Tovuti Hii Imefungwa. Tumehamia Kwenye Parstoday Kiswahili
Jumanne, 05 Machi 2013 15:10

Matatizo ya Familia katika Nchi za Magharibi (11)

Matatizo ya Familia katika Nchi za Magharibi (11)

Assalamu Alaykum wasikilizaji wapenzi na karibuni kujiunga nami tena katika kipindi chetu hiki kinachojadili matatizo ya familia katika nchi za Magharibi. Mtakumbuka kuwa katika kipindi cha juma lililopita nilizungumzia taathira mbaya za aidiolojia ya ufeminism kwa familia kama mpambano baina ya mwanamke na mwanaume, kuzuia ndoa na kuasisi familia.  Katika kipindi cha leo nitaanza kuchunguza taathira nyingine hasi za fikra za ufeminism kwa taasisi ya familia katika nchi za Magharibi. Tafadhalini kuweni nami hadi mwisho wa makala hii.

XXXX

Moja ya athari mbaya za harakati ya ufeminism kwa familia ambayo inatambuliwa kama mbegu ya awali kabisa ya jamii, ni kudunishwa nafasi ya mwanamke ya kuwa  mke kwa mumewe, mama wa nyumbani na mama ndani ya familia.  Baadhi ya wafeministi wanadai kuwa majukumu ya mwanamke kama mke au mama ndani ya familia ni mambo ambayo yamebuniwa na mfumo dume ambao umeimarishwa na kuenezwa kote dunia kwa shabaha ya kudhoofisha na kumdhibiti mwanamke.

Mary Wolsstonecraft ambaye ni miongoni mwa vinara wa harakati ya ufeminism huko Ufaransa, alitambua kuwa kujishughulisha mwanamke na kazi za nyumbani na kunyimwa uhuru na fursa za kijamii ndio sababu kuu ya kudunishwa wanawake na aliamini kuwa iwapo vizuizi hivyo vitaondolewa, wanawake pia wangekuwa na uwezo wa kufikiri na wa kiutendaji sawa na ule wa wanaume. Kinyume na madai ya mfeministi huyu, kuweko mwanamke nyumbani hakumzuii kuwa huru na kufanya shughuli zake za kijamii. Licha ya hayo, wanawake hutoa mchango mkubwa zaidi nyumbani. Ni kwa sababu hiyo ndiyo maana tunaona kuwa watu wenye shakhsiya adhimu na kubwa walilelewa na akinamama werevu, wawajibikaji na wanaotambua vyema wajibu na mchango wao. Wahenga wanasema kuwa mafanikio ya kila mwanaume yanapatikana kutokana na mchango wa mama au mke aliyejitolea na anayetambua vyema majukumu yake.

Jessica Anderson, tabibu wa Kimarekani anapinga mitazamo ya kufurutu ada kuhusiana na ulazima wa mwanamke kufanya kazi nje ya nyumba na majukumu ya familia na kuandika kuwa: Kazi ni sehemu ya maisha na si maisha yote ya mwanadamu. Anasema, jukumu kuu la mwanamke ni kulea watoto na kizazi bora na sambamba na wajibu huo anaweza pia kufanya kazi nje ya nyumba. Hata hivyo utamaduni wa Kimagharibi umejalia suala la  mwanamke kufanya kazi nje ya nyumba kuwa ndio wajibu na jukumu lake kuu na la kwanza na majukumu ya mama yamekuwa jambo la pembeni kabisa na la daraja la pili. Jessica Anderson anamalizia kwa kusema kuwa: Kuendelea kwa hali hii kunawazidishia wanawake na akinamama wa Kimagharibi mashinikizo makubwa ya kiroho na kinafsi."

Japokuwa Uislamu unatambua jukumu la msingi la mwanamke kuwa ni kushughulikia masuala ya nyumbani na familia, kuwa mama kwa maana halisi ya neno hilo na kulea watoto na kizazi bora, lakini pia umemfungulia mwanamke njia bora na yenye taathira katika masuala ya jamii. Wanawake pamoja na kufuatilia na kushughulikia masuala ya ndani ya nyumba, wanaweza pia kujifunza taaluma zinazohitajika na kushiriki katika nyuga mbalimbali za kielimu, kitamaduni, kisiasa na kijamii na kupata mafanikio makubwa. Katika Uislamu thamani ya mama anayejishughulisha na kazi za nyumbani si ya chini ikilinganishwa na ile ya kufanya kazi nje ya nyumba. Hadithi zilizopokewa kutoka kwa Mtume Muhammad (saw) na Ali zake watoharifu zinasema kwamba: "Mwenyezi Mungu humtazama kwa jicho la rehma mwanamke anayejishughulisha na masuala ya nyumbani kwake." Kuwa mama wa nyumbani na kushughulikia ipasavyo masuala ya faamilia katika utamaduni wa Kiislamu ni kazi tukufu na yenye heshima kubwa. Kazi ya mama ndani ya nyumba huwa na taathira kubwa katika mustakbali wa jamii na ni sanaa iliyochanganyika na hisia safi na nyepesi za mama.

Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu Ayatullah Ali Khamenei anasema kuhusiana na suala hilo kuwa: Uislamu umempa heshima na kumtukuza mwanamke kwa maana halisi na kama dini hiyo inasisitiza juu ya nafasi ya mama na utukufu wake ndani ya familia, au nafasi ya mwanamke na taathira zake, haki, majukumu na mipaka ya mwanamke ndani ya familia, suala hilo halina maana ya kumzuia kushiriki katika masuala ya kijamii na kujiunga na harakati za mapambano na shughuli za kijamii." Mwisho wa kunukuu.

XXXX

Mtazamo wa mafeministi wa kufurutu ada kwa suala la familia na majukumu ya mama, ni mtazamo kinyume kikamilifu na tofauti kabisa. Baadhi ya wafeministi wenye misimamo mikali wanaitambua nafasi ya mwanamke kama mama kuwa ndio chanzo cha kubaguliwa na kukandamizwa wanawake. Shulamith Firestone, mfeministi mwenye misimamo mikali anasema kuwa "Nafasi ya mama inapaswa kufutwa kabisa katika utamaduni wa mwanadamu. "Firestone anadai kuwa, kuwapa watoto maziwa kwa kutumia chupa na shule za chekechea kumefuta haja ya mwanadamu kwa kazi na majukumu ya mama katika jamii."

Kwa mtazamo wa Uislamu nafasi ya mwanamke kama mama ndani ya familia ndio sehemu muhimu zaidi ya maisha yake. Kwa mtazamo wa dini hiyo ni kwamba majukumu ya mama ya mwanamke si kwamba hayamzuii kujihusisha na kazi nyingine za kijamii bali pia ni sehemu ya maumbile yake ambayo yanamwezesha kulea watoto salama na kuwakabidhi kwa jamii ya mwanadamu. Hatuwezi kukana mashaka makubwa anayokumbana nayo mama katika majukumu yake kama mama mithili ya mashaka ya kipindi cha ujauzito, wakati wa kujifungua, kunyonyesha watoto na kuwalea lakini pia ni muhimu kutambua kuwa hisi ya kuwa mama ndani ya ujudi na uwepo wa mwanamke na mapenzi yake makubwa kwa mwanaye humfanya mama na wanawake wasahau na kustahamili mashaka hayo. Uislamu pia umesisitiza juu ya upande wa kimaanawi na kiroho wa majukumu ya mama na kufanya jitihada za kuboresha uzima wa kinafsi na kuimarisha hisia za matumaini za akinamama. Inaonekana wazi kuwa katika dunia ya leo ambapo mama wamejitenga na watoto wao kutokana na kufanya kazi kwa muda mrefu nje ya nyumba, hakuna kitu kingine kinachoweza kuchukua nafasi ya mama katika jamii. Ni wazi kwamba chekechea na vituo vya kulea matoto wadogo hata vile vyenye zana za kisasa kabisa haviwezi kuwa mbadala wa hisia nyepesi, upendo, huruma, utulivu wa kiroho na hisia za matumaini za mama kwa mtoto wake.

Miongoni mwa taathira mbaya za mitazamo ya mfumo wa feminism kwa taasisi ya familia ni maingiliano eti "huru" ya kujamiiana kati ya jinsia mbili za mwanamke na mwanaume. Mafeministi wenye misimamo mikali ambao wanatambua mahusiano ya kujamiiana kati ya mke na mume kuwa ni miongoni mwa sababu muhimu za kutekwa mwanamke na kufungwa kwenye minyororo ya wanaume, wanamhimiza mwanamke kujikomboa na kujiondoa kwenye mahusiano kama hayo. Hata hivyo mafeministi hao hao hawana tatizo lolote na mahusiano na maingiliano ya kingono yasiyokuwa na mpaka wowote baina ya mwanamke na mwanaume au hata baina ya watu wawili wenye jinsia moja. Baadhi ya mafeministi hao hususan huko Marekani wamekuwa wakiwashajiisha wanawake kufanya maingiliano ya kujamiiana nje ya mipaka ya familia zao.  Kwa msingi huo baadhi ya wanafikra wa Kimagharibi wanasema kuwa fikra za mfumo wa feminism ni hadaa nyingine iliyotokana na aidiolojia ya mfumo mpya wa dunia ambayo inamtumbukiza mwanamke wa Kimarekani katika ufuska na kuharibu maisha ya mamilioni ya watu.

Mtaalamu wa masuala ya wanawake wa Marekani Henry Makow anafanya ulinganisho kati ya mwanamke wa Kiislamu na asiye wa Kiislamu wa Marekani akisema: "Jambo linalopewa kipaumbele na mazingatio makubwa na mwanamke Muislamu ni familia yake. Familia kwa mwanamke Muislamu ni sawa na tundu la kidege chake kichanga ambako huzaliwa na kulelewa. Mwanamke Muislamu ndiye anayejenga tundu hilo yeye mwenyewe na huwa mhimili wake unaolinda maisha ya kiroho ya familia. Huwa mlezi wa watoto wake na msaidizi na makimbilio ya mume wake." Henry Makow anaendelea kusema kuwa: "Mkabala wake mwanamke anayejali urembo wa kidhahiri wa Marekani ambaye hutembea nusu uchi hamu yake kubwa ni kujidhihirisha mbele ya macho ya mamilioni ya watu akiwa uchi. Huyu ndiye mfeministi ambaye hufungamana na nafsi yake tu lakini kimatendo ni milki ya watu wote. Si mke wa mtu makhsusi bali ni wa watu wote anayejiuza kwa mnunuzi mwenye donge kubwa zaidi na daima huwa katika hali ya kujipiga mnada."

Henry Makow anamalizia kwa kusema: "Nchini Marekani thamani ya mwanamke huainishwa na kupimwa kwa mvuto wake katika upande wa hisi za ngono na matokeo ya mtazamo kama huo ni kupatikana wanawake wasiokuwa na utambulisho, wachoyo, wanaopenda mizozano na wenye matatizo ya kinafsi ambao hawastahiki kuwa mke au mama."

XXXX

Wasikilizaji wapenzi muda wa kipindi hiki umefika ukingoni natumai kuwa mumenufaika na yale niliyowaandalia katika kipindi basi hadi wakati mwingine nawaageni nikiwatakia kila la kheri maishani kwaherini.

XXXX

Andika maoni


Msimbo salama (Security code)
Upyesha (Refresh)