Tovuti Hii Imefungwa. Tumehamia Kwenye Parstoday Kiswahili
Jumatatu, 11 Machi 2013 13:46

Matatizo ya Familia katika Nchi za Magharibi (12) + Sauti

Matatizo ya Familia katika Nchi za Magharibi (12) + Sauti

Assalamu Alaykum wasikilizaji wapenzi wa Idhaa ya Kiswahili Sauti ya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran. Ni wakati na siku nyingine imewadia tena kujiunga nasi katika mfululizo huu wa vipindi vinavyozungumzia matatizo ya familia katika ulimwengu wa Kimagharibi. Nataraji kuwa mtakuwa nami hadi tamati ya kipindi karibuni.

Dini ya Kikristo ilikuwa ikidhibiti tamaduni zote za Magharibi hadi kabla ya karne ya 4 Miladia. Baada ya hapo pia nadharia nyingi zinanohusiana na thamani na masuala ya kiroho zilitolewa katika mafundisho ya kitabu cha Biblia. Hata hivyo kwa bahati mbaya utendaji  unaokinzana wa viongozi wa kanisa, kutotiliwa maanani neema za kidunia, ukosefu wa kitabu cha ufunuo na wahyi ambacho hakijapotoshwa na kutokuwepo sheria kamili za masiala ya kijamii katika Ukristo ilikuwa sababu iliyowafanya watu wengi wasiwe na imani na dini katika kubuni mfumo wao wa kimaadili huko katika nchi hizo za Magharibi. Matokeo ya hali hiyo ni kwamba wanafikra wa zama za Renaissance walifanya juhudi za kubuni mfumo wa kiakhlaqi na kimaadili usio na uhusiano na dini na hatimaye mfumo wa kimaadili wa kisekulari ukaasisiwa. Katika kipindi hiki cha 12 cha Matatizo ya Familia katika Nchi za Magharibi, nitaanza kuzungumzia changamoto za kiakhlaqi na kimaadili zinazoikabili jamii ya Magharibi ambazo zimeyumbisha vikali taasisi ya familia. 

XXXXX

Moja ya ishara za wazi za kutupiliwa mbali akhlaqi na maadili katika jamii za Kimagharibi ni kuenea zinaa na mahusiano haramu ya kujamiiana. Ulimwengu wa leo wa Kimagharibi umeporomoka sana kutokana na utovu mkubwa wa maadili na kuwa kwake mbali na akhlaki njema. Ustadh Murtadha Mutahhari mwanafikra mashuhuri wa Kiirani anasema kuwa ulimwengu wa Kimagharibi umepinduka na kugeuka nyuzi daraja 180 katika masuala yanayohusiana na maingiliano ya kujamiiana baina na mwanamke na mwanaume ikilinganishwa na miaka ya huko nyuma. Anaongeza kuwa hii leo suala la uhuru na kuondolewa vizuizi vyote linazungumziwa sana katika nchi za Magharibi huku wengi wakighafilika kwamba mkuki mkubwa zaidi uliosibu maadili na akhlaki katika nchi hizo ni huu uliopewa jina la uhuru."

Mtazamo usio wa kiakhlaki katika masuala mbalimbali katika jamii za Kimagharibi umefikia mahala ambapo wamiliki wa duka moja kubwa huko Ujerumani wamechukua hatua ya kustaajabisha wakati wa sherehe ya ufunguzi wa duka hilo na kutangaza kwamba wateja ambao watakwenda kwenye duka hilo kwa ajili ya kununua bidhaa wakiwa uchi wa kuzaliwa wanaruhusiwa kuchukua bure bidhaa zenye thamani ya Euro 270! Mwenendo kama huo huenda unatambuliwa na baadhi ya watu kuwa ni uhuru katika mwenendo wa mtu binafsi. Hata hivyo ukilitazama suala hilo kwa undani zaidi utaona kuwa watu wenye fikra alili na zenye maradhi wanakusudia kutumia vibaya uhuru ili kutia dosari misingi ya akhlaqi na maadili katika jamii. Kwa maneno mengine ni kuwa mwenendo kama pendekezo hilo lililotolewa na duka hilo au mingine yenye kufanana na huo inaonyesha kuwa jamii za Kimagharibi zinakabiliwa na changamoto nyingi za kiakhlaqi na kimaadili. Taathira za jambo hilo zinaweza kuzidisha migogoro ya kifamilia na maafa ya kijamii.

Baadhi ya wasomi wametaja sababu mbalimbali za kuweko mporomoko wa maadili katika nchi za Kimagharibi. Kuhusu suala la ufuska na kukithiri zinaa na maingiliano haramu ya kujamiiana katika nchi za Magharibi hususan Marekani, Mahmoud Hakimi mwandishi wa Kiirani ameandika katika kitabu alichokipa jina la "Magharibi Inaumwa" kwamba: Mambo matatu ya kishetani yameungana na kuzingira dunia yetu na kuanza kuwasha moto wa aina moja kwa ajili ya watu wa dunia hii. Kwanza ni fasihi chafu na iliyouchi iliyoanza kuenea kwa kasi ya kushangaza baada ya Vita vya Pili vya Dunia. Pili ni filamu zinazochochea hisia za ngono na uhuru wa zinaa na tatu ni kuporomoka kwa maadili kati ya wanawake kwa ujumla ambao unadhihiri na kuonekana zaidi katika mavazi yao au hata katika kutembea uchi na kuingiliana ovyo na wanaume." Mwisho wa kunukuu.

Kwa sasa jamii za Magharibi zinakabiliwa na matatizo mengi kutokana na mporomoko mkubwa wa maadili hususan katika suala la zinaa na kujamiiana ovyo. Moja kati ya madhara yaliyoikumba jamii hiyo ni kuenea kwa maradhi ya zinaa kama Ukimwi ambao umepewa jina la "Tauni ya Karne". Katika muongo wa 80 sambamba na kutangazwa habari kuhusu ugonjwa huo, duru nyingi za kitiba pamoja na fikra za walio wengi duniani ziliuhusisha ugonjwa wa Ukimwi (AIDS) na maingiliano kinyume na maumbile yaani kujamiiana baina ya watu wenye jinsia moja na hata baadhi ya duru za kielimu ziliamini kwamba maradhi hayo ni adhabu kutoka kwa Mwenyezi Mungu kwa wale wanaoingiliana kinyume na maumbile na kinyume na mafundisho ya dini. Wakati huo kifo cha mcheza filamu wa Kimarekani wa Holywood aliyekuwa na mashabiki wengi Rock Hudson, ambacho kilitokana na maradhi ya Ukimwi, kiliishtua sana jamii ya Magharibi. Wasiwasi mkubwa ulienea katika sehemu kubwa ya watu baada ya kueleweka kuwa wanaume na wanawake wanakabiliwa na hatari ya virusi vya ugonjwa huo kwa kiwango sawa, na watu wengi nchini Marekani na huko Ulaya walielewa kwamba maingiliano ovyo ya kujamiiana nje ya ndoa na zinaa vinaweza kuwa na taathira hatari. XXXX

Ni zaidi ya miaka ishirini sasa ambapo tahadhari nyingi zimetolewa kuhusu Ukimwi, lakini kwa bahati mbaya maradhi hayo yameuawa mamilioni ya watu huku mamilioni ya wengine katika pembe tafauti za dunia wakiwa wameambukizwa virusi vya Ukimwi. Jambo lililo wazi ni kuwa kwa kuzingatia hatari kubwa ya ugonjwa wa Ukimwi kwa watu wa nchi mbalimbali khususan katika nchi zinazoendelea, suala la kukabiliana na hatari hiyo linapasa kuwa katika mipango mikuu na ya kwanza ya serikali za nchi hizo. Vilevile weledi wa mambo wanaamini kuwa, uaminifu kwa familia, kuheshimu ndoa na kujiepusha na ngono nje ya ndoa ni miongoni mwa njia zinazoweza kudhibiti ugonjwa wa ukimwi.

Ni vyema kuashiria kuwa vitendo vya kujamiiana watu wenye jinsia moja ni moja ya sababu za kudhoofika na kuporomoka taasisi ya familia katika nchi za Kimagharibi. Katika hali ya kimaumbile, mwanamke na mwanaume wanaweza kuasisi familia na kuandaa mazingira mazuri ya kuzaa watoto na kulea kizazi bora. Kwa msingi huo kuweko hitilafu na mabadiliko ya aina yoyote katika hali hiyo ya kimaumbile ya ndoa baina ya mwanamke na mwanaume kutakuwa na matokeo mabaya. Kwa hiyo ndoa inapaswa kufanyika baina ya watu wawili wenye jinsia tofauti. Kuna dalili au sababu nyingi za kuthibitisha ukweli huo.  Mwenyezi Mungu ameumba muundo wa anatomia ya mwili wa mwanadamu kwa ajili ya mahusiano ya kujamiiana kati ya mwanaume na mwanamke na elimu viumbe yaani biolojia inathibitisha kwamba maingiliano kama hayo yanapaswa kufanyika kati ya mwanamke na mwanaume. Hii ni katika hali ambayo hakuna sababu yoyote ya kibaiolojia inayothibitisha uhusiano wa watu wenye jinsia moja au kuunga mkono jambo hilo. Mbali na hayo, hisia za mapenzi zinazotokana na uhusiano baina ya mke na mume hazipatikani katika maisha ya watu wawili wenye jinsia moja. Katika upande mwingine Mwenyezi Mungu ameweka uwezo wa kuzaa ndani ya uhusiano wa mke na mume ili kujenga mfungamano imara zaidi na ladha kubwa kati ya wawili hao.

Utovu wa maadili katika jamii za Magharibi umeitumbukiza taasisi ya familia katika mgogoro mkubwa. Kwa sasa tunashuhudia athari hizo mbaya za utovu wa maadili hususan katika masuala ya maingiliano ovyo ya kujamiiana katika mikataba na sheria za kimataifa kama mkataba wa kuondoa ubaguzi dhidi ya wanawake. Mkataba huo wa kufuta ubaguzi dhidi ya wanawake umetambua zinaa na ukahaba kuwa ni kazi kama zilivyo kazi nyingine za wanadamu. Kwa msingi huo kamati ya mkataba huo mwaka 2000 iliitaka serikali ya China isiwaadhibu wanawake wanaofanya ukahaba na kuuza miili yao. Kamati hiyo pia ilizishinikiza nchi kama Russia, Mexico, Romania, Ufilipino na Peru ili zihalalishe umalaya na kuacha kuwaadhibu wanawake wanaouza miili yao.

Hapana shaka kuwa matatizo hayo ya kijamii na kusambaratika nguzo na misingi ya taasisi ya familia katika nchi za Magharibi kunatokana na kuwa mbali na maadili na masuala ya kiroho. Vyombo vya habari na mawasiliano ya umma vya nchi za Magharibi vinachochea zaidi hali hiyo na kuzidisha hisia za maingiliano ovyo ya ngono kupitia filamu na vipindi mbalimbali. Ni kwa msingi huo ndiyo maana wataalamu wanasema kuwa tiba mujarabu ya maradhi hayo ya jamii za nchi za Magharibi ni kurejea kwenye maadili, mafundisho ya dini na masuala ya kiroho.    

XXXX

Wapenzi wasikilizaji muda wetu umefikia tamati ,tukutane juma lijalo panapo majaliwa yake Allah, kwaherini.

Sauti na Video

Andika maoni


Msimbo salama (Security code)
Upyesha (Refresh)