wanaosikiliza miziki kama hii kwa kawaida huwa hawajumuiki na wanachama wengine wa familia zao na hupendelea kujitenga na pengine kuwadhuru wazazi na marafiki zao wenyewe. Matatizo na maradhi yanayosababishwa na miziki kama hiyo pia yanaweza kuisababishia familia gharama kubwa mno za matibabu yake.

XXXX

Muziki kama ule wa Rap kwa kawaida husikilizwa kwa sauti ya juu. Asilimia 80 ya miziki ya aina hii huhimiza ukatili na vitendo vya kutumia mabavu. Miziki hii ya Rap kwa kawaida huteka akili na bongo za wasikilizaji wake na kuwahimiza kupigana, kutumia mabavu na hata kuua. Kwa mfano tu siku kadhaa zilizopita vyombo vya habari viliripoti kuwa watu karibu elfu khamsini waliokuwa katika tamasha ya muziki wa Rap katika mji wa Melbourne nchini Australia walitekwa na kupatwa na jazba na midadi na kuanza kushambuliana ghafla wao kwa wao. Habari zinasema hadi polisi wanafika mahala hapo watu kadhaa walikuwa wameuawa kwa kudungwa visu, baadhi ya wanawake walibakwa na kunajisiwa na wengine wengi kujeruhiwa. Vilevile ripoti za kitaalamu zinasema kuwa, baadhi ya mapigano yanayotokea kwenye familia nyingi za Magharibi na kusababisha vifo vya wake au waume zao hutokana na kusikiliza mno miziki ya Rap au ile ya Metal inayosababisha matatizo ya kiakili na kinafsi.

Utafiti uliofanywa na Dakta Ralph J. Di Clemente wa Marekani kuhusu taathira za muziki wenye midundo inayoamsha hisi za kutumia mabavu na ukatili na ile inayochochea hisi za matamanio ya ngono kama ile ya Rap na Metal kwa vijana 522 wa Kimarekani, ulibaini kuwa vijana wengi wanaosikiliza kwa wingi miziki ya aina hii huwa na mienendo ya kikatili na utumiaji mabavu katika maisha yao. Uhakiki huo umeonesha kuwa vijana hawa hupenda kuwadhuru wazazi wao, walimu na hata wanafunzi wenzao. Mbali na hayo huwa na hamu ya kutumia vileo na kasumba kama pombe, bangi, dawa za kulevya na kujitumbukiza kwenye masuala ya ngono haramu.

Moja ya madhara makubwa ya kusikiliza miziki ya aina hii ni madhara yake makubwa kwa mfumo wa neva wa mwili. Sauti za miziki hiyo ambazo huteka na kudhibiti neva huvuruga taratibu nguvu na uwezo wa akili na fikra za mwanadamu na kumfanya mtu apatwe na wendawazimu na matatizo ya kinafsi. Ni wazi kuwa mtu anayepatwa na maradhi hayo hawezi kutekeleza vyema majukumu yake ya kifamilia na suala hilo husababisha matatizo na dosari katika mahusiano yake na mke, wazazi na watoto wake.

Dakta Arnold Friedmany ambaye ni tabibu katika Hospitali ya New York na Mwenyekiti wa Kliniki ya Matatizo ya Kichwa amethibitisha kwa kutumia chombo cha elektroniki kinachoainisha mawimbi ya ubongo na utafiti wake mwingine kwa maelfu ya wagonjwa waliokwenda kwake kwa ajili ya kutibiwa kwamba, moja ya sababu ya uchovu wa kifikra na kinafsi na maumivu ya misuli ya neva ni kusikiliza miziki yenye midundo inayochochea hisi za ukatili na utumiaji mabavu.

Kwa ujumla hali ya sasa ya dunia ya Magharibi inadhoofisha mno misingi ya familia. Wepesi wa vijana na watu wazima kukutana na kuwa na mawasiliano na mahusiano na mtu mwenye jinsia tofauti yaani wepesi wa mahusiano haramu baina ya mwanaume na mwanamke umezidisha pia ufuska na mporomoko wa maadili katika nchi hizo na zile zinazoiga na kufuata mtindo wao wa kimaisha. Utumiaji usiofaa wa zana za teknolojia ya kisasa kama kumpyuta na simu za mkononi zinazotuma na kupokea picha na miziki isiyokuwa na staha na yenye madhara kwa roho na mwili wa mwanadamu vimewafanya watu wengi katika nchi za Magharibi na nchi nyingine za dunia kuwa watu wanaopendelea kujitenga na wenzao na kukaribia zaidi hatari ya kutumbukia kwenye ufuska na matatizo mengine ya kinafsi.

Kwa upande wake Uislamu umehimiza mno kazi yoyote yenye faida kwa mtu binafsi, familia na jamii na kuharamisha amali yoyote ile yenye taathira mbaya au madhara kwa mwili na roho ya mwanadamu. Kwa msingi huo ni wajibu wa wazazi wawili kutambua vyema mazingira yanayotawala nyumba, harakati za watoto wao na hata nyenzo na zana wanazowatayarishia watoto wao kwa ajili ya kazi zao za kila siku. Wanapaswa kuwaelimisha watoto wao kuhusu hatari za utumiaji mbaya wa zana za mawasiliano na kuzuia mapema uwezekano wa watoto hao kutumbukia katika janga la ufuska na matatizo mengine ya kimwili na kinafsi.

XXXX

Wapenzi wasikilizaji tuna mengi ya kusema, lakini muda hauturuhusu kuendelea mbele. Basi hadi juma lijalo panapo majaliwa yake Mola Karima, nawaageni nikiwatakia kila la kheri maishani, kwaherini.

Sauti na Video

Andika maoni


Msimbo salama (Security code)
Upyesha (Refresh)