Tovuti Hii Imefungwa. Tumehamia Kwenye Parstoday Kiswahili
Jumapili, 09 Machi 2014 15:54

Bustani ya Uongofu (49)

Bustani ya Uongofu (49)

Assalaamu Alaykum wapenzi wasikilizaji na karibuni katika sehemu nyingine ya kipindi hiki cha Bustani ya Uongofu, kipindi ambacho kinaendelea kubainisha kwa mukhtasari, mitazamo ya Bwana Mtume SAW na Ahlul Bayt wake AS kuhusiana na masuala mbalimbali. Wiki hii kipindi chetu kitazungumzia familia na suala la malezi. Kuweni nami hadi mwisho katika sehemu hii ya 49 kutegea sikio kile nilichokuandalieni kwa leo. Karibuni.

Familia ni kituo na taasisi tukufu ambayo jiwe lake la msingi huwekwa kwa jinsia mbili yaani jinsia ya kike na ya kiume kuoana na kituo hicho hukamilika mara wanapozaliwa watoto ambao huja na kuimarisha misingi na nguzo za familia hiyo. Wananadharia wanaamini kuwa, familia ndio taasisi ya kwanza ya dharura kwa ajili ya kukidhi mahitaji ya maisha, huba na kubakia jamii. Familia ni nguzo ya jamii na inahesabiwa kuwa ni msingi muhimu. Uislamu umeweka mipango na mikakati maalumu ya kuboresha familia, kiasi kwamba, Bwana Mtume SAW anasema:

"Hakuna jengo lililojengwa katika Uislamu ambalo ni tukufu  zaidi na lenye kupendwa zaidi mbele ya Mwenyezi Mungu kuliko ndoa." Utendaji wa familia katika jamii ni sawa kabisa na utendaji wa seli katika kiumbe hai, na kadiri seli hizo zinavyokuwa salama zaidi na zenye nguvu ndivyo mwili wa kiumbe hai unavyokuwa salama na wenye nguvu zaidi. Ndoa baina ya mke na mume, ni mfungamano wa kimaumbile na mahaba baina ya wanandoa hao, mfungamano ambao ni wa lazima kwa shabaha ya kuendeleza kizazi. Hata hivyo mtazamo huu unahitajia miongozo na usimamizi, kwani kinyume na hivyo, utaleta madhara na uharibifu. Katika Uislamu kuna vigezo vilivyoainishwa kwa ajili ya kujenga familia. Kadiri nguzo zinazounda familia zitakavyotabikiana na kuoana na vigezo hivyo, ni kwa kiwango hicho hicho basi ustahiki na ubora utakavyokuwa. Katika hadithi kumebainishwa sifa nyingi za ubora na ustahiki wa wanawake na wanaume ambapo katika maneno ya Maasumina AS pia kuna miongozo kuhusiana na hilo ambapo kupitia kwayo mtu anaweza kuitambua familia stahiki na bora. Kwa msingi huo basi, tunaweza kusema kiujumla kwamba,  familia bora na stahiki kwa mtazamo wa Uislamu ni ile ambayo misingi, nguzo na mahusiano yake yanatawaliwa na mafundisho ya dini na hivyo basi katika familia kama hiyo, hulelewa na kuondokea watu ambao ni wastahiki na wenye taathira. Mtume SAW na Ahlul Bayt AS walikuwa mbioni kubainisha mtazamo wa Qur'ani kwa familia katika jamii ya mwanadamu. Qur'ani Tukufu inautambulisha uwepo wa mke kuwa ni aya miongoni mwa aya za Allah na ishara miongoni mwa ishara za nguvu na hekima ya Mwenyezi Mungu.  Aidha Qur'ani inatambua huba na mapenzi ya mume na mke kuwa ni katika hekima za Mwenyezi Mungu.  Hii ni kwa sababu, katika kivuli cha huba na mapenzi haya, misingi ya familia huimarika na kuwa na nguvu. Mwenyezi Mungu anasema katika Surat Rum aya ya 21 kwamba:  "Na katika Ishara zake ni kuwa amekuumbieni wake zenu kutokana na nafsi zenu ili mpate utulivu kwao. Naye amejaalia mapenzi na huruma baina yenu. Hakika katika haya bila ya shaka zipo Ishara kwa watu wanao fikiri."

Kwa kuzingatia kwamba, familia ina nafasi muhimu katika saada na kutengemaa au nakama, ihlaki na kuharibika watu katika kila jamii, Uislamu umetilia mkazo maalumu juu ya suala la ndoa na kujenga familia na likaweka vigezo vya tabia na maadili katika suala zima la kuchagua mke. Ndoa yenye saada na mafanikio ni ile ambayo misingi yake imesimama kwa ajili ya kuunda familia salama, imara na yenye nishati, uchangamfu na bashasha. Kwa hakika mwanadamu ni majimui yenye vipaji tele na uwezo tayarifu na hivyo ndoa inaweza kuandaa mazingira mwafaka kwa ajili ya kustawi na kuchanua vipaji vilivyojificha katika ujudi wa mwanadamu huyu na dafina iliyoko katika kila ujudi wa ndani wa mtu. Mapenzi, kudhamini hawaiji za maisha, usimamizi wa familia, mamlaka, kujitosheleza, kupigania ukamilifu, kujikurubisha kwa Mwenyezi Mungu na kuwalea watu wema na wastahiki ni mambo ambayo yanawezekana kupatikana kwa kuweko ndoa. Miongoni mwa nukta muhimu katika maktaba ya malezi ya Mtume SAW na Ahlul Bayt wake wema, ni mtazamo wao wa kimaanawi kuhusiana na suala la ndoa na upande wa utukufu wake. Ibara tunazozishuhudia katika katika hadithi zinathibitisha hili kwa njia tofauti. Miongoni mwa hadithi hizo ni ile iliyopokelewa kutoka kwa Bwana Mtume SAW akisema: Mwenye kufunga ndoa amekamilisha nusu ya dini yake. Au hadithi isemayo: "Miongoni mwa nyakati za kushuka rehma za Mwenyezi Mungu ni wakati wa shughuli ya akidi, nikaha na kufunga ndoa."

Vile vile kuna hadithi nyingi ambazo zinaonesha kuwa, akthari ya miamala ya kifamilia inahesabiwa kuwa sawa na kufanya ibada. Mtume SAW amenukuliwa akisema kwamba:

"Mwanaume anayefanya bidii kwa ajili ya familia yake, ni sawa na mujahidi katika njia ya Mwenyezi Mungu."

Katika hadithi nyingine Mtume SAW anasema:

"Jihadi ya mwanamke ni kuwa na mwenendo mwema kwa mumewe."

Kwa hakika ibara zote hizi zinaonesha jinsi Uislamu unavyoshajiisha juu ya suala la ndoa. Vile vile kunajitokeza uhakika huu kwamba, masuala ya maisha ya dunia yanaweza kuwa njia ya kuelekea katika ukamilifu wa kimaanawi na kiakhera. Miongoni mwa athari za kisaikolojia za ndoa, ni kuathiriana pakubwa mume na mke. Kila mmoja yaani mke na mume huathirika pakubwa na miamala, fikra na hata mtazamo wa mwenzake. Ni kwa kuzingatia uhakika huo ndio maana maktaba ya kimalezi ya Mtume SAW na Ahlul Bayt AS ikakakoteza na kutilia mkazo juu ya kuzingatia suala la kuchagua mume au mke kabla ya kuoa au kuolewa na kuzingatia zaidi suala la thamani za kiakhlaqi.

Kwa hakika ndoa ambayo wanandoa wake wamechaguana kwa kuzingatia masuala ya kimaanawi na maadili mema huwaandalia uwanja wa ukamilifu na saada ya dunia na akhera. Mtume SAW na watu wa nyumba yake tukufu walifanya juhudi kubwa kueneza utukufu wa ndoa baina ya watu. Ni kwa kuzingatia uhakika huo ndio maana Bwana Mtume SAW amenukuliwa katika hadithi mashuhuri akisema:  Ndoa ni miongoni mwa sunna zangu na mwenye kutenda kinyume na sunna zangu si katika mimi." Au hadithi hii iliyonukuliwa kutoka kwa Imam Sadiq AS inayosema: Rakaa mbili za mwenye kuoa ni bora na zenye thamani kubwa kuliko rakaa sabini za mtu ambaye hajaoa. Katika mtazamo wa Mtume SAW na dhuria wake wema ni kuwa, endapo mke na mume watakuwa na sifa tatu za elimu, ustadi na tabia njema wanaweza kuiongoza na kuisimamia nyumba na familia kwa njia bora kabisa. Katika familia kama hii, mwanaume atakuwa kiongozi laiki, mstahiki, mwenye hima na mpole. Atadhamini mahitaji ya familia yake kwa njia za halali. Kwa msingi huo atakuwa mume mwema na mwenye mapenzi kwa familia yake. Uongozi na usimamizi wake kwa familia yake hautakuwa na misingi ya kukata kutawala na utumiaji mabavu. Atakuwa mwanaume mwenye kuihami na kulinda familia yake na atakuwa ni mwenye kufanya jitihada kwa ajili ya kutoa miongozo na himaya kwa familia yake na bila shaka atawashajiisha wana familia kuelekea upande wa masuala ya kimaanawi. Nafasi ya mwanamke pia katika familia ina umuhimu mkubwa mno. Kwa mujibu wa mafundisho ya Kiislamu, jukumu muhimu la mwanamke ndani ya nyumba baada ya kutekeleza taklifu za kidini ni kumkidhia mumewe haja za kindoa. Subira na ustahamilivu wa mwanamke na kuwa pamoja na mumewe katika dhiki na faraja, katika matatizo ya kijamii na kiuchumi na vile vile kutokuwa na matarajio yaliyo nje ya uwezo wa mumewe ni mambo ambayo yanaweza kuandaa uwanja mwafaka wa kuweko uhusiano mwema, mzuri na unaofaa baina ya mume na mke; uhusiano ambao bila shaka utaimarisha pendo lao na kuizatiti ndoa yao. Katika upande mwingine, mwanamke ni kituo cha huba na mapenzi katika familia na jukumu la kuwalea watoto wema, wastahiki na wenye imani liko katika mabega yake kabla ya mtu mwingine yeyote yule. Dini Tukufu ya Kiislamu imewatambulisha Ahlul Bayt wa Mtume SAW kuwa ni vigezo na ruwaza njema na kamili kwa familia bora. Mwenyezi Mungu amewatakasa waja hao wema wa Mwenyezi Mungu kunako uchafu wa aina yoyote ile.  Mwenyezi Mungu anasema katika aya ya 33 ya Surat al-Ah'zab:

"Hakika Mwenyezi Mungu anataka kukuondoleeni uchafu, enyi Watu wa Nyumba ya Mtume, na kukusafisheni baarabara."

Wapenzi wasikilizaji kila lenye mwanzo halikosi kuwa na mwisho, muda wa kipindi hiki umenipa mkono sina budi kukomea hapa kwa leo. Ninakuegeni nikitaraji kwamba, mtajiunga nami tena wiki ijayo. Kwaherini.

 

Andika maoni


Msimbo salama (Security code)
Upyesha (Refresh)