Tovuti Hii Imefungwa. Tumehamia Kwenye Parstoday Kiswahili
Jumatatu, 24 Machi 2014 09:44

Bustani ya Uongofu (51)

Bustani ya Uongofu (51)

Assalaamu Alaykum wapenzi wasikilizaji na karibuni katika sehemu nyingine ya kipindi hiki cha Bustani ya Uongofu. Kama mnavyojua kipindi hiki huzungumzia mitazamo ya Mtume SAW na Ahlul Bayt AS kuhusiana na masuala mbalimbali. Ni matumaini yangu kuwa mtakuwa nami hadi mwisho wa kipindi hiki, hii ikiwa ni sehemu ya 51 ambapo tutaendelea kuzungumzia suala la familia na umuhimu wake. Karibuni.

Miongoni mwa mambo yaliyousiwa katika maktaba ya malezi ya Mtume SAW na Ahlul Bayt AS ni jinsi ya kuzungumza, na sauti inavyopaswa kuwa wakati wa kuzungumza na mtu. Kwa mujibu wa mafundisho ya Uislamu mazungumzo ya wanafamilia yanapaswa kuwa kwa namna ambayo yatakuwa na ishara ya huba, mapenzi na heshima ndani yake. Sauti ya mzungumzaji inapaswa kuwa ya upole yaani isiwe kali na ya ukemeaji na iwe na heshima ndani yake. Hii ni kusema kuwa, sauti ya mwanafamilia kwa mwenzake haipaswi kuwa ya kejeli na dharau. Aidha mume na mke kila mmoja anapaswa kumuita mwenzake kwa jina zuri na sauti yake iwe imejaa huruma na mapenzi. Yaani mume au mke amuite mwenzake kwa jina analopenda kuitwa. Kwa hakika katika suala la kuchagua mke au mume kuna haja ya kuzingatia kumchagua mtu ambaye unalingana naye kifikra na kimtazmo wa kidini na kama tulivyosema juma lililopita, jambo hili lina taathira kubwa katika kuimarisha misingi ya familia na hivyo kuifanya ndoa ya mke na mume kuwa imara na yenye huba na mapenzi ya dhati. Fauka ya hayo, hatua ya mume na mke kuwa na imani thabiti ya dini huifanya familia wanayoijenga au wanayotaka kuijenga kuwa na usalama wa kisaokolojia na hivyo wanafamilia kuwa na ukamilifu wa kimaanawi. Kutonufaika baadhi ya familia na neema hii ya imani, huifanya ikabiliwe na matatizo mbalimbali maishani ambapo Qur’ani inawataja watu wa aina hiyo kwamba, watakabiliwa na maisha magumu na yenye dhiki. Mwenyezi Mungu anasema katika aya ya 124 ya Surat Taha kwamba:

"Na atakayejiepusha na kunikumbuka (kutekeleza mafundisho yangu), basi kwa yakini atapata maisha yenye dhiki, na Siku ya Kiyama tutamfufua hali ya kuwa kipofu."

Kwa msingi huo basi, imani na itikadi ni jambo ambalo lina nafasi muhimu katika maisha na kuacha itikadi za dini hupelekea mtu kupokonywa utulivu na ladha za kimaanawi katika maisha. Itikadi muhimu kabisa ya kidini ni kumuamini Mwenyezi Mungu na kumpwekesha. Kumuamini Mwenyezi Mungu huufanya mtazamo wa mtu kwa ulimwengu na maisha kuwa mtazamo wenye malengo na wenye kubeba maana. Kwa hakika kumuamini Mwenyezi Mungu huithiri miamala yote ya familia. Mtu ambaye anamhesabu Mwenyezi Mungu kwamba, anayaona mambo yake yote, hufanya hima anapoamiliana na wanafamilia ya kutekeleza vyema majukumu yake ya kifamilia. Upole, mapenzi, kutawakkali kwa Mwenyezi Mungu na kutegemea nguvu zake Subhanahu Wataala ni miongoni mwa athari za kumuamini Mwenyezi Mungu ambazo huwa na taathira za kimuujiza katika mahusiano ya kifamilia.

Jambo jingine na ambalo ni miongoni mwa nukta muhimu katika familia ni  kusaidiana katika masuala ya usimamizi wa nyumba. Muawana na ushirikiano  au madadi katika familia ni msingi wa maisha ya ndoa. Mafundisho ya Uislamu yamegawanya majukumu katika familia kwa namna ambayo, watu wote wana masuuliya na ili kwa njia hiyo familia iweze kufanya mambo yenye taathira na endelevu. Nukta muhimu katika hili ni amara na kusaidiana mume na mke katika masuala ya nyumba.

Katika matamshi ya mawalii na viongozi wa dini kuna nukta muhimu na za kuvutia zinazoshajiisha kusaidiana mume na mke katika maisha yao ya kila siku. Nukta hizo za kuvutia zinabainisha na kutoa msukumo wa kusaidiana zaidi. Imam Jafar Sadiq AS anazungumzia hima ya mwanamke katika mazingira ya familia na kusema: “Mwanamke ambaye atampa mumewe bilauri ya maji ya kunywa basi thamani ya kimaanawi ya kitendo hicho ni zaidi ya mwaka mmoja wa ibada ambao nyakati zake za mchana mtu afunge na usiku asimame kufanya ibada.”

Mtume SAW amenukuliwa akisema: “Mwanamke ambaye anafanya bidii katika kuboresha mambo ya nyumba, Mwenyezi Mungu anamtazama kwa jicho la rehma na mtu ambaye anatazamwa na Mwenyezi Mungu kwa jicho hili la rehma, basi Allah hatamuadhibu." Aidha Mtume SAW amenukuliwa akizungumzia kazi na msaada wa mwanaume kwa kazi za nyumbani akisema:  “Mwanaume ambaye anamsaidia mkewe katika kazi za nyumbani, Mwenyezi Mungu humpa ujira wa Mitume wenye subira kama Nabii Daud, Nabii Yaqub na Nabii Issa AS. Mtu ambaye hakatai kuihudumia familia yake, Mwenyezi Mungu huliandika jina lake baina ya mashahidi.”

Kwa hakika nasaha hizi hupelekea kutokea joto la mahaba katika mazingira ya familia na hivyo kusaidia kuimarisha mahusiano baina ya wanafamilia. Muawana na ushirikiano katika familia humfanya kila mwanafamilia kutojifikiria yeye tu bali kuwafikiria watu wote katika familia huku lengo likiwa ni kuleta utulivu katika familia nzima.

Jambo jingine linalochangia kuimarisha familia ni kuwa nyumbani na kuwa pamoja na familia. Mtume SAW amenukuliwa akisema kuwa, kuwa kando ya familia kunapendwa zaidi na Mwenyezi Mungu kuliko kukaa itikafu na kufanya ibada katika msikiti mtakatifu wa Madina. Aidha wanafamilia kula pamoja ni jambo ambalo nalo limetiliwa mkazo mno katika mafundisho ya Uislamu. Katika zama hizi ambapo jamii imekumbwa na mazonge mengi, kawaida mume na wakati mwingine mke kutokana na kufanya kazi, huwa nje ya nyumba hadi usiku mkubwa na wakati mwingine anaporejea nyumbani hupata watoto wakiwa wameshalala kwa hakika nasaha hizi ni muhimu mno kwao. Bila shaka kuwa pamoja wanafamilia ni jambo lenye taathira katika kupunguza mivutano ya kila siku na wakati huo huo huongeza mapenzi baina ya wanafamilia. Kwa hakika miongozo hata midogo kuhusiana na familia iliyotolewa na Bwana Mtume SAW na Ahlul Byat wake AS inaonesha ni kwa namna gani mahusiano ya kifamilia ni jambo lenye umuhimu mkubwa. Bila shaka haya yote ni kwa ajili ya kulinda nguzo za familia. Hii ni kutokana na kuwa, familia inapotengamaa basi huandaliwa uwanja wa kupatikana jamii bora.

Jambo jingine linaloimarisha mapenzi na kuleta uhusiano mzuri katika familia ni mume na mke kila mmoja kuthamini mchango wa mwenzake. Katika mazingira ya familia kushukuru na kutaja ujazi na neema za Mwenyezi Mungu nalo ni jambo lenye umuhimu na husaidia kuwafanya watu waridhike na maisha waliyonayo.

Miongoni mwa ada nyingine muhimu katika familia ni kupeana zawadi katika minasaba ya furaha na siku za sikuu au mtu anaporejea kutoka safari. Kwa hakika jambo hili huzidisha mapenzi kati ya mume na mke au wazazi na watoto wao. Mtume SAW amenukuliwa akisema: "Peaneni zawadi ili mapenzi yaongezeke na hivyo kuondoka vumbi la chuki katika nyoyo." Aidha amesema: Unaporejea kutoka safari iletee zawadi familia yako kwa kadiri ya uwezo wako.

Maisha ya ndoa ya Imam Ali bin Abi Talib AS na bibi Fatma Zahra AS ni kigezo miongoni mwa vigezo bora vya familia kwa mtazamo wa Uislamu. Maisha mema ya wawili hawa yalijaa nukta za kimalezi na kimiongozo kwa ajili ya watu wanaotaka kujenga familia kwa mujibu wa mafundisho ya dini na hivyo kuwafanya wastaladhi na kupata utulivu katika maisha.

Wapenzi wasikilizaji muda wa kipindi hiki umefikia tamati, hivyo sina budi kukomea hapa kwa leo, nikitaraji kuwa mtajiunga nami wiki ijayo. Wassalaamu Alaykum Warahmatullahi Wabarakatuh.

 

Andika maoni


Msimbo salama (Security code)
Upyesha (Refresh)