Tovuti Hii Imefungwa. Tumehamia Kwenye Parstoday Kiswahili
Jumatatu, 07 Aprili 2014 13:26

Bustani ya Uongofu (53)

Bustani ya Uongofu (53)

Ni matumaini yangu kuwa, hamjambo wapenzi wasikilizaji na karibuni katika kipindi kingine cha mfululizo huu wa Bustani ya Uongofu, kipindi ambacho huzungumzia mitazamo ya Bwana Mtume SAW na Ahlul Bayt AS kuhusiana na masuala mbalimbali ya kijamii, kisiasa, kielimu, kidini, kifamilia na kadhalika. Tukiwa tunaendelea kuzungumzia mitazamo ya Mtume SAW na Ahlul Bayt wake kuhusiana na suala la familia na baada ya kubainisha baadhi ya haki za mke na watoto, katika sehemu hii ya 53 tutazungumzia haki za wazazi. Kuweni nami hadi mwisho wa dakika hizi chache kusikiliza niliyokuandalieni kwa leo.

Katika maktaba ya malezi ya Mtume SAW na Ahlul Bayt AS, kuwa na uhusiano mzuri na wazazi kunahesabiwa kuwa miongoni mwa miamala bora ya kidini. Katika mwenendo wa shakhsia wakubwa wa kidini, baba na mama wana daraja ya juu. Akibainisha nafasi, adhama na daraja ya wazazi wawili yaani baba na mama, Bwana Mtume SAW anasema: "Mwenyezi Mungu hufurahi kutokana na furaha ya wazazi na hughadhibika wanapoghadhibika wazazi." Maneno ya Mtume SAW yanataka kuonesha zingatio maalumu la Mwenyezi Mungu kwa nafasi na daraja ya juu ya baba na mama. Daraja hiyo ni kubwa kiasi kwamba, ridhaa ya Mwenyezi Mungu inategemea kufurahi baba na mama. Kuwatendea wema baba na mama ni jambo lenye umuhimu mkubwa katika dini ya Kiislamu kiasi kwamba, katika Qur'ani Tukufu baada ya amri ya kumuabudu Mwenyezi Mungu watu wametakiwa kuwatendea wema baba na mama. Aya ya 23 ya Surat al-Israa inasema: "Na Mola wako Mlezi ameamrisha kuwa msimuabudu yeyote ila Yeye tu, na muwatendee wema wazazi wawili. Mmoja wao akifikia uzee, naye yuko kwako, au wote wawili, basi usimwambie hata: Ah! Wala usiwakemee. Na sema nao kwa msemo wa hishima."

Aidha Qur'ani Tukufu imeziweka haki za wazazi wawili katika faharasa ya majukumu ya Kimwenyezi Mungu. Aya aya ya 14 ya Surat Luqman inasema:

"Na tumemuusia mtu kwa wazazi wake, mama yake amebeba mimba yake kwa udhaifu juu ya udhaifu, na kumwachisha ziwa baada ya miaka miwili, kwamba, unishukuru Mimi na wazazi wako; marudio ni kwangu."

Kwa hakika kuwatendea wema wazazi kuna taathira muhimu sana kwa mtu hapa duniani na kesho akhera. Mtume SAW amenukuliwa akisema kwamba, mtu ambaye anapenda kuwa na umri mrefu na kupanuliwa rizki yake, basi na awatendee wema baba na mama yake.

Kwa mtazamo wa Uislamu ni kuwa, mtoto awe wa kike au kiume ana majukumu kwa wazazi wake ya kuwasaidia kifedha, kiroho na kisaokolojia hata baada ya kuondoka nyumbani na kuoa au kuolewa bado jukumu hilo liko katika mabega yake. Hususan baada ya wazazi wake hao kuzeeka na kuwa watu wazima, hapo tena majukumu yake huwa makubwa zaidi.

Nukta muhimu na ya kuzingatia ni hii kwamba, watoto wana majukumu kwa wazazi wao bila mpaka wala masharti yoyote. Kiasi kwamba, hata kama wazazi watakengeuka njia ya haki au kutoheshimu haki za watoto wao bado watoto wana majukumu kwa wazazi wao hao na katu udhuru wa watoto wa kutowahudumia wazazi wao haukubaliki. Aya ya 15 ya Surat Luqman inasema:

"Na pindi wakikushikilia kunishirikisha na ambayo huna ilimu nayo, basi usiwatii. Lakini kaa nao kwa wema duniani, nawe ishike njia ya anayeelekea kwangu. Kisha marejeo yenu ni kwangu Mimi, na Mimi nitakuambieni mliyo kuwa mkiyatenda."

Kwa hakika watoto wanapaswa kuwa walinzi wa johari hizi mbili zenye thamani na katika kipindi cha uhai wao wanapaswa kuwatendea wema na baada ya kufariki kwao dunia wawafurahishe kwa sadaka na kuwataja kwa wema. Imam Ali bin Abi Talib AS anasema: "Taklifu kubwa zaidi na muhimu zaidi ya Allah (kwa mja wake) ni kuwatendea wema baba na mama."

Imam Jaafar Sadiq AS anazungumzia kazi bora kabisa na kusema kuwa, kazi bora kabisa ni tatu: Kusali kwa wakati, kuwatendea wema baba na mama na kupigana jihadi katika njia ya Mwenyezi Mungu. Kwa upande wake Bwana Mtume SAW anazungumzia  umuhimu wa kuwatii baba na mama na kusema: Mtu ambaye anawatii wazazi wake wawili (baba na mama) na Mola wake , basi Siku ya Kiyama atakuwa katika daraja ya juu kabisa."

Siku moja kijana mmoja alimuendea Bwana Mtume SAW na kumwambia: Baba na mama yangu ni wazee na kutokana na kufungamana kwao sana na mimi hawako tayari niende vitani kupigana jihadi. Mtume SAW akamwambia kijana yule: bakia na wazazi wako. Ninaapa kwa Mola ambaye roho yangu iko mikononi mwake kwamba, kufungamana (kuanisika) kwao na wewe kwa siku moja ni bora zaidi kuliko kupigana jihadi kwa mwaka mmoja. (tabaani, kama kupigana jihadi huko kutakuwa sio wajibu kwa kila mmoja katika jamii). Kuwatendea wema wazazi wawili, chimbuko lake ni maarifa ya juu aliyonayo mtu kuhusiana na Mola wake na ili kupata ridhaa za Mwenyezi Mungu basi hakuna amali bora na yenye taathira kama kuwatendea wema baba na mama. Kwa hakika mafundisho ya Uislamu yanamtaka mtu awaheshimu wazazi wake, awatunze, awakidhie mahitaji yao ya lazima ya kimaisha, aishi nao kwa wema, asiwakemee na wala asinyanyua juu sauti yake kuliko wao wakati anapozungumza nao. Azungumze nao kwa mapenzi, huruma na upole. Moja ya nasaha muhimu katika maktaba ya Ahlul Bayt kuhusiana na wazazi ni mtu kutomuita baba au mama yake kwa jina lake, bali amuite kwa majina ya baba au mama.

Mtume SAW alikuwa akimtaka binti yake mwema Fatma Zahra AS amuite kwa jina la baba na sio kwa majina na vyeo vingine kama Mtume wa Allah na kadhalika.

Waaidha mtoto anapaswa kuwa mtiifu na mnyenyekevu mbele ya mzazi wake na hata wakitembea pamoja basi hapaswi kuwatangulia mbele, asiketi kabla yao na wala hapaswi kuwatazama kwa jicho kali na la hasira hata kama wazazi wake hao wamemfanyia ubaya.  Kwa hakika kuwatazama wazazi kunahesabiwa kuwa ni ibada na vile vile kuwabusu wazazi kunahesabiwa katika maneno ya Ahlul Bayt AS kuwa ni ibada. Ni kawaida kadiri umri wa wazazi unavyokuwa mkubwa na kukaribia zaidi katika uzee ndivyo wazazi hao yaani baba na mama wanapokabiliwa na matatizo mengi. Ni kwa kuzingatia uhakika huo, ndio maana suala la kuwatunza wazazi na kuwasaidia kukidhi haja zao katika kipindi chao cha uzeeni limetiliwa mkazo mno. Jambo la kuzingatia zaidi ni kuwa, katika maktaba ya kimalezi ya Mtume SAW kumetiliwa mkazo mno suala la kumtembea wema mama. Tukirejea maneno ya viongozi wa dini tunapata kuwa, wametilia mkazo  juu ya suala la kumtendea wema mama kuliko baba. Hapana shaka kuwa, hakuna mtu yeyote anayeweza kulipa wema wa mama na usumbufu alioupata tangu wakati wa ujauzito hadi katika kipindi cha kujifungua na baada ya hapo kumlea. Bila shaka sote tunaelewa ugumu wa kipindi cha ujauzito na jinsi mama anavyokosa usingizi wakati akikichunga na kukilea kichanga chake, sambamba na mateso anayopata wakati mwanawe anapokuwa mgonjwa. Kwa hakika mwanadamu ni mwingi wa kusahau, pindi mtu anapokuwa anasahau usumbufu wa wazazi na jinsi walivyomhangaikia akiwa mdogo na asiyejiweza, je kuna kutokuwa na shukurani kama huku? La kufahamu ni kwamba, kuwatendea wema wazazi wawili na kujaribu kufidia wema wao ni sawa na kushukuru neema za Mwenyezi Mungu, jambo ambalo liko nje ya uwezo wa mtu kwani hakuna mtu anayeweza kushukuru neema za Allah kadiri inavyotakiwa. Kwa msingi tunachoweza kukifanya ni kuonyesha unyenyekevu kama inavyosema Qur'ani Tukufu aya ya 24 ya Surat al-Israa kwamba:

"Na uwainamishie bawa la unyenyekevu kwa kuwaonea huruma. Na useme: Mola wangu Mlezi! Warehemu kama walivyo nilea utotoni."

Wapenzi wasikilizaji muda wa kipindi hiki umefikia tamati kwa leo tukutane tena wiki ijayo. Asanteni na kwaherini.

Andika maoni


Msimbo salama (Security code)
Upyesha (Refresh)