Tovuti Hii Imefungwa. Tumehamia Kwenye Parstoday Kiswahili
Jumatatu, 31 Machi 2014 11:58

Bustani ya Uongofu (52)

Bustani ya Uongofu (52)

Assalaamu Alaykum wapenzi wasikilizaji na karibuni katika sehemu nyingine ya kipindi hiki cha Bustani ya Uongofu. Katika sehemu hii ya 52 ya kipindi hiki tutazungumzia nafasi ya baba na mama katika malezi ya watoto na kutupia jicho mitazamo ya Mtume SAW na Ahlul Bayt wake AS kuhusiana na suala hili. Ni matumaini yangu kuwa mtakuwa nami hadi mwisho wa kipindi hiki kutegea sikio yale niliyokuandalieni kwa leo. Karibuni.

Ni jambo lililowazi kwamba, wazazi wawili yaani baba na mama wana masuuliya na jukumu la kuwafunza na kuwalea watoto wao. Kama mnavyojua, watoto huzaliwa wakiwa na fitra na kuja hapa duniani wakiwa na maumbile asili na safi huku wakiwa na mlolongo wa vipaji vilivyojificha ambapo huhitajia malezi bora, mazingira mazuri na bora ya kimaisha, kisaikolojia, kijamii na kihaki kutoka kwa wazazi wao ili vipaji vyao viweze kuchanua na kunawiri. Malezi ya mtoto ni kazi na jukumu zito kabisa lililoko katika mabega ya wazazi wawili yaani baba na mama. Mtoto ana haki ya kupata mapenzi ya familia chini ya kivuli cha uwepo wa baba na mama. Watoto wana haki ya kunufaika na mipango bora na yenye taathira ya mbinu za kimalezi.

Haki hiyo inabainishwa katika maneno ya Bwana Mtume SAW pale anaposema:

"Miongoni mwa haki walizonazo watoto kwa wazazi wao, ni kupata mafunzo na malezi sahihi, kufunzwa kuogelea, kulenga shabaha na kupata riziki safi na halali. Thaminini shakhsia ya watoto wenu na waleeni kwa wema ili mpate rehma za Mwenyezi Mungu."

Aidha Imam Ali AS amenukuliwa akisema kuwa, "baba haachi mirathi yenye thamani zaidi kuliko malezi bora kwa mwanawe."  Katika maktaba ya malezi ya Mtume SAW na Ahlul Bayt AS ni kuwa, moja ya haki walizonazo watoto ni kuwapa majina mazuri na katika kuchagua jina zuri la mtoto, mzazi anapaswa kuzingatia kwamba, jina zuri linaweza kuwa na taathira muhimu sana katika malezi ya mtoto na hata shakhsia yake. Imam Ali AS anasema:  "Haki ya mtoto kwa baba yake ni mzazi kumpa jina zuri mtoto wake."

Mtoto anapozaliwa hufahamu sauti ya jina lake kuliko neno jingine lolote lile. Kwa msingi huo kama mtoto atakuwa na jina zuri na lenye kubeba maana nzuri, hupata hisia ya kuwa na shakhsia yenye thamani.  Jambo hilo humpa mtoto izza ya nafsi na jambo hilo kuwa na taathira muhimu katika uzima wa kinafsi na kisaikolojia.

Nukta nyingine muhimu katika suala la malezi ya watoto ni kutukuza na kuheshimu shakhsia yake.  Kumsifia mtoto na kumpongeza mara anapofanya jambo zuri ni hatua yenye taathira muhimu katika kujenga izza ya kinafsi ya mtoto. Mtume SAW na Ahlul Bayt AS walilipa umuhimu mno suala la kuizingatia shakhsia ya mtoto. Walikuwa wakiwaita watoto wao kwa lakabu na majina mazuri tena kwa mapenzi na huba ya hali ya juu. Kwa mfano tukirejea sira na maisha ya Bibi Fatma Zahra AS tunashuhudia jinsi alivyokuwa na mapenzi makubwa kwa wanawe. Kwa mfano alikuwa akiwaita wanawe kwa majina kama tunda la moyo wangu, mboni ya jicho langu, nuru ya macho yangu na kadhalika. Kuzingatia suala la usalama wa nafsi, utulivu, nishati na uchangamfu wa watoto ni muhimu mno kiasi kwamba, Mtume SAW anasema hivi kuhusiana na jambo hili: "Kila mtu ambaye atambusu mtoto wake Mwenyezi Mungu Azza Wajalla atamuandikia jema; na kila mtu ambaye atamfurahisha mwanawe, basi Allah atamfurahisha Siku ya Kiyama."

Sisitizo la Uislamu juu ya wazazi kuwaonyesha mapenzi watoto wao lengo lake ni kudhamini uzima wa kinafsi na kisaikolojia wa watoto. Viongozi wa dini wameusia mno suala  la mapenzi kwa watoto, kiasi kwamba, kuzungumza na mtoto kwa huruma, kumtazama kwa mapenzi, kumpangusha kichwani mtoto na kumkumbatia ni mambo yenye ujira wa kimaanawi. Mtume SAW alikuwa akionyesha mapenzi hata kwa watoto wa watu wengine na kwa njia hiyo akawa akiwashajiisha watu kuwaonesha mapenzi watoto wao. Wakati mwingine Mtume SAW alikuwa hata akicheza na watoto kama njia moja ya kuonyesha huba na mapenzi makubwa aliyonayo kwa watoto.

Katika maktaba ya malezi ya Bwana Mtume SAW na Ahlul Bayt AS, kuamiliana na watoto kunafanyika katika sehemu mbili za huba na malezi. Kwa mtazamo wao kumuonyesha huba na mapenzi mtoto ni njia  ya kuelekea katika malezi bora. Katika maktaba ya kimalezi ya Mtume na dhuria wake kiramu, amali bora kabisa ni kuwalea watoto wema na wenye imani na Mwenyezi Mungu. Jambo  hilo lina umuhimu mno kiasi kwamba, Imam Jafar Sadiq AS anasema: "Anapokufa mwanadamu, hubakia vitu vitatu baada ya kuondoka kwake. Mosi, sadaka yenye kuendelea kwa tawfiki ya Allah ambayo hubakia baada ya kifo chake. Pili, jina lake zuri aliloacha mtu (kutokana na kufanya wema) na tatu ni mtoto mwema anayemuombea dua."

Miongoni mwa malengo ya mafunzo na malezi katika maktaba ya Mtume SAW na Ahlul Bayt AS ni kumtambua Mwenyezi Mungu, kujitambua, kuwa na mawasiliano yenye taathira na watu wengine, kukubali kubeba majukumu ya kijamii, kujifunza elimu na maarifa na kujifunza stadi za maisha ambapo baba na mama wana nafasi isiyo kifani katika haya.  Imam Sajjad Zeinul Abidin AS anasema katika risala yake ya haki maarufu kwa jina la Risalatul Huquq anapozungumzia haki za mtoto kwa wazazi wake kwamba:

"Haki ya mtoto wako ni wewe kutambua kwamba, yeye ni sehemu ya uwepo wako na utaulizwa (Siku ya Kiyama) kuhusiana na kumfundisha yeye kuhusiana na Mwenyezi Mungu, kumlea na kufunza adabu na kumsaidia katika kutii na kufuata haki." Katika hili Imam Sajjad AS anaashiria mbinu mbili. Anasema:  Tumia njia mbili katika hili. Mosi, kwa amali na matendo yako na jingine ni miongozo na mafunzo utakayompatia. Endapo utajihimu japo kidogo basi una ujira katika hilo na kama utazembea japo kidogo basi utalaumiwa."

Makusudio ya Imam Sajjad AS ni kwamba, kunapaswa kuweko umoja katika nadharia na matendo ya mzazi, kiasi kwamba, watoto wawaamini wazazi wao. Baba na mama kwanza kabisa wanapaswa kufanya kila wanachokisema na kisha baadaye kuwafundisha watoto wao. Wakati wazazi wanakapokuwa mbele hatua moja mbele katika malezi, bila shaka watafanikiwa katika kazi yao. Jambo jingine muhimu katika suala la malezi ya watoto ni kuzingatia uwezo na kipaji cha mtoto. Kwa maana kwamba, mzazi anapaswa kutambua uwezo na kipaji cha mtoto wake na hivyo kutotaraji kutoka kwa mwanae mambo makubwa ambayo yako nje ya uwezo wa mtoto wake huyo. Kwa maneno mengine ni kuwa, wazazi wanapaswa kuamini uhalisia wa mambo ulivyo kuhusiana na watoto wao na kuwasaidia watoto wao ili waweze kukuza vipaji vyao.

Muda wa kipindi hiki naona umenipa mkono, hivyo sina budi kukomea hapa kwa leo, nikitaraji kwamba, mtakuwa pamoja nami wiki ijayo. Ninakuageni nikikutakieni mafanikio mema katika malezi ya watoto wenu.

Andika maoni


Msimbo salama (Security code)
Upyesha (Refresh)