Tovuti Hii Imefungwa. Tumehamia Kwenye Parstoday Kiswahili
Jumatatu, 15 Aprili 2013 13:58

Matatizo ya Familia katika Nchi za Magharibi (17) + Sauti

Matatizo ya Familia katika Nchi za Magharibi (17) + Sauti

Ni wakati mwingine umewadia wasikilizaji wapenzi wa kuwa nanyi katika kipindi hiki kinachotupia jicho mgogoro na matatizo ya familia katika nchi za Magharibi. Hii leo tovuti na mitandao ya intaneti imekuwa na taathira kubwa katika mahusiano ya watu, ada na desturi, utamaduni na hata silika na maisha ya watu wa familia. Katika kipindi chetu cha leo tutajaribu kutupia jicho athari za baadhi ya wavuti za intaneti kwa taasisi ya familia. Tafadhalini endeleeni kuwa nasi hadi mwisho wa matangazo haya.  

XXXXXX

Utumiaji wa wavuti na vituo vinavyokiuka maadili vya intaneti katika dunia ya leo umesababisha matatizo mengi kwa familia katika nchi mbalimbali. Moja kati ya taathira mbaya za kutembelea vituo vichafu na vyenye matangazo yanayokiuka maadili vya intaneti ni wanawake na wanaume kupatwa na uraibu wa kutembelea mara kwa mara vituo hivyo. Uraibu huo na kutekwa na tabia ya kutembelea vituo vyenye programu chafu na zinazokiuka maadili vya intaneti husababisha maradhi ya kiroho na kinafasi kwa wakati mrefu na kuzusha hitilafu za kifamilia na hata kuwa mbali na kujitenga na mke au mume ndani ya nyumba katika maisha ya kila siku. Dakta Destin Stewart ambaye ni mtaalamu wa elimu nafsi katika Chuo Kikuu cha Florida nchini Marekani anasema: Wagonjwa wengi wamekuwa wakinijia na sababu ya maradhi yao ya kinafsi ni uraibu wa waume au wake zao wa kutazama filamu na tovuti zenye vipindi na filamu chafu na zinazokiuka maadili."

Utumiaji wa mara kwa mara wa tovuti na mitandao ya intaneti yenye picha, filamu chafu za ngono na programu nyingine zinazokiuka maadili ni aina fulani ya uraibu. Wataalamu wa mwenendo wa mwanadamu wanasema kuwa waraibu wa tovuti za aina hiyo wameathirika kutokana na kupatwa na maradhi ya kutekwa na mitandao kama hiyo. Wanasema muathirika hutumbukia katika ada hiyo chafu kwa kutazama mara kwa mara picha, filamu na makala chafu na kujikuta ametekwa na hivyo hujaribu kujiridhisha kwa kutembelea mitandao hiyo. Tabia na ada hiyo chafu humuondoa mwathirika katika maisha halisi ya kawaida na kupunguza kwa kiasi kikubwa uhusiano wake na mke au mume wake. Tabia na uraibu huo wa mitandao na tovuti zinazoonesha filamu, picha na makala zinazozungumzia masuala ya ngono na utovu wa maadili huwa na taathira mbaya sana katika maisha ya kijamii na kazi za watu hususan wanaume ambao ndio wanaowajibika kutayarisha mahitaji ya familia zao. Wanaume ambao hutumia baadhi ya wakati wao kazini kwa ajili ya kutazama picha chafu au kutembelea tovuti zenye programu chafu anapogundulika hujikuta pabaya na wakati mwingine kukatwa mishahara au kufukuzwa kazi. Suala hili huacha taathira na uharibifu mkubwa kwa taasisi ya familia. Takwimu zinaonesha kuwa sababu ya talaka nyingi zinazotokea katika nchi za Magharibi ni uraibu wa wanaume au wanawake kwa tovuti chafu na mitandao ya ngono na uasherati na kupungua hisi zao za kubeba majukumu mkabala wa familia zao.

Matangazo ya kibiashara ya tovuti na mitandao ya intaneti huwa na taathira kubwa kwa familia sawa kabisa na yalivyo matangazo ya biashara ya runinga na televisheni. Matangazo hayo kwa kawaida, huibua haja bandia ndani ya familia na kuweka bidhaa zisizo za lazima mahala pa bidhaa muhimu na za dhaura za maisha ya kila siku. Matangazo hayo kwa kawaida huambatana na picha mbalimbali za kuwavutia watu kama fenicha zenye mandhari ya kupendeza, majumba ya fahari, maeneo maridadi na ya kuvutia na sura au maumbo ya wanawake warembo ambayo huwa kivutio cha watu wengi. Vitu hivyo ambavyo huvutia macho na wengi huwa wasila na wenzo wa kueneza utamaduni wa Kimagharibi na masuala yanayokiuka maadili katika  medani ya familia. Mbali na hayo matangazo hayo huwafanya watu watumie fedha nyingi katika masuala ya anasa na bidhaa zisizo za dharura badala ya kutumiwa katika masuala ya kimsingi.

Katika upande mwingine takwimu zinaonesha kuwa Wazayuni wana nafasi muhimu katika kuendesha vyombo vya habari kama magazeti, majarida na wavuti ambazo huchapisha, kuonesha na kutangaza filamu na picha za ngono na uasherati zinazoteteresha misingi na nguzo za familia na jamii nzima kwa ujumla.

    XXXXXX

Moja ya mambo yanayotumiwa mno katika mitandao ni kuchati kupitia vyumba makhsusi. Kitendo hicho kina manufaa na hatari zake kubwa hususan kwa vijana. Kuchati katika intaneti mara nyingi huzusha uhusiano haramu na pengine ufisadi wa kimaadili. Miongoni mwa taathira mbaya za uraibu wa kuchati katika vyumba vya intaneti ni kueneza filamu chafu na zinazokengeuka maadili, kusalitiana kwa wanandoa, kuzungumzia masuala ya binafsi baina ya watu wasiokuwa mume na mke, kuondoa haya na soni baina ya watu wanaoshiriki kwenye vyumba hivyo vya kuchati na kudhoofisha misingi ya familia. Takwimu pia zimeonesha kuwa wasichana wamekuwa wahanga wakubwa wa vyumba hivyo vya kuchati katika intaneti. Anga hiyo ya majazi ya intaneti pia imekuwa ikitumiwa na wahuni, ayari na mafasiki kuwinda wahanga wao hususan wale wanaotumia mtandao kwa ajili ya kutafuta washirika wao katika maisha ya ndoa, biashara, nafasi za kazi, elimu na kadhalika.

Kwa sasa kuna wavuti nyingi kama Google, Yahoo na kadhalika ambazo kila uchao zinaboresha uwezo wao wa kutoa huduma kubwa zaidi katika uwanja wa kuchati hususan kwa wale wanaotafuta wachumba na eti wapenzi hususan baada ya kuanzisha huduma ya kuzungumza uso kwa uso katika vyumba hivyo kwa kutumia picha na video. Uhusiano unaoanzishwa kupitia mitandao hiyo au "mapenzi ya kiintaneti" aghlabu huwa haudumu na husababisha matatizo ya kinafsi kwa wahusika wanaojikuta wamehadaiwa hususan wasichana wenye umri mdogo ambao baada ya tajiriba hiyo hukosa kabisa hamu ya kuolewa na kuanzisha familia.

Mara nyingine na kutokana na kutojua vyema malengo ya wahuni wa mtandaoni, watu wa familia hujikuta wakiweka picha zao za kifamilia katika mitandao hiyo ambazo baadaye hutumiwa vibaya. Suala hili huwa na matokeo mabaya mno ambayo mara nyingine huwa ni muhali kufidika. XXXXXX

Athari mbaya zaidi ya wavuti zinazoeneza picha na filamu chafu ni kudhoofisha maadili na kuhalalisha au kwa uchache kutetea maingiliano ya kujamiiana nje ya ndoa. Utafiti uliofanywa na Patricia Welch wa Marekani unasema kuwa kiwango cha uuzaji wa majarida ya picha chafu na utumiaji wa wavuti zenye filamu na picha za aina hiyo katika kila moja kati ya majimbo ya Marekani kina uhusiano wa moja kwa moja na idadi ya vitendo vya ubakaji na kunajisiwa watu katika majimbo hayo.

Vilevile mtafiti wa masuala ya jamii Andy Bennett anasema kuwa, kutazama wavuti zenye picha na filamu chafu huchochea hamu za kujamiiana ovyo, kudhihirisha matendo hayo ya uasherati kuwa ni jambo la kawaida, kupunguza haya na soni baina ya watu wanaotembelea wavuti hizo na matokeo yake ni kuwatumbukiza vijana katika maingiliano ya aina hiyo wakiwa bado na umri mdogo. Mtaalamu huyo anasisitiza kwamba, kukithiri kwa jambo hilo katika jamii za nchi za Magharibi kunatishia mno taasisi ya familia.

Madhara haya yote ya wavuti na mitandao yamezilazimisha baadhi ya nchi kubuni mbinu na mikakati ya kufunga wavuti kama hizo. Vilevile taathira hizo mbaya zinawalazimisha wazazi hususan mke na mume, serikali na hata asasi za masuala ya jamii kusimamia na kudhibiti ipasavyo utumiaji wa chombo chenye faida nyingi lakini hatari sana cha intaneti. Udhibiti huo unaweza kusaidia jitihada za kuzuia kusambaratika zaidi kwa familia mbalimbali na kuwafichua wahuni na majambazi wa intaneti ambao hutumia chombo hicho kwa ajili ya kuwinda wahanga wao.   

XXXXXX

Wapenzi wasikilizaji muda wa kipindi chetu cha leo umemalizika. Msikose kujiunga name wiki ijayo kusikiliza sehemu nyingine ya makala hii. Kwaherini.

Sauti na Video

Andika maoni


Msimbo salama (Security code)
Upyesha (Refresh)