Tovuti Hii Imefungwa. Tumehamia Kwenye Parstoday Kiswahili
Jumatatu, 19 Januari 2015 15:25

Tatizo la mzio au allergy

Tatizo la mzio au allergy

Ni matumaini yangu kuwa hamjambo wapenzi wasikilizaji na karibuni katika kipindi kingine cha Ijue Afya Yako. Leo tutatungumzia tatizo la mzio au alegi. Ili kufahamu tatizo hilo na kujua jinsi ya kukabiliana nalo ungana nami hadi mwisho wa kipindi hiki.


&&&&&

Mzio au aleji (allergy) ni matokeo ya mpambano uliopitiliza kati ya kinga ya mwili na kitu chochote ambacho kwa ujumla huwa hakina madhara kwa mwili pale inapotokea kimeingia ndani ya mwili au kimegusa sehemu fulani ya mwili. Mpambano huu ndio husababisha mtu kuwa na dalili za aleji au mzio. Kwa kawaida kinga ya mwili huulinda mwili dhidi ya vitu mbalimbali hatari kwa afya kama vile vimelea vya magonjwa kama bakteria na virusi, lakini wakati mwingine inaweza kupambana pia na vitu ambavyo havina madhara yeyote kwa mwili ambavyo huitwa allergens. Baadhi ya vitu vinavyosababisha mzio ni pamoja na vumbi, baadhi ya dawa, baadhi ya vyakula, kung'atwa na wadudu kama vile nyuki, aina fulani ya uyoga, vumbi vumbi la maua (pollens) na kadhalika. Kuwa na mzio ni jambo la kawaida. Haishangazi kuona kuna baadhi ya watu wanaopatwa na mafua karibu kila siku au wengine kushindwa kuvaa baadhi ya nguo, vitu kama saa au cheni za dhahabu kwa vile tu huvimba mwili au kuwashwa pindi wanapofanya hivyo. Watu wenye aleji au mzio huwa na hisia zisizo za kawaida za mwili dhidi ya baadhi ya vitu. Mwili unapokumbana na vitu vinavyosababisha aleji mfumo wa kinga ya mwili huzalisha kemikali mbalimbali ikiwemo histamine ambayo hupambana na allergens hizo. Matatizo ya kijenetiki pamoja na hali tofauti tofauti za kimazingira zote zinahusika katika kusababisha mtu kuwa na mzio. Wapo baadhi ya watu ambao hukumbana na mzio pindi wanapokuwa katika mazingira ya joto au baridi, huku wengine hupatwa na mzio pindi wanapopigwa na jua kali. Wakati mwingine, hata msuguano mdogo tu wa ngozi unaweza kuwasababishia baadhi ya watu dalili fulani fulani za mzio. Kwa kawaida, mzio wa aina fulani huwa haurithishwi miongoni mwa wanafamilia. Kwa mfano kama mzazi ana aleji na baridi si lazima watoto wake pia wawe na aleji hiyo hiyo ya baridi ingawa wanaweza kuwa na aina nyingine ya aleji. Uwezekano wa mtoto kupata aleji huongezeka zaidi iwapo wazazi wote wawili wana aleji na vitu fulani fulani na huwa zaidi iwapo mama ndiye mwenye aleji.


&&&&&

Nini dalili za mtu mwenye aleji?
Dalili za aleji ni nyingi kwa kutegemea eneo husika la mwili, lakini kwa ujumla kama ni mfumo wa hewa ndiyo ulioguswa, mtu anaweza kuwa na matatizo katika kupumua yaani akapata kikohozi au kubanwa na pumzi, makamasi na kuziba kwa pua, muwasho kwenye pua na koo, au kupumua kwa kutoa sauti kama mtu anayepiga filimbi. Lakini kama macho yataguswa, muhusika huhisi hali ya macho kuchoma, kutiririkwa na machozi na muwasho kwenye macho, macho kuvimba na kuwa mekundu na kadhalika. Iwapo mtu atakula kitu ambacho ana aleji nacho anaweza kuwa na dalili kama vile kuharisha, kichefuchefu, kutapika, kusokotwa au kuumwa na tumbo na hata hali mbaya ya kutishia maisha. Vinavyosababisha mzio au allergens vinapogusa ngozi vinaweza kusababisha ngozi kuwa na mabaka mabaka, kubabuka, kuvimba, muwasho, kuota vipele na malengelenge, michubuko au ngozi kuwa nyekundu. Aleji zinazohusisha mwili mzima zinaweza kuwa na mkusanyiko wa dalili zote tulizozitaja. Wakati mwingine aleji inaweza kushadidisha hali ya baadhi ya watu wenye magonjwa kama ugonjwa wa ngozi wa eczema au pumu na kufanya hali iwe mbaya zaidi.
Vipimo na uchunguzi wa mzio
Mgonjwa ataulizwa kuhusu historia ya tatizo lake, ni lini lilianza na vitu gani humfanya awe hivyo. Aidha tabibu pia atapenda kufahamu kuhusu dalili nyingine zinazoambatana na tatizo linamlomkabili mgonjwa. Baadaye vipimo vya aleji vinaweza kufanyika ili kufahamu hasa ni kitu gani mgonjwa ana aleji nacho na kama kweli dalili alizo nazo zinatokana na aleji au zinatokana na sababu nyingine. Hii ni kwa sababu, kuna baadhi ya mambo yanayoweza kumsababishia mtu dalili zinazofanana kabisa na mtu aliye na aleji ya kitu fulani. Kwa mfano matumizi ya aina fulani ya dawa yanaweza kumsababishia mtu mikwaruzo au michubuko katika ngozi inayofanana na aleji nyingine, au mtu anaweza kuwa na mafua au kikohozi kwa sababu ya maambukizi ya bakteria au virusi na si kwa sababu ya aleji. Kipimo maarufu kabisa cha kutambua aleji kwa mtu ni kipimo cha ngozi (skin testing) ambapo mgonjwa huwekewa baadhi ya vitu vinavyokisiwa kumletea aleji juu ya ngozi yake na kisha ngozi huchomwa kidogo kwa sindano, ili hivyo vitu viweze kuingia ndani ya ngozi na wakati huo daktari akichunguza kama kuna mabadiliko yeyote kama vile uvimbe au ngozi kuwa nyekundu katika eneo lilichomwa. Kipimo cha namna hii hufaa zaidi kwa watoto wadogo kwa vile ni rahisi kufanyika kwao bila usumbufu mkubwa. Aina nyingine ya kipimo cha aleji cha ngozi hufanyika kwa kubandika vitu vinavyohisiwa kuleta mzio kwenye ngozi kinachojulikana kama (patch testing) au kuchoma sindano zenye allergens sehemu ya juu ya ngozi na kuchunguza uwepo wa mabadiliko yeyote katika ngozi.
Vipimo vingine ni pamoja na vipimo vya damu ambavyo huonesha ongezeko la immunoglobin E ambayo huashiria uwepo wa vitu vinavyosababisha aleji, na kipimo cha damu chenye kuonesha ongezeko la eosinophil iwapo kuna aleji, ambayo ni sehemu ya chembe nyeupe za damu. Lakini pia daktari anaweza kumshauri mgonjwa kuepuka baadhi ya vitu hasa dawa au aina fulani za vyakula ili kuona kama atapata nafuu yeyote au kumshauri kutumia baadhi ya vitu anavyohisi vitamletea matatizo ili kuona kama atapata dalili zozote zile.


&&&&&&&


Je mzio au aleji inatibika?
Njia bora zaidi ya kutibu na kupunguza uwezekano wa kupata aleji ni kutambua kitu au vitu vinavyokusababishia hali hiyo na kuviepuka. Kama ni chakula au dawa au kemikali, epuka kabisa matumizi yake, na kama ni vumbi jitahidi kukaa mbali nalo. Kadhalika shambulio kali la aleji linaweza kusababisha muhusika kulazwa hospitali kwa vile lisipodhibitiwa kifo kinaweza kutokea. Zipo aina mbalimbali za dawa zinazotumika kutibu na kuzuia aleji, kulingana na jinsi daktari atakavyoona inafaa kwa kuzingatia ukali wa tatizo, dalili zake, umri wa mgonjwa pamoja na hali yake ya kiafya kwa ujumla. Dawa hizi ni pamoja na za jamii ya antihistamines, za jamii ya corticosteroids ambazo ni maalumu kwa kutuliza mcharuko mwilini ambazo huwa katika miundo mbalimbali kama vile krimu, matone ya kuweka machoni au masikioni, za kuvuta au kupulizia, sindano au vidonge. Kwa wale wenye mafua na kuziba kwa pua, hushauriwa kutumia dawa zinazosaidia kufungua pua, hata hivyo dawa hizi hazina budi kutumiwa kwa uangalifu hasa kwa watu wenye magonjwa ya shinikizo la damu au moyo. Dawa nyingine ni zile zinazosaidia kuzuia vitu vinavyosababisha aleji. Aina nyingi za aleji hutibika kwa urahisi kwa kutumia dawa. Wapo baadhi ya watu khususan watoto wanaoweza kujenga hali ya aleji dhidi ya aina fulani za vyakula, hali wanayoweza kuendelea nayo mpaka ukubwani. Kwa kawaida, kitu kikimletea mtu aleji utotoni huendelea kumuathiri daima. Madhara ya aleji ni pamoja na kupata shambulio kali ambalo linaweza kusababisha kifo kama matibabu hayatofanywa haraka. Kuna baadhi ya watu ambao, kwa mfano, wakila baadhi ya vyakula huvimba mwili na kushindwa kupumua mpaka kuhitaji kulazwa hospitali na kusaidiwa kupumua kwa mashine. Madhara mengine ni pamoja na shida ya kuvuta pumzi au kushuka kwa shinikizo la damu (kupata shock). Namna ya kujikinga na aleji
Kuna baadhi ya watu wanaonasibisha aleji na itikadi za kichawi suala ambalo si sawa, kwani mzio ni tatizo linalojulikana kitiba na pia kuweza kutibika. Pindi mtu anapopatwa na aina fulani ya aleji, kinga bora ni kukwepa mambo yote yanayoweza kuchochea kutokea kwa shambulizi la aleji. Kama ni chakula, ajitahidi kuepuka aina hiyo ya chakula na kama aleji inasababishwa na dawa, basi muathiriwa aache matumizi ya dawa hizo na pia amueleze daktari wake au muuguzi kuhusu hali hiyo mapema kabla hajapatiwa dawa hizo pindi anapokwenda hospitali kwa matibabu ya matatizo mengine. Wapo watoto wachanga ambao hupatwa na aleji mara tu wanaponyweshwa maziwa ya ng'ombe kwa mara ya kwanza. Hii hutokana na aina fulani ya protini iliyopo kwenye maziwa hayo. Ili kuwakinga wasipatwe na aina hii ya aleji, mama hushauriwa kumnyonyesha mtoto wake angalau kwa miezi
minne ya mwanzo huku akiepuka kumpa maziwa ya ng'ombe katika umri huu. Baadhi ya kinamama hudhani kwamba kubadilisha aina ya chakula wakati wa kunyonyesha kunaweza kusaidia kumuepuesha mtoto na aleji. Hii si kweli kwa kuwa imeonekana kuwa, kitendo hiki hakisaidii kumkinga mtoto dhidi ya mzio.
Uchunguzi umewahi kuonesha kuwa watoto waliozaliwa katika mazingira yenye vumbi na mifugo ambako kuna kiasi kikubwa cha manyoya ya wanyama na vumbi, wana uwezekano mdogo wa kupata aleji ya vitu vya aina hii pindi watakapokuwa wakubwa, ikilinganishwa na wale waliozaliwa katika mazingira yasiyo na hali hizo. Hii ni kwa vile, mazingira ya vumbi huwajengea watoto hawa aina fulani ya kinga dhidi ya aleji, tofauti na wenzao. Hata hivyo, watoto waliohamia katika mazingira haya wakiwa na umri mkubwa wameonekana kuathirika kwa vile wamekosa ile kinga ya utotoni.


&&&&&&&&&&&

 

 

 

Andika maoni


Msimbo salama (Security code)
Upyesha (Refresh)

Hadithi ya Uongofu (39)

Ni matarajio yangu kuwa, hamjambo wapenzi wasikilizaji na tunakutana tena katika sehemu nyingine ya kipindi hiki cha Hadithi ya Uongofu. …

Ufeministi, Itikadi na Misingi yake (26)

Assalaamu Alaykum wafuatiliaji wa kipindi hiki na karibuni kuwa nasi katika sehemu nyingine ya kipindi hiki kinachokosoa itikadi ya ufeministi …

Ulaji wa Lishe Bora katika Kipindi Chote cha Maisha

Wataalamu wa Afya wanasema kuwa, awamu mbalimbali za maisha zinahitajia ulaji wa chakula wa aina tofauti. Iwapo wewe ni mtoto, …

Maua mawili ya Mtume wa Allah (31) Sauti

Bismillahir Rahmanir Rahim. Assalaamu Alaykum Warahmatullahi Wabarakaatuh Karibuni wapenzi wasikilizaji wa Idhaa ya Kiswahili Radio Tehran na wasomaji wa mtandao …