Tovuti Hii Imefungwa. Tumehamia Kwenye Parstoday Kiswahili
Jumanne, 26 Februari 2013 15:00

Matatizo ya Familia katika Nchi za Magharibi (9) + Sauti

Matatizo ya Familia katika Nchi za Magharibi (9) + Sauti

Hamjambo wapenzi wasikilizaji na karibuni kuwa nami tena katika sehemu hii ya tisa ya kipindi cha matatizo ya familia katika nchi za Magharibi. Katika kipindi cha wiki iliyopita tuliendelea kueleza mifumo ya kifikra na aidiolojia zilizochangia kwa kiasi kikubwa katika mporomoko wa familia kwenye nchi za Magharibi. Tulisema kuwa miongoni mwa ailidiolojia hizo ni mfumo wa feminism. Tulisema kuwa feminism ni harakati au aidiolojia iliyojitokeza huko Magharibi baada ya kipindi cha mwamko na ustawi wa Ulaya (Renaissance) katika karne za 14, 15 na 16 juu ya misingi ya humanism, liberalism na securalism na lengo lake lilikuwa ni kurejesha haki za wanawake.  Nadharia au fikra za feminism kwa madai ya waasisi wa mfumo huo  zilikuwa jibu kwa ukiukaji wa haki za wanawake katika kipindi chote cha historia ya Magharibi. Tulisisitiza kuwa tofauti na ilivyo katika utamaduni wa Uislamu, mwanamke hakuwa na nafasi nzuri na ya kuridhisha katika utamaduni wa Kimagharibi. Tunapotazama historia ya nafasi ya mwanamke katika nchi za Magharibi tunaona kuwa, alikuwa akikabiliana na dhulma kubwa na udhalilishaji. Tulisema kuwa katika jamii hizo mwanamke alitambuliwa kuwa ni bidhaa tu na mara nyingi alihesabiwa kuwa ni sehemu ya mali na milki za mwanaume.

Kipindi chetu cha leo kitaendelea kutupia jicho taathira mbaya za fikra za feminism kwa taasisi ya familia katika nchi za Magharibi.  XXXX

Katika kipindi cha karne za 14, 15 na 16 wanawake katika ulimwengu wa Kimagharibi hawakuwa na haki ya kushiriki katika masuala ya kijamii, kisiasa na kadhalika. Kwa mfano huko Ugiriki na Roma mwanamke hakuwa na thamani yoyote na alikuwa akiuzwa na kununuliwa kama mnyama. Baadhi ya wasomi wa Kimagharibi kama Arthur Schopenhauer, mwanafalsafa wa Kijerumani  wa karne ya 18 na Saint Augustinus ambaye alikuwa msomi wa Kikristo wa karne za kati, waliwatambua wanawake kuwa ni sawa na wanyama. Baadhi ya wasomi hao pia waliamini kuwa, wanawake ni wachafu na duni zaidi kuliko wanyama. Wasomi na wanafikra hao wa Ulaya walimtambua mwanamke kuwa anatokana na kizazi cha shetani!

Katika dini zilizopotoshwa kama zile za Kiyahudi na kinasara pia wanawake walidunishwa na kudharauliwa. Katika dini ya Kiyahudi mwanamke anatambuliwa kuwa aliumbwa kutoka kwenye ubavu wa kushoto wa mwanaume na kwamba ndiye chanzo na sababu ya kufanya dhambi. Kitabu muhimu zaidi cha Mayahudi baada ya Taurati yaani Telmud kinasema kuhusu mwanamke kwamba: Mwanadamu anawajibika kuomba dua hizi tatu zenye baraka kila siku: "Ametukuka Mwenyezi Mungu aliyetufanya sisi kuwa Mayahudi, hakutuumba tukiwa wanawake na wala hakutuumba tukiwa wajinga."

Katika mafundisho yaliyopotoshwa ya kinasara pia mwanamke alitambuliwa kuwa mtu wa daraja la pili na Eva au Hawa alitambulishwa kuwa ndiye aliyemrubuni na kumhadaa mwanaume wa kwanza yaani Nabii Adam huko peponi. Ni kwa msingi huo ndiyo maana Mayahudi wanaamini kuwa, Mwenyezi Mungu ameumba uchungu wa uzazi kwa mwanamke anayejifungua kwa ajili ya kumtakasa Eva na kuwasafisha wanawake wengine. Kwa mfano tu katika kitabu cha Agano Jipya imeandikwa kuwa: Mwanamke anapaswa kunyamaza kimya na kujifunza kwa kumtii kikamilifu mwanaume. Mwanamke haruhusiwi kufunza au kumdhibiti mume bali anapaswa kunyamaza kimya, kwa sababu kwanza aliumbwa Adam na baadaye akaumbwa Eva. Adam hakuhadaiwa (huko peponi) bali mwanamke ndiye aliyehadaiwa na kufanya makosa. Hata hivyo ataokoka kutokana na machungu ya uzazi iwapo atabakia thabiti katika imani, upendo, usafi na ucha Mungu."

Wakati huo huo na kinyume na mitazamo ya uchupaji mipaka dhidi ya mwanamke, dini ya Uislamu imewapatia wanawake heshima na tokea mwanzoni mwa kudhihiri kwake iliwashirikisha katika nyuga zote za kielimu, kijamii, kisiasa na kiutamaduni. Inatosha kwa ajili ya kuitambua nafasi ya juu ya mwanamke katika Uislamu kusoma hadithi ya Mtume Muhammad (saw) ambaye amesema: Watoto wenu bora zaidi ni wale wa kike.  XXXX

Kuibuka kwa mfumo wa feminism ni matokeo ya mazingira ya ubaguzi na dhulma ya ulimwengu wa Kimagharibi dhidi ya mwanamke. Kuenea na kukita mizizi kwa fikra za secularism, humanism na liberalism kulichangia mno katika kuanzizishwa mrengo wa feminism. Mbali na matukio hayo, mfumo wa ubepari na wimbi la ustawi wa kiviwanda katika ulimwengu wa Magharibi sambamba na kuasisiwa tabaka la matajiri na la wafanyakazi na dhulma na ukandamizaji wao dhidi ya mwanamke viliibua wimbi jipya la malalamiko ya wanawake katika kalibu ya harakati ya feminism.

Harakati hiyo ya kijamii ya wanawake awali ilianza huko Ufaransa na kisha Marekani na baadaye ikaenea katika nchi za Magharibi zilizokuwa zikipinga dhulma na kutokuweko usawa wa kisheria, kiuchumi, kisiasa na sheria za kidhamu kuhusiana na wanawake. Kuanzia muongo wa 1890 baadhi ya nchi za Magharibi zilitambua rasmi haki ya kupiga kura ya wanaume wote.  Jambo hilo lilidhihirisha zaidi ubaguzi uliokuwa ukifanywa dhidi ya wanawake katika nchi hizo. Kwa msingi huo wimbi la kwanza la ufeminism ambalo lilifahamika kwa jina la "harakati ya kupigania haki ya kura" lilianza katika nusu ya kwanza ya karne ya 19. Hatimaye baadhi ya nchi ziliwapatia wanawake haki ya kura baada yamalalamiko mengi ya kudai haki ya kupiga kura na kueleza maoni yao katika jamii. Kwa mfano Uingereza ilikuwa nchi ya kwanza ya Magharibi kutambua haki ya kupiga kura wanawake hapo mwaka 1918 na kufuatiwa na Marekani mwaka 1920.

Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu ya Iran Ayatullah Ali Khamenei anasema kuhusu haki ya kupiga kura ya wanawake katika nchi za Magharibi kwamba: Hadi kufikia muongo wa pili ya karne ya 20, hakuna mwanamke yoyote huko Ulaya aliyekuwa na haki ya kupiga kura. Kuanzia miaka ya 1916 hadi 1918 taratibu nchi za Ulaya ziliamua kuanza kumpa mwanamke haki ya kutoa maoni, kusimamia mali zake na kupewa haki za kijamii sawa na mwanaume. Kwa msingi huo Ulaya imechelewa kutoka usingizini na ilichelewe pia kufahamu mambo. Sasa inaonekana kuwa watu wa Ulaya wanataka kufidia kubaki kwao nyuma katika suala hilo kwa kuzusha makeleleo na propaganda za urongo" mwisho wa kunukuu.

Wimbi la pili la feminism lilianza katika muongo wa 1960 kwa kuianishwa  thamani na ufeminisim.  Wimbi hilo limejengeka juu ya misingi ya nadharia zinazoonekana kidhahiri kuwa ni za kielimu. Waungaji mkono wa wimbi hilo la pili walikuwa wakifanya jitihada za kuchambua hali ya wanawake na sababu za kudunishwa kwao, hali bora na stratijia yao kwa ajili ya dunia nzima.  Mirengo muhimu zaidi ya ufeminism ya wimbi la pili ilikuwa ile yenye misimamo mikali na mitazamo ya kiliberali ambayo ilifanikiwa kwa kiasi fulani kubuni ajenda moja kwa ajili ya mapambano yao. Miongoni mwa malengo ya makundi haya ya wimbi la pili la ufeminism ni kuzuia ubaguzi wa pande zote, haki ya mwanamke kwa mwili wake na suala la kupambana na ukatili dhidi ya wanawake. Baadhi ya vinara wa wimbi hili la pili la ufeminism ni mwanafalsafa wa Kifaransa Bi Simone De Beauvoir na mwandishi habari wa Kimarekani Betty Friedan.

Kuanzia nusu ya pili ya mwaka 1990 kulijitokeza nyanja za kudhihiri wimbi la tatu la fikra za ufeminism ambalo zaidi lilifungamana na mabadiliko yaliyosababishwa na mfumo wa ubepari, mjadala juu ya kipindi cha baada ya maendeleo na ustawi na radiamali zilizosababishwa na mitazamo mikali na ya upande mmoja ya wimbi la pili la ufeminism.

Ala kulli hal, tunasisitiza kuwa harakati ya feminism ilikuwa radiamali na jibu dhidi ya dhulma na hali ya kutokuwepo usawa iliyokuwa inatawala katika ulimwengu wa Magharibi dhidi ya mwanamke. Hata hivyo harakati hiyo si tu kwamba haikutatua matatizo ya mwanamke bali pia ilizidisha uhasama baina ya wanawake na wanaume na kuteteresha misingi ya familia na kuangamiza thamani za kimaadili.    XXXX

Wapenzi wasikilizaji muda wa kipindi hiki umefikia tamati. Tutakutana tena katika kipindi cha wiki ijayo kutazama kwa undani taathira mbaya za fikra na mitazamo ya kifeministi katika taasisi ya  Familia kwenye Nchi za Magharibi. Na hadi wakati huo nawaageni nikiwatakia kila la kheri maishani kwaherini.

Sauti na Video

Andika maoni


Msimbo salama (Security code)
Upyesha (Refresh)