Tovuti Hii Imefungwa. Tumehamia Kwenye Parstoday Kiswahili
Jumatatu, 14 Aprili 2014 18:24

Bustani ya Uongofu (54)

Bustani ya Uongofu (54)

Ni matumaini yangu kuwa, hamjambo wapenzi wasikilizaji na karibuni katika sehemu nyingine ya kipindi hiki cha Bustani ya Uongofu; kipindi ambacho hukujieni kila juma kupitia Idhaa ya Kiswahili Sauti ya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran. Katika kipindi chetu cha leo ambacho ni sehemu ya 54 tutaendelea kubainisha mitazamo ya Mtume SAW na Ahlul Bayt AS kuhusiana na haki walizonazo baba na mama pamoja na jinsi watoto wanavyopaswa kuamiliana na wazazi wao. Tafadhalini kuweni nami hadi mwisho wa kipindi hiki. Karibuni.

Hekima ya Mwenyezi Mungu inaonesha kuwa, katika mfumo wa ulimwengu na uumbaji, baba na mama ni wenzo muhimu wa Mwenyezi Mungu anaoutumia ambao una nafasi muhimu sana katika maisha ya mwanadamu. Kwa msingi huo basi, kutambua haki, kuwa na huruma na kuwashukuru wazazi yaani baba na mama ni jambo la kawaida na la kibinadamu ambalo linapaswa kufanyika pasina masimango yoyote kwa wazazi.

Kwa mujibu wa mtazamo wa Kiislamu ni kuwa, daraja na nafasi ya baba na mama ni ya juu mno na wazazi hao wana haki nyingi ambazo wanapaswa kufanyiwa na watoto wao. Katika maktaba ya malezi ya Mtume SAW na Ahlul Bayt AS, namna ya kuamiliana na kuwasiliana na baba na mama limechanganyika na adabu, heshima na unyenyekevu. Kwa maana kwamba, mtu anapoamiliana na baba au mama yake anapaswa kuamiliana naye kwa heshima, adabu na unyenyekevu. Kutokana na kuwa, baba na mama ndio sababu ya kuwepo mwanadamu, tunaweza kusema kuwa, hakuna mtu aliye karibu kwa mtu zaidi ya baba na mama miongoni mwa wanafamilia. Vile vile hakuna mtu mwenye huruma na mtu mwingine kuliko baba na mama kwa mtoto wao. Kwa maana kwamba, hakuna mtu anayeweza kuwa na huruma na mtu mwingine kuliko huruma ya baba au mama kwa mwanawe. Baada ya Mwenyezi Mungu, bila shaka mtu ni mdaiwa wa maisha yake kwa baba na mama. Viumbe hawa wawili wenye huruma, ndio waliomlea kwa huba na mapenzi makubwa mtoto wao katika kipindi cha udhaifu na hali ya kutojiweza ya utoto wake hadi wakamfanya kuwa mtu mwenye nguvu na mwenye kujiweza. Baba na mama huwa tayari walale njaa lakini wahakikishe watoto wao wamekula na kushiba.

Baba na mama hujitolea kwa kufumbia macho mambo mengi wanayoyahitajia na kukubali kuyakosa lakini mtoto wao apate. Kwa msingi huo basi, nafasi ya baba na mama katika maisha ya watoto ni yenye thamani kubwa na bila shaka haikanunishiki. Kwa muktadha huo, watoto wanapaswa kutambua thamani ya baba na mama na kuwakirimu kwa huba na kuishi nao kwa wema sambamba na kuwakidhia mahitaji yao ya lazima. Kwa hakika nafasi ya baba na mama ni kubwa na aali na inaheshimiwa na dini zote za mbinguni.

Mtume SAW na Ahlul Bayt wake AS wamebainisha mara chungu nzima nafasi na daraja ya wazazi na kuwausia watu kwamba, wasighafilike na suala la kuwaheshimu na kuwatendea wema baba na mama. Umuhimu wa jambo hilo ni mkubwa mno kiasi kwamba, katika Qur'ani na katika hadithi zilizopokewa kutoka kwa watu wa nyumba ya Bwana Mtume SAW imeusiwa mno juu ya mtu kuheshimu haki za wazazi hata kama baba na mama watakuwa ni wafuasi wa dini na madhehebu mengine.

Siku moja bwana aliyejulikana kwa jina la Muammar bin Khalad alimuuliza Imam Ridha AS kwamba: Je niwaombee dua ya kheri baba na mama yangu ambao hawako katika njia ya haki? Imam Ali bin Mussa Ridha AS akamjibu kwa kusema: Waombee dua, na utoe sadaka kwa niaba yao na kama wako hai na hawatambui njia ya haki, basi nenda nao taratibu! Kwani Mtume SAW amesema: Mwenyezi Mungu amenituma kwa rehma na huruma na sio kwa ajili ya kukata uhusiano."

Zakaria bin Ibrahim mmoja wa wapokezi wa hadithi na miongoni mwa masahaba wa Imam Jaafar Sadiq AS anasema kuwa, mimi niikuwa mkristo, kisha nikasilimu na kuwa Mwislamu na baadaye nikapata tawfiki ya kwenda kuhiji Makka. Katika safari yangu ya Hija nilibahatika kumtembelea Imam Jaafar Sadiq  AS na katika mazungumzo yangu  na yeye nikamueleza kwamba, nilikuwa Mkristo na kwa sasa nimesilimu na kuwa Mwislamu. Hata hivyo baba na mama yangu pamoja na ndugu zagu wengine wamebakia katika dini ya Ukristo na mama yangu ni kipofu. Je inajuzu kwangu kuishi pamoja nao na kuwa na maingiliano nao? Imam Sadiq AS akasema: Kuishi na kuamiliana nao hakuna tatizo. Kisha akaongeza kuwa, kuhusiana na mama yako kuwa makini. Mtendee hisani na wema na pindi atakapofariki dunia wewe mwenyewe umkafini na kumzika.

Zakari bin Ibrahim anaendelea kusimulia kwa kusema: Niliporejea kutoka safari ya Hija na kuwasili mjini Kufa, nilimuonyesha mapenzi na huruma kubwa mama yangu kama alivyonitaka Imam Sadiq AS. Nikawa nikimlisha mwenyewe sambamba na kukunja nguo zake na hata kumchana nywele. Kwa kifupi nikawa nikimhudumia kwa kila hali. Baada ya mama yangu kuona mabadiliko haya akaniuliza, zama ambazo ulikuwa katika dini yangu hukuwa ukinifanyia yote haya, nini kimekufanya ubadilike na kunifanyia wema na huba kubwa kiasi hiki baada ya kuwa Mwislamu? Nikamjibu kwa kumwambia, mmoja wa wajukuu wa Bwana Mtume SAW ameniamrisha nifanye hivi. Mama yangu akasema: Haya ni miongoni mwa mafundisho ya Mitume, dini yako ni bora kuliko dini yangu, hivyo naomba uniongoze ili niwe Mwislamu. Nikamfundisha mama yangu Uislamu na akasilimu na kuwa Mwislamu. Akasali Sala ya Adhuhuri na Alasiri na Magharibi na Ishaa na kwa bahati mbaya akaanza kuugua katikati ya usiku. Mimi nilibakia pembeni yake huku nikimuuguza. Akaniambia, mwanangu! Nibainishie tena itikadi za Kiislamu. Nikarejea tena kumbainishia mama itikadi za Kiislamu na usiku huo huo akafariki dunia. Siku iliyofuata kundi la Waislamu lilishiriki katika mazishi ya mama yangu mimi nilisimama na kumsalia kisha nikaingia kaburini na kumzika kwa mikono yangu."

Wapenzi wasikilizaji Imam Jaafar Sadiq AS anasema kuhusiana na tafsiri ya aya isemayo  "na wazazi wawili uwatendee wema" ambayo imekuja mara kadhaa katika Qur'ani Tukufu kwamba:  Hisani na wema hapa ni kuishi nao kwa wema na wakati huo huo baba na mama wasilamizike kukuomba kitu wanachohitajia, bali wewe unapaswa kuwakidhia mahitaji yao kabla ya wao kukutaka kufanya hivyo na udiriki hali na matatizo waliyonayo.

Kwa mtazamo wa Uislamu ni kuwa, kukidhi mahitaji ya baba na mama ni jambo la wajibu kwa watoto wenye uwezo na kama baba na mama watashindwa kujiendeshea mambo yao, basi harija ya maisha ni lazima kwa watoto wao.

Miongoni mwa haki nyingine za wazazi ambazo watoto wao wanapaswa kuzitekeleza ni watoto kutofanya mambo ambayo yatapelekea wazazi hao kuchukia, wajiepushe kufanya mambo ambayo yatapelekea hadhi na shakhsia ya wazazi katika jamii kutiwa dosari.

Inanukuliwa kutoka kwa Imam Mussa al-Kadhim AS ya kwamba, amesema kwamba:

Bwana mmoja alimuuliza Mtume SAW kuhusiana na haki za baba yake. Katika kumjibu Mtume SAW akasema: Usimuite baba yako kwa jina lake, usimtangulie wakati wa kutembea, usikae kabla yake na usifanye mambo ambayo yatapelekea alaaniwe au jina lake kuchafuliwa.

Wapenzi wasikilizaji muda wa kipindi hiki umefikia ukingoni kwa leo. Ninakuegeni nikikutakieni kila la kheri na mafanikio katika kuwatendea wema baba na mama na sote tujitahidi kuwaridhisha wazazi wetu na tusifanye mambo ambayo yawatwaudhi na kuwakera. Wassalaamu Alaykum Warhmatullahi Wabarakaatuh.

 

Andika maoni


Msimbo salama (Security code)
Upyesha (Refresh)