Tovuti Hii Imefungwa. Tumehamia Kwenye Parstoday Kiswahili
Jumatatu, 17 Februari 2014 15:39

Bustani ya Uongofu (46)

Bustani ya Uongofu (46)

Assalaamu Alaykum wapenzi wasikilizaji na karibuni katika sehemu nyingine ya kipindi hiki cha Bustani ya Uongofu, kipindi ambacho hutupia jicho na kuzungumzia mitazamo ya Mtume SAW na Ahlul Bayt AS kuhusiana na masuala mbalimbali ya kisiasa, kielimu, kijamii na kadhalika. Kipindi chetu kilichopita kilizungumzia nafasi muhimu ya malezi na mafunzo na jinsi mambo hayo yalivyokuwa na nafasi isiyo kifani katika miongozo ya waja hao wema wa Mwenyezi Mungu. Sehemu hii ya 46 itaendelea na maudhui hii. Kuweni nami hadi mwisho wa dakika hizi chache kusikiliza yale niliyokuandalieni kwa wiki hii.

Mtume SAW na Ahlul Bayt wake wema AS walifanya hima na idili kubwa na kutumia mbinu na mikakati tofauti katika kubainisha suala la malezi na mafunzo. Kiasi kwamba, fikra za kimalezi na sira ya kivitendo ya Mtume Muhammad SAW na Ahlul Bayt wake AS inarejea katika sehemu muhimu ya historia ya Kiislamu.

Miongoni mwa masuala muhimu ya malezi ya Kiislamu ni kugundua misingi, mbinu na mikakati ya mafunzo katika sira ya Mtume SAW na Maasumina (AS).  Kwani waja hao wema wa Mwenyezi Mungu ni kigezo na ruwaza njema kamilifu kwa ajili ya mwanadamu, ambapo wanadamu wanaweza kuweka jiwe la msingi imara kwa ajili ya akhera yao kwa kuwafuata na kuwa wafuasi wa njia na mikakati yao. Mtume SAW na Ahlul Bayt wake walikuwa na ufahamu kamili juu ya Mwenyezi Mungu, mwanadamu na ulimwengu. Walifikia daraja ya kudiriki uhakika wa hayo na wakayafanyia kazi. Kwa mtazamo wao ni kuwa,  maisha ya hapa duniani ni utangulizi kwa ajili ya kufikia maisha ya akhera na kwamba, mtu anapaswa kuitumia fursa hii ya kuweko hapa duniani kwa ajili ya kujiandalia mazingira mazuri ya kesho akhera. Kwa msingi huo basi, mwanaadamu anapaswa kutambua kwamba, dunia hii ni mapito na badala yake kuna ulimwengu mwingine unaotusubiri baada ya maisha haya ya hapa duniani. Mwanadamu anapaswa kuitumia vyema dunia na kuifanya kuwa konde na shamba kwa ajili ya Akhera. Kama ambavyo Bwana Mtume SAW anasema: Dunia ni shamba la Akhera.  Mbinu ya mafunzo na malezi ya Bwana Mtume SAW na Ahlul Bayt wake AS ilikuwa kwa namna ambayo kwa mtazamo wa kielimu na kisaikolojia ilikuwa na taathira mno kwa walengwa. Hii ni kutokana na kuwa, chimbuko lake lilikuwa ni kufahamu uhakika wa mwanadamu pamoja na mahusiano baina ya wanadamu. Miongozo ya Mtume SAW iliegemea katika misingi miwili ya kutakasa nafsi na kufundisha. Hii ni katika hali ambayo, watukufu hao walikuwa wakizingatia suala la malezi na kuliona kuwa ndio asili ilhali yaliyotambua mafundisho kuwa utangulizi wa hilo. Kwa kuzingatia kwamba, akili ina nafasi muhimu na sifa za kipekee kwa mwanadamu, Mtume SAW na Ahlul Bayt wake AS walisisitiza juu ya suala la akili. Mtume SAW na Ahlul Bayt wake AS wakistafidi na msaada wa sifa hii ya mwanadamu walimtambulisha mwanadamu huyu nafasi yake ulimwenguni pamoja na daraja yake na sifa zake za kipekee. Kisha baada ya hapo wakafanya hima ya kumlea ili awe na moyo wa kutafuta uhakika.

Kwa hakika, kuleta mabadiliko kwa mwanadamu bila ya kuwa na taswira na sifa sahihi na kutazama mambo kwa uhalisia wake ni jambo lisilowezekana.  Kwa msingi huo, katika kila mfumo wa malezi kumtambua mtu na sifa zake ni sawa na kuweka jiwe la msingi. Hii inatokana na kuwa, pande zote za mfumo wa malezi kwa namna fulani ni muangalizi wa hali ya mwanadamu. Masuala kama mwanadamu anapaswa kuongozwa kuelekea wapi, harakati yake kuelekea huko inapaswa kuwaje na kwa mbinu gani, yote haya yanafungamana na kutegemea suala la kumjua mwanadamu. Mafunzo na mbinu za malezi za Mtume SAW na Ahlul Bayt wake AS yanatambulisha engo za shakhsia ya mtu na kumpeleka mja huyo upande wa Mwenyezi Mungu katika kivuli cha akili na fikra. Ni kwa kuzingatia uhakika huo, ndio maana Bwana Mtume SAW alikuwa akitambua kwamba, hakuna ibada bora kama kutafakari. Tukirejea sira na mwenendo wa Bwana Mtume SAW na dhuria wake tunapata kwamba, wao waliufanya  msingi wa kazi zao katika suala la malezi kuwa ni utambuzi, welewa na yakini na wakakataza kufuata kitu ambacho mtu hana elimu wala ufahamu nacho.  Ni kwa msingi huo ndio maana tunapata kuwa, msingi muhimu kabisa wa mfumo wa mafunzo na malezi ya Kiislamu katika sira na mwenendo wao ni kumtambua Mwenyezi Mungu, mwanadamu na ulimwengu. Kwa maneno mengine ni kuwa na imani na misingi na matawi ya dini ya Kiislamu. Mtume alifanya hima ya kuwafanya Waislamu wazingatie misingi hiyo ili kupitia njia hiyo malengo ya mfumo wa Kiislamu yaweze kufikiwa. Hii ni kutokana na kuwa, hima na juhudi zao zingekuwa na faida wakati walengwa watakapokuwa na imani na misingi ya Uislamu. Ni kutokana na sababu hiyo ndio maana moja ya mambo ya malezi waliyoyazingatia katika kuwalea watu ni kuwafundisha maarifa ya dini. Aidha lililopewa kipaumbele katika mafundisho hayo ni kuwafanya watu wazingatie suala la kutambua na kufahamu chimbuko la kuumbwa. Mwenyezi Mungu ni Mmoja na kila kitu kinaendeshwa na Yeye ni miongoni mwa yaliyokuwa masuala muhimu na ya kimsingi katika maktaba ya Mtume SAW na Ahlul Bayt wake watoharifu AS. Kuhusiana na hili, Imam Ali bin Abi Talib anasema kwamba: Jiwe la msingi la Uislamu ni kumtambua Mwenyezi Mungu.

Lengo jingine la shakhsia wakubwa wa dini katika suala la mafunzo na malezi, ni kuwafanya watu wazingatie suala la kufufuliwa tena baada ya kufa, Utume, Wahyi na Uimamu. Kwa hakika waja hao wema walikuwa wakifuatilia kuhakikisha kwamba, wanaweka msingi wa ujenzi wa mfumo wa kimalezi ambao kupitia njia ya Mtume SAW na Qur'ani Tukufu, utaishia kwa Mwenyezi Mungu mtukufu.

Jambo jingine lililokuwa moja ya malengo ya malezi ya Bwana Mtume SAW na Ahlul Bayt wake watoharifu AS ni kuwafanya Waislamu walizingatie suala la maadili na adabu za kijamii pamoja na taqwa na uchaji Mungu. Shakhsia hao hawakuyasema hayo kwa vinywa vyao tu, bali wao wenyewe walikuwa kiigizo na ruwaza njema katika kutekeleza hayo kivitendo. Hii ni kutokana na kuwa, hatua ya kwanza ya kufanikiwa katika lile mtu analolilingania ni yeye mwenyewe kwanza kuwa mstari wa mbele katika hilo. Hapana shaka kuwa, hatua ya awali ya kutaka kuwafunza watu malezi na maadili ni mlezi mwenyewe kujitengeneza. Imam Ali bin Abi Talib AS anasema: "Mtu yeyote anayetaka kuwa kiongozi wa watu, kwanza anapaswa kujifunza adabu na maadili kabla ya kuwafunza wengine hayo na kuwafunza watu wengine kunapaswa kuwa kwa vitendo na sio kwa maneno."

Wapenzi wasikilizaji, Mtume SAW na Ahlul Bayt AS walitumia mbinu tofauti katika suala la mafunzo na malezi. Kuna wakati walifanikisha hayo kwa njia isiyo ya moja kwa moja, au kwa njia ya maswali na majibu au kwa kuonesha radiamali mwafaka kuhusiana na matukio fulani na kadhalika. Kwa msingi huo basi, mbinu na mkakati wa malezi ni jambo analopaswa kulizingatia mtu katika suala zima la mafunzo na malezi.

Muda wa kipindi hiki umetuishia sina budi kukomea hapa kwa leo. Ninakuageni nikikutakieni kila la kheri.

Wassalaamu Alaykum Warahmatullahi Wabarakaatuh.

Andika maoni


Msimbo salama (Security code)
Upyesha (Refresh)