Tovuti Hii Imefungwa. Tumehamia Kwenye Parstoday Kiswahili
Jumatatu, 09 Juni 2014 12:03

Bustani ya Uongofu (59)

Bustani ya Uongofu (59)

Assalaamu alaykum wapenzi wasikilizaji na karibuni katika sehemu nyingine ya mfululizo huu wa Bustani ya Uongofu, kipindi ambacho hubainisha mitazmo ya Mtume SAW na Ahlul Bayt AS kuhusiana na masuala mbalimbali. Sehemu hii ya 59 ya kipindi hiki itabainisha mitazamo ya Maimamu watoharifu kuhusiana na Mtume SAW pamoja na kubaathiwa na kupewa kwake Utume. Jiungeni nami hadi mwisho wa kipindi hiki. Karibuni.

Katika kipindi chote cha historia ya dini, ni mara chache mno kumpata Mtume mwenye sifa kama za Bwana Mtume SAW ambaye sifa zake zimenakiliwa katika vitabu vya historia kwa uwazi kama ilivyokuwa kwa mbora wa viumbe Mtume Muhammad SAW. Mtume SAW alikuwa dhihirisho la ujamali na uzuri na utukufu wa Mwenyezi Mungu na yeye ndiye mjumbe wa mwisho wa Mwenyezi Mungu. Tukirejea kitabu cha Qur'ani tunapata jinsi Mwenyezi Mungu alivyotaja sifa za Mtume Muhammad SAW kwamba, yeye ni rehma kwa walimwengu wote na kwamba, ana tabia njema. Kwa hakika ndimi na kalamu zimeshindwa kutaja wasifu wa Mtume SAW kama inavyotakiwa.  Licha ya kuwa wahakiki na waandishi wa masuala ya historia wamebainisha engo tofauti za  maisha ya Bwana Mtume SAW, lakini Maimamu watoharifu wamebainisha kwa aina yake tena kwa umakini mkubwa shakhsia isiyo na kifani ya Bwana Mtume SAW. Aidha Maimamu watoharifu AS walifanya hima na idili kubwa katika kuhuisha sunna na sira pamoja na mwenendo wa Mtume na walikuwa wako tayari kujitolea maisha yao kuhakikisha kwamba, dini ya Mwenyezi Mungu na sunna za Bwana Mtume SAW zinabaki hai na kufanyiwa kazi. Kama juhudi hizi zisingelikuweko, basi hadithi nyingi za Mtume SAW zingepotea na sunna zake kuachwa.

Imam Ali AS ambaye amelelewa katika maktaba ya Bwana Mtume SAW amebainisha kwa mbinu nzuri na kwa mtindo makini wa kilugha na kifasihi kuhusiana na adhama Mtume SAW tena kwa mapenzi, imani na unyenyekevu mkubwa.

Katika hotuba ya 96 katika Nahaj al-Balagha Imam Ali bin Abi Talib anabainisha sifa za Bwana Mtume SAW kwa kusema:

Mahala pa makazi yake ni mahali bora, na asili yake ni asili iliyo bora mno kuliko asili zote, ni asili ya heshima na susu iliyo salama. Nyoyo za watu wema zimeelekezwa kwake, na hatamu za macho zimegeuzwa kumuelekea yeye. Mwenyezi Mungu amezizika chuki kupitia yeye, na kwa yeye amezima mashambulizi ya kulipiza kisasim kwa yeye ameunganisha udugu na kupitia yeye amewatukuza waliokuwa dhalili, maneno yake ni ubainifu na kunyamaza kwake ni hekima."

Katika sehemu nyingine Imam Ali AS anamtaja Bwana Mtume SAW kuwa ni tabibu wa roho  ambaye alitoa matibabu katika zama ambazo fikra zilikuwa zimechanganyika na ujahili na nyoyo zilikuwa zimetanda kutu na uchafu wa dhambi.  Vile vile katika hotuba ya 108 ya Nahaj al-Balagha Imam Ali AS anasema kumhusu Bwana Mtume SAW kwamba:

Yeye - yaani Nabii (SAW) - alikuwa mfano wa tabibu anayezunguka na tiba yake, aliyeimarisha malhamu yake, azungukaye na aliye tayari na dawa zake. Anazitumia  mahali ambapo ipo haja, ili kuziponya nyoyo za vipofu, na masikio ya viziwi na ndimi za mabubu, kwa dawa zake hufuatilia mahali ulipotawala mghafala na mahali penye mashaka na matata."

Kwa hakika wakati alipobaathiwa na kupewa Utume, Mtume Muhammad SAW alifanya mabadiliko makubwa katika jamii ya Waarabu. Katika kivuli cha mafundisho ya Mtume wa Uislamu na katika jamii ya Kiislamu, Tawhidi na kumpwekesha Mwenyezi Mungu vikachukua nafasi ya kuabudu masanamu. Mbora huyo wa viumbe akabadilisha ujahili na ujinga na kuwa elimu na ujuzi. Aidha mafundisho ya Bwana Mtume SAW yalibadilisha hali iliyokuwa ikitawala katika jamii hiyo ambapo udugu, utu na utukufu wa kibinaadamu ulikuja na kuchukua nafasi ya chuki, adawa na hitilafu. Shakhsia na watu wakubwa wakiwa katika njia ya kufikia malengo makuu na matukufu, sio tu kwamba, huwa tayari kustahamili na kuvumilia magumu na vikwazo, bali huwa tayari kujitolea maisha yao kutokana na mapenzi na imani thabiti waliyonayo. Kwa maana kwamba, vikwazo katu haviwezi kuwazuia kufikia malengo yao. Mtume SAW akiwa na lengo la kuhakikisha kwamba, kalimatullah yaani neno la Allah linakuwa juu na kutekeleza majukumu ya risala yake ya Utume, alionesha ushujaa mkubwa katika medani ya vita, alisimama kidete na bila kutetereka na kusukuma mbele gurudumu la risala yake.

Imam Ali bin Abi Talib AS ambaye ushujaa wake katika vita na medani ya vita unafahamika na kila mtu na historia ya Uislamu inaliweka wazi hilo, anabainisha ushujaa mkubwa wa Bwana Mtume SAW. Anasema kuwa, kila mara moto wa vita ulipokuwa ukishadidi basi tulikuwa tukikimbilia kwa Mtume SAW na kumfanya kuwa kinga yetu. Kwa hakika Ahlul Bayt AS walikumbana na mazingira magumu mno katika kipindi cha kilele cha utawala wa Bani Umaiyya na baada ya hapo Bani Abbas; hata hivyo walistahamili yote hayo na kuweza kuhuisha vizuri turathi na utamaduni wa Bwana Mtume SAW na wakaandaa uwanja na mazingira mazuri kwa ajili ya kulea na kutayarisha maulama na wasomi wakweli.

Katika kipindi ambacho sunna asili za Mtume SAW zilikuwa katika kufifizwa kwa namna ambayo hata riwaya na hadithi  zilikuwa katika hali ya kugeuzwa, shakhsia kama Imam Baqir AS na Imam Sadiq AS waliweza kukusanya hadithi  na kufanya hima kubwa ya kueneza mafundisho sahihi ya dini tukufu ya Kiislamu. Kwa msingi huo viongozi hao wa Waislamu wakaweza kuzuia dini hii ya Mwenyezi Mungu kupotoshwa na sunna za Mtume SAW kutofanyiwa kazi. Kutokana na jukumu la Uimamu kuwa nyeti mno, Imam alikuwa akisisitiza na kuainisha mrithi na Imam atakayekuja baada yake tena kwa kumtaja kwa jina.

Historia inaonesha kuwa, kila Imam miongoni mwa Maimamu wa Ahlul Bayt AS alifanya hima kubwa katika kipindi cha uhai wake na kuitumia sehemu kubwa ya umri wake kwa ajili ya kueneza mafundisho sahihi ya Kiislamu na kuweka wazi njia ya hidaya ya uongofu iliyoletwa na Mtume Muhammad SAW.

Historia inashuhudia kwamba, Ahlul Bayt wa Mtume SAW walifasiri na kubainisha kwa usahihi mafundisho ya dini na hivyo kuwa na nafasi muhimu katika kuhifadhi na kubakia mafundisho ya Kiislamu. Hii leo  Ahlul Bayt wa Mtume SAW wametuachia turathi yenye thamani ya sira na hadithi zao ambazo zimejaa miongozo katika kila nyuga. Licha ya kuwa kile ambacho kimetufikia leo ni sehemu ndogo tu ya bahari yenye maarifa tele ya shakhsia hawa wakubwa; lakini hata funda la bahari hii nalo pia ni neema kubwa kwa wenye kiu ya ukweli. Pamoja na mafundisho ya Mtume SAW na watu wa nyumba yake Tukufu kuzungumzia masuala mbalimbalia ya kijamii, kiitikadi, kimaadili na masuala ya mtu binafsi; lakini shakhsia hao walikuwa na nafasi muhimu na maalumu katika kueleza na kubainisha masuala ya kimsingi na ya itikadi ya Uislamu. Laiti kusingekuweko hima na juhudi yao kubwa katika uga wa kubainisha masuala ya kimsingi na ya kiitikadi, hii leo mafundisho ya Kiislamu yasingebakia isipokuwa upotovu mtupu. Licha ya watu wa nyumba ya Bwana Mtume SAW kukumbana na vikwazo na masaibu mengi, lakini masuala hayo hayakuwa sababu ya kupungua kwa hima na idili yao katika kutekeleza majukumu yao ya kuwafikishia watu mafundisho sahihi ya dini ya Kiislamu. Jitihada zao zilipelekea kuasisiwa ustaarabu adhimu  wa Kiislamu wenye misingi ya Tawhidi.

Wapenzi wasikilizaji muda wa kipindi hiki umefikia tamati. Kwa leo sina budi kuishia hapa, tukutane tena wiki ijayo katika sehemu ya mwisho ya mfululizo wa Bustani ya Uongofu. Ninakuageni nikikutakieni kila la kheri.

Andika maoni


Msimbo salama (Security code)
Upyesha (Refresh)