Tovuti Hii Imefungwa. Tumehamia Kwenye Parstoday Kiswahili
Jumatatu, 18 Machi 2013 16:27

Matatizo ya Familia katika Nchi za Magharibi (13)

Matatizo ya Familia katika Nchi za Magharibi (13)

Wasikilizaji wapenzi ni wasaa na wakati mwingine wa kuwa nanyi katika mfululizo huu wa kipindi cha 13 cha Matatizo ya Familia katika Nchi za Magharibi. Nadhani mnakumbuka kuwa katika kipindi cha juma lililopita niliashiria baadhi ya changamoto cha kimaadili za ulimwengu wa Kimagharibi na kusema kuwa zinaa, maingiliano ya watu wenye jinsia moja na ndoa zisizo za kawaida na zilizo nje ya fremu ya familia, zimeisababishia matatizo jamii ya kimagharibi na kudhoofisha taasisi ya familia. Katika kipindi chetu leo tutaanza kuchunguza baadhi ya matatizo ya kijamii na kiakhlaqi yanayoikabili jamii ya Kimagharibi. Natumai kuwa mtakuwa nami hadi mwisho wa kipindi, karibuni kunitegea sikio.

XXXX

Moja ya changamoto muhimu au kubwa zilizoitia jamii ya Kimgharibi katika matatizo chungu nzima ni kupungua ndoa na kuongeza kiwango cha talaka. Tumesema kuwa misingi inayotawala jamii ya Kimagharibi ni uhuru wa maingiliano ya ngono, ubinafsi na kupenda starehe na anasa. Fikra hizo zimewafanya watu katika ulimwengu wa Magharibi kukimbia majukumu, ndoa na suala la kuanzisha familia.

David H. Olson mhadhiri wa chuo kikuu nchini Marekani ameandika kuwa: "Katika jamii zetu watu wengi huoa kwa kuchelewa na wengi husema kuwa hawataki kukabiliwa na talaka kama ilivyowatokea wazazi, marafiki na jamaa zao. Jamii ya kimagharibi haina tena kigezo bora cha kufuata." mwisho wa kunukuu.

Hata mtaalamu wa masuala yanayohusiana na masuala ya uhusiano kati ya wanadamu katika jarida moja la Kifaransa alimuusia mwanamke mmoja aliyetaka kuolewa akimwambia afunge ndoa na mbwa kwa sababu mnyama huyo ndiye kiumbe pekee kitakachompenda zaidi kuliko nafsi yake mwenyewe.

Hii leo jamii ya mwanadamu inashuhudia ongezeko kubwa la kiwango cha talaka katika jamii za nchi zilizoendelea kiviwanda jambo linalotishia kuangamia taasisi ya familia. Marekani ni moja ya nchi zilizo na kiwango cha juu cha talaka duniani. Jarida la News Week linalochapishwa nchini Marekani limeandika kuwa kutolewa talaka nchini humo ni jambo jepesi mithili ya kukodi taksi, na licha ya kuwa baada ya talaka, mwanamke wa Kimarekani hudhani kuwa ana uhuru kushinda hata uhuru wenyewe, lakini kinyume chake mwanamke mmoja kati ya wanne wanaotalikiwa huangukia katika ulevi huku kiwango cha kujiuwa wanawake wa aina hiyo kikiwa mara tatu zaidi ikilinganishwa na wanawake walio na waume zao."

Pamoja na nchi ya Marekani kusumbuliwa na kasi kubwa ya kusambaratika kwa familia na idadi kubwa ya watu wanaodai talaka, serikali ya Washington imepasisha "sheria ya talaka bila ya sababu maalumu" yaani talaka kati ya wanandoa wawili bila ya tatizo lolote na inayotolewa kufuatia ombi la mmoja wao. Mwandishi mmoja wa Kimarekani ameandika kuwa: Sheria hiyo kiujumla inamuunga mkono mwanandoa yeyote anayedai talaka hata kama atakuwa ndiye mwenye makosa. Sheria hiyo ya talaka bila ya sababu au kosa lolote katika nchi za Magharibi imezifanya familia zitengane na kusambaratika kwa urahisi.

Sylvia Ann Hewlett, Mchumi na Naibu Mwenyekiti wa Taasisi ya Utafiti ya Umoja wa Mataifa ameandika kuhusiana na suala hilo kwamba: "Iwapo suala la talaka litazidi kurahisishwa siku baada ya siku, ni wazi kuwa wanaume  watakuwa wakiwaacha wake zao na kuamua kuoa wake wengine warembo zaidi na wakina mama watalikiwa ndio ambao hulazimika kuwalea watoto wao wenyewe katika familia yenye mzazi mmoja."

Idadi ya familia zenye mzazi mmoja imeongezeka sana kutokana na kuongezeka kiwango cha talaka katika nchi za Magharibi. Mwandishi wa Kimagharibi Dakta James C. Dobson ameandika kuhusiana na ongezeko la familia zenye mzazi mmoja katika jamii za Magharibi kuwa: " Idadi ya familia zinazotunzwa na kusimamiwa na mama asiye na mume au baba pekee zimeongezeka kwa asilimia 65. Hii leo watoto wasioishi na baba au mama  zao wanakabiliwa na taathira mbaya za maisha ya aina hiyo kuliko wakati mwingine wowote." Vilevile Cornel West mwandishi wa Kimarekani ameandika kuwa: Utafiti mwingi wa kustaajabisha umeonesha kuwa watoto wa wazazi waliotalikiana wanasumbuliwa na masuala mengi kama matatizo ya kiuchumi, kufeli masomoni na matatizo ya kisaikolojia na kinafsi. Anaongeza kuwa mbali na matatizo hayo, mara zote inapotokea talaka na familia kusambaratika waathirika wakubwa zaidi huwa ni watoto wa kike wa familia husika.

XXXX

Utoaji mimba ni vielelezo viingine vya kupuuzwa maadili katika ulimwengu wa Kimagharibi. Utoaji mimba na kuungwa mkono kitendo hicho na baadhi ya jamii za Kimagharibi, kunakofanyika chini ya anwani na nara potofu kama ile ya " haki ya mwanamke ya kumiliki mwili wake", ni aina fulani ya mauaji. Utoaji mimba ni kitendo kisicho cha kibinadamu na kinachopingana na maumbile ya mwanadamu. Vitendo hivyo visivyo vya kimaadili vimeongezeka sana katika baadhi ya nchi kama Marekani, Uingereza na Canada. Hali ya utovu wa maadili na akhlaki imekuwa mbaya sana katika nchi za Magharibu kuhusu suala la kutoa mimba na kuua vitoto vidogo kiasi kwamba sasa vijusi hivyo vinatumiwa katika masuala ya biashara.

Mwandishi William Gadner wa Canada ameandika kuwa: "Seli za mimba pevu au mtoto aliyeuliwa punde tu baada ya kuzaliwa ambazo ni salama na safi kabisa zinatumiwa kwa ajili ya uchunguzi wa kitiba. Iwapo kijusi hicho kingekuwa hai hadi mwisho, utumiaji wa seli na ngozi yake huwa na thamani kubwa kuliko seli nyinginezo."

Nukta ya kusikitisha zaidi hapa ni kuwa hii leo baadhi ya madaktari wa Ulaya wanatumia mafuta yatokanayo na vijusi hivyo yaani mimba zinazotolewa zikiwa changa, kutengenezea vipodozi ili kutajirika kibiashara. Profeda Chris Bagley ambaye ni Mhadhiri wa Chuo Kikuu na mmoja wa madaktari wanaounga mkono suala la utoaji mimba anatoa maoni yake ya kuogofya kuhusu namna mauaji hayo yenye malengo ya kibishara yanavyotendeka akisema kuwa: "Mafuta ya vijusi vinavyouliwa yanahitajika sana katika sekta ya vipodozi vya urembo." Tabibu huyo fidhuli anasema anatoa mimba pevu na kwamba ni aibu kutupa vijusi hivyo katika taka wakati vinaweza kutumiwa vyema zaidi.  Hayo yote ni kielelezo cha utovu maadili, akhlaqi na ukatili katika nchi za Kimagharibi kwa wanadamu walio hai lakini wadogo, ambao hufanyiwa mateso na ukatili huo na kuuawa.

Vitendo vya utoaji mimba vimeongezeka sana nchini Marekani. Mimba karibu milioni moja na laki tano hutolewa kila mwaka nchini humo. Mtafiti mmoja wa Kimarekani alifunga chombo cha kuchukua picha ndani ya mwili  wa mwanamke ambaye alikuwa akitoa mimba yenye umri wa wiki 12 na kutengeneza filamu aliyoipa jina la" Kilio cha Kimyakimya" ili kuonyesha ukubwa wa maafa ya kuuawa watoto wadogo bila ya sababu. Filamu hiyo iliyohuzunisha na kuathiri nyoyo za watu, ilikuwa ikionyesha namna kijusi kilichokuwa tumboni mwa mama kinavyokimbia chombo cha kuavya mimba huku sehemu za maungo ya kijusi hicho yakikatwa kimoja baada ya kingine na kutolewa nje ya mwili wa mama.

Mbali na hayo yaliyopita, dini ya kibinadamu ya Uislamu inakitambua kitendo cha utoaji mimba kuwa ni jinai na uhalifu mkubwa na mtu yeyote hana haki ya kuavya mimba bila sababu ya maana au kibali cha daktari kinachothibitisha kwamba maisha ya mama yatakuwa hatarini iwapo mimba hiyo haitatolewa. Dini ya Kiislamu inaona kuwa kijusi kilicho ndani ya tumbo la mama ni binadamu kama wanadamu wengine na kina haki ya hai na kuishi. Kwa sababu hiyo inawatia hatiani madaktari, wazazi na walezi kutokana na kutoa mimba bila ya kuwa na sababu ya kisheria. Kijusi pia kina haki zake kama walivyo watu wengine ambapo iliyo na umuhimu kuliko zote ni kuzaliwa kikiwa hai na kuwa mtoto. Hakuna mtu yeyote hata wazazi wa kijusi hicho kilicho tumboni aliye na haki ya kukiangamiza kiumbe hicho kisicho na hatia kama ambavyo hata baada ya kuzaliwa wazazi hawana haki ya kumdhuru mtoto huyo.

XXXX

Wakati uliotengwa kwa ajili ya kipindi hiki unaelekea ukingoni na kwa hivyo sina budi kukuageni nikiwa na matumaini ya kukutana nanyi tena katika kipindi kijacho. Kwaherini.

Andika maoni


Msimbo salama (Security code)
Upyesha (Refresh)