Tovuti Hii Imefungwa. Tumehamia Kwenye Parstoday Kiswahili
Jumatatu, 17 Machi 2014 14:31

Bustani ya Uongofu (50)

Bustani ya Uongofu (50)

Ni matumaini yangu kuwa hujambo mpenzi msikilizaji na karibuni kujiunga nami tena juma hili katika kipindi cha Bustani ya Uongofu. Katika sehemu hii ya 50 ya kipindi hiki tunaendelea kuzungumzia maudhui ya familia pamoja na kubainisha mitazamo ya Mtume SAW na Ahlul Bayt wake kuhusiana na taasisi hii muhimu katika jamii. Kuweni nami hadi mwisho wa kipindi. Karibuni.

Familia ni msingi muhimu mno wa jamii na inahesabiwa kuwa nguzo kuu za jamii. Familia ndio ambayo yenye kuweza kumjenga mtu au kumbomoa kulingana na malezi anayopata mhusika. Hakuna mtu asiyehitajia familia. Kila mtu hujifakharisha na kujinasibisha na familia yake hata kama ni masikini na isiyojiweza.  Uislamu umekokoteza na kutoa miongozo maalumu kuhusiana na suala la kujenga familia na kuimarisha misingi yake. Mtume SAW na Ahlul Bayt wake AS walifanya hima ya kubainisha mtazamo wa Uislamu kuhusiana na familia. Kwa kuzingatia kwamba, familia ina nafasi katika kupata saada au kupotea kila jamii, Uislamu umetilia mkazo maalumu kuhusiana na suala la ndoa na kuchagua mke  au mume na kutoa kipaumbele maalumu juu ya suala la tabia njema na maadili bora.

Miongoni mwa marhala na hatua ambazo ni muhimu katika kuainisha mustakabali wa familia ni hatua ya kuchagua mke au mume; kwani akthari ya matatizo na mizozo katika uhusiano wa familia  chimbuko lake  ni pupa na kutofanya utafiti vizuri wakati wa kuchagua mke au mume. Kumchagua mtu ambaye atakuwa mshirika wako wa maisha ni hatua ya kwanza na muhimu katika mchakato wa ndoa jambo ambalo linapaswa kuzingatiwa kwani kivuli cha chaguo hilo daima kitakuweko katika maisha ya wana ndoa. Kivuli hicho wakati mwingine huwa chepesi na hivyo kuleta raha, maelewano na utulivu kati ya mke na mume na wakati mwingine huwa kizito kiasi kwamba, huwa vigumu kustahamili, na matokeo yake ni nyumba kutawaliwa na mizozo na mivutano isiyokwisha. Katika maktaba ya malezi ya Mtume SAW na Ahlul Bayt AS kabla ya mtu kuoa au kuolewa anapaswa kuzingatia vigezo vya thamani za kiakhlaqi na maadili ili kwa njia hiyo kuweze kuandaliwa mazingira ya ukamilifu wa mume na mke. Katika Uislamu sifa za kushikamana na dini na imani, ni mambo ambayo yametiliwa mkazo na mafundisho ya Uislamu katika suala zima la kuchagua mume au mke.

Kuhusiana na hilo Mtume SAW anasema:  "Mtu ambaye Mwenyezi Mungu amempa moyo wa shukurani na ulimi wa kutaja na kudhukuru haki na mke mwenye imani ambaye anamsaidia katika mambo ya dunia na akhera basi kwa hakika amempa mema ya dunia na akhera na amemuepusha na adhabu ya moto wa Jahanamu."

Kwa hakika Uislamu umezingatia mno suala la kufungamana kivitendo na mafundisho ya dini na katika baadhi ya hadithi, imeelezwa kwamba, usafi na utunzaji amana una taathira chanya katika ndoa.

Katika Surat Hujuraat aya ya 13 Mwenyezi Mungu anataja taqwa na kumcha Yeye kuwa kigezo cha bora cha  wanaomfuata Mwenyezi Mungu  na kwamba, hao ni watu wabora na watukufu zaidi. Aya hiyo inasema: "Hakika aliye mtukufu zaidi kati yenu kwa Mwenyezi Mungu ni huyo aliye mcha Mungu zaidi katika nyinyi."

Katika familia bora, mke na mume ni wacha Mungu na ni wenye kumuogopa Mwenyezi Mungu na wao ni wenye kuchunga mipaka ya Mwenyezi Mungu. Kuhusiana na suala la kujenga familia Uislamu umetilia mkazo mno juu ya nukta hii na unamtambua mume bora kwamba, ni yule mwenye kumcha Mungu.

Bwana mmoja aliamua kushauriana na Imam Hassan Mujtaba AS kuhusiana na suala la ndoa ya binti yake. Imam akamwambia, muoze binti yako kwa mwanaume ambaye ana taqwa na uchaji Mungu; kwani kama atampenda binti yako huyo basi atamheshimu na kama atakuwa hana mapenzi naye, hawezi kumdhulumu."

Maktaba ya kimalezi ya Ahlul Bayt inatilia mkazo suala la kubadilisha mitazamo na fikra za kiutamaduni zisizo sahihi na kukokoteza juu ya suala la umuhimu wa kuwa na tabia njema na kushikamana na dini.

Bwana mmoja alimuandikia barua Imam Jawad AS akimtaka ushauri kuhusiana na kumuzoesha binti yake na akamwambia katika barua hiyo kwamba, hajapata mtu anayelingana na binti yake. Katika majibu yake kwa Bwana huyo Imam Jawad AS aliandika hivi:

"Kile ambacho umekibainisha kuhusiana na binti yako na kwamba, hujampata mume anayelingana na sifa za binti yako, nimekuelewa, rehema za Allah ziwe pamoja nawe.  Liweke jambo hilo kuwa kigezo na sharti la kumuozesha binti yako. Kwani Bwana Mtume SAW amenukuliwa akisema kwamba:  Akikijueni yule ambaye mnaridhika na dini na maadili yake basi muozesheni, kwani kutofanya hivyo kutapelekea kutokea ufisadi mkubwa katika ardhi."

Kwa mujibu wa hadithi hii ni kuwa, dini ya mtu, imani yake na kufungamana kwake na mafundisho ya dini ndilo jambo linalopaswa kuzingatiwa pindi mtu anapotaka kumuozesha binti yake na sio mali, haiba, nasaba au elimu.

Katika maktaba ya malezi ya Mtume SAW na Ahlul Bayt wake AS imeusia na kutiliwa mkazo kuangaliwa thamani za kidini na maadili ya mtu pamoja na kufungamana kwake na dini katika suala zima la ndoa. Hii ni kutokana na kuwa, katika maisha kuna mitihani mingi na kama mtu hajashikamana na dini basi ni rahisi ndoa kuvunjika mara moja. Jambo jingine lenye nafasi katika suala zima la kujenga familia na kuifanya iwepo ni baba wa familia kuwa na uwezo wa kuendesha familia, aina ya kazi anayofanya na uwezo wa kutafuta kipato kwa ajili ya kukidhi mahitaji ya familia yake. Jambo hili limetiliwa mkazo mno katika maktaba ya malezi ya Mtume SAW na Ahlul Bayt AS.

Kiasi kwamba, hatua ya mwanaume ya kuongoza na kusimamia familia yake inahesabiwa kuwa ni sawa na kupigana jihadi katika njia ya Mwenyezi Mungu. Viongozi wa dini pia wamelihasabu suala la tabia njema kuwa kigezo muhimu katika ndoa. Makusudio ya tabia njema ni mtu kuwa na muamala mzuri na unaofaa katika maisha na ambao unaendana na watu wanaomzunguka. Msingi wa maisha ya ndoa ni kuweko maelewano na ushirikiano kati ya mume na mke na bila shaka jambo hili litawezekana tu katika kivuli cha wawili hao kujipamba na tabiua njema.

Katika maktaba ya malezi ya Ahlul Bayt AS kumfurahisha mke ni miongoni mwa mambo yanayopewa kipaumbele katika maisha. Imam Ali bin Mussa Ridha AS amenukuliwa akisema kwamba: Kila mwanaume ambaye atamfurahisha mkewe, basi Mwenyezi Mungu atamfurahisha siku ya Kiyama. Wapenzi wasikilizaji muda wa kipindi hiki umefikia ukingoni hivyo sina budi kukomea hapa kwa leo. Tukutane tena wiki ijayo katika sehemu nyingine ya kipindi hiki cha Bustani ya Uongofu.

Wassalaam Alaykum Warahmatullahi Wabarakatuh.

 

Andika maoni


Msimbo salama (Security code)
Upyesha (Refresh)