Tovuti Hii Imefungwa. Tumehamia Kwenye Parstoday Kiswahili
Jumapili, 23 Februari 2014 19:53

Bustani ya Uongofu (47)

Bustani ya Uongofu (47)

Ni wasaa na wakati mwingine wa kujiunga nami katika sehemu nyingine ya kipindi hiki cha Bustani ya Uongofu, hii ikiwa ni sehemu ya 47 ya mfululizo huu. Ni matumaini yangu kuwa, mtakuwa nami hadi mwisho wa kipindi hiki. Katika kipindi kilichopita tulibainisha misingi ya malezi katika sira na mwenendo wa Mtume SAW na Ahlul Bayt AS. Sehemu hii ya 47 ya kipindi hiki itazungumzia baadhi ya mbinu na mikakati ya mafunzo na malezi katika sira na mwenendo wa Maasumina AS. Ni matumaini yangu kuwa, mtakuwa nami hadi mwisho wa kipindi hiki. Karibuni.

Moja ya mbinu na mikakati ya mafunzo na malezi katika sira na mwenendo wa Mtume SAW na Maasumina AS ilikuwa ni kuwapa watu msukumo, kuwashajiisha na kuwaletea raghba na shauku ya kufanya mambo. Makusudio ya  shauku na msukumo ni mtu kuwa na raghba ya ndani kutaka kujifunza kitu. Kwa mfano, kuwa na hisia ya udadisi katika ujudi wa mtu wa kutaka kujifunza kitu. Kuhusiana na hili, katika hatua ya awali, Maasumina AS walikuwa wakiwafanya watu wawe na ufahamu kuhusiana na ujinga wao na kisha baada ya hapo waliwafanya wawe na hali ya ndani ya kuhitajia elimu na kutaka kujifunza kitu. Imenukuliwa kwamba, siku moja Mtume SAW aliingia msikitini na haukupita muda, Bwana mmoja naye akawa ameingia msikitini hapo. Bwana yule akasali na baada ya kumaliza Sala, akaja kwa Mtume SAW na kumsalimia. Mtume aliitikia salamu yake kisha akamwambia: Rudi ukaswali tena kwani hujasali! Bwana yule akaenda na kuswali upya na baada ya kumaliza akaja kwa Mtume SAW ambapo Mtume alimwambia nenda ukaswali tena kwani hujaswali. Yule Bwana akaenda na kuswali tena na alifanya hivyo hivyo hadi ikafika mara tatu ambapo alikuwa hajui tena afanye nini na wala hakuelewa Sala yake ilikuwa na mapungufu gani. Ndipo alipokata shauri na kumwambia Mtume, ewe mjumbe wa Mwenyezi Mungu, ninaapa kwa Mola aliyekuumba, hakika mimi sifahamu namna ya kusali zaidi ya hivi, hivyo nakuomba unifundishe. Baada ya kusema maneno hayo, Mtume SAW alimfundisha namna na kuswali kwa njia sahihi. Wapenzi wasikilizaji, katika mbinu hii, Mtume SAW angeweza kumfundisha Bwana yule namna ya kuswali kwa usahihi tangu awali, lakini hakufanya hivyo; hii ni kutokana na kuwa, Bwana yule alikuwa akijiona kuwa anajua kuswali hivyo hakuwa na haja ya kujifunza. Hivyo basi, Mtume SAW alitaka kumtanabahisha Bwana yule kupitia ujinga wake wa kutojua kuswali na amtambulishe kupitia hilo kwamba, hajui kuswali hivyo analazimika kujifunza namna ya kuswali kwa njia sahihi. Kwa maana kwamba, awali alitaka Bwana yule ahisi hitajio la yeye kutaka kujifunza Sala na kisha kwa ombi lake mwenyewe akafundishwa namna ya kusali kwa njia sahihi.

Wapenzi wasikilizaji, katika upande mwingine, hatua ya Maasumina ya kuwashajiisha na kuwakirimu wasomi na watafiti wa masuala ya kielimu ilikuwa mbinu yao nyingine iliyopelekea kuleta msukumo na shauku baina ya watu. Imam Baqir AS amenukuliwa akisema kwamba: Baba yangu Zeinul Abidiin kila alipokuwa akikutana na wasomi vijana na watafiti wa masuala ya kielimu alikuwa akiwakaribia na kuwaambia, hongereni sana. Nyinyi ni watunza amana ya elimu. Kuna matumaini kwamba, nyinyi ambao kwa sasa ni vijana wa kaumu hii, baadaye mtakuwa shakhsia wakubwa wa kaumu nyingine.

Hebu sasa tegeeni sikio kisa kifuatacho: Siku moja, mwarabu mmoja wa jangwani  alikwenda kwa Imam Hussein bin Ali AS na kumwambia, ewe mjukuu wa Mtume SAW! Ninadaiwa dia kamili na sina uwezo wa kuilipa. Nikajisemea moyoni bora nikaombe msaada kwa mtu mkarimu kabisa, na kwa hakika sijaona watu wakarimu kama wa nyumba ya Bwana Mtume SAW. Imam Hussein akasema, ewe ndugu yangu, nitakuuliza maswali matatu, kama utajibu swali moja kati ya maswali hayo matatu, nitakulipia kiasi cha theluthi moja ya dia yako na kama utajibu maswali mawili kati ya matatu nitakulipia theluthi mbili ya dia yako na kama utajibu maswali yangu yote, basi nitakulipia dia yako yote. Mwarabu yule ya jangwani akasema, Yaa Ibna Rasulillah!, je mtu mwenye elimu na fadhila kama wewe atamuuliza mtu kama mimi? Imam Hussein AS akasema: Ndio; nimesikia kutoka kwa babu yangu Mtume SAW akisema kwamba, kuwafanyia watu wema kunapaswa kwenda sambamba na kiwango cha maarifa yao. Kisha Imam akauliza maswali yake na mwarabu yule wa jangwani akayajibu yote. Kisha Imam Hussein AS akampatia mwarabu yule wa jangwani pete pamoja na mfuko uliokuwa na maelfu ya dinari kisha akamwambia: Dinari zitumie kulipa madeni yako, amma pete hiyo iuze na fedha utakazopata zitumie kama harija na ukidhi hawaiji zako za kimaisha. Wapenzi wasikilizaji, miamala kama hii ya Maasumina ndio iliyokuwa ikiwashajiisha masahaba zao kutafuta elimu na kuwa na msukumo na shauku kubwa kwa ajili ya kujifunza na kutafuta elimu.

Mbinu nyingine ya kutoa mafunzo katika sira na mwenendo wa Maasumina AS ilikuwa ni kustafidi na fursa mwafaka katika kuwafundisha watu mambo mbalimbali. Mbinu hii kwa upande mmoja ilipelekea suala la kutoa mafunzo kuwa sahali na jepesi na kwa upande wa pili likawa chimbuko na sababu kuenea na kusambaa elimu. Imekuja katika vitabu vya historia kwamba, katika vita vya Badr, Waislamu waliwachukua mateka maadui wengi ambapo kila mmoja wao ili aachiliwe huru alitakiwa kutoa kiwango fulani cha fedha au kuwafundisha Waislamu kusoma na kuandika. Kwa maneno mengine ni kuwa, katika zama ambazo watu waliokuwa wakijua kusoma na kuandika walikuwa wachache baina ya Waislamu, Mtume SAW alitumia fursa hiyo iliyojitokeza na kuwatumia maadui kuwafundisha Waislamu kusoma na kuandika. Kwa hakika katika sira na mwenendo wa Maasumina, suala la mafunzo halikuwa na zama wala mahala maalumu. Kwa mfano aghalabu, Maasumina walikuwa wakijishughulisha kutoa mafunzo na malezi msikitini baada ya kuchomoza jua, lakini mafunzo yao hayakumalizikia katika wakati na mahala hapo tu, bali walikuwa wakifanya hilo popote ilipolazimu kufanya hivyo.

Muda wa kipindi hiki umefikia ukingoni sina budi kukomea hapa kwa leo, hata hivyo kuvunjika kwa koleo sio mwisho wa uhunzi, tukutane tena wiki ijayo. Kwaherini.

 

Andika maoni


Msimbo salama (Security code)
Upyesha (Refresh)