Tovuti Hii Imefungwa. Tumehamia Kwenye Parstoday Kiswahili
Jumatatu, 22 Aprili 2013 14:28

Matatizo ya Familia katika nchi za Magharibi (18)

Matatizo ya Familia katika nchi za Magharibi (18)

Hamjambo wasikilizaji wapenzi na karibuni tena kuwa nami katika dakika chache za kipindi cha Mgogoro wa Familia katika Nchi za Magharibi. Suala la kulea watoto hupewa daraja la kwanza na umuhimu mkubwa katika familia yenye uzima na mwelekeo sahihi. Katika familia kama hii wazazi wawili wanaoendesha familia kwa njia sahihi hufanya jitihada za kuwapa watoto wao nyenzo zote za malezi sahihi, burudani halali na kadhalika. Ni wazi kuwa baada ya mtoto kuingia katika mazingira ya familia wazazi wawili hufanya kila wawezalo kumhami na kutayarisha mazingira bora zaidi ya kukua kwake na kufikia daraja za juu za kiroho, kielimu na kiafya. Wataalamu wanaamini kuwa utumiaji wa zana sahihi za mawasiliano ya umma na usimamizi sahihi wa wazazi huwa na taathira kubwa katika malezi ya mtoto. Hata hivyo baadhi ya bidhaa na nyezo za mawasiliano ya umma zisizokuwa salama zinazotumiwa na watoto katika dunia ya leo zinatatiza sana kazi ya kutoa elimu na malezi bora kwa watoto. Katika kipindi chetu cha leo tutajaribu kutupia jicho athari mbaya za utumiaji wa baadhi ya katuni, simu za mkononi na miziki isiyofaa kwa watu wa familia hususan watoto wadogo na vijana katika nchi za Magharibi. Ni matumiani yangu kuwa mtaendelea kuwa kando ya redio zenu kusikiliza niliyokuandalieni.  

XXXX

Katuni ni miongoni mwa matunda ya kuvutia ya filamu ambayo si tu kwamba yanawavutia mno watoto bali hata watu wazima. Filamu za katuni zinaweza kuwa na mchango muhimu sana katika shakhsia ya baadaye na watoto wanaozitazama. Filamu hizo za katuni pia huwa na taathira kubwa kwa roho na nafsi ya watoto wadogo. Watafiti wanasema kuwa, watoto wenye umri wa miaka mitatu hadi mitano huwa watazamaji tu na kwa kawaida hawana uwezo wa kiakili wa kuweza kumaizi baina ya mambo mabaya na mazuri. Kwa msingi huo kila wanachokiona hukiamini na kukitambua kuwa ni uhakika na kweli. Kwa msingi huo filamu za katuni huwaathiri mno watoto na taratibu hubadilisha misingi ya kiutamaduni na kimalezi ya watoto hao. Jambo la kusikitisha sana ni kuwa hii leo vitendo vya ukatili na utumiaji mabavu na hata masuala yanayowahusu watu wazima kama mambo ya ngono na kujamiiana yamekuwa yakijadiliwa na kuoneshwa katika filamu za katuni. Na kwa kuwa watoto wadogo hawana uwezo wa kutosha wa kuchambua na kunyambua mambo, filamu hizo za katuni zinaweza kubadilisha na hata kuharibu mustakbali wa watoto.

Mwanafalsafa mashuhuri wa Kigiriki Plato amesema: Wajibu wetu wa kwanza ni kuwachunguza na kuwasimamia watu wanaobuni hadithi na visa mbalimbali. Iwapo watabuni na kusimulia hadithi na visa vizuri tuvikubali, na kama watabuni na kuandika hadithi na visa vibaya tuvikatae." Plato anaendelea kusema kuwa: "Kina mama na walezi wa watoto wadogo wanapaswa kulazimishwa kusimulia visa na hadithi nzuri zilizokubaliwa na watu wenye hikima na busara. Tunapaswa kutambua kuwa malezi yanayoingia katika roho ya mtoto kupitia simulizi za visa na hadithi ni mengi na makubwa zaidi ya yale unayoyapata mwili wake kupitia njia ya michezo." Mwisho wa kunukuu.

Hadi kufikia muongo wa 70 na mwanzoni mwa muongo wa 90 filamu zote za kawaida na katuni zilizokuwa zikioneshwa kwenye televisheni ziliwekewa mipaka maalumu. Mipaka hiyo ni pamoja na kuainishwa filamu makhsusi kwa ajili ya watu wenye umri makhsusi na marufuku ya kutumiwa maneno yenye taathira hasi. Kwa mfano tu silaha za mauaji hazikuwa zikionyeshwa katika filamu hizo na wala maisha ya mtoto hayakuoneshwa kuwa hatari katika filamu hizo za katuni. Hata hivyo filamu za katuni zinazotengenezwa katika zama hizi zimejitenga kabisa na mazingira ya wakati huo na imekuwa vigumu mno kuweza kupata katuni isiyochafua umaasumu na roho safi na changa ya watoto wadogo. Filamu kama zile za Harry Potter na Narnia zinazamisha fikra na akili za watoto katika masuala ya hurafa na itikadi za kichawi huku katuni zinazotengenezwa katika zama hizi zikilenga zaidi akili na bongo za watoto.       

XXXX

Kwa sasa makampuni ya kutengeneza filamu yanatumia mamilioni ya dola za Kimarekani kwa ajili ya kutayarisha katuni za watoto. Filamu hizo haziwalengi watoto wadogo tu bali hata watu wazima. Mwaka 2009 kulitengenezwa filamu za katuni zilizotumia teknolojia makhsusi ya kumputa kwa ajili ya kusimulia hadithi na visa vya kale na vya sasa. Filamu hizo ni kama zile za Christmas Carol, Ponyo, Mary and Max na kadhalika. Mwenendo huo uliendelea mwaka 2010 kwa kutengenezwa filamu za katuni kama Toy Story 3, Shrek Forever After,  Ratatouille, Ice Age,  Barnyard, Madagascar,  WALL·E na Phenomenal.

Shakhsia zenye mvuto za nyota wa filamu hizo huwa mwakilishi na mhubiri wa utamaduni, mtindo wa maisha, thamani na itikadi za jamii ya Kimagharibi kote duniani ili ziwe kigezo cha kuigwa na walimwengu tangu zama za utotoni mwao. Matatizo ya kimaadili kama jinsi ya kuamiliana watoto wenye jinsia tofauti, mavazi ya shakhsia na nyota wa filamu hizo, densi zao, muziki unaotumiwa, mahusiano ya kimapenzi na ngono haramu ambayo ndio chimbuko la matatizo mengi ya sasa ya nchi za Magharibi na kupuuzwa kwa thamani za kimaadili ni miongoni mwa mambo yanayoonekana kwa wingi katika filamu hizo na ambayo yanateteresha sana nguzo na misingi ya familia. Kwa mfano tu vipengee vinavyoonesha hisi za mapenzi na ngono katika baadhi ya sehemu za filamu ya katuni ya Toy Story 3 vimeifanya filamu hiyo isioane na kiwango cha umri cha watoto wanaoitazama. Suala hilo limezidisha wasiwasi wa wataalamu wanaoamini kuwa, masuala hayo yanaelezwa mapema kwa watoto wadogo na wala hayalingani na umri wao. Wanasisitiza kuwa mandhari za filamu kama hizo zina taathira mbaya kwa roho, fikra na nafsi ya watoto.

Filamu ya Shrek Forever iliyotengenezwa mwaka 2010 inajadili na kuonesha masuala ya dunia ya watu wazima na hisi za mapenzi na kuchukiana kwa mume na mke, suala ambalo huwafanya watoto wadogo wanaoitazama wabalehe mapema. Uchunguzi wa maoni uliofanyika umebaini kuwa watu wazima waliotazama filamu hiyo ya katuni wanasema kuwa si sahihi kueleza masuala yanayohusiana na maisha ya mke na mume kwa watoto tena kwa kiwango hicho cha waziwazi kinachoonekana katika filamu hiyo.

Ala kulli hali, sanaa kama zile za filamu za katuni zinazotengenezwa katika zama hizi zina taathira kubwa katika kutoa mwongozo na mwelekeo kwa kizazi cha baadaye. Familia pia nazo zimeathirika mno na  filamu kama hizo na kwa msingi huo wataalamu wa elimu na malezi wanasisitiza mno juu ya udharura wa kutengenezwa athari na kazi za sanaa zinazofaa na kutoa mafunzo na utumiaji sahihi wa kazi hizo.  

XXXX

Wenzo mwingine wa mawasilino ya umma katika zama hizi ni simu za mkononi. Simu hizo zinaweza kuwa na mchango mkubwa katika ustawi na mawasiliano iwapo zitatumiwa ipasavyo. Ripoti iliyotolewa na Benki ya Dunia inasema kuwa idadi ya watu wanaotumia simu za mkononi imepanda kutoka watu bilioni moja mwaka 2000 na kufikia watu bilioni sita mwaka 2012. Jarida la Mawasiliano pia limeandika kuwa, idadi ya simu za mkononi zinazotumiwa yumkini ikazidi idadi ya jamii watu wote duniani hivi karibuni.

Watumiaji wa simu za mkononi wanapaswa kufaidika na matunda ya teknolojia hiyo mpya na wakati huo huo kujiepusha na matumizi yasiyofaa ya chombo hicho. Kama tunavyojua sote kutazama picha chafu au kusikiliza muziki usiofaa au kusoma makala zinazochochea uasherati na uzinzi huwa na madhara makubwa ya kiroho, kinafsi na kimwili ambayo iwapo hayatatibiwa mapema yanaweza kuwa na madhara makubwa kwa watumiaji wa chombo hicho. Madaktari wanasisitiza kuwa waraibu wa picha, makala na miziki kama hiyo inayochochea hisi za ngono husumbuliwa na matatizo ya kupumua, mapigo yasiyokuwa ya kawaida ya moyo, uchovu wa kifikra na kiakili, utukutu na kukosa utulivu, kupoteza hamu ya kula, kukosa usingizi na kadhalika.

Moja ya athari mbaya za miziki inayochochea hisi za kujamiiana na uasherati ni mporomoko wa maadili na akili katika ujudi wa mwanadamu. Mwanamuziki Theodor Adorno wa Kimagharibi anasema kuwa, miziki ya kisasa huwafanya watu wazima kuwa na mienendo ya kitoto na kuwaweka mbali na dunia ya fikra na kutafakari. Anaongeza kuwa muziki wa leo umekuwa bidhaa zinazomilikiwa na makampuni ya kibiashara. Wakati huo huo mwandishi Leon Rosseleson anaamini kuwa namna ya uzalishaji wa bidhaa fulani huainisha jinsi ya kutumia bidhaa husika. Anasema sekta ya uzalishaji wa miziki ya kisasa duniani ina aidiolojia na itikadi za mfumo wa kibepari.

XXXX

Wapenzi wasikilizaji muda wa kipindi chetu cha leo umemalizika. Tukutane tena juma lijalo panapo majaaliwa ya Mungu katika sehemu nyingine ya makala hii. Asanteni kwa kunitegea sikio na kwaherini.

Andika maoni


Msimbo salama (Security code)
Upyesha (Refresh)