Tovuti Hii Imefungwa. Tumehamia Kwenye Parstoday Kiswahili
Jumatatu, 04 Machi 2013 14:39

Matatizo ya Familia katika Nchi za Magharibi (10) + Sauti

Matatizo ya Familia katika Nchi za Magharibi (10) + Sauti

Hamjambo wasikilizaji wapenzi na karibuni kuwa nami tena katika makala hii inayozungumzia mgogoro wa familia katika nchi za Magharibi. Katika kipindi kilichopita cha mfululizo huu tulisema kuwa mitazamo ya kifeminism imekuwa na taathira mbaya kwa maisha ya mtu binafsi na jamii katika familia za Magharibi. Kipindi chetu cha leo kitatupia jicho baadhi ya taathira hizo mbaya za mitazamo ya kifeminism kwa taasisi ya familia kwenye jamii za Magharibi. Karibuni.

Moja kati ya taathira haribifu za Ufeminism kwa taasisi ya familia ni sisitizo la harakati hiyo juu ya makabiliano na mpambano wa daima baina ya mwanamke na mwanaume. Wafeministi wanaona kuwa wanaume ni maadui ambao ni muhali kuweza kupatana na wanawake. Wanasema wanawake wanapaswa kujitenga na wanaume kadiri inavyowezekana ili kuweza kujikomboa na kuepuka udhibitiwa wao.  Wafeministi wanaamini kuwa, kwa kuwa taasisi za kijamii zimeundwa kwa msingi wa kulinda maslahi ya mwanaume, wanawake wanapaswa kujiweka mbali na ushawishi wa taasisi hizo ili kupata uhuru. Ufeminisim wa kufurutu ada na wenye misimamo mikali unaamini kwamba, wanawake wana maslahi ya pamoja kwa sababu wote hao wanakandamizwa na kudhulumiwa na wanaume. Kwa msingi huo wanawake wanaunda tabaka linalopingana na lile la wanaume. Baadhi ya mafeministi wa kufurutu ada wakati mwingine wamekuwa wakitoa wito wa wanawake kuishi katika jamii au kisiwa kilichojitenga na jamii ya wanaume.

Kama ambavyo inabainika katika fikra hizi za ufeminisim, mwanamke na mwanaume si tu kuwa hawako pamoja na hawakamilishani bali wanakabiliana kikamilifu huku mmoja wao akiwa kheri na mwingine akiwa ni shari. Mtazamo huo umesababisha kuongezeka uadui kati ya mwanaume na mwanamke ambao unaathiri kwa kiasi kikubwa jamii nzima.

Hata hivyo katika Uislamu tofauti na mtazamo wa kifemisism, mwanamke na mwanaume hutegemeana na kukamilishana. Mwanaume anatambuliwa kuwa ni mlinzi wa familia ambaye huwajibika kuidhaminia familia yake mahitaji ya kimaisha. Mwanamke pia ana jukumu na wajibu wa kulinda anga ya upendo, huruma na mahaba katika familia yake. Kwa mujibu wa mtazamo wa Kiislamu kila mmoja kati ya mke na mume ana nafasi na mchango muhimu katika kuongoza familia kwa ufanisi. Kila mmoja kati ya mke na mume huwa mithili ya vazi maridadi kwa mwenzake na hupaswa kuonyesha makosa na dosari za mwenzake kwa kuasisi uhusiano uliojaa upendo na mahaba kati yao. Kwa hiyo himaya na mashirikiano miongoni mwa wanandoa wawili huwa nguzo imara kati yao ambayo huwalinda na mashaka na matatizo ya aina mbalimbali.

Kwa haakika mafundisho ya Uislamu yanamfanya mwanaume amtazame mkewe kama mshirika muhimu na mwenye huruma, upendo, hisia nyepesi na mwenye kuleta utulivu ndani ya nyumba huku mwanaume naye akionekana mbele ya mkewe kama dhihirisho la uaminifu, matumaini na kujitolea.

Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu ya Iran Ayatullah Ali Khamenei anasema kuhusiana na suala hilo kwamba: "Dini ya Uislamu inamtambua mwanaume kuwa nguzo na mdhamini wa masuala ya wanawake katika familia na inamtambua mwanamke kama ua lenye harufu nzuri. Jambo hilo si kumdhalilisha mwanamke wala mwanaume na wala si kupuuza haki ya mwanamke au mwanaume, bali ni kutambua uhalisia wa maumbile ya kila mmoja wao. Anasema, uzito wa viwili hivyo unalingana kikamilifu unapowekwa kwenye mizani...."

Wasomi mbalimbali hii leo wanatambua kuweko tofauti za kimwili na kinafsi kati ya mwanamke na mwanaume kuwa ni jambo la kawaida na wanaamini kuwa, tofauti hizo zinaweza kutumika katika kuboresha maisha ya ndoa.  Katika utafiti wake wa kisayansi, Steven Rhoades mtafiti na mhadhiri katika Chuo Kikuu cha Virginia nchini Marekani amethibitisha upotofu wa kipindi cha miaka 40 wa harakati ya ufeministi. Rhoades ameandika katika kitabu chake alichokipa jina la jina la "Taking Sex Differences Seriously" kwamba: uwajibikaji wa wanaume kama mume na baba katika familia, unaumuhimumkubwa sana katika kudhamini usalama na malezi bora ya watoto. XXXX

Miongoni mwa misimamo ya kifeminism iliyotoa dharba na pigo kubwa kwa taasisi ya familia ni suala la kupinga ndoa na kuunda familia. Mafeministi wanaitambua ndoa, kubeba mimba na kulea watoto kuwa ni suala duni na hakiri. Hii ni kwa sababu kwa mtazamo wa aidiolojia za harakati hiyo, msingi wa masuala hayo ni udhibiti wa mwanaume juu ya mwanamke. Wanaamini kwamba hatua ya mwanamke kukubali majukumu ya ndani ya nyumba inapingana na uhuru wake. Kwa msingi huo wanasisitiza juu ya udharura wa kufanyika mapinduzi ya jinsia ya mwanamke dhidi ya mwanaume, fikra ambayo matokeo yake ni kukataa kuolewa, kupinga suala la kuwa na mume mmoja na vilevile kupinga suala la kuwa mama.

Bi Simone De Beauvoir, mwandishi mfeministi wa Kifaransa ameshambulia vikali mfumo wa familia ambao ndio msingi wa uhai wa jamii na kulea wanadamu katika maadili bora na kuitaja ndoa kuwa ni chanzo cha matatizo ya wanawake. Bi Simone pia anasema moja ya masuala nyeti ya harakati ya ufeminism ni kupinga uhusiano wa ndoa na kuzaa. Hata hivyo baadae Bi De Beauvouir alikiri makosa yake kuhusiana na kupinga nafasi ya wanawake katika jamii khususan ile ya kuwa mama.

Miongoni mwa taathira za kuenea fikra za kifeminism ni kuongezeka kiwango cha talaka katika nchi za Magharibi huku ndoa rasmi zikipungua. James Q. Wilson ambaye ni mtaalamu wa masuala ya jamii wa Marekani anaandika kuwa: "Awali ndoa katika jamii yetu ilikuwa tukio takatifu na baadaye ikabadilika na kuwa makubaliano ya mkataba na sasa imekuwa utaratibu maalumu tu unaopangwa na mwanamke na mwanaume. Anaendelea kuandika kuwa: "Kizazi cha vijana wa leo wa Marekani katika barua na mazungumzo yao wanasema kwamba hawataki kuwa mke au mume. Matokeo ya maisha mapya ya aina hii ni kuwa, vijana hawa hukimbia na kuhepa suala la kubeba majukumu."

Kwa sasa idadi ya watoto wanaozaliwa nje ya ndoa au wanaharamu katika nchi za Magharibi inaongezeka kwa kasi kubwa. Nusu ya watoto wa aina hiyo huishi katika familia zenye mzazi moja na wengi wao huishi na mama pekee na huwenda hawajawahi hata siku moja kuwaona baba zao. Wanawake wengi wanapoteza fursa mwafaka ya kuolewa, kuwa na familia na kubeba mimba katika nchi hizo kutokana na kukanyagwa thamani za familia.

Janice Shaw Crouse, mwandishi wa vitabu na magazeti wa Kimarekani ameandika kuwa: "Hii leo idadi ya wanawake ambao hawajaolewa wenye umri wa kati ya miaka 20 hadi 45 ni kubwa zaidi nchini Marekani kuliko wakati wowote mwingine. Anasema watu ambao hufunga ndoa kwa kuchelewa hutumia mamilioni ya dola kwa ajili ya kutibu tatizo la kutopata mtoto." Mwisho wa kunukuu.

Mafeministi wengi wanapinga vikali suala la kuolewa na kuunda familia. Wanaamini kuwa wanawake hawapasi kupewa uhuru wa kuanzisha familia kwa mtindo wa kijadi. Viongozi wa harakati hiyo kama Shere Hite wa Marekani wanafurahishwa mno kuona idadi ya watoto wengi waliozaliwa nje ya ndoa katika jamii ya Marekani. Wanaamini kuwa familia si taasisi takatifu. Kwa mujibu wa mtazamo huo potofu, taasisi ya familia imejengeka kwa msingi wa dhulma ya mwanaume dhidi ya mwanamke. Ni kwa sababu hiyo ndiyo maana mafeministi wengi wameamua kuoa au kuolewa na wanawake wenzao. Mafeministi hawa wanasema sasa ndoa za watu wenye jinsia moja yaani ndoa baina ya mwanaume na mwanaume mwenzake, na baina ya mwanamke na mwanamke mwenzake ndio kigezo bora zaidi cha maisha ya pamoja. Uhasama na uadui wa mafeministi dhidi ya familia na ndoa umekuwa mkubwa kiasi kwamba hata nyaraka za mkutano wa kimataifa wa Beijing uliofanyika mwaka 1995 si tu kwamba hazikuwa na maneno kama "mume" au "mke", bali pia nafasi ya maneno kama "mama" na "familia" ilichukuliwa na mameno ya yaya na mwenza nyumbani.

Kwa kutilia maanani yote yaliyosemwa inatupasa kusema kuwa ni kweli kwamba katika baadhi ya familia kunatendeka dhulma na ukatili dhidi ya wanawake, lakini pia tunapasa kusisitiza kuwa njia ya kupambana na ukatili huo si kufuta taasisi yenye thamani ya familia. Utafiti unaonesha kwamba taasisi ya familia ina taathira kubwa katika kupunguza matatizo ya mtu binafsi na ya kijamiii ya watu na kuwapa watu hao utulivu wa kiroho na hali ya kujiamini. Wanadamu huweza kukidhi na kudhamini mahitaji yao ya kiroho, kijamii, kiuchumi na mahusiano na mume na mke chini ya kivuli cha familia, suala ambalo hufuatiwa na utulivu wa kiroho na ukamilifu wa mwanadamu. Ni chini ya kivuli cha ndoa yenye mafanikio, mpenzi msikilizaji ndipo mwanamke na mwanaume wanapoweza kupata ukamilifu halisi na kuweza kulea watoto na kizazi chema kwa ushirikiano.

Sauti na Video

Andika maoni


Msimbo salama (Security code)
Upyesha (Refresh)