Tovuti Hii Imefungwa. Tumehamia Kwenye Parstoday Kiswahili
Jumapili, 11 Mei 2014 19:15

Bustani ya Uongofu (57)

Bustani ya Uongofu (57)

Ni matumaini yangu kuwa, hamjambo wapenzi wasikilizaji na karibuni katika sehemu nyingine ya kipindi hiki cha Bustani ya Uongofu. Kipindi chetu cha juma lililopita kilibainisha na kuelezea vizIto viwili yaani Qur'ani Tukufu na Ahlul Bayt na jinsi Mtume SAW alivyowausia Waislamu kushikamana navyo na kwamba, mwenye kushikamana navyo katu hawezi kupotea. Kama tulivyosema juma lililopita ni kuwa, vizito hivi viwili tulivyoachiwa na Bwana Mtume SAW vinashikamana na vina uhusiano usiokanushika.

Qur’ani Tukufu ni Kitabu cha hidaya na uokozi na baada ya Qur’ani Tukufu, Ahlul Bayt wa Mtume SAW ndio njia pekee ya kuyafikia maarifa aali yaliyopo ndani ya Qur’ani. Aidha tulisema kuwa, kwa wale ambao wanatafuta saada na hidaya ya hapa duniani na kesho akhera, basi bila shaka hawana budi kuyatafuta hayo katika vizito hivi viwili yaani Qur’ani Tukufu na Ahlul Bayt wa Mtume tena kwa sura ya pamoja, yaani sio kukishika kimoja na kuacha kingine.

Sehemu yetu ya 57 ya mfululizo huu itaendelea kuzungumzia maudhui hii. Tafadhalini kuweni nami hadi mwisho wa kipindi hiki. Karibuni.

Miongoni mwa natija za kushikamana na Qur'ani Tukufu pamoja na Ahlul Bayt zake (AS) ni kupotea na kuwa potofu juhudi zozote zile za kushikamana na kimoja hiki na kukiacha kingine. Kwa muktadha huo basi, watu ambao walianzisha nara ya "Qur'ani inatutosha" sio tu kwamba, walijiharamishia hidaya na uongofu wa Ahlul Bayt AS, bali waliondokea kuwa mbali na ukweli na uhakika wa Qur'ani Tukufu. Wao badala ya kushikamana na Qur'ani waliamua kufuata kitu walichotengeneza wao wenyewe.

Vile vile watu ambao walidai kuwa ni wafuasi wa Ahlul Bayt na wakaiweka kando Qur'ani Tukufu, kimsingi walijiharamishia kuifuata Qur'ani na Ahlul Bayt na wakakumbwa na upotofu. Kwa hakika uhusiano wa Qur'ani na Ahlul Bayt ni uhusiano wa kimaanawi na wa kina ambapo kulitambua hilo ni jambo ambalo litatusaidia sisi kuidiriki na kuifahamu dini kwa njia sahihi. Inaeleweka wazi kwamba, daima uhusiano wa vitu hivi viwili katika ulimwengu unatokana na kunasibiana kwake. Kwa hakika Qur'ani ni nuru; nuru ambayo inaangaza haki kutoka katika batili.

Ahlul Bayt AS nao, kwa upande wao ni nuru na nafasi yao ya kuwaongoza watu katika kipindi chote cha historia ni jambo ambalo liko wazi kwa kila mtu. Qur'ani iko kwa namna ambayo, hawaifahamu na kudiriki uhakika wake isipokuwa watu wasafi; na Ahlul Bayt AS ndio waja wema na wasafi. Sifa hizo mbili na kufungamana na vizito hivyo viwili kumepelekea kutokea mfungamano wa mbinguni baina ya amana hizi mbili za Mwenyezi Mungu. Kiasi kwamba, kukifuata kimoja na kuacha kingine kati ya vitu hivi viwili ni jambo lisilowezekana.

Imam Sajjad AS anasema: Imam anaongoza kuelekea Qur'ani; na Qur'ani inaongoza kuelekea Imam na hii ndio pale Mwenyezi Mungu aliposema: "Hakika hii Qur'ani inaongoa kwenye ya yaliyonyooka kabisa."

Moja ya sifa muhimu kuhusiana na mahusiano yaliyopo kati ya Qur'ani na Ahlul Bayt AS ni kwamba, baada ya Mtume SAW, Ahlul Bayt AS ndio mhimili mkuu wa kubainisha madhumuni ya Qur'ani  na tafsiri ya aya zake.  Ahlul Bayt AS walikuwa wakifahamu vyema makusudio na madhumuni ya Qur'ani Tukufu na walikuwa wakiwabainisha hilo watu. Imam Muhammad Baqir AS anasema:

"Sisi ni hazina ya elimu ya Mwenyezi Mungu, wabainishaji wa Wahyi wa Mwenyezi Mungu na ni mahuja wa Mwenyezi Mungu kwa wakazi wote wa ardhini."

Miongoni mwa juhudi zinazodhihirika wazi katika sira na mwenendo wa Bwana Mtume SAW na Ahlul Bayt zake ni kwamba, waja hao wateule wa Mwenyezi Mungu walikuwa wakitaka kuwabainishia watu maarifa na fadhila za Qur'ani ili wawafanye watu wawe na ufahamu kuhusiana na Kitabu hiki.

Kwa hakika wao walikuwa wakikitambua Kitabu cha Qur'ani kwamba, ni kitabu cha hidaya na uongofu kwa ajili ya wanadamu ambacho kinawaongoza kutoka katika kiza cha ujahili na upotofu, kuelekea katika mwanga wa elimu na saada. Aidha Mtume SAW na Ahlul Bayt AS hawakuitambua Qur'ani Tukufu kuwa ni  maalumu kwa ajili ya eneo, lugha, utamaduni au taifa fulani na maalumu.

Kwa muktadha huo basi, Qur'ani ni Kitabu cha walimwengu wote. Imam Sadiq AS anazungumzia suala la kwamba, Qur'ani ni kwa ajili ya watu wote pale anaposema kuwa, Qur'ani ina majibu ya mahitaji yote ya jamii ya mwanadamu mpaka siku ya Kiyama. Aidha kuhusiana na uwezo wa Qur'ani wa kutoa majibu kwa mahitaji ya kifikra, Imam Sadiq AS anasema:

Naapa kwa Mola Mlezi kwamba, Mwenyezi Mungu katika Qur'ani hakuacha kitu ambacho waja wanakihitajia, isipokuwa alishusha katika Qur'ani. Kiasi kwamba, hakuna mja ambaye anaweza kudai kwamba, ya laiti maudhui hii ingekuweko katika Qur'ani.

Nukta nyingine ya wazi katika maisha ya Mtume SAW na Ahlul Bayt zake AS ni kushikamana kwao na Qur'ani katika pande zote. Kufungamana huku kulikuwa kukubwa kiasi kwamba, wao walikuwa dhihirisho la aya za Qur'ani Tukufu. Ndimi zao zilikuwa zimefungamana na Qur'ani huku akili na fikra zao zikifungamana na kuainisika na maana ya aya za Kitabu hicho kitukufu. Vitendo na miamala yao kwa hakika ilikuwa ikiakisi dhihirisho la kweli la Qur'ani. Sira na mwenendo wa watukufu hao inaonesha jinsi walivyokuwa na mapenzi makubwa na Qur'ani Tukufu. Historia inaonesha kuwa, Mtume SAW alikuwa na mapenzi makubwa mno na Qur'ani, kiasi kwamba, wakati wa usiku Mtume SAW alikuwa akijishughulisha na kusoma sura maalumu za Qur'ani na hakuacha mwendo huo hata wakati anapokuwa yu mgonjwa sana. Huba na mapenzi ya Mtume kwa Qur'ani yalikuwa makubwa mno kiasi kwamba, wakati mwingine alikuwa akikariri aya moja kuanzia usiku mpaka asubuhi. Wapenzi wasikilizaji kwa hakika kuna mengi ya kusema kuhusiana na kushikamana Mtume SAW na Ahlul Bayt AS na Qur'ani Tukufu, lakini muda wa kipindi hiki umefikia tamati tukutane tena wiki ijayo ambapo tutaendelea na maudhui yetu ya Qur'ani na Ahlul Bayt.

Wassalaamu Alaykum Warahmatullahi Wabarakaatuh.

Na Salum Bendera

Andika maoni


Msimbo salama (Security code)
Upyesha (Refresh)