Tovuti Hii Imefungwa. Tumehamia Kwenye Parstoday Kiswahili
Jumanne, 20 Mei 2014 15:45

Bustani ya Uongofu (58)

Bustani ya Uongofu (58)

Ni matumaini yangu kuwa hamjambo wapenzi wasikilizaji na karibuni katika sehemu nyingine ya kipindi hiki cha Bustani ya Uongofu. Kama tulivyosema katika kipindi chetu kilichopita,  Ahlul Bayt AS walikuwa na uhusiano wa kina na wa kimanaawi na Qur'ani Tukufu. Engo zao zote za maisha, uwepo wao na shakhsia yao ilikuwa imechanganyika na mafundisho pamoja na maarifa ya Qur'ani Tukufu. Daima Ahlul Bayt AS walikuwa wakibainisha masuala mbalimbali yanayohusiana na maarifa ya Kiislamu kama vile kuwalingania watu Tawhidi, kubainisha daraja ya Utume, Uimamu na kubainisha sheria za Kiislamu na falsafa yake. Waliyafanya hayo wakitumia hoja za Qur'ani sambamba na kubainisha tafisiri sahihi ya aya za Kitabu hicho kitukufu. Sehemu hii ya 58 ya kipindi hiki itaendelea kubainisha maudhui ya Qur'ani na Ahlul Bayt. Kuweni nami hadi mwisho wa kipindi hiki kusikiliza yale niliyokuandalieni kwa leo. Karibuni.

Imenukuliwa kuwa, katika sira na mwenendo wa Imam Muhammad Baqir AS, kama walivyokuwa Maimamu wengine watoharifu kutoka katika kizazi cha Mtukufu Mtume SAW, yeye alikuwa mfasiri na wakati huo huo mlinzi na mwenye kuhifadhi Qur'ani na aina yoyote ile ya upotoshaji. Imam Baqir AS alikuwa akisisitiza juu ya kufanyiwa kazi Qur'ani Tukufu katika jamii na kuwalea wanaadamu kwa misingi ya Qur'ani. Inanukiwa kwamba, Imam Baqir AS alikuwa akiandaa vikao vya Qur'ani kwa masahaba wake na watu wengine kwa ujumla na kubainisha mambo mbalimbali yanayohusiana na Kitabu hicho cha Mwenyezi Mungu. Watu na maulama kutoka maeneo mbalimbali walihudhuria vikao hivyo na walikuwa wakiuliza kuhusiana na halali na haramu na vile vile kuhusiana na tafsiri ya Qur'ani. Hakuna mtu ambaye alikuwa akitoka katika kikao hicho pasina ya kupata jibu la kukinaisha kutoka kwa Imam Muhammad Baqir AS.  Imam Baqir AS alikuwa akiitambua Qur'ani kuwa ni mhimili wa mambo yote ya maisha na kigezo sahihi cha njia ya maisha na alikuwa akisisitiza sana kuhusiana na nukta hii kwamba, mtu hawezi kuwa miongoni mwa marafiki wa Ahlul Bayt AS madhali hajaitanguliza na kuifanya Qur'ani kuwa mhimili wa maisha yake na kuathiriwa na vigezo vyenye thamani vya Kitabu hiki kitakatifu.

Imam Baqir AS anasema kuhusiana na hilo kwamba: "Tambua kwamba, huwezi kuwa miongoni mwa wanaotupenda sisi isipokuwa kama utafuata njia ya Qur'ani, na Qur'ani inapotaka watu wafanye Zuhdi, wewe ufanye zuhdi na uogope onyo, indhari na hofu inayobainishwa na Qur'ani. Katika mazingira kama haya, hata kama watu wote wa mji watakuwa dhidi yako na waseme kwamba, wewe ni mtu mbaya, maneno hayo hayatakukasirisha na kama watakusifia na kusema wewe ni mtu mstahiki, basi maneno yao hayo hayatakufurahisha na kukufanya uridhike.

Kuanisika na kushikamana na Qur'ani Tukufu zilikuwa miongoni mwa sifa za Imam Jaafar Sadiq AS na alitambuliwa mno kwa hilo. Imam Sadiq alikuwa akiamini kwamba, kusoma Qur'ani Tukufu ndio sababu pekee ya kupata utulivu wa ndani na wa nafsi. Aidha Imam Sadiq AS alikuwa akiamini kwamba, kusoma Qur'ani kunapaswa kuambatana na masharti yake. Amenukuliwa akisema kwamba: Msomaji wa Qur'ani anahitajia vitu vitatu: Moyo wenye unyenyekevu, mwili huru (ulioacha kila kitu) na sehemu tulivu. Wakati moyo wake utakapokuwa na unyenyekevu  na khushui kwa ajili ya Mwenyezi Mungu, shetani  atamkimbia, wakati anapoufanya mwili kuwa huru na kila kitu cha kidunia, wakati huo moyo wake huwa tayari kuipokea Qur'ani na wakati huo roho yake huainisika na kufungamana na Mwenyezi Mungu, na hivyo kuonja utamu wa mazungumzo ya Mwenyezi Mungu na waja wake wema na kwa muktadha huo, rehma za Mwenyezi Mungu humdhihirikia.

Malik bin Anas kiongozi wa madhehebu ya Kisuni ya Maliki anasema kuhusiana na kufungamana Imam Sadiq AS na Qur'ani Tukufu kwamba: Kwa hakika sikumpata Imam Sadiq AS isipokuwa katika hali tatu. Nilimpata imma anasali, amefunga au anasoma Qur'ani Tukufu.

Katika kipindi ambacho harakati za upotofu zilikuwa tishio kubwa kwa akthari ya jamii za Kiiislamu, Imam Jaafar Sadiq AS alinyanyua juu bendera ya haki na ukweli wa Uislamu na kubainisha maarifa asili ya dini tukufu ya Kiislamu. Alisimama kukabiliana na makundi ambayo yalikuwa yakieneza baina ya watu ufahamu usio sahihi kuhusiana na Qur'ani. Imam Sadiq AS alikuwa akiitambua Qur'ani Tukufu kuwa ni maagizo na amri za Allah kwa ajili ya mwanadamu na daima alikuwa akiwausia masahaba na wafuasi wake kwamba, wayaunde na kuyatengeneza maisha yao na Qur'ani Tukufu. Kwa hakika mshikamano na mfungamano uliopo kati ya Qur'ani na Ahlul Bayt AS sio kitu ambacho kimepatikana kutokana na athari ya kujifunza na kufundisha au ni kitu ambacho kina mfungamano wa nje na ambacho kutokana na mazingira ya maisha kubadilika, basi maisha hupata nguvu au kudhoofika. Bali uhusiano na mfungamano huu mkubwa na usiosambaratika umepatikana kwa irada ya Mwenyezi Mungu.

Wapenzi wasikilizaji, kwa upande wa Imam Mussa al-Kadhim AS inanukuliwa kwamba, alikuwa amefungamana mno na Qur'ani Tukufu, kiasi kwamba, wakati alipokuwa akisoma Qur'ani msikilizaji alikuwa akiathirika mno. Inanukuliwa kwamba, Imam Ali bin Mussa al-Ridha AS alikuwa ameshikamana mno na Qur'ani Tukufu kiasi kwamba, hata katika lahadha ya mwisho ya maisha yake alikuwa akisoma Qur'ani Tukufu. Imam Ridha AS aliitambulisha Qur'ani kwamba, ni mhimili wa hidaya na uongofu na kusema: "Qur'ani ni maneno ya Mwenyezi Mungu. Usitafute hidaya na uongofu katika kitu kingine kisichokuwa Qur'ani, kwani kufanya hivyo kutakufanya upotee."

Katika sira na mwenendo wa Imam Jawad AS inanukuliwa kwamba, alikuwa ameshikamana na Qur'ani na alikuwa akiitumia kutoa majibu dhidi ya upotofu wa watawala wa zama zake. Aidha aliitumia Qur'ani kubatilisha hadithi potofu na za kupandikiza zilizokuwa zikinasibishwa kwa Mtume SAW. Mtume SAW anasema wakati alipokuwa akibainisha umuhimu wa Qur’ani katika maisha ya wanadamu kwamba: Pindi mtakapofikwa na fitna na kukuchanganyeni kama usiku wenye kiza, basi ni juu yenu kushikamana na Qur'ani. Kwa hakika hapa Bwana Mtume SAW alikuwa akibainisha umuhimu wa risala ya Qur’ani yaani hidaya na kuongoza watu. Kwa hakika Qur’ani ndicho kitabu ambacho kinaweza kumuongoza mwanadamu kuelekea katika saada na ukamilifu na kuwa kama taa aliyoshika mkononi ambayo inammulikia  na kumuonyesha njia ya saada na ufanisi. 

Katika sehemu nyingine Bwana Mtume SAW anasema: "Qur'ani ina dhahiri na batini, dhahiri yake ni hukumu na batini yake ni elimu, dhahiri yake ni yenye kustaajabisha na nzuri, na batini yake ina kina."  Katika maneno haya Bwana Mtume SAW anazibainisha hukumu na sheria za Mwenyezi Mungu kuwa ni dhahiri ya Qur’ani na kwamba, ni dawa ya kutibu mienendo ya wanadamu. Aidha anaitaja batini ya Qur’ani kuwa inadhamini mahitaji ya ndani na ya kifikra. Kwa upande wake Imam Ali bin Abi Talib AS anaitaja Qur’ani kuwa ni wenzo wa amani, chimbuko la hukumu za Mwenyezi Mungu, msimu wa machipuo wa nyoyo na chemchemi za elimu."

Wapenzi wasikilizaji kutokana na kumalizika muda wa kipindi hiki sina budi kukomea hapa kwa leo nikitaraji kwamba, mtajiunga nami wiki ijayo katika sehemu nyingine ya kipindi hiki.

Wassalaamu Alaykum Warahmatullahi Wabarakaatuh

Andika maoni


Msimbo salama (Security code)
Upyesha (Refresh)