Tovuti Hii Imefungwa. Tumehamia Kwenye Parstoday Kiswahili
Jumapili, 15 Juni 2014 17:23

Bustani ya Uongofu (60) - sehemu ya mwisho

Bustani ya Uongofu (60) - sehemu ya mwisho

Assalaamu Alaykum wapenzi wasikilizaji na karibuni katika sehemu nyingine ya kipindi hiki cha Bustani ya Uongofu hii ikiwa ni sehemu ya 60 na ya mwisho ya mfululizo. Ni matumaini yangu kuwa, mtakuwa nami hadi mwisho wa kipindi hiki. Karibuni.

Kama tulivyotangulia kusema huko nyuma, Uislamu ndio dini ya mwisho na bora kuliko dini zote za Mwenyezi Mungu; na Mtume SAW ndiye aliyekuja na dini hii kwa ajili ya wanadamu wote. Akipata auni na msaada wa maarifa asili na uhakika wa milele wa Uislamu, kwa kipindi kifupi sana Bwana Mtume SAW aliweza kuibadilisha jamii ya wakati huo na kuitoa katika kinamasi cha ujahili na taasubi; na umma huo kuwa miongoni mwa umma zenye taathira kubwa na zilizopiga hatua katika fasihi na maadili ya kibinadamu. Mwenyezi Mungu aliteremsha sheria na mafundisho aliyoyahitajia mwanadamu katika fremu ya aya zenye nuru za Qur'ani Tukufu kupitia kwa Mtume Muhammad SAW katika kipindi cha miaka 23; na mbora huyo wa viumbe akawafikishia watu ujumbe huo. Kando ya misingi na mafundisho hayo, maneno na muamala wa Mtume SAW nao ulibainisha na kukamilisha mafundisho ya dini hiyo ya Mwenyezi Mungu. Pamoja na kuweko upinzani wote ule, hasama, adawa na uadui sambamba na njama za ukwamishaji mambo za watu majahili, maktaba ya Kiislamu ilipiga hatua kuelekea katika ukamilifu wake. Akiwa angali hai, Bwana Mtume SAW mbali na kuwafikishia watu mafundisho ya Kiislamu huku akistahamili na kupambana na matatizo, vikwazo na vizingiti vingi, alijishughulisha pia kuyalinda mafundisho hayo na hurafa na upotofu wa kifikra na kivitendo na kutoa miongozo ya lazima katika uga huo ili Waislamu wasingekeuke na kupotea njia ya haki. Tangu mwanzoni mwa risala yake, Mtume SAW aliwatahadharisha Waislamu na suala la uwezekano wa kutokea hitilafu na mifarakano baina ya Waislamu baada ya kuondoka kwake na kurejea kwa Mola wake.

Moja ya mbinu zake za kuzuia mifarakano hiyo ni kutambulisha na kuirafisha daraja ya juu ya Ahlul Bayt na kuwataja kuwa warithi na viongozi wa Waislamu baada yake. Kwa msingi huo zimenukuliwa hadithi nyingi zinazobainisha nafasi muhimu waliyonayo Ahlul Bayt AS ya kuendeleza risala na ujumbe wa mbora huyo wa viumbe.  Miongoni mwa hadithi hizo ambazo zinapatikana pia katika vitabu vya Waislamu wa Kisuni ni hadithi mashuhuri na mutawatir yaani yenye mapokezi mengi ya Thaqalain yaani vizito viwili. Mtume SAW anasema katika hadithi hiyo kwamba:

Hakika nimekuachieni vitu viwili vizito; Kitabu cha Mwenyezi Mungu na Ahlu Bayt wangu, vitu ambavyo iwapo mtashikamana navyo sawasawa basi hamtapotea kamwe baada yangu. Amenipasha habari Mwenyezi Mungu, mrehemevu na mjuzi wa mambo yote kuwa, vitu viwili hivi havitatengana hadi vitakaponijia pembeni ya Hodhi. Basi tazameni mtaniwakilisha (mtaamiliana) vipi kwenye vitu hivi baada yangu."

Imenukuliwa katika vitabu vya historia kwamba, zaidi ya masahaba ishirini wamehadithia hadithi hii ya Thaqalain yaani vizito vizwili kwa njia tofauti tofauti. Kujikariri hadithi hii katika vitabu mbalimbali kunaonesha msisitizo na uzingatiaji wa Bwana Mtume SAW kuhusiana na nafasi muhimu ya Kitabu cha Qur'ani pamoja na Ahlul Bayt wake watoharifu. Kuwekwa Ahlul Bayt pamoja na Qur'ani katika hadithi ya vizito viwili ya Mtume SAW kuna maana ya udiriki na ufahamu mkubwa na wa hali ya juu walionao Ahlul Bayt kuhusiana na mafahimu na maamrisho na makatazo ya Qur'ani Tukufu. Ni kwa msingi huo ndio maana kushikamana na Qur'ani Tukufu sambamba na kuwafuata Ahlul Bayt ni jambo litakalomzuia mtu na upotofu na kukengeuka njia ya haki. Hii ni kutokana na kuwa, Ahlul Bayt AS ni wafasiri wakweli wa Qur'ani na ambao wanayafanyia kazi yaliyomo ndani ya Kitabu hicho kwa ukamilifu.

Nukta nyingine muhimu ni hii kwamba, kutokuweko utengano baina ya Qur'ani na Ahlul Bayt wa Mtume SAW ni ishara ya kubakia na kudumu Uislamu asili na sunna za Mtume SAW kupitia sira na mwenendo wa dhuria hao wa Mtume ambao Mwenyezi Mungu amewatakasa na kuwatoharisha kabisa.

Katika hadithi nyingine Mtume SAW anawataja Ahlul Bayt wake kwamba, ni safina ya uokozi na ambayo inamkinga mtu na kupotea, kiasi kwamba, kutopanda safina hiyo hakuna natija nyingine ghairi ya kupotea na kuangamia katika tufani ya upotofu. Mtume SAW anasema katika hadithi hiyo kwamba:

"Bila shaka mfano wa watu wa nyumba yangu ni kama Safina ya Nuhu, atakayeipanda ataokoka na mwenye kuiacha ataangamia."

Katika hadithi hii Bwana Mtume SAW anawaarifisha Ahlul Bayt wake AS kuwa ni Safina ya wokovu, kimbilio na marejeo ya kuokoka na upotovu; kiasi kwamba, kutopanda katika Safina hii yaani kutoshikamana na Ahlul Byat hawa wa Mtume SAW hakuna natija nyingine ghairi ya kuangamia na kukumbwa na tufani ya upotovu.

Kwa hakika Bwana Mtume SAW alikuwa na wasi wasi mkubwa na umma wake baada yake; yaani pindi atakapofariki dunia na kurejea kwa Mola wake. Historia inaonesha kuwa baada ya Bwana Mtume SAW kufariki dunia na kurejea kwa Mola wake, Ahlul Bayt wake watoharifu walifanya harakati kama Safina na kupiga hatua kuelekea katika njia ya Mwenyezi Mungu huku wakipita milima na mabonde katika njia hiyo; njia ambayo wakati mwingine walilazimika kukaza mwendo na wakati mwingine kwenda taratibu. Katika safari hii nahodha wa meli na safina hiyo ndiye aliyekuwa akibadilika; lakini ratiba ya safari ilikuwa ni ile ile. Kila nahodha kati ya manahodha hawa wenye ujuzi alikuwa akiongoza na kuendesha safina hiyo kulingana na mazingira yaliyokuwa yakitawala na kwenda kwa mwendo maalumu kulingana na hali ya hewa na mazingira yaliyokuwa yakitawala. Wote hawa walikuwa wakifikiria kupata radhi za Mwenyezi Mungu pamoja na saada ya mwanadamu kesho akhera; na walikuwa wakiiendesha safina ya umma wa Kiislamu kuelekea upande huo.

Ahlul Bayt wa Mtume SAW ambao ni waongozaji wa jamii kuelekea katika mambo mazuri, kuna wakati kutokana na mazingira yaliyokuwa yakitawala walijenga na kuanzisha vituo vya kielimu kwa ajili ya kufundisha sambamba na kuandaa midahalo na mijadala na wakati mwingine walilazimika kusimama na kupambana ili kutetea matukufu ya Kiislamu, kukabiliana na upotoshaji wa dini na kwa ajili ya saada ya umma wa Kiislamu.

Kwa hakika Ahlul Bayt wa Mtume SAW ni nuru ya uongofu. Elimu na maarifa vimeenezwa, na wao na fikra za Tawhidi zimepata nguvu kutokana na tafsiri na ubainishaji wa watukufu hao. Kwa msingi huo basi, njia bora kabisa ya kuwatambua shakhsia na dhuria hawa wa Bwana Mtume SAW ni kufahamu fikra na mitazamo yao katika masuala ya kiitikadi, kimaadili, kijamii na kadhalika. Kuhusiana na jambo hili Imam Ali bin Mussa Ridha AS amenukuliwa akisema:

"Mwenyezi Mungu amrehemu kila mwenye kuhuisha jambo letu." Akaulizwa nini maana ya kuhuisha jambo lenu? Imam akajibu kwa kusema, kuhuisha jambo letu ni mtu kujifunza elimu kwetu na kisha akaenda kuwafundisha hayo watu wengine. Kwani, kama watu wangekuwa wanafahamu maneno na maarifa yetu yenye thamani basi wangekuwa na ufahamu na hivyo wangetufuata."

Wapenzi wasikilizaji kwa leo tunakomea hapa na kipindi hiki ndicho cha mwisho katika mfululizo wa vipindi hivi vya Bustani ya Uongofu. Katika vipindi hivi tumejaribu kubainisha japo kwa mukhtasari mitazamo mbalimbali ya Mtume SAW na Ahlul Bayt wake watoharifu AS. Ninawashukuru wale wote waliofanikisha kukuleteeni mfululizo huu. Mimi ni Salum Bendera niliyekuwa mtayarishaji na msimulizi wa mfululizo huu. Ninakushukuruni na tunasubiri maoni na mapendekezo yenu anuani yetu ya Email ni This email address is being protected from spambots. You need JavaScript enabled to view it. . Hadi tutakapokutana tena katika kipindi au makala nyingine mpya ninakuegeni nikimuomba Allah atujaalie kuwa wafuasi wakweli wa Mtume SAW na Ahlul Bayt wake.

Wassalaamu Alaykum Warahmatullahi Wabarakaatuh.

 

 

 

Zaidi katika kategoria hii: « Bustani ya Uongofu (59)

Andika maoni


Msimbo salama (Security code)
Upyesha (Refresh)