Tovuti Hii Imefungwa. Tumehamia Kwenye Parstoday Kiswahili
Jumatatu, 27 Januari 2014 13:34

Bustani ya Uongofu (45)

Bustani ya Uongofu (45)

Ni matumaini yangu kuwa, hamjambo wapenzi wasikilizaji na karibuni katika kipindi kingine cha Bustani ya Uongofu kipindi ambacho hukujieni kila juma siku na wakati kama huu kupitia Idhaa ya Kiswahili, Sauti ya ya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran. Katika sehemu hii ya 45 ya mfululizo huu tutazungumzia nafasi ya mafunzo na elimu katika mtazamo na sira ya Bwana Mtume SAW na Ahlul Bayt wake watoharifu. Ni matarajio yangu kuwa, mtakuwa nami hadi mwisho wa kipindi hiki. Karibuni.

Katika sira na mwenendo wa Bwana Mtume SAW na Ahlul Bayt wake AS, kuna misingi kadhaa muhimu ambapo wao wakiwa viongozi wa kidini na kisiasa wa jamii waliifanya misingi hiyo kuwa nguzo muhimu katika harakati zao. Kwa hakika misingi hiyo ina nafasi muhimu katika ustawi wa kielimu na kiutamaduni wa jamii ya Kiislamu katika zama zozote zile. Miongoni mwa misingi hiyo ni mafunzo na malezi. Kushajiisha watu kutafuta elimu na kujifunza mambo na vilevile kusisitiza juu ya suala la malezi ya kidini ni miongoni mwa mafundisho muhimu ya Kiislamu. Mtume SAW na Ahlul Bayt wake AS walitumia mbinu na mikakati mbalimbali sambamba na kufanya hima na idili kubwa kwa minajili ya kuwabainishia Waislamu msingi huu. Kimsingi malezi ni kuondoa vizingiti na kuandaa uwanja na mazingira ambayo yatapelekea vipaji vya watu kuchanua na kukamilika. Kwa muktadha huo, kuna haja ya kuondoa njiani kila jambo ambalo ni kizingiti na kikwazo cha kunawiri vipaji vya watu na wakati huo huo kuandaa mazingira ambayo yanavishughulisha na kuvipa changamoto vipaji vya watu na kumfanya kila mwenye kipaji ajitokeze na kuonesha kipaji chake na ustadi alionao katika uga fulani. Tab'ani, hili ni jambo ambalo linawezekana na kuwa sahali kwa mtu mwenyewe kufanya hima na idili. Katika malezi suala la mwelekeo wa kifitra na kimaumbile wa mtu pamoja na kipaji chake huzingatiwa. Maneno mawili ya mafunzo na malezi yana maana ya kutoa mafundisho na kulea vipaji vya watu. Sira na mwenendo wa Mitume wa Mwenyezi Mungu ulikuwa ni kumfikisha mwanadamu katika daraja ya juu ya ukamilifu wa kiakili na kiroho; kwani Mwenyezi Mungu alikwishampatia mwanadamu huyu kipaji hiki lililobakia ni kukishughulisha kipaji husika. Mtume SAW amenukuliwa akisema kuwa: "Watu ni madini, kama yalivyo madini ya dhahabu na fedha."  Ukweli wa mambo ni kuwa, ili kumuandalia mwanadamu huyu mwenye kipaji, mazingira ya kuchanua kipaji chake kuna haja ya kumlea na kutumia mbinu na mikakati mbali mbali. Mtume SAW na viongozi wa Uislamu walitumia mbinu na mikakati tofauti kulingana na mazingira waliyokumbana nayo ili kumlea na kumuongoza mwanadamu huyu. Wakati mwingine walitumia mazungumzo, maneno ya upole na ukumbusho; na wakati mwingine msamaha na kufumbia macho baadhi ya vitendo ili kuwaongoza wafuasi wao na kuwalingania wapotofu katika njia nyoofu.

Katika misingi ya malezi ya Mtukufu Mtume SAW suala la fitra na maumbile ya mwanadamu limezingatiwa sambamba na kuifanya Tawhidi kuwa mhimili wa malezi. Mtume SAW alikuwa akizungumza na kila mtu kulingana  na uwezo wa ufahamu wake.  Katika aya ya 33 ya Surat Tawba, Qurani Tukufu inazungumzia malengo ya risala na ujumbe wa Mtume SAW kwa kusema:

"Yeye ndiye aliye mtuma Mtume wake kwa uwongofu na Dini ya Haki ipate kushinda dini zote, ijapo kuwa washirikina watachukia."

Katika kuwalingania watu Uislamu na katika suala zima la malezi na mafunzo, Bwana Mtume SAW alianza kazi yake hiyo akitumia mbinu mbili za uonyaji na ubashiriajI. Hii ni kutokana na kuwa, mbora huyo wa viumbe akiwa mtawala wa Kiislamu alikuwa na jukumu la kuwafundisha watu waliokuwa ndio kwanza wameingia katika Uislamu na kwa hakika alifanya hima na idili kubwa katika uwanja huo kuwahakikisha kwamba, watu wanakuwa na malezi ya Kiislamu. Kwa hakika Bwana Mtume SAW alikuwa amejipamba kikamilifu kwa mafundisho ya Qur'ani ambapo miamala yake na watu ilikuwa dhihirisho la wazi la Qur'ani Tukufu. Ni kutokana na sababu hiyo ndio maana Bwana Mtume SAW anatambulika kuwa msingi na jengo la kwanza refu la utamaduni na mfumo wa malezi wa Kiislamu. Mwenyezi Mungu anasema katika aya ya 21 ya Surat al-Ahzab:

"Hakika nyinyi mnayo ruwaza njema kwa Mtume wa Mwenyezi Mungu kwa anaye mtaraji Mwenyezi Mungu na Siku ya Mwisho, na akamkumbuka Mwenyezi Mungu sana."

Qur'ani Tukufu inamuarifisha na kumtambulisha Mtume SAW kuwa ndiye kigezo na ruwaza njema kabisa kwa wanaadamu. Utambulisho huu kwa hakika  ni ubainishaji mkubwa  kabisa wa tofauti iliyopo kati ya maktaba ya malezi ya Mitume na maktaba nyingine. Kwani maktaba ya Mitume ina sifa ya kivitendo na kiamali.

Kwa mujibu wa bainisho la wazi la Qur'ani Tukufu ni kwamba, kama kusingekuweko malezi ya Mwenyezi Mungu yaliyoletwa na Mitume wateule wa Allah, basi suala la kuwaongoza wanadamu lisingekuwa jambo jepesi na kwa msingi huo wanadamu wangebakia katika giza totoro la upotovu na dhalala. Uhakika huo unabainishwa na aya ya 2 ya Suratul Jum'a inayosema:

"Yeye ndiye aliye mpeleka Mtume kwenye watu wasio jua kusoma, awasomee Aya zake na awatakase, na awafunze Kitabu na hekima, ijapo kuwa kabla ya haya walikuwa katika upotofu ulio dhaahiri."

Kwa mujibu wa aya hii tukufu ni kwamba, suala la kutakasa nafsi, kujipamba na sifa ya taqwa na uchaji Mungu, kuwafundisha watu Kitabu na hekima ni mambo ambayo yanahesabiwa kuwa miongoni mwa malengo ya kubaathiwa na kutumwa Mitume wa Mwenyezi Mungu. Kazi ya Bwana Mtume SAW katika kipindi cha ujahilia ilikuwa ni kuwapa mafunzo na malezi watu ambao walikuwa mbali na ustaarabu na utamaduni. Mtume aliweza kuifanya kwa ustadi kazi hiyo na kufanikiwa kuwajenga vizuri watu na kuwafanya kuwa wastahiki.  Historia inaonesha kwamba, Mtume SAW alikuwa akitilia mkazo mno suala la kufundisha elimu na vile vile malezi ya kidini. Ni kwa msingi huo ndio maana mbora huyo wa viumbe alipambana na thamani zote batili za zama za kijahilia na badala yake akaleta fikra na mafundisho ya Mwenyezi Mungu. Aidha alikabiliana vilivyo na hurafa na hali ya kumili kuelekea katika mambo mabaya. Kukataa kuiga na kufuata mambo yasiyo na msingi wowote kutoka kwa waliotangulia na kusimama kidete mkabala na ada za kijamii zisizokubalika ni miongoni mwa mafundisho ya awali ya Kiislamu. Mtume SAW alikuja na kuleta baina ya watu mwamko, shauku na vuguvugu la kutaka kusoma na kujifunza elimu.

Mtume SAW akalifanya suala la kutafuta elimu kuwa ni wajibu kwa Waislamu wote bila kujali matabaka yao au jinsia zao. Aidha hakulifanya suala la kutafuta elimu kuwa ni maalumu kwa ajili ya zama fulani tu. Sehemu ya kwanza ya kufundishia watu ilikuwa msikitini.

Muda wa kipindi hiki umefikia tamati tukutane tena wiki ijayo. Wassalaamu Alayakum Warhmatullahi Wabarakaatuh.

Andika maoni


Msimbo salama (Security code)
Upyesha (Refresh)