Tovuti Hii Imefungwa. Tumehamia Kwenye Parstoday Kiswahili
Jumapili, 27 Aprili 2014 17:19

Bustani ya Uongofu (55)

Bustani ya Uongofu (55)

Assalaamu Alaykum wapenzi wasikilizaji na karibuni katika sehemu nyingine ya kipindi hiki cha Bustani ya Uongofu. Vipindi vyetu kadhaa vilivyopita vilizungumzia uhusiano wa kifamilia pamoja na haki za watoto pamoja na wazazi na jinsi watoto wanavyopaswa kuamiliana na wazazi wao yaani baba na mama. Sehemu hii ya 55 ya mfululizo huu itatupia jicho mitazamo ya Mtume SAW na Ahlul Bayt AS kuhusiana na suala la kuunga udugu. Ni matumaini yangu kuwa, mtakuwa nami hadi mwisho wa kipindi hiki. Karibuni.

Moja ya vielelezo muhimu vya jamii salama na yenye saada ni kuweko mahusiano sahihi na miamala inayoambatana na mapenzi na huba baina ya wanajamii. Kwa hakika dini tukufu ya Kiislamu imezingatia engo zote za uwepo wa mwanadamu. Dini ya Kiislamu ikiwa na lengo la kuandaa uhusiano wa mwanadamu na wanadamu wenzake, umeweka sheria zenye thamani ambapo miongoni mwa sheria hizo ni Swilat Rahm yaani kuuunga udugu au kuweko mawasiliano na mahusiano ya kifamilia au ya wanandugu. Kwa hakika kujenga udugu na kuweko mawasiliano na maingiliano baina ya wanandugu ni jambo lenye nafasi maalumu na jambo hili limekokotezwa na kutiliwa mkazo mno. Katika utamaduni wa Kiislamu kuunga udugu maana yake ni mtu kuwatendea wema na hisani ndugu zake ikiwa ni pamoja na kukutana nao na kuwatatulia matatizo yao. Kiujumla tunaweza kusema kuwa, kila kazi au kitendo kinachopelekea kuunga udugu na wanandugu kinaitwa Swilat Rahm" hata kama itakuwa kazi ndogo sana kama kusalimia vizuri, kujibu salamu au kumpa mtu maji ya kunywa. Mkabala na hayo, kila kitendo cha kuwapuuza ndugu na kutowatekelezea haki zao kinaitwa kuwa ni kukata udugu jambo ambalo hupelekea kutokea pengo baina ya wanandugu.

Ada na sunna ya kuunga udugu ni miongoni mwa ratiba bora kabisa za kidini katika mazingira ya maisha na kuamiliana na watu. Jambo hilo lina nafasi maalumu katika sira na mwenendo wa Mtume SAW na Ahlul Bayt zake AS. Licha ya kuwa maisha ya kisasa na shughuli nyingi za kila siku pamoja na mazonge yake, wakati mwingine hulifanya jambo hili kukabiliwa na changamoto kadha wa kadha, lakini kulinda thamani na ada zenye faida na ambazo zina mizizi ya dini ni miongoni mwa mambo yanayoimarisha mahusiano na maingiliano ya kifamilia. Mtume SAW alitilia mkazo mno juu ya sunna na ada nzuri ya kuunga udugu. Hata mwanzoni mwa kazi yake ya kuwafikishia watu risala na ujumbe wake kutoka kwa Mwenyezi Mungu, Mtume SAW aliwazingatia ndugu zake wa karibu katika hilo na kwa amri ya Mwenyezi Mungu akawaita na kuwalingania Uislamu. Mtume SAW alikuwa akiutambua udugu kuwa ni mwanga wa rehma za Alllah. Mtume SAW amenukuliwa akisema kuwa, "udugu ni mwanga na ishara za rehma za Mwenyezi Mungu."

Kwa hakika Mtume SAW alikuwa akilipa umuhimu suala la mahusiano ya kidugu kiasi kwamba, kama itatokea hajamuona mmoja wa masahaba zake basi alikuwa alikuwa akiulizia habari zake. Akisikia kwamba, mmoja wa masahaba zake yu mgonjwa au ana tatizo, basi alikuwa akifunga safari na kwenda kumtembelea kwa shabaha ya kwenda kumjulia hali na akifika huko humliwaza na kumpa moyo. Ahlul Bayt wa Mtume SAW nao walikuwa namna hii na daima walikuwa wakitilia mkazo suala la mahusiano na kuimarisha uhusiano wa kidugu na kifamilia. Kwa kutumia aya za Qur'ani Tukufu na hadithi za Maimamu watoharifu tunaweza kuugawa mara mbili utekelezaji wa Swilat Rahm au kuunga udugu. Mambo kama kusalimia, kuwaombea dua nduguzo, kuwataja kwa wema na kujitenga mbali na kuwasengenya, kuwatuhumu, kuwatusi, kuwasema kwa ubaya na kuacha kufitinisha ni miongoni mwa mambo yanayohesabiwa kuwa ni ya kuunga udugu kwa njia ya ulimi. Aidha kuwatembelea, kwenda kufanya nao mazungumzo, kwenda katika nyumba zao na kuwaalika kwako, kuanzisha nao urafiki baada ya kununiana, na kujitokeza ugomvi baina yenu, kuwatembelea wakiwa wagonjwa, kushiriki katika mazishi, kurekebisha na kuondoa ufisadi baina ya wanandugu ni mambo ambayo yanaweza kuhesabiwa kuwa ni kuunga udugu kivitendo.

Kuna hadithi nyingi zilizopokewa kutoka kwa Bwana Mtume SAW na Ahlul Bayt zake watoharifu AS zinazobainisha faida nyingi zinazopatikana kutokana na kuunga udugu. Baadhi ya faida za kuunga udugu ni za kiroho na kisaikolojia  na ni nyingine zinaashiria kuboreka maisha na kuleta marekebisho katika mahusiano ya watu sambamba na kuongeza huba, mapenzi na kuzikurubisha pamoja fuadi na nyoyo za watu katika jamii. Hapana shaka kuwa, kuwa na mahusiano yaliyojaa mapenzi baina ya wanandugu, ni miongoni mwa mambo ambayo huondoa wasi wasi mwingi na huiweka mbali roho ya mtu na tashwishi. Jambo hilo linasaidia katika uzima wa kisaikolojia wa mtu na lina taathira pia katika uzima wa mwili. Ni kwa kuzingatia ukweli huo, ndio maana Imam Jaafar Sadiq AS amenukuliwa akisema kwamba, mtu anayetaka kuwa na umri mrefu na uzima basi na aunge udugu. Ni kwa kuzingatia uhakika huo, ndio maana ikatajwa katika hadithi kwamba, moja ya mambo yanayochangia kuongezeka umri wa mtu ni kuunga udugu. Kwani katika kivuli cha mawasiliano na ndugu, mivutano na wasi wasi usio na maana huondoka na kupelekea kupatikana nishati, uchangamfu, utulivu na hata matumaini. Haya ni mambo ambayo yana taathira kubwa katika umri wa mtu. Imam Muhammad Baqir AS anasema: "Kuunga udugu huzifanya amali za mtu kuwa safi, huongeza mali, huondoa mabalaa, huifanya hesabu ya mtu siku ya Kiyama kuwa nyepesi na huchelewesha kifo cha mtu."

Kufanya jambo jema ni kuzuri na kwenye faida na humridhisha Allah kiasi kwamba, wakati mwingine hubadilisha kadari ya  Allah ambapo Mwenyezi Mungu hutoa jaza na ujira wa kumuongeza mja huyo umri kutokana na kitendo hicho kizuri alichokifanya. Imam Ali AS anasema: "Kuweni na maingiliano na ndugu zenu, hata kama wao wamekata uhusiano na nyinyi."

Mafundisho ya Kiislamu yanaonesha kuwa,  hata kama kuna mtu ameandaa uwanja wa kutuudhi, basi sisi hatuna haki ya kukata uhusiano na yeye. Siku moja bwana mmoja alikwenda kwa Mtume SAW na kumwambia: Yaa Rasulallah! Mimi nina ndugu ambao nina mahusiano na maingiliano nao, lakini wamekuwa wakinifanyia maudhi. Hivyo nimekata shauri kuachana nao, yaani kukata mahuasino nao. Mtume SAW akasema: Ukifanya hivyo, basi naye Allah atakuacha. Bwana yule akauliza, basi nifanye nini ewe Mtume wa Mwenyezi Mungu? Mtume SAW akamwambia, mtu ambaye amekunyima, wewe mpatie, mtu ambaye amekuacha wewe wasiliana naye, mtu ambaye amekufanyia dhulma, wewe msamehe. Ikiwa utafanya hivyo wakati wowote, basi Mwenyezi Mungu atakuwa ni mwenye kukuhami wewe.

Imenukuliwa kwamba, siku moja Bwana mmoja alimuuliza Imam Sadiq AS kwamba, baadhi ya ndugu zangu wana fikra na mitazamo inayokinzana na fikra zangu. Je wana haki juu yangu? Imam Jaafar Sadiq AS akasema: Ndio! Wana haki juu yako, haki ya kwanza ni haki ya udugu na familia, na haki ya pili ni haki ya Uislamu na Muislamu.

Wapenzi wasikilizaji muda wa kipindi hiki umefikia ukingoni kwa leo tukutane tena wiki ijayo katika sehemu nyingine ya mfululizo huu wa Bustani ya Uongofu, kipindi ambacho hutupia jicho na kuchambua kwa mukhtasari baadhi ya mitazamo ya Bwana Mtume SAW na Ahlul Bayt wake AS kuhusiana na masuala mbalimbali ya kielimu, kisiasa, kidini, kimalezi, kijamii na kadhalika.

Wassalaam Alaykum Warahmatullah Wabakaatuh.

 

Andika maoni


Msimbo salama (Security code)
Upyesha (Refresh)