Tovuti Hii Imefungwa. Tumehamia Kwenye Parstoday Kiswahili
Jumapili, 29 Disemba 2013 20:45

Bustani ya Uongofu (42)

Bustani ya Uongofu (42)

Assalaamu Alaykum wapenzi wasikilizaji na karibuni katika sehemu nyingine ya kipindi hiki cha Bustani ya Uongofu. Sehemu ya 42 ya mfululizo huu itaendelea kuzungumzia maudhui ya siasa na utawala katika Uislamu na kubainisha mitazamo ya Bwana Mtume saw na Ahlul Bayt as kuhusiana na jambo hili. Kuweni nami hadi mwisho wa kipindi hiki.

Suala la utawala na siasa katika Uislamu ni jambo muhimu mno kiasi kwamba, Mtume (s.a.w) alilifikiria suala la kiongozi wa Waislamu baada yake. Katika aya ya 67 ya Surat al-Maida, Mwenyezi Mungu anamtaka Mtume Wake afikishe aliyoteremshiwa kutoka kwa Mwenyezi Mungu kwani kama hatafanya hivyo basi atakuwa hajafikisha ujumbe wa Allah. Aya hiyo inasema:

"Ewe Mtume! Fikisha uliyo teremshiwa kutoka kwa Mola wako Mlezi. Na ikiwa hukufanya hayo basi hukufikisha ujumbe wake. Na Mwenyezi Mungu atakulinda na watu. Hakika Mwenyezi Mungu hawaongoi watu makafiri."

Kwa mujibu wa aya hii suala la uongozi na utawala ni muhimu mno kiasi kwamba, kutokuweko kwake ni sawa na kwamba, dini haijafikishwa na kwamba, Mtume atakuwa hajafikisha risala ya Mwenyezi Mungu na ujumbe aliopatiwa kuwafikishia wanadamu kama inavyotakiwa. Aya tuliotangulia kuisoma ndio aya inayobainisha kwa uwazi kabisa miongoni mwa aya za Qur'ani tukufu kuhusiana na suala la ukhalifa na uongozi baada ya Bwana Mtume (s.a.w). Aya hiyo inamtaka Mtume (s.a.w) asiuache umma wa Kiislamu na Waislamu bila ya kiongozi baada ya yeye kufariki dunia na kurejea kwa Mola wake. Yaani asiiache dini ya Allah bila ya kiongozi, msimamiaji mambo na mlinzi. Hapana shaka kuwa, jukumu la kiongozi ni kuwaongoza watu, kulinda dini na thamani za Kiislamu na wakati huo huo ajishughulishe na kazi ya kusimamia na kuiongoza jamii.  Kwa maana kwamba, awe kiongozi wa watu na hivyo alete nidhamu, mipango na usalama katika jamii na aitetee dini na kulinda ardhi za Waislamu na jamii ya Kiislamu dhidi ya hujuma za maadui.  Ukweli wa mambo ni kuwa, mambo haya muhimu hayawezi kufanywa isipokuwa na mtu mstahiki kabisa miongoni mwa watu. Kwa amri ya Mwenyezi Mungu, Mtume (s.a.w) alimtangaza rasmi Imam Ali bin Abi Talib (a.s) kuwa kiongozi wa Waislamu baada yake katika Hija ya mwisho katika eneo la Ghadir Khum.  Hata hivyo matukio yaliyojitokeza baada ya Bwana Mtume (s.a.w) kuaga dunia, yalimfanya Imam Ali awe mbali na cheo cha kuwaongoza kwa Waislamu kwa muda wa miaka 25. Katika miaka hiyo, jamii ya Kiislamu ilikumbwa na hali ya panda shuka nyingi, mifarakano na hitilafu nyingi kutokana na Waislamu kutofuata maelekezo na wasia wa Bwana Mtume (s.a.w).

Hatimaye baada ya kupita miaka 25 Waislamu wakamrejea Imam Ali AS na kumtafadhalisha awe kiongozi wao kutokana na kuhisi udharura wa kuweko uadilifu katika jamii. Hiyo ilitokana na kuwa, viongozi waliochukua uongozi baada ya kufariki dunia Mtume (s.a.w) hawakuweza kuongoza kama inavyotakiwa. Uongozi wa Imam Ali (a.s) kwa Waislamu uliodumu kwa muda mfupi, ulikuwa na matunda tele kutokana na kiongozi huyo kufanya kila awezalo kuhakikisha uadilifu na usawa unatawala katika jamii ya Kiislamu. Hata hivyo baadhi ya watu wenye tamaa na uchu walishindwa kuvumilia uadilifu wa Imam Ali (a.s) kwani ulikuwa kikwazo cha kufikia malengo yao. Kwa mtazamo wa Imam Ali (a.s) ni kuwa, uongozi na utawala sio kwa ajili ya kulinda maslahi ya watawala, bali ni kwa ajili ya kuleta fadhila na umanawi katika umma sambamba na kujenga jamii ambayo imesimama juu ya misingi ya hadhi na utukufu wa mwanadamu na fadhila za kimaadili. Imam Ali alikuwa akiamini kwamba, uongozi ni amana aliyopatiwa mtawala ili aiihifadhi na kwa kutumia amana hiyo asimamishe haki na kuangamiza batili. Kwa muktadha huo basi, wanajidanganya wale wanaodhani kwamba, kupatiwa uongozi wa idara fulani, wizara, shirika au serikali ndio kuula na kupata mafanikio kimaisha. Kwani watawala wanapaswa kuwa mstari wa mbele katika kulinda, kuchunga na kuheshimu misingi na thamani za kimaadili wakati wa kutoa maamuzi, kuratibu mambo na katika kuamiliana na watu na jamii kwa ujumla na vile vile katika mahusiano yao kimataifa bila kusahau kwamba, hawapaswi kumfanyia upendeleo mtu fulani kwa misingi ya nasaba, udugu, urafiki au ukabila. Kwa mtazamo wa Imam Ali bin Talib (a.s) watawala na vongozi daima wanapaswa kufungamana na thamani za Kiislamu pamoja na misingi ya kimaadili na hawapaswi kuyafumbia macho hayo katika mazingira yoyote yale. Kwani kukanyaga moja kati ya misingi hii huwafanya watawala wakose ustahiki wa kuongoza na wakati huo huo utawala wao kukabiliwa na hali ya kukosa uhalali wa kuongoza. Taqwa na uchaji Mungu ni miongoni mwa sifa muhimu ya mtawala wa Kiislamu kwa mujibu wa mtazamo wa Imam Ali bin Abi Talib (a.s).  Katika Nahaj al-Balagha, neno taqwa na minyambuliko yake ni miongoni mwa maneno na lafudhi zilizokaririwa mno katika kitabu hicho. Imam Ali (a.s) anaamini kwamba, taqwa na uchaji Mungu ni kipando ambapo humpeleka peponi mpandaji wake.

Imam Ali (a.s) anaitaja taqwa na uchaji Mungu kwa  watawala na wananchi kwamba, ni chimbuko la kupatiwa ufumbuzi matatizo mengi ya kisiasa na kijamii. Anasema: Mtu ambaye amekhitari taqwa na uchaji Mungu huyafukizia mbali mazonge na mambo magumu baada ya kumkaribia, huyafanya mambo machungu kuwa matamu, huyasambaratisha mawimbi ya hatari, huyafanya masaibu na mambo magumu kuwa mepesi, huifanya adhama na ukubwa uliomtoka kurejea tena kwake kama yanavyodondoka matone ya mvua, humiminikiwa na rehma za Mwenyezi Mungu, neema za Mwenyezi Mungu hujitokeza kama chemchemi na baraka zilizopungua huongezeka."

Kwa mtazamo wa Imam Ali (a.s) taqwa na uchaji Mungu ni husuni na ngome imara na isiyopenyeka ambayo huwazuia magavana na viongozi na hali ya  kutetereka, kuangukana, hatari katika wakati nyeti. Kwa mtazamo wa Imam Ali bin Talib (a.s), jambo jingine lenye thamani kubwa katika uga wa kisiasa ni suala la uadilifu wa kijamii na kuleta uwiano sahihi au ukuaji wa kila upande na wenye mlingano katika jamii. Imam Ali (a.s) anaamini kwamba, uadilifu ndio dhihirisho bora kabisa ambalo linaweza kulinda hali ya mlingano katika jamii na kuwafanya watu waridhie na wakati huo huo kuifanya jamii kuwa salama, yenye amani na utulivu. Dhulma na ukandamizaji ni njia pofu ambayo haimfikishi dhalimu palipokusudiwa. Imam Ali bin Abi Talib (a.s) ambaye mwenyewe ni dhihirisho la uadilifu wa Mwenyezi Mungu katika mgongo wa ardhi na shahidi mkubwa katika njia ya uadilifu katika historia yote ya mwanadamu anawataja viongozi na maliwali waadilifu kuwa ni watu bora na wanaopendwa zaidi mbele ya Mwenyezi Mungu Mtukufu na kwamba, viongozi na maliwali madhalimu ni watu wabaya kabisa mbele ya Allah. Kwa mtazamo wa Imam Ali (a.s) ni kuwa, kufanya uadilifu huyafanya mambo katika jamii kutengemaa na kwamba, jamii ambayo ndani yake haina uadilifu, haina uhai wa kibinaadamu na maisha ya kimaanawi na vile vile utawala ambao lengo lake sio uadilifu na kuleta uadilifu katika jambo umo katika njia ya kuangamia.

Kutokana na kumalizika muda wa kipindi hiki sina budi kukomea hapa kwa leo, tukutane tena wiki ijayo.  Wassalaamu Alaykum Warahmatullahi Wabarakaatuh....

Andika maoni


Msimbo salama (Security code)
Upyesha (Refresh)