Tovuti Hii Imefungwa. Tumehamia Kwenye Parstoday Kiswahili
Jumapili, 31 Machi 2013 21:43

Mgogoro wa Familia katika Nchi za Magharibi (15)

Mgogoro wa Familia katika Nchi za Magharibi (15)

Hamjambo wapenzi wasikilizaji na karibuni kuwa nasi tena katika makala hii inayotupia jicho mgogoro wa familia katika nchi za Magharibi. Kama bado mnakumbuka katika kipindi cha wiki iliyopita tulizungumzia taathira mbaya za vyombo vya habari kama redio na televisheni kwa taasisi ya familia katika nchi za Magharibi na kusema kuwa aghlabu ya vyombo hivyo vya habari vimeweka ukatili na utumiaji mabavu sehemu ya upendo, mahaba na udugu katika familia. Kipindi chetu cha leo kitaendelea kuzungumzia taathira mbaya za vyombo vya habari na matangazo yao hususan filamu za zisizokuwa na heshima wala murua kwa familia. Karibuni.  XXXX

Familia ni nguzo kuu ya jamii sahihi, yenye utanashati na mlingano. Katika zama hizi familia inahujumiwa na kukabiliwa na mashambulizi makali ya kiutamaduni, kijamii na kisiasa kuliko wakati wowote mwingine. Ustawi na maendeleo ya vyombo vya mawasiliano ya umma umeleta mabadiliko makubwa ya kiutamaduni na mageuzi katika thamani zinazotumiwa katika jamii mbalimbali. Moja ya taathira mbaya za suala hilo ni kufifia na kufubaa thamani za familia na kuyumbayumba msingi wa taasisi hiyo muhimu katika jamii. Ongezeko la talaka katika jamii mbalimbali ni kielelezo cha kuyumba na mpasuko mkubwa wa jamii ambao daima hufuatiwa na matatizo mengine kama umaskini, uhalifu na ongezeko la watoto wasio na walezi au wasimamizi.

Weledi wa masuala ya jamii wanaona kuwa bidhaa za kazi za kiutamaduni na sanaa za vyombo vya habari na mawasiliano ya umma katika nchi za Magharibi ni miongoni mwa sababu za kushadidi mgogoro wa familia. Jarida la Economist linalochapishwa London nchini Uingereza limeandika kuwa, moja ya njia za kuziunganisha tamaduni mbalimbali na kuanzisha utamaduni wa aina moja unaofuatiliwa na nchi za Magharibi ni kuondoa mipaka ya kiakhlaki na kimaadili.

Dakta Shafii Sarustani ambaye ni mtafiti wa Kiirani katika kitabu cha Utambuzi wa Sera za Kutetea Haki za Wanawake anaashiria mkakati huo wa nchi za Magharibi na kuchunguza ratiba na vipindi vya redio katika nchi za Marekani, Ufaransa na Ujerumani kisha anafikia natija kwamba, vipindi vya vyombo hivyo vya habari vinavyorushwa hewani katika nchi mbalimbali duniani vinateteresha na kuyumbisha misingi ya familia katika nchi hizo.

Kwa kawaida familia ndio taasisi ya kwanza kabisa ambayo huwa ya kwanza kulengwa kwa ajili ya kutokomeza thamani za kidini na kibinadamu. Hii ni kwa sababu ni wazi kuwa mabadiliko yoyote katika muundo, nafasi na wadhifa wa kila mmoja kati ya wanachama wa familia husababisha mabadiliko katika taasisi na viungo vingine vya kijamii. Moja ya sababu za kutokea mabadiliko, hitilafu na dosari katika familia ni uenezaji wa filamu zilizojaa hisi za ngono, kujamiiana na mandhari zisizo na staha katika jamii za nchi za Magharibi. Filamu za aina hii zimekuwa na taathira kubwa kwa vijana, watoto na hata wazazi wao yaani mume na mke. Miongoni mwa taathira mbaya za filamu kama hizi ni kuondoa hali ya kuaminiana kati ya mume na mke na kudhihirisha tendo la kujamiiana nje ya ndoa baina na mwanaume na mwanamke kuwa ni kitu cha kawaida. Mke na mume katika familia hizo huathiriwa na filamu hizo na kushibisha matakwa yao nje ya ndoa na hivyo kushindwa kutimiza wajibu wao au hata kuonesha mapenzi kwa wake au waume zao wa ndoa.

Kundi la Media Scope limefanya uhakiki kuhusu watu wanaojihusisha na vitendo vya kujamiiana nje ya ndoa na kuandika kuwa, filamu zisizo na staha na za matendo ya kujamiiana zinazooneshwa kwenye vipindi vya televisheni na runinga zimelifanya jambo hili kuwa kitu cha kawaida kwa watu wa familia akiwemo mume na mke.

Wanafikra na wasomi wengi wa nchi za Magharibi wanasema kuwa matatizo mengi yanayotokea hivi sasa ndani ya familia kwenye jamii za nchi hizo ambayo mwisho wake ni kusambaratika taasisi ya familia, chanzo chake ni filamu chafu na zisizo na stara zinazooneshwa kwenye vipindi vya televisheni au zile zinazotengenezwa Hollywood huko Marekani.

Mwandishi na mwanahabari wa Kimarekani Susan Faludi anasema kuwa matatizo mengi ya kijamii na mporomoko wa maadili ndani ya familia na katika jamii ya Marekani ikiwa ni pamoja na maingiliano kinyume na maumbile, kuavya mimba, kujiua na wanawake kuanza kulala kwenye maboksi ni matokeo ya taathira mbaya za vipindi vya televisheni na filamu za Hollywood. Mwandishi huyo anatoa mfano kwa kuashiria filamu kama "Today", "Sally Field" Fatal Attraction, Submission na Family Guy, na vipindi vya televisheni kama "Prime Time" na "Thirty Something."

Utengenezaji wa filamu chafu kama hizo na kuenea kwake katika jamii ya Marekani na nchi nyingine za Magharibi kumewafanya wanawake, wanaume hususan vijana watupilie mbali jitihada za kuanzisha familia sahihi na salama. Chris Hedges ambaye ni ripota na mhadhiri msaidizi wa chuo kikuu huko Marekani ameandika kuwa: "Filamu elfu 13 za pono na chafu hutengenezwa kila mwaka nchini Marekani na hakuna taasisi au jumuiya yoyote yenye jukumu na mamlaka ya kusimamia au kudhibiti filamu za aina hiyo." Ameongeza kuwa: "Kwa mfano kampuni ya General Motors inamiliki Direct TV ambayo kila mwezi hutengeneza picha milioni arubaini za vitendo vya ngono na vichafu na kuziuza kwenye nyumba za Wamarekani."   XXXX

Kama tulivyosema hapo awali kupungua kiwango cha ndoa ni miongoni mwa taathira mbaya za filamu chafu za vitendo vya ngono zinazooneshwa katika vyombo vya habari vya nchi za Magharibi. Hii ni kutokana na ukweli kwamba chini ya mafundisho ya uliberali, vijana hawana jukumu lolote na hushibisha matakwa yao ya kujamiiana eti kwa njia "huru". Kuhusu suala hilo mtafiti wa Kimagharibi Robert Johnson anaashiria nukta nyingine akisema kuwa: Moja ya taathira mbaya za kutazama filamu chafu za vitendo vya kujamiiana ovyo ni kwamba zinawaonesha wasichana taswira iliyopotoshwa kuhusu wanaume. Filamu hizo huwadhihirisha wanaume kama makatili na madhalimu ambao humtambua mwanamke kama wenzo na chombo cha kushibisha matamanio yao. Taswira na picha hiyo iliyopotoshwa ya mwanaume, anaendelea kusema Robert Johnson, mbali na kuwa yumkini ikawafanya wasichana wasiwe na hamu yaa kuolewa, vilevile inapunguza hali ya uaminifu baina ya wanandoa."

Moja ya vyombo vya mawasiliano ya umma vyenye nguvu na taathira kubwa ni televisheni za satalaiti. Kutokana na sifa zake za kipekee, televisheni za satalaiti huweza kurusha matangazo yake ya picha na sauti maeneo ya mbali ya dunia na kufikia idadi kubwa ya watu. Televisheni za satalaiti zinaweza kutumiwa kutangaza habari za matukio mbalimbali ya dunia, kuonyesha utafiti na chunguzi mbalimbali, kutoa mafunzo na kadhalika kama zinavyotumiwa kurusha hewani filamu chafu na kuchochea ngono na maingiliano haramu ya kujamiiana kwa kadiri kwamba wataalamu wa masuala ya jamii na utamaduni wameamua kuketi chini na kutafuta njia za kuikinga jamii hususan familia na taathira mbaya za filamu na matangazo kama hayo. Mhadhiri wa chuo kikuu wa Marekani Bi Sharon M. Kai anasema kuwa, kuoneshwa filamu kama hizo zinazokebehi na kufanyia maskhara thamani za kimaadili kunafanyika katika fremu ya kueneza utamaduni wa fikra za kiliberali. Hii ni kutokana na ukweli kuwa, moja ya malengo ya mfumo wa ubepari wa Magharibi ni kufifiza thamani za kifamilia katika jamii.

Dakta Muhammad Sadiq Homayun ambaye ni mhadhiri wa chuo kikuu nchini Iran anasema kuwa, filamu hizo za Magharibi ni kielelezo cha kigezo cha maisha ya familia za Magharibi. Lengo la filamu kama hizo ni kueneza utamaduni wa Kimagharibi na kuharibu thamani za kimaadili kama haya na kuwa na ghera baina ya wanawake na wanaume. Anaendelea kusema kuwa, filamu kama hizo hupunguza hisi za wivu na ghera baina ya wanawake na wanaume na mara nyingine kuwa sababu ya talaka na kutengana na mwishoni kusambaratika familia.

Katika upande mwingine mafundisho ya dini yamesisitiza mno juu ya udharura wa kuimarishwa misingi ya familia. Mafundisho hayo yanasisitiza kuwa uhusiano wa kimapenzi baina ya mke na mume unapaswa kufanyika tu ndani ya nyumba na katika fremu ya ndoa. Hii ni kutokana na ukweli kwamba dini inatilia mkazo kwamba uzima na usalama wa familia ndio uzima na usalama wa jamii nzima. Mafundisho ya dini ya Uislamu yanasema kuwa, siri ya kuimarika misingi ya familia ni kutiliwa maanani thamani na mafundisho ya kidini na kuheshimiwa thamani za kibinadamu. Mafundisho hayo yameainisha wadhifa na nafasi ya kila mtu ndani ya familia na kuwataka wanachama wote wa taasisi hiyo muhimu ya jamii kuheshimu mipaka na majukumu yake.   XXXXXX

Wapenzi wasikilizaji muda uliotengwa kwa ajili ya kipindi hiki umemalizika. Sina budi kuishia hapa kwa leo nikiwa na matumaini ya kukutana nanyi tena wiki ijayo katika sehemu nyingine ya makala hii. Asanteni kwa kunitegea sikio na kwaherini.

Andika maoni


Msimbo salama (Security code)
Upyesha (Refresh)