Tovuti Hii Imefungwa. Tumehamia Kwenye Parstoday Kiswahili
Jumapili, 22 Disemba 2013 17:07

Bustani ya Uongofu (41)

Bustani ya Uongofu (41)

Ni wasaa na wakati mwingine mpenzi msikilizaji wa kujiunga nami Salum Bendera katika sehemu nyingine ya kipindi hiki cha Bustani ya Uongofu, kipindi ambacho hukujieni siku na wakati kama huu kupitia Idhaa ya Kiswahili Sauti ya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran. Katika sehemu hii ya 41 ya mfululizo huu tutaendelea na maudhui ya utawala na siasa katika sira na mwenendo wa Bwana Mtume saw na Ahlul Bayt wake (a.s).  Nina wingi wa matumaini kwamba, mtakuwa nami hadi mwisho wa kipindi hiki.

Kama tulivyosema katika kipindi kilichopita, akthari ya mafundisho ya Uislamu haiwezekani kuyatenganisha na utawala. Hii ni kutokana na kuwa, Uislamu ni dini ambayo imekuja kwa ajili ya kumuongoza mwanadamu na imekuja na sheria na kanuni ambazo zinatoa majibu na kukidhi mahitaji yote ya mwanadamu katika nyuga mbalimbali. Uislamu unazingatia mahitaji ya maisha ya mtu binafsi na jamii kwa ujumla na daima umo katika kukidhi mahitaji hayo. Dola au utawala ni wenzo ambao unausaidia Uislamu katika njia ya kufikia malengo. Utambulisho wa sheria za Kiislamu, udharura wa kulinda na kutetea dini na kuthibiti malengo matukufu ya Kiislamu katika jamii ni hoja nyingine zinazounga mkono juu ya udharura wa kuweko utawala. Baada ya Bwana Mtume (s.a.w) kubaathiwa na kupewa Utume alibainisha malengo ya maisha  na kuweka wazi juu ya usawa baina ya wanadamu mbele ya Mwenyezi Mungu na kwamba, hakuna mtu aliyebora mbele ya Allah kwa kujifakharisha kwa rangi yake, nasaba, cheo au jinsia yake na kwamba, haya ni mambo ambayo mbele ya Allah hayana thamani yoyote ile. Kwa hakika kuanzishwa dola na utawala  na Mtume (s.a.w) mjini Madina ilikuwa dalili na hoja bora kabisa kwamba, dini na siasa ni mambo mawili yaliyoshikamana na ambayo hayatengani.

Mkakati wa Bwana Mtume (s.a.w) mjini Madina katika kuasisi dola na utawala na kusimamia masuala ya kisiasa ya jamii na kutotosheka na masuala ya kiibada na kimaadili ni mambo yanayobainisha nafasi muhimu ya utawala na uongozi katika Uislamu.  Mtume alizingatia udharura huu na yeye mwenyewe akawa ni msimamiaji na mtekelezaji wa sheria pamoja na mipango ya Uislamu sambamba na kushughulikia masuala ya jamii.

Sehemu muhimu na ya kuzingatia ya kazi ya da'awa ya Mtume (s.a.w) na kuwalingania watu Uislamu ilijikita zaidi katika masuala ya kisiasa na kijamii. Hii ni kutokana na kuwa, mbora huyo wa viumbe alikuwa na lengo la kuanzisha jamii salama ambayo imesimama juu ya fikra safi za dini. Ni kwa kuzingatia uhakika huo, ndio maana katika fursa ya kwanza tu mjini Madina, Mtume (s.a.w) aliasisi utawala wa Kiislamu. Aidha baada ya Mtume kuingia Madina alifunga mikataba na makabila mbalimbali na akaleta maafikiano na udugu baina yao ikiwemo hatua yake ya kuunganisha udugu baina ya Muhajirina na Ansari na kwa msingi huo akawa ameimarisha misingi ya utawala wa Kiislamu mjini Madina. Kisha akaufanya msikiti kuwa kituo cha kukusanyikia Waislamu. Kuunda jeshi, kutuma wajumbe katika ardhi nyingine ili wakafikishe risala ya Uislamu, kutoa hukumu, kutekeleza mipango ya kiutamaduni, kutoa kipaumbele masuala ya elimu na kuwashajiisha Waislamu kutafuta elimu sambamba na kupambana na hurafa na fikra za kijahilia ni miongoni mwa hatua na mipango muhimu iliyotekelezwa na Bwana Mtume (s.a.w) katika kivuli cha utawala wa Kislaamu.

Hatua ya Bwana Mtume ya kuleta suala udugu wa Kiislamu ni jambo lililokuwa na nafasi muhimu katika kuleta umoja na mshikamno na hivyo kuimarisha misingi ya dini. Hiyo ilikuwa ni hatua kubwa ya kisiasa ambayo ilifanyika kutokana na jitihada kubwa. Udugu wa Kiislamu uliandaa mazingira ya kuasisi umma mkubwa wa Kiislamu. Tukiitupia jicho mipango na hatua alizozichukua Bwana Mtume (s.a.w) tutadiriki kwamba, kutokana na kuwa, mbora huyo wa viumbe alikuwa na fikra ya kilimwengu ya kueneza Tawhidi na kumpwekesha Mwenyezi Mungu katika kila kona ya dunia, alianzisha harakati zake katika nyuga mbili za ndani na nje. Katika upande wa ndani, Mtume alifunga mikataba ya suluhu, aliwalea na kuwaandaa mubalighina kwa ajili ya kuwafundisha watu dini. Katika da'awa na kuwalingania watu Bwana Mtume saw alifuata misingi na mikakati maalumu na kimsing,i misingi hii ndio iliyokuwa misingi ya sera za kigeni za serikali ya Mtume saw.

Moja ya mbinu za Mtume saw hususan katika kuwalingania watu Uislamui ni upole na ulaini. Moja ya sababu za kuenea Uislamu na Mtume saw kukubalika na watu sambamba na kuteka nyoyo zao ni muamala wake ulioambatana na upole na ulaini. Qur'ani Tukufu inautaja muamala wa Bwana Mtume saw na watu kuwa ni rehma toka kwa Mwenyezi Mungu. Aya ya 159 ya Surat al-Imran inasema:

"Basi ni kwa sababu ya rehema itokayo kwa Mwenyezi Mungu ndio umekuwa laini kwao. Na lau ungeli kuwa mkali, mwenye moyo mgumu, bila ya shaka wangeli kukimbia. Basi wasamehe, na waombee maghfira, na shauriana nao katika mambo. Na ukisha kata shauri basi mtegemee Mwenyezi Mungu. Hakika Mwenyezi Mungu huwapenda wanao mtegemea."

Upole na ulaini wa Mtume ulimsaidia mbora huyo wa viumbe katika kufikia malengo yake ya muda mrefu. Hata hivyo ulaini huo haukuwa ukimfanya Mtume saw aweke kando maslahi ya Waislamu na kukanyaga misingi muhimu.

Jambo jingine muhimu katika sera za kigeni za Bwana Mtume saw ni kutumia vyema nukta za pamoja. Mtume alikuwa akitumia nukta za pamoja kuwaita katika Uislamu wapinzani. Moja ya mifano hiyo ni barua za bwana Mtume saw kwa Kisra mfalme wa wakati huo wa Iran na  kwa Najashi mfalme wa Uhabeshi yaani Ethiopia ya leo. Sehemu moja ya barua ya Bwana Mtume saw kwa Mfalme Najashi inasema:

Kwa jina la Allah, Mwingi wa rehma Mwenye kurehemu. Kutoka kwa Muhammad mjumbe wa Allah kwenda kwa Najashi mfalme wa Uhabeshi. Mimi pamoja na wewe tunamuabudu Mungu Mmoja ambaye hapana apasae kuabudiwa isipokuwa yeye, mtakakasifu, asie na mapungufu na mlinzi. "

Sehemu hii ya barua ya Bwana Mtume saw inaonesha jinsi Bwana Mtume saw alivyokuwa akitumia nukta za pamoja katika kuwalingania watu Uislamu. Mkakati na mbinu nyingine aliyoitumia Mtume saw katika sera zake za kigeni ni kuishi kwa wema na watu. Sira na mwenendo wa Bwana Mtume saw unaonesha kuwa, kwake vita ilikuwa njia ya mwisho kabisa; kwani katika hatua ya awali alitumia njia za barua na mazungumzo katika kuwalingania Uislamu.

Kwa leo tunakomea hapa. Tukutane tena wiki ijayo Inshaallah...

Andika maoni


Msimbo salama (Security code)
Upyesha (Refresh)