Tovuti Hii Imefungwa. Tumehamia Kwenye Parstoday Kiswahili
Jumatatu, 13 Januari 2014 12:40

Bustani ya Uongofu (44)

Bustani ya Uongofu (44)

Ni wasaa na wakati mwingine mpenzi msikilizaji wa kujiunga nami katika sehemu nyingine ya kipindi hiki cha Bustani ya Uongofu. Kipindi chetu cha leo kitaendelea kujadili suala la utawala na siasa katika sira na mwenendo wa Ahlul Bayt AS. Ni matumaini yangu kuwa, mtakuwa nami katika dakika hizi chache kusikiliza kile nilichokuandalieni kwa leo. Karibuni.

Licha ya kuwa katika sira na matamshi ya Maimamu watoharifu wa Ahlul Bayt AS kuna suala la udharura wa kuundwa serikali na dola, lakini kutokana na Maimamu hao kukabiliwa na mazingira mabaya na yasiyofaa ukiwemo udhibiti mkali wa Bani Umayya na Bani Abbas kwa Ahlul Bayt AS, jambo hilo halikuweza kufanywa na watukufu hao. Pamoja na hayo, Ahlul Bayt AS walibainisha misimamo yao katika nyakati na minasaba tofauti kuhusiana na hali mbaya ya kijamii na kisiasa ya zama zao. Msimamo wa kila Imam wa Ahlul Bayt AS dhidi ya watawala madhalimu wa zama zake ilikuwa mbinu ya kiakili kabisa na inayofaa.

Katika matukio mbalimbali waja hao wema wa Mwenyezi Mungu walibainisha mitazamo yao kuhusiana na utawala na uongozi sahihi wa mambo ya jamii na vilevile sifa na wasifu wa watawala waadilifu na wastahiki. Misimamo hiyo ilikuwa inaonesha kwamba, kuongoza jamii na kuunda utawala kwa ajili ya kusukuma mbele gurudumu la malengo ya Kiislamu ni miongoni mwa mambo yaliyokuwa na umuhimu kwao. Kuendesha vita na kujitenga kwao Maimamu na vyombo vya utawala ilikuwa ni aina fulani ya kuonesha malalamiko na kutoridhishwa kwao na tawala ghasibu za zama zao ambapo hatua yao hiyo ilipelekea tawala hizo kutiliwa alama ya swali juu ya ustahiki wake.

Kujikita kwa mtazamo huo kulihesabiwa kuwa ni hatari kubwa kwa utawala wa wakati huo. Hii ni kutokana na kuwa, kama watu watakuwa hawana imani tena na uhalali wa mfumo fulani, basi yamkini wakati wowote ule wakasimama kwa ajili ya kukabiliana na utawala huo. Maimamu watoharifu AS hawakujitenga mbali wao tu na tawala za wakati huo, bali walikuwa wakiwakataza pia wafuasi wao kufanya mambo ambayo ni kwa maslahi ya tawala hizo.

"Kwa mfano Imam Mussa al-Kadhim AS alimwambia Safwan bin Jammal mmoja wa masahaba zake kwamba: Safwan, wewe ni mtu mzuri katika mambo yote, isipokuwa katika jambo moja tu. Kwa nini unamkodishia Haruna ngamia wako? Safwan anasema kwamba, nikamwambia Imam, kwani kuna ubaya gani mimi kumkodishia Haruna ngamia wangu ili awatumie kwa ajili ya kubebea mizigo katika safari zake za kuelekea Makka? Hasa kwa kutilia maanani kwamba, simpatii bure, bali nachukua ujira kutoka kwake? Imam Kadhim AS akamwambia Safwan, je unapenda Haruna arejee salama kutoka katika safari zake ili akulipe ujira wako? Nikamjibu Imam kwa kumwambia, ndio. Imam akasema: Hiki hiki kiwango chako cha wewe kutaka dhalimu aendelee kubakia hai ni dhambi. Safwan anasema kuwa, baada ya hapo nikaamua kuuza ngamia wangu wote kabla ya msafara wa Haruna kuondoka kuelekea Makka."

Wapenzi wasikilizaji, sambamba na Imam Mussa al-Kadhim AS kuwakataza wafuasi wake kutoshirikiana na tawala za wakati huo, alikuwa akiwaruhusu pia kufanya kazi na tawala hizo baadhi ya watu ambao kwa kutumia vyeo na madaraka yao wangeweza kuisaidia jamii ya Waislamu. Aliwaruhusu watu wa aina hiyo kuingia katika utawala na kukubali vyeo wanavyopatiwa kama alivyomruhusu Ali bin Yaqtin mmoja wa masahaba zake aliyekuwa na daraja ya juu katika taqwa, elimu, siasa na uchaji Mungu. Alimtaka aendelee kubakia kuwa waziri katika utawala wa Haruna Rashid na afiche itikadi yake ili kupitia cheo hicho aweze kuwasaidia watu.

Tab'ani, jambo la kuzingatia hapa ni kwamba, kila Imam miongoni mwa Maimamu watoharifu AS alitumia mbinu, sera na mikakati maalumu kulingana na mazingira ya kisiasa na kijamii yaliyokuwa yakitawala katika zama zake. Tukirejea sira na maisha ya kisiasa ya Imam Ridha AS tunapata nukta moja muhimu na ya kuzingatiwa mno. Nayo ni hatua ya Imam Ridha ya kukubali kwa kukirahika cheo cha mrithi wa mtawala Maamum aliyekuwa khalifa wa ukoo wa Bani Abbas katika zama hizo.

Mazingira ya kisiasa na kijamii yaliyotawala baada ya Imam Ridha AS, yaani katika zama za Imam Jawad, Imam Hadi na Imam Hassan AS yalikuwa kwa namna ambayo, watawala wa zama hizo waliwalazimisha Maimamu hao waondoke mjini Madina na kwenda katika makao ya tawala za Kiabbasi huko Baghdad na Samarra. Katika kipindi cha miaka sita cha kuwa kwake mjini Samarra, Imam Askary AS imma alikuwa amefungwa jela na kama alikuwa huru basi alikuwa chini ya uangalizi mkali na kupigwa marufuku kukutana na watu.

Aidha Maimamu Hadi na Askary AS walikaa Samarra kwa kukirahishwa na kulazimishwa ili makhalifa na watawala wa Bani Abbas waweze kudhibiti nyendo zao pamoja na mawasiliano yao na wafuasi wao.

Ukweli wa mambo ni kuwa, wafuasi wa Ahlul Bayt AS walikuwa wakiamini kwamba, haki ya uongozi wa Maimamu wao imeporwa na kughusubiwa na watawala madhalimu na kwa msingi huo walikuwa wakitumia kila njia kumfikishia Imam na kiongozi wao, Khumsi, zawadi, kafara, nadhiri na haki nyingine za kisheria walizopaswa kutoa kama zaka na kadhalika. Imam Askary AS alikuwa chini ya uangalizi mkali, kiasi kwamba, baadhi ya nyakati maafisa wa utawala wa Maamuun walikuwa wakivamia nyumba yake usiku na kufanya upekuzi.

Kwa msingi huo basi inafahamika kwamba, Ahlul Bayt wa Mtume SAW walikuwa katika mazingira magumu mno na kwa hali hiyo, walikuwa wamepokonywa nguvu na uwezo wowote wenye taathira hasi dhidi ya watawala. Pamoja na hayo, Maimamu walitumia fursa finyu walizopata kufichua utambulisho wa kidhalimu wa watawala wa Bani Umayya na Bani Abbas na ni kwa kuzingatia hilo, ndio maana watawala hao hawakuwa na jingine ghairi ya kufanya njama mbalimbali kuwauwa shahidi Maimamu watoharifu.

Hata hivyo kwa mapenzi ya Mwenyezi Mungu, Imam wa mwisho yaani, Imam Mahdi AF ambaye ni mwana wa Imam Hassan Askary AS amebakia hadi hii leo na atadhihiri katika wakati anaoujua Mwenyezi Mungu ili aje kuunda utawala ambao ndani yake ahadi za Mwenyezi Mungu zitatimia kwani ataujaza ulimwengu huu uadilifu na usawa baada ya kuwa umejaa dhulma na uonevu.

Wapenzi wasikilizaji kutokana na kumalizika muda wa kipindi hiki, sina budi kukomea hapa kwa leo nikitaraji kwamba, mmenufaika vya kutosha na yale niliyokuandalieni kwa leo na mtajiunga nami wiki ijayo katika sehemu nyingine ya kipindi hiki cha Bustani ya Uongofu. Ninakuageni nikikutakieni kila la kheri.

Wassalaamu Alaykum Warahmatullahi Wabarakaatuh.

Andika maoni


Msimbo salama (Security code)
Upyesha (Refresh)