Tovuti Hii Imefungwa. Tumehamia Kwenye Parstoday Kiswahili
Jumatatu, 05 Mei 2014 15:45

Bustani ya Uongofu (56)

Bustani ya Uongofu (56)

Ni matumaini yangu kuwa, hamjambo wapenzi wasikilizaji na karibuni katika sehemu nyingine ya kipindi hiki cha Bustani ya Uongofu. Kama tulivyotangulia kusema katika vipindi vyetu vilivyopita lengo la kipindi hiki ni kuzungumzia mitazamo ya Mtume SAW na Ahlul Bayt AS kuhusiana na masuala mbalimbali ya kielimu, kidini, kisiasa na kadhalika. Juma lililopita tulizungumzia Swilat Rahm yaani kuunga udugu na kubainisha mitazamo ya Mtume SAW na Ahlul Bayt wake AS kuhusiana na suala hilo. Tuliona jinsi kuunga udugu kulivyokokotezwa na kutiliwa mkazo katika Uislamu. Aidha tulibainisha faida za kimaanawi, kidunia na kiakhera. Kipindi chetu cha juma hili kitazungumzia japo ni kwa mukhtasari mfungamo wa Qur'ani Tukufu na Ahlul Bayt AS. Kuweni nami hadi mwisho wa kipindi hiki.

Qur'ani Tukufu imejumuisha maarifa aali ya Mwenyezi Mungu katika uga wa kumtambua Allah na uhakika wa Tawhidi, sifa za Mitume wa Mwenyezi Mungu, siri za ulimwengu wa ghaibu, ada zilizotawala katika jamii ya mwanadamu, kumtambua mwanadamu pamoja na hatima yake. Qur'ani pia ina nukta zinazohusiana na mifumo ya kijamii, haki, mifumo ya kiuchumi na kisiasa ambayo wanaadamu wanaihitajia kwa ajili ya saada na mafanikio yao. Kitabu hiki cha Mwenyezi Mungu kinamuonesha mwanadamu njia ambayo kama ataifuata basi itamuokoa na utumwa wa madhalimu na itamuondoa pia katika umateka na kufunguliwa kutoka katika minyororo ya ujinga, hurafa na upotovu. Qur'ani ina vigezo madhubuti vya kuitambua haki kutoka katika batili. Kutambua sifa na vigezo hivi ndiko kunakomfanya mwanadamu adiriki adhama na kuwa juu Qur'ani Tukufu. Kutokana na kuwa kukitambua Kitabu hiki cha Mwenyezi Mungu na kustafidi nacho, kunatofautiana kulingana na vipawa vya watu, vile vile kudiriki adhama yake nalo ni jambo litakalokuwa tofauti. Hivyo basi, kutambua uhakika wa Qur'ani Tukufu na kuwa na ufahamu nayo yote, ni jambo ambalo haliwezekani kwa urahisi isipokuwa kwa watu wenye moyo mtoharifu na ambao fuadi na nyoyo zao zina nafasi maalumu ya kupokea nuru ya Qur'ani. Kwa muktadha huo, ili kutambua engo mbalimbali za adhama na fadhila za Qur'ani hatuna budi kurejea kwa watu ambao ni wabebaji wa elimu za Mwenyezi Mungu na ambao wanatambua siri za kitabu hiki adhimu yaani Mtume SAW na Ahlul Bayt zake watoharifu AS; na kupitia kivuli cha mafundisho yao tuweze kukifahamu kitabu hiki pamoja na adhama yake.

Kama mnavyojua mwisho mwa umri wake mtukufu, Bwana Mtume SAW aliwausia Waislamu washikamane na vizito viwili vyenye thamani kubwa pale aliposema: "Hakika mimi ninakuachieni vizito viwilivya thamani nakama mtashikamana navyo vyote viwili, kamwe hamtapotea baada yangu. Navyo ni Kitabu cha Mwenyezi Mungu na Ahlul Bayt zangu."

Hapana shaka kuwa, vizito hivi viwili tulivyoachiwa na Bwana Mtume SAW vinashikamana na vina uhusiano usiokanushika. Qur'ani Tukufu ni Kitabu cha hidaya na uokozi na baada ya Qur'ani Tukufu, Ahlul Bayt wa Mtume SAW ndio njia pekee ya kuyafikia maarifa aali yaliyopo ndani ya Qur'ani. Kwa msingi huo basi, kushikamana na Qur'ani Tukufu kunapaswa kuambatana na kufuata miongozo ya Ahlul Bayt wa Mtume SAW. Ni kwa kuzingatia uhakika huo, ndio maana miongoni mwa masuala muhimu na yenye thamani katika maarifa ya dini ya Kiislamu hususan Madhehebu ya Kishia ni kuwafuata Ahlul Bayt AS sambamba na kuifuata Qur'ani Tukufu.

Kwa hakika Mtume SAW anakutambua kushikamana na Qur'ani na Ahlul Bayt AS kuwa ni chimbuko la hidaya na kizuizi cha kupotea. Katika sehemu nyingine Mtume SAW anawataja Ahlul Bayt AS kuwa ni safina ya uokozi wa umma.  Mtume SAW amenukuliwa kuhusiana na hilo akisema kwamba:

"Bila shaka mfano wa Ahlul Bayt wangu kwenu, ni kama safina ya Nuhu, mwenye kuipanda ataokoka na mwenye kuiacha ataangamia." Katika hadithi hii Bwana Mtume SAW anawaarifisha Ahlul Bayt wake AS kuwa ni Safina ya wokovu, kimbilio na marejeo ya kuokoka na upotovu; kiasi kwamba, kutopanda katika Safina hii yaani kutoshikamana na Ahlul Bayt hawa wa Mtume SAW, hakuna natija nyingine ghairi ya kuangamia na kukumbwa na tufani ya upotovu. Kwa hakika sisitizo hili la Bwana Mtume SAW la kushikamana na Ahlul Bayt AS linabainisha juu ya ulazima wa kustafidi na elimu ya Maasumina isiyo na kikomo pamoja na nafasi yao ya kipekee katika kubainisha na kufasiri maarifa ya Qur'ani. Kwa wale ambao wanatafuta saada na hidaya hapa duniani na kesho akhera, basi bila shaka hawana budi kuyatafuta hayo katika vizito hivi viwili yaani Qur'ani Tukufu na Ahlul Bayt wa Mtume tena kwa sura ya pamoja, yaani sio kukishika kimoja na kuacha kingine. Hatua ya Bwana Mtume  SAW ya kuwausia Waislamu washikamane na Thaqalein yaani vizito viwili inaonesha nafasi muhimu ya vizito hivi viwili katika kuwaongoza wanaadamu na kuainisha jukumu la Waislamu katika kuvifuata vizito hivi viwili.

Wakati wa kushuka aya za mwanzo za Kitabu Kitukufu cha Qur'ani katika zama za Bwana Mtume SAW, suala la kuzingatia maana na mafahimu ya Wahyi lilizingatiwa sana sambamba na umuhimu kufikia na kuelewa ujumbe aali na uliofungamana na Qur'ani. Mtume SAW alikuwa mfasiri wa kwanza wa Qur'ani ambaye alibainisha ujumbe muhimu uliokuwako katika maneno ya Allah na akalionesha na kuliweka wazi hilo katika sira yake ya kivitendo. Baada ya Mtume SAW, Ahlul Bayt wa Mtume ndio wafasiri wa kweli wa Qur'ani Tukufu. Mwenyezi Mungu anasema katika aya ya 7 Surat al-Imran kwamba:

"Na wala hapana ajuaye maana yake ila Mwenyezi Mungu. Na wale waliozama katika elimu." Kwa mujibu wa hadithi nyingi zinazopatikana katika vyanzo vya historia ni kuwa kusudio la waliobobea na kuzama katika elimu ni Ahlul Bayt wa Mtume SAW. Watu ambao Allah amewaepusha na kila aina ya uchafu na ubatili kama anavyosema katika aya ya 33 ya Surat al-Ahzab kwamba:

"Hakika Mwenyezi Mungu anataka kukuondoleeni uchafu watu wa Nyumba ya Mtume, na kukutakaseni sanasana.

Hatua ya Mtume SAW na Ahlul Bayt AS ya kuwafundisha watu maarifa ya Qur'ani kwa upande mmoja ililenga kuandaa uwanja wa watu kudiriki adhama ya Qur'ani na kwa upande mwingine hatua yao ya kubainisha adhama ya Qur'ani ilikuwa na lengo la kuwashajiisha watu wakirejee zaidi Kitabu hicho Kitakatifu.

Kwa hakika kubainishwa adhama ya Qur'ani kulikofanywa na Mtume SAW na Ahlul Bayt AS ulikuwa ni utangulizi kwa ajili ya kuandaa uwanja wa kifikra na kiroho baina ya watu kwa ajili ya kuzingatia ustahiki wa Qur'ani Tukufu na kustafidi na maarifa yenye kuleta uhai. Sira ya kivitendo na msimamo wa Bwana Mtume SAW na Ahlul Bayt zake AS inaweka wazi hilo katika mazungumzo na jinsi walivyokabiliana na wapinzani ambapo waliiweka Qur'ani na kuifanya kuwa mhimili wa hidaya.

Mtume SAW anasema wakati alipokuwa akibainisha umuhimu wa Qur'ani katika maisha ya wanadamu kwamba: Pindi mtakapofikwa na fitna na kukuchanganyeni kama usiku wenye kiza, basi ni juu yenu kushikamana na Qur'ani.

Kwa hakika hapa Bwana Mtume SAW alikuwa akibainisha umuhimu wa risala ya Qur'ani yaani hidaya na kuongoza watu. Kwa hakika Qur'ani ndicho kitabu ambacho kinaweza kumuongoza mwanadamu kuelekea katika saada na ukamilifu na kuwa kama taa aliyoshika mtu mkononi ambayo inammulikia  na kumuonyesha njia ya saada na ufanisi.  Katika sehemu nyingine Bwana Mtume SAW anasema: Qur'ani ina dhahiri na batini, dhahiri yake ni hukumu na batini yake ni elimu, dhahiri yake ni yenye kustaajabisha na nzuri na batini yake ina kina."

Katika maneno haya Bwana Mtume SAW anazibainisha hukumu na sheria za Mwenyezi Mungu kuwa ni dhahiri ya Qur'ani na kwamba, ni dawa ya kutibu mienendo ya wanadamu. Aidha anaitaja batini ya Qur'ani kuwa, inadhamini mahitaji ya ndani na ya kifikra. Kwa upande wake Imam Ali bin Abi Talib AS anaitaja Qur'ani kuwa ni wenzo wa amani, chimbuko la hukumu za Mwenyezi Mungu na msimu wa machipuo wa nyoyo na chemchemi za elimu.

Wapenzi wasikilizaji kwa leo nalazimika kukomea hapa kutokana na kumalizika muda wa kipindi hiki. Tukutane tena wiki ijayo katika sehemu nyingine ya kipindi hiki. Kwaherini.

Andika maoni


Msimbo salama (Security code)
Upyesha (Refresh)