Tovuti Hii Imefungwa. Tumehamia Kwenye Parstoday Kiswahili
Jumatatu, 06 Januari 2014 10:46

Bustani ya Uongofu (43)

Bustani ya Uongofu (43)

Ni matumaini yangu kuwa, hamjambo wapenzi wasikilizaji na karibuni katika sehemu nyingine ya mfululizo wa kipindi hiki cha Bustani ya Uongofu. Kwa wale wafuatilia wa kipindi hiki bila shaka wanakumbuka kwamba, lengo la kipindi hiki ni kuzungumzia mitazamo ya Bwana Mtume SAW na Maimamu watoharifu AS kuhusiana na masuala mbalimbali ya kijamii, kielimu, kisiasa, kiutawala, kijamii na kadhalika. Sehemu hii ya 43 ya kipindi chetu itaendelea kuzungumzia suala la utawala na uongozi katika Uislamu na kubainisha mitazamo ya watu wa nyumba tukufu ya Bwana Mtume SAW kuhusiana na suala hilo. Nina wingi wa matumani kwamba, mtakuwa nami hadi mwisho wa kipindi hiki. Karibuni.

Baada ya kuaga dunia Bwana Mtume SAW na kurejea kwa Mola wake, Imam Ali bin Abi Talib AS hakuwa na lengo jingine ghairi ya kuhakikisha kwamba, kunakuweko na utawala wa haki sambamba na kutekelezwa malengo na matukufu ya Bwana Mtume SAW. Ni kwa kuzingatia hilo, ndio maana katika kipindi cha uongozi wake wa miaka minne na ushei akistafidi na miongozo ya Bwana Mtume SAW, Imam Ali AS alifanya hima na idili isiyo na mithili ili kuhakikisha kwamba, kunakuweko utawala wa kidini na akalifanya hilo kuwa miongoni mwa ajenda zake kuu katika sera na siasa zake. Kama mnavyojua wapenzi wasikilizaji, katika fikra za kisiasa kuna mitazamo tofauti kuhusiana na namna ya kuweza kushika madaraka. Kuna kundi lenye mtazamo huu kwamba, ili kufanikiwa kushika hatamu za uongozi, mtu anapaswa kutumia wenzo na njia yoyote ile.

Kwa mujibu wa mtazamo huu, siasa haina haja ya kuwa na kitu kama thamani za kimaadili na fadhila za kiutu bali lengo la mwanasiasa ni kutumia nguvu kwa ajili ya kuitawala jamii na kuwa na udhibiti. Kundi jingine au mtazamo wa pili ni ule ambao umesimama juu ya msingi wa thamani za kibinadamu. Katika mtazamo huu, mwanasiasa hana ruhusa ya kutumia wenzo na suhula yoyote kwa ajili ya kuingia madarakani na kushika hatamu za uongozi. Sira ya kisiasa na kiutawala ya Imam Ali bin Abi Talib AS ilikuwa imesimama juu ya msingi na mtazamo huu. Kwa mtazamo wa Imam Ali AS ni kuwa, lengo la utawala mbali na kuwafanya wanadamu wafikie ukamilifu wa kimaada, utawala huo unapaswa kuwafanya pia watu wafikie katika umaanawi na kwa muktadha huo kuweko na uadilifu wa kijamii.

Imam Ali AS alikuwa mhuishaji wa utawala na siasa zilizowekewa jiwe la msingi na Mtume SAW. Wakati Imam Ali AS aliposhika hatamu za uongozi alikuwa akitambua kwamba, ili kuirejesha jamii katika sira na mwenendo wa Mtume SAW na mafundisho ya Qur'ani Tukufu alipaswa kufanya idili maradufu.

Miongoni mwa mambo ambayo Imam Ali AS alikuwa akiyazingatia na kuyapa kipaumbele ni kuwa mtu wa sheria na kutekeleza sheria za Mwenyezi Mungu. Kama ikitokea kwamba, mtu amefanya jambo ambalo ni kinyume cha sheria basi alikuwa akitekeleza sheria ya Mwenyezi Mungu dhidi ya mtu huyo bila kujali cheo chake, nasaba yake au wadhifa alionao na katu hakuwa akikubaliana na upatanishi au maelekezo ya mtu yeyote kuhusiana na suala hilo.

Imepokewa kutoka kwa Imam Muhammad Baqir AS kwamba, maafisa wa serikali katika kipindi cha utawala wa Imam Ali bin Abi Talib AS walimtia mbaroni mtu mmoja wa kabila la Bani Asad ambaye alikuwa amefanya uhalifu na wakampeleka kwa Imam Ali. Ndugu wa Bwana yule wakamuendea Imam Ali AS na kumuomba atengue uamuzi wake wa kutaka kumuadhibu bwana yule wa kabila la Bani Asad. Hata hivyo, Imam Ali AS alitekeleza sheria ya Mwenyezi Mungu na kumuadhibu Bwana yule kulingana na kosa alilokuwa amefanya. Kisha akasema: Ninaapa kwa Mola, mimi sio mmiliki wa jambo hili hata niweze kumsamehe."

Kwa hakika Imam Ali AS alikuwa akiutambua uadilifu kuwa ni msingi muhimu na uti wa mgongo wa utawala na alikuwa akitilia mkazo jambo hilo kwa kauli na kwa vitendo. Kwa mtazamo wa Imam Ali AS ni kuwa, uadilifu ni nguzo muhimu kabisa ya siasa. Kimsingi ni kuwa, fikra ya kisiasa ya Imam Ali AS haiwezekani kuidiriki pasina ya kuweko uadilifu. Katika amali na vitendo, Imam Ali AS hakuwa na kigugumizi wala kulegalega katika kutekeleza uadilifu licha ya kuwa msimamo wake huo thabiti haukuwa ukiwafurahisha baadhi ya watu. Kusimama kidete kwa Imam Ali  AS katika kutekeleza uadilifu kulimgharimu mno na hata kupelekea kutwishwa vita  kama vya Jamal.

Katika sira na mwenendo wa utawala, Imam Ali AS alikuwa akifanya kila awezalo kuhakikisha kwamba, watu wema na wastahiki tu ndio anaowachagua kwa ajili ya kushika nyadhifa mbalimbali.

Katu Imam Ali AS hakuwa akiruhusu watu ambao sio wastahiki kuongoza na kusimamia mambo ya watu. Katika zama hizo kuna watu waliokuwa wamepatiwa nyadhifa mbalimbali za kuwaongoza watu na kusimamia mambo yao kwa upendeleo, kirafiki, kinasaba au kifamilia. Muawiyya bin Abi Sufian ni mfano wa wazi kwani licha ya kuwa katika zama hizo alikuwa ameuzuliwa katika utawala wa Sham, lakini aliendelea kutawala na baadaye akaja kupigana vita na Imam Ali.

Mtukufu Imam Ali AS anazungumzia suala la kumteua mtu bora na mstahiki  kwa ajili ya kuongoza na kutaja sifa anazopaswa kuwa nazo kwa kusema:

"Enyi watu! Watu bora kabisa kwa ajili ya utawala ni wale ambao wana uwezo (wa jambo lenyewe) miongoni mwa watu, na ambao ni wajuzi zaidi wa sheria za Mwenyezi Mungu."

Wapenzi wasikilizaji, Licha ya kuwa Imam Ali AS alikuwa makini mno katika kuteua na kuchagua maafisa bora na wastahiki kwa ajili ya uongozi kama magavana  na maliwali, lakini hakuwa akiwaacha tu wajifanyie mambo kama watakavyo, bali alikuwa akifuatilia kazi zao na alikuwa akiwatahadharisha daima na kuwapa miongozo huku akiwaonya wasije wakaangukia  na kunasa katika mitego ya upotofu.

Imam Ali As anasema katika sehemu moja ya barua zake kwa Ash'ath bin Qays mmoja wa magavana wake kwamba:  Utawala sio windo na tonge nono na laini ambalo umelishikilia mkononi, bali ni amana yenye majukumu mengi iliyoko mabegani mwako.  Aliyeko juu yako (yaani Ali bin Abi Talib) naye anakutaka ulinde na kuheshimu haki za watu. Huna haki ya kufanya udikteta baina ya watu na kukifanya kila ukitakacho."

Kwa hakika miongoni mwa mambo ya dharura kwa kila utawala wa wananchi na utawala bora ni kuweko mfungamano baina ya watawala na wananchi. Mtawala anaweza kufikia hilo wakati atakapodiriki matatizo na machungu ya raia, atambue mahitaji yao na afanye hima ya kuyapatia ufumbuzi kwa kuzingatia welewa na utambuzi huo.

Tunakamilisha kipindi chetu cha wiki hii kwa kusema kuwa, nguvu, cheo na madaraka ni mambo ambayo kwa mtazamo wa Imam Ali AS sio lengo; na ndio maana katika kipindi chote cha maisha yake, hakuna wakati ambao Imam Ali AS alifanya harakati kwa ajili ya cheo na uongozi.

Na hadi hapa wapenzi wasikilizaji ndio tunafikia tamati ya kipindi chetu kwa juma hili, hadi tutakapokutana tena wiki ijayo ninakuageni nikikutakieni kila la kheri.

Andika maoni


Msimbo salama (Security code)
Upyesha (Refresh)