Tovuti Hii Imefungwa. Tumehamia Kwenye Parstoday Kiswahili
Jumatano, 05 Machi 2014 10:11

Bustani ya Uongofu (48)

Bustani ya Uongofu (48)

Ni wasaa na wakati mwingine wa kujiunga nami katika sehemu nyingine ya kipindi hiki cha Bustani ya Uongofu, hii ikiwa ni sehemu ya 48 ya mfululizo huu.

Kwa wale wafuatiliaji wa kipindi hiki bila shaka mnakumbuka kwamba, kipindi hiki huzungumzia na kujadili mitazamo ya Mtume SAW na Ahlul Bayt wake AS kuhusiana na masuala mbalimbali ya kidini, kijamii, kisiasa, kifamilia na kadhalika. Kipindi chetu kilichopita kilizungumzia baadhi ya mbinu na mikakati ya mafunzo na malezi katika sira na mwenendo wa Mtume SAW na Maasumina AS.

Kipindi chetu cha wiki hii kitaendelea na maudhui hii. Ni matumaini yangu kuwa, mtakuwa nami hadi mwisho wa kipindi hiki kusikiliza niliyokuandalieni kwa leo. Karibuni.

Kama mnakumbuka, tulisema katika kipindi kilichopita kwamba, moja ya mbinu na mikakati ya mafunzo na malezi katika sira na mwenendo wa Mtume SAW na Maasumina AS ilikuwa ni kuwapa watu msukumo, kuwashajiisha na kuwaletea hali ya raghba na shauku ya kufanya mambo. Makusudio ya shauku na msukumo ni mtu kuwa na raghba ya ndani kutaka kujifunza kitu. Kwa mfano, kuwa na hisia ya udadisi katika ujudi wa mtu ya kutaka kufahamu au kujifunza kitu.

Kuhusiana na hili, katika hatua ya awali, Maasumina AS walikuwa wakiwafanya watu wawe na ufahamu kuhusiana na ufahamu wao mdogo au kutofahamu kwao na kisha baada ya hapo waliwafanya wawe na hali ya ndani ya kuhitajia elimu na kutaka kujifunza kitu.

Wapenzi wasikilizaji Maasumina walikuwa wakitumia kila kisingizio ili kufungua mlango wa mazungumzo na kubadilisha mazungumzo hayo kuwa kikao cha elimu na mafunzo. Kisa cha Imam Ali bin Abi Talib na mwarabu wa jangwani katika medani ya vita ni mashuhuri sana. Marhumu Sheikh Saduq mmoja wa maulama wakubwa ameandika katika kitabu cha Tawhid kwamba:

Mwarabu mmoja wa jangwani alimuuliza Imam Ali AS wakiwa katika medani ya vita kwamba: Je wewe unasema Mungu ni mmoja? Watu wakamjia juu na kumlalamikia mwarabu yule wa jangwani na kumwambia, wewe vipi? kwani huoni kwamba, Amirul Muuminina Ali AS yuko katika kulitayarisha jeshi?  Wakimaanisha kwamba, huo haukuwa wakati mwafaka wa kuuliza swali.

Lakini Imam Ali AS akasema, mwacheni! Kwa hakika kile anachouliza mwarabu huyu wa jangwani, ndio kitu ambacho sisi tumesimama kupigana na kaumu hii. Kisha baada ya hapo Imam Ali AS akamjibu swali lake.

Kwa hakika Maasumina wote walikuwa namna hii; yaani mafunzo yao mengi waliyatoa katika fursa zisizo rasmi bali katika muamala wao na masahaba zao na watu wengine.

Upole na kuamiliana vizuri na watu, tawadhui na unyenyekevu, huruma, uraufu na kuheshimu haki za wengine, ni miongoni mwa zilizokuwa mbinu za malezi katika sira na mwenendo wa Bwana Mtume SAW na Ahlul Bayt wake wema na watoharifu AS. Mbinu nyingine athirifu katika mafunzo na malezi ni kuambatana elimu na amali katika sira na mwenendo wa watukufu hao. Shakhsia hao, walikuwa wakikifanyia kazi kile walichokuwa wakikisema. Imam Jafar Sadiq AS anaashiria nukta hii na kuwatanabahisha watu kwa kusema:

"Walinganieni watu kwa amali na vitendo vyenu vizuri na msitosheke kwa kutamka tu." Mawaidha mazuri ni mbinu nyingine iliyokuwa ikitumiwa na Mtume SAW na Ahlul Bayt wake katika mafunzo na malezi kwa watu. Mawaidha au maneno mazuri ni agizo la Qur'ani Tukufu katika kuwalingania watu dini na njia ya Mwenyezi Mungu.

Maneno yaliyopimwa ambayo yanaambatana na hekima, nasaha nzuri, kuchagua maneno mazuri na matamu ya kutumia wakati unapozungumza na mtu au kutumia lugha nzuri, mtoaji nasaha kuwa na nia ya kumtakia kheri anayemnasihi, adabu na murua katika kuzungumza ni miongoni mwa sifa maalumu za mawaidha mazuri.

Mtume SAW na Ahlul Bayt wake wema walitumia mbinu hii katika kutoa mafunzo na malezi kwa watu. Mbinu hii sambamba na hoja za kielimu walizokuwa wakizitoa kwa hakika ilikuwa na taathira muhimu mno hususan katika vikao vya midahalo na mijadala ya Ahlul Bayt AS. Katika nasaha zake kwa mwanawe Hassan, Imam Ali AS anamwambia kwamba: "Huisha moyo wako kwa mawaidha."

Mbinu na mkakati mwingine uliokuwa ukitumiwa na Mtume SAW na Ahlul Bayt AS katika mafunzo na malezi ni kutoa hotuba. Waja hao wema wa Mwenyezi Mungu walikuwa wakitumia njia ya kutoa hotuba na kubainisha mambo mbalimbali kulingana na hali ya kijamii na kisiasa iliyokuwa ikitawala katika jamii ya wakati huo. Walitumia mbinu na mkakati huo kufikia malengo yao ya mafunzo na malezi. Kwa mfano Imam Ali bin Abi Talib AS alitoa hotuba mbalimbali katika kipindi cha utawala wake ambapo mbali na kutoa mafunzo na maelekezo ya kimalezi ya kidini alikuwa wakitoa mafunzo ya kiitikadi.

Katika kitabu cha Nahaj al-Balagha moja ya hotuba mashuhuri katika kitabu hicho ni ile ambayo, Imam Ali AS anabainisha sifa za wacha Mungu. Sehemu ya hotuba hiyo inasema, Nyoyo zao (yaani wacha Mungu) zimejaa masikitiko, wamehifadhika na maovu, miili yao ni myembamba, mahitajio yao ni machache, na nyoyo zao zipo safi. Wao wamevumilia shida kwa kitambo kidogo na badala yake wamejipatia starehe za muda mrefu. Hiyo ni biashara iliyorahisishwa na Mola kwa ajili yao. Dunia inawatamani wao, lakini wao hawaitamani kamwe. Dunia iliwateka, lakini wao walijifanya huru kwa malipo.  Mwisho wa kunukuu.

Tukirejea sira na historia ya Mtume SAW na Ahlul Bayt AS tunapata kuwa kuna hotuba nyingi zinazobainisha miongozo ya kimalezi pamoja na mafunzo.  Kwa mfano hotuba za Imam Ali AS katika kitabu cha Nahaj al-Balagha zimejaa mafunzo tele ya kiitikadi, kimalezi, kumpwekesha Mwenyezi Mungu na hata miongozo ya masuala mbalimbali ya kijamii, kisiasa na kiutawala.

Hata katika kipindi ambacho Maimamu watoharifu walipokuwa chini ya mashinikizo ya watawala madhalimu wa Bani Umayyah na Bani Abbas hawakusita kutumia fursa ya kutoa hotuba waliyopata kubainisha na kufichua sifa mbaya za tawala za wakati huo. Tukitazama kwa makini hotuba zao tutapata kwamba, zimejaa miongozo ya kimalezi na mafunzo mbalimbali.

Wapenzi wasikilizaji, kwa leo tunakomea hapa kutokana na kumalizika muda uliotengwa kwa ajili ya kipindi hiki, hivyo basi ninakuageni nikiwa na matumaini ya kukutana nanyi wiki ijay. Kwaherini.

 

Andika maoni


Msimbo salama (Security code)
Upyesha (Refresh)