Tovuti Hii Imefungwa. Tumehamia Kwenye Parstoday Kiswahili
Jumanne, 17 Februari 2015 12:48

Aleji au mzio unaosababishwa na dawa

Aleji au mzio unaosababishwa na dawa

Ni matumaini yangu kuwa hamjambo wapenzi wasikilizaji na karibuni katika kipindi kingine cha Ijue Afya yako. Wiki iliyopita tulianza kuzungumzia tatizo la aleji au mzio, mada ambayo leo pia tutaendelea kuijadili. Pia tutazungumzia aleji inayosababishwa na dawa na namna ya kujikinga nayo. Tafadhalini jiungeni nami hadi mwisho wa kipindi.

&&&&&&

Kama tulivyosema wapenzi wasikilizaji mzio au aleji ni matokeo ya mpambano uliopitiliza kati ya kinga ya mwili na kitu chochote ambacho kwa ujumla huwa hakina madhara kwa mwili, inapotokea kimeingia ndani ya mwili au kimegusa sehemu fulani ya mwili. Unachopaswa kukijua kuhusu mzio ni hali inayotokea wakati seli za mwili wako zinapokataa kitu ambacho kwa mtu wa kawaida hakina madhara. Mzio hujitokeza kwa alama au dalili mbalimbali na huleta matokeo yenye ishara nyingi mwilini. Kuna aina mbili kuu za mizio, zile zinazosababishwa na kitu ambacho kiko nje ya mwili na husababishwa na mazingira ya nje ya mwili wako. Aina nyingine kuu ya mzio ni ile ambayo iko ndani ya mwili wako ambayo inaweza kuletwa na kinasaba cha kurithi au na kitu kilichoko ndani ya mwili wako.
Mzio wa ngozi au aleji inayojitokeza kwenye ngozi ni tatizo linaloweza kukupata kutokana na mwili wako kukataa kitu fulani, hutokana na sababu kadhaa ikiwemo hewa na hata chakula tunachokula. Kuna vitu ambavyo huibua mzio kama vumbi katika nyumba, mavi ya panya, manyoya ya wanyama na hewa yenye aina ya spiriti. Mzio unaweza kukufanya uwe na ukurutu, mafua, pumu na hata kuvimba kwa mwili. Wapo watu ambao hupata tatizo la ngozi, kuwashwa na hata kuvimba. Katika dunia ambayo inatamba sana na teknolojia, tatizo la mzio ni kubwa na hasa kutokana na kemikali zinazotumika katika vyakula na hata urembo vinapotibua kemikali zinazotengeneza aleji katika mwili.
Wakati kitu chochote kinaweza kuwa alejeni lakini kuna vitu vingine ambavyo husababisha mzio zaidi kupita kiwango cha kawaida. Alejeni zinaweza kuwa vumbi na mazingira yaliyochafuliwa kwa poleni (unga wa mimea na maua), vipodozi na marashi ya kujipaka au ya kupuliza, vyakula mbalimbali kama mayai, karanga, kemikali zinazotumika kuhifadhia vyakula na vinywaji ambazo mtu huzila kwenye chakula au kuzinywa kwenye vinywaji hivyo. Mzio unaweza kusababishwa na mabaki au uchafu wa kemikali kutoka viwandani, moshi wa magari machakavu na makukuu utokao kwenye ekzosi, mwanga wa jua, nyuzi za nguo zinazotengenezwa viwandani, baadhi ya dawa kama penicillin na kadhalika, manyoya, sufi ya ngozi za wanyama, wadudu mbalimbali kama mchwa na mende, manyoya ya paka na mbwa na hata harufu inayotokana na rangi mbalimbali.

&&&&&

Wasikilizaji wapenzi mzio unaosababishwa na dawa au drug allergy ni hali isiyo ya kawaida inayooneshwa na mfumo wa kulinda mwili kutokana na dawa. Dawa za aina yeyote zinaweza kuleta aleji kuanzia zinazoruhusiwa kununuliwa kwenye duka la dawa bila cheti yaani over-the-counter drugs, zilizoandikwa na daktari au hata dawa za mitishamba. Hata hivyo mzio husababishwa zaidi na dawa za hospitalini. Aleji inayosababishwa na dawa huweza kuleta madhara makubwa kwa mtu, na kuonesha dalili jumla mara moja, hali inayojulikana kama Anaphylaxis ambayo hutishia maisha kwa kuathiri viungo kadhaa vya mwili. Mwili unaweza kuonesha aleji za dawa za aina mbalimbali, kuanzia muwasho kidogo kwenye ngozi hadi athari zinazoweza kusababisha madhara makubwa mwilini. Lakini mara nyingi dalili za mzio uliosababishwa na dawa huonekana kwenye ngozi. Kwa kawaida aleji inayosababishwa na dawa huwa haijitokezi mara ya kwanza dawa inapotumiwa, bali pale dawa inapotumiwa tena. Kama mzio utajitokeza mara ya kwanza mtu anapotumia dawa fulani, kwa kawaida huwa amewahi kutumia dawa hiyo lakini bila kujua. Hii ni kwa sababu mzio hautokei mara ya kwanza dawa inapoingia mwilini bali mara hiyo mwili hutengeneza kingamwili au zindiko na seli za kumbukumbu za lymphocyte kwa ajili ya dawa hiyo ambayo huchukuliwa kama kitu kisichotakiwa na mwili au antijeni. Wakati dawa hiyo inapotumiwa tena na kuingia mwilini seli za kingamwili huzalisha kemikali zinazoitwa 'mediator'. Mfano wa seli hizo ni Histamine ambazo athari yake kwa viungo ni dalili ambazo hudhihirika kama aleji.
Aleji ya dawa si sawa na athari ya dawa, inayoweza kujitokeza baada ya kula dawa ya aina fulani, ambayo kwa kawaida huambatanishwa na maelezo ya dawa. Mzio unaosababishwa na dawa pia ni tofauti na sumu ya dawa ambayo hutokea pale dawa inapotumiwa kwa kiasi kikubwa. Kuna baadhi ya dawa ambazo husababisha sana mzio kuliko nyinginezo. Dawa hizo kwanza kabisa ni antiobiotics kama vile penicillin, tetracycline na dawa zenye sulfa ambazo hutumika kutibu ugonjwa wa malaria. Asprini na dawa nyinginezo za kutuliza maumivu na kupunguza uvimbe zinazojulikana kama NSAID kwa mfano ibuprofen na indometacine. Pia dawa za kutibu saratani, dawa za kupooza mfumo wa kulinda mwili au zinazotibu magonjwa yanayosababishwa na hali hiyo kama vile rheumatoid fever na arthritis na krimu au lotion aina ya corticosteroid. Nyinginezo ni dawa zinazotumiwa na watu wenye Ukimwi na pia dawa za kutibu kifafa kama vile phenytoin au carbamezapine. Nyinginezo ni dawa au bidhaa zinazotokana na asali ya nyuki na pia mmea wa Echinacea ambao hutumika sana kama dawa.
Uwezekano wa aleji kujitokeza ni mkubwa zaidi pale dawa inapotumiwa mara nyingi, inapopakwa juu ya ngozi au kudungwa mwilini kwa sindano, kuliko wakati inaponywewa kupitia mdomo. Kwa maneno mengine tunaweza kusema kuwa, mzio wa dawa humaanisha kuwa mwili umekataa dawa fulani au haupatani nayo.

&&&&&&

Dalili za aleji inayosababishwa na dawa kwa kawaida hutokea katika kipindi cha saa moja baada ya kutumiwa dawa. Mara chache aleji huweza kutokea pia baada ya masaa, siku au wiki kadhaa. Miongoni mwa dalili za mzio wa dawa ni vipele vya ngozi, muwasho, kuvimba, macho kutoa machozi na ngozi kubadilika rangi. Dalili nyinginezo za aleji ya dawa ni homa, kuvimba, kubanwa na pumzi, makamasi na kupumua kwa kutoa sauti kama mtu anayepiga filimbi hali inayojulikama kitaalamu kama wheezing.
Mara chache mzio wa dawa huweza kusababisha madhara makubwa kwa mtu ambapo mwili huonesha dalili ya jumla inayohatarisha maisha ijulikanayo kama Anaphylaxis ambayo hukwamisha utendaji wa mfumo wa mwili. Viashiria vya hali hiyo ni kubwanwa njia ya hewa na koo, suala linalopelekea kushindwa kupumua. Kichefuchefu au maumivu ya tumbo yasiyo ya kawaida, kuharisha au kutapika, kizunguzungu au kuhisi kichwa chepesi, mwili kudhoofika na mapigo ya moyo kwenda mbio. Pia mwenye hali hiyo presha yake hushuka, huwa na dalili za kifafa na kupoteza fahamu.
Vilevile kuna matatizo ambayo yanaweza kujitokeza baada ya siku au wiki kadhaa baada ya kutumia dawa, ambayo yanaweza kubakia kwa muda mrefu hata baada ya kuacha kutumia dawa. Matatizo hayo ni ugonjwa wa Serum ambao husabisha homa, maumivu ya viungo, vipele, kuvimba na kichefuchefu. Tatizo jingine ni ukosefu wa damu ambapo chembe nyekundu za damu hupungua na pia kuvimba figo na kutokewa na vipele vinavyoambatana na matatizo katika seli nyeupe za damu.

&&&&&&

Mpenzi msikilizaji iwapo utatumia dawa na kwa bahati mbaya zikakuletea aleji unapaswa kumuona daktari mara moja au kwenda hospitali haraka ili kupata matibabu na kuondoa aleji. Iwapo utapata dalili zinazoashiria Anaphylaxis kama tulivyoeleza kabla unapaswa kuomba haraka msaada wa kitiba ili kuokoa maisha. Pia unapaswa kuacha kutumia dawa iliyokusababishia dalili kali za mzio.
Na kufikia hapo wapenzi wasikilizaji hatuna la ziada, natumaini mmefaidika vya kutosha. Tukutane tena wiki ijayo panapo majaaliwa na tusisahau kuzitunza afya zetu!

 

 

 

Andika maoni


Msimbo salama (Security code)
Upyesha (Refresh)

Hadithi ya Uongofu (39)

Ni matarajio yangu kuwa, hamjambo wapenzi wasikilizaji na tunakutana tena katika sehemu nyingine ya kipindi hiki cha Hadithi ya Uongofu. …

Ufeministi, Itikadi na Misingi yake (26)

Assalaamu Alaykum wafuatiliaji wa kipindi hiki na karibuni kuwa nasi katika sehemu nyingine ya kipindi hiki kinachokosoa itikadi ya ufeministi …

Ulaji wa Lishe Bora katika Kipindi Chote cha Maisha

Wataalamu wa Afya wanasema kuwa, awamu mbalimbali za maisha zinahitajia ulaji wa chakula wa aina tofauti. Iwapo wewe ni mtoto, …

Maua mawili ya Mtume wa Allah (31) Sauti

Bismillahir Rahmanir Rahim. Assalaamu Alaykum Warahmatullahi Wabarakaatuh Karibuni wapenzi wasikilizaji wa Idhaa ya Kiswahili Radio Tehran na wasomaji wa mtandao …