Tovuti Hii Imefungwa. Tumehamia Kwenye Parstoday Kiswahili
Jumatatu, 08 Aprili 2013 17:39

Matatizo ya Familia katika Nchi za Magharibi (16)

Matatizo ya Familia katika Nchi za Magharibi (16)

Hamjambo wasikilizaji wapenzi wa Idhaa ya Kiswahili, Sauti ya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran. Natumai kuwa mko kando ya redio zenu mkisubiri kwa hamu kutegea sikio kipindi chetu hiki kinachochunguza na kujadili matatizo mbalimbali ya kiakhlaqi na kimaadili katika jamii ya Kimagharibi.

Moja ya mambo yanayoathiri uhusiano wa watu wa familia ni Intaneti na michezo ya kompyuta. Katika kipindi chetu cha 16 cha Matatizo ya Familia katika Nchi za Magharibi nitazungumzia taathira za jambo hilo kwa taasisi ya familia. Tafadhalini kuweni nami hadi mwisho wa kipindi. XXXXXX 

Leo hii teknolojia ya mawasiliano licha ya matumizi yake mbalimbali imeathiri pia maisha ya mwanadamu katika nyanja tofauti. Watu katika maeneo mbalimbali ya dunia hivi sasa wanaweza kuanzisha uhusiano kati yao na kupata habari na taarifa kwa urahisi kupitia Intaneti. Aidha utumiaji wa kompyuta na Intaneti kati ya watoto na vijana umeongeza zaidi. Mtandano na Intaneti imekuwa mithili ya kisu ambacho kinaweza kutumiwa vizuri na kutumiwa vibaya pia. Miongoni mwa matumizi mazuri au chanya ya Intaneti  ni pamoja na utoaji mafunzo, kufanya utafiti, kupashana taarifa na kupata kwa haraka habari muhimu. Kwa msingi huo tunashuhudia kuasisiwa mahusiano na mawasiliano baina ya watu wa tamaduni na mataifa mbalimbali katika Intaneti.

Hata hivyo teknolojia hiyo ya kisasa licha ya kuwa na faida chungu nzima inaweza pia kutumiwa vibaya. Kufumbiwa macho taathira hasi zinazosababishwa na Intaneti kunaweza kuisasababishia matatizo mengi taasisi ya familia. Moja ya athari hizo haribifu ni kuongezeka mikwaruzano kati ya vijana na familia.  Kizazi cha leo cha vijana kinapuuza thamani kuu za familia ukilinganisha na vizazi vilivyotangulia huku utumiaji wa kompyuta usiodhibitiwa ukiwatumbukiza watoto katika matatizo mengi ya kimwili na kinafsi.  Mazoezi ya viungo na harakati za kijamii ni mambo yenye udharura kwa afya na uzima wa watoto. Kwa msingi huo iwapo mtoto atatumia muda mwingi katika programu mbalimbali za mitandao na kompyuta hatokuwa na fursa ya kujishughulisha na michezo na harakati nyingine zenye umuhimu kwa mwili na afya yake kwa ujumla. Leo hii Kunenepeana kupita kiasi (Obesity) kunakosababsihwa na harakati chache miongoni mwa watoto ambao wanajishughulisha sana na michezo ya kompyuta na kadhalika kunaongezeka kwa kasi kubwa.

Dakta Oded Bar-Or, Mkurugenzi wa Kitengo cha Lishe ya Watoto katika Hospitali ya Hamilton huko Canada anasema kuwa: Kutokuwa na harakati za kimwili na michezo kunaweza kuwa chanzo hatari kwa watu wazima khususan watoto na kusababisha maradhi mbalimbali kama ya moyo, kuongezeka  shinikizo la damu, maradhi ya mifupa n.k.

Utumiaji wa Intaneti ni kazi inayochukua muda, jambo ambalo linaweza kupunguza muda wa watu wa familia kuwa pamoja. Mbali na hilo utumiaji wa tovuti ambazo muhtawa na yaliyomo hayaoani na umri wa mtoto husabababisha mabishano na mivutano kati ya wazazi na watoto. Wazazi huhofia kuwa Intaneti humshughulisha zaidi na kumtenga mtoto na masuala ya kimasomo na ya kijamii. Kiujuma ni kuwa moja ya taathira haribifu za Intaneti kwa watoto ni kuwa huwaweka mbali watoto na masuala yenye manufaa na ya kawaida yanayolingana na umri wao.

Athari nyingine haribifu ya Intaneti kwa wanachama wa familia hususan watoto ni kuwatia kasumba ya tovuti na kuwafanya waraibu wa Intaneti. Kama ambavyo Intaneti huwafanya watoto watekwe haraka na michezo ya Intaneti na hata kuwatumbukiza katika tovuti chafu na zinazochochea uasherati.

Utumiaji wa Intaneti usiodhibitiwa pia unaweza pia kuwa na madhara makubwa kwa mwenendo wa vijana. Pale kijana anapoghiriki kwenye utumiaji wa Intaneti, hamu yake ya kuwa karibu na wenzake hupungua pia kwa kiwango kikubwa. Profesa San Keoly ambaye ni mtaalamu wa elimu nafsi wa Kikorea baada ya utafiti mkubwa kuhusu wanafunzi 435 amefikia natija kwamba: Asilimia 11 ya vijana wamekumbwa na kasumba na uraibu mkubwa wa Intaneti. Anasema: "Vijana wanaotazama sana Intaneti wamekuwa wakipatwa sana na matatizo ya mfadhaiko na msononeko. Mfadhaiko huo unatokana na kughiriki sana katika tovuti na Intaneti.  XXXXXX

Athari nyigine haribifu ya Intaneti ni mikwaruzano kati ya wanachama wa familia hususan mke na mume. Intaneti inaacha taathira hasi kwa utendaji wa familia. Wale wote wanaotumia tovuti na mitandano ya Intaneti kupindukia hupoteza muda mwingi katika suala hilo jambo ambalo huwa na taathira mbaya katika utendaji wao wa kazi za kijamiii na kifamilia. Matokeo ya jambo hilo ni kuwa mume hughafilika kuwa ana wajibu kwa mkewe na wanawe. Kitendo hicho huzusha mivutano ya kifamilia, kuibua pengo kati ya wanandoa na kuathiri anga ya upendo ndani ya familia. Kwa mujibu wa utafiti uliofanywa kuhusu suala hilo, asilimia 50 ya watu wa familia kadhaa wamekiri kuwa mawasiliano baina yao hupungua sana pale wanapojishughulisha na masuala ya Intaneti huku asilimia 41 wakikiri kwamba katika kipindi hicho hujifunza mienendo na masuala yaliyo dhidi ya mahusiano ya kijamii. Ni wazi kuwa kutumia Intaneti kwa muda mrefu huathiri uhusiano wa mke na mume na kusababisha ufa mkubwa kati ya wawili hao ambao unaweza kupunguza zaidi muda wa kuwa pamoja wanandoa hao sambamba na kupunguza uhusiano wa kimapenzi baina yao. Miongoni mwa bidhaa za vyombo vya mawasiliano ya umma ambao zina taathira kubwa katika utendaji na mienendo ya familia ni michezo ya Intaneti. Moja ya athari nyingi hasi za michezo hiyo ni utumiaji mabavu unaoshuhudiwa ndani yake. Utafiti unaonyesha kuwa athari hasi za kutazama picha zenye kuonyesha matukio ya utumiaji nguvu na ukatili husalia katika ubongo kwa masaa kadhaa. Miamala hiyo ya kimabavu na vitendo vya kikatili hudhihiri kwa urahisi katika familia. Wataalamu wa elimu nafsi wameonyesha katika utafiti wao kuwa michezo ya vitendo na harakati za utumiaji mabavu ya Intaneti huathiri vibaya bongo na akili za watazamaji hususan watoto na vijana. Kwa msingi huo moja ya sababu za kuongezeka mivutano ndani ya familia ni michezo ya ukatili na vitendo vya kutumia mabavu ya Intaneti. Jarida la kila mwezi la Reader’s Digest limeandika kuwa: “Sasa hatuna tena michezo ya chemsha bongo na burudani. Michezo ya Intaneti imegeuka na kuwa chombo cha kujifunzia mambo mabaya na tumekuwa tukiwafundisha watoto wetu bila ya kujua hisi anayoipata mtu kwa kumfyatulia risasi mwenzake. XXXXXX

Earl Hunsinger mtafiti wa Kimarekani anaamini kuwa viongozi wa sekta ya michezo ya Intaneti hawako tayari kivyovyote kukiri kuwa michezo hiyo ina maafa makubwa kutokana na faida nono wanayopata katika michezo hiyo. Serikali za nchi za Magharibi pia zinatumia michezo ya Intaneti kama wenzo na silaha katika vita baridi dhidi ya nchi nyinginezo. Michezo hiyo huonyesha wazi utamaduni na maadili ya Kimagharibi na kuipigia debe Marekani pamoja na kudhihirisha utamaduni wa nchi hiyo kuwa ni wenye thamani bora zaidi. Michezo hiyo ya Intaneti huwachochea wachezaji wake kuwa wanaweza kuwashambulia wenzao na kuwaangamiza kabisa kwa kisingizio cha kumuokoa mwanadamu.

Wataalamu wa elimu nafsi wana wasiwasi juu ya kupenya na kuingia vigezo vya mienendo ya kikatili ya Kimarekani katika familia mbalimbali. Hii ni kwa sababu watoto na vijana huiga vitendo vya wanajeshi wanaopenda kutumia mabavu wa Marekani. Hadi sasa kumetokea maafa makubwa katika jamii za nchi za Magharibi kutokana na taathira mbaya za michezo hiyo ya kikatili. Kwa msingi huo matumizi yasiyo sahihi ya Intaneti na michezo yake yamebadili mtindo wa maisha ya watu, suala ambalo ni moja ya malengo ya mfumo wa ubepari wa kuubadili utamaduni wa nchi mbalimbali na kuufanya sawa na ule wa maisha ya Kimagharibi. Suala la kubadili kigezo cha uhusiano na mwenendo wa kifamilia linapewa umuhimu mkubwa katika mikakati hiyo ya kutaka kubadilisha utamadumi wa dunia na kuufaanya sawa na ule wa Kimagharibi. Moja ya nyenzo zinzotumiwa na Wamagharibi kwa ajili ya kutimiza malengo yao ni kusambaza bidhaa chafu na zisizofaa katika familia mbalimbali. Kwa msingi huo udhibiti wa Intaneti na kuwafundisha watoto matumizi sahihi ya chombo hicho kunaweza kusaidia sana juhudi za kupunguza taathira mbaya zinazotokana na tovuti na Intaneti.

 Kwa ujumla mke na mume wanapaswa kuwa macho sana katika kutumia tovuti na Intaneti nyumbani. Katika dini ya Kiislamu wazazi wawili hususan baba wamepewa jukumu kubwa la kusimamia na kulea vyema watoto. Aya ya Sita ya Suratu Tahrim inasema: Enyi mlioamini! Zikingeni nafsi zenu na ahli zenu (familia) na moto ambao kuni zake ni watu na mawe..) Hivyo basi familia hususan wazazi wawili wanaweza kutekeleza vyema majukumu yao katika medani ya utamaduni kwa usimamizi mzuri wa pande zote na kuinua kiwango cha maarifa ya familia husika.  XXXXXX

Wapenzi wasikilizaji kipindi chetu cha wiki hii kinaishia hapa. Ni matumaini yetu kuwa mumefaidika na niliyokuandalieni kwa leo. Basi hadi wiki ijayo na katika kipindi kingine nakutakieni kila la kheri. Kwaherini.

Andika maoni


Msimbo salama (Security code)
Upyesha (Refresh)